KUITWA ILI UMTUMIKIE MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Watu wengi sana MUNGU Baba amewaita katika Wokovu ili wamtumikie lakini sio wote walimtumikia hata kama sauti ya kuitwa waliisikia.
Luka 10:2 ''Akawaambia, Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.''
ROHO MTAKATIFU kama msimamizi wa Kanisa la KRISTO duniani amewapa karama waliookoka wengi tu ili wamtumikie KRISTO katika injili.
Kumbuka kumtumikia YESU KRISTO ndio pia kumtumikia MUNGU.
Biblia inasema kwamba YESU KRISTO na MUNGU Baba ni umoja.
Ukimuona YESU KRISTO maana yake umemuona MUNGU.
Ukimwendea YESU KRISTO maana yake umemwendea MUNGU, Ukimtumikia YESU KRISTO maana yake unamtumikia MUNGU pekee aliye hai na aliyeumba mbingu na dunia.
Yohana 10:30 '' Mimi na Baba tu umoja.''
Ndio Maana Biblia inasema   ''Aliyeniona mimi(YESU) amemwona Baba(MUNGU)-Yohana 14:9.
Kwahiyo ninapokujulisha somo hili naomba utambue kwamba ninapotaja kumtumikia MUNGU ni sawa na ninapotaka kumtumikia YESU KRISTO. Nimeamua nijulishe hili ili kuwasaidia wale ndugu ambao wao hujiita watumishi wa MUNGU wakati hawamtumikii YESU KRISTO. Ukweli ni kwamba hakuna mtumishi wa MUNGU nje na KRISTO YESU.
Na katika kumtumikia MUNGU ni lazima ujue kiini cha utumishi wako ni kuwaleta watu kwa YESU, 
Marko 16:15-16 ''Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. ''
Yaani kuwafanya watu waokolewe na Bwana YESU. Hakuna utumishi sahihi nje na kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa YESU wanaoishi maisha matakatifu. Ukiona mtu anajiita mtumishi na hawafanyi watu kuokolewa na Bwana YESU ujue huyo sio mtumishi wa MUNGU.
Sasa tuendelee. 
MUNGU hashindwi kukuita ili umtumikie haijalishi uko katika mazingira gani, hali gani.
MUNGU anaweza kukuita ili umtumikie haijalishi una muda au huna muda, umesoma au haujasoma.
BWANA anaweza akamuita mtu yeyote katika maisha yake ili amtumikie.

Nabii Amosi alipoitwa kumtumikia MUNGU alikuwa wala hahusiani na watumishi wa MUNGU kama ilivyokuwa imezoeleka katika Israeli, hadi makuhani akina Amazia wakamfanyia fitina.
Amosi 7:14-15 ''Ndipo Amosii akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye BWANA akanitwaa, katika kufuatana na kundi; BWANA akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.''
Amosi alikuwa mchungaji wa wanyama na mtunzaji wa bustani ya miti ya mikuyu alikuwa anafuatana na watu wa MUNGU  na MUNGU akamuita ili amtumikie.
Hata wewe inawezekana umeokoka tu na huhudhuria ibada tu, ndugu, MUNGU anaweza kukuita kibinafsi kabisa  ili ufanye kazi yake aliyokupangia.
Ndugu, ukisikia sauti ya Bwana YESU ya utumishi hakikisha unamtumikia.
Yeremia aliitwa akiwa bado mdogo lakini MUNGU alimpa nafasi ya kutumika kama ambavyo anaweza akakuita wewe umtumikie katika injili.
Yeremia 1:4-8 " Neno la BWANA lilinijia, kusema,
Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.
Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini BWANA akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA."


 Kuitwa kwako na MUNGU ili umtumikie haitegemei elimu yako, kipato chako, hadhi yako wala hali yako.
Kuitwa kwako na MUNGU ili umtumikie katika Kanisa lake huwa haitegemei umri wako tena haitegemei Unajua nini na wala haitegemei unakubalikaje kwa wanadamu.
Kuitwa kwako na MUNGU ili umtumikie katika injili inategemea wewe kukubali wito, kuishi maisha matakatifu na kukubali kufundishwa na ROHO MTAKATIFU huku ukilitumia Neno la MUNGU kwa haki.

1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana.''

Katika kujua zaidi juu ya kuitwa kwako na KRISTO inakupasa ujue kutofautisha katika ya wito wa MUNGU na ule wito wa watu.
Kuna tofauti kati ya wito unaotokana na watu na wito wa MUNGU.
Watu wanaweza kukuona kwamba unafaa kuwa kiongozi wao, huo ni wito unaotokana na wanadamu.
Watu wanaweza kukuona unafaa kuwa Mchungaji wao au kiongozi wao wa kiroho, huo ni wito wa wanadamu.
Kama wito huo utakuwa tofauti na wito wa MUNGU basi hakika wito wa wanadamu unaweza kukushinda baadae.
Tunahitaji wito wa MUNGU na sio wito unaotokana na wanadamu tu.
Watu wanaweza kumuona mtu anawafaa sana kuwa kiongozi wao wa kiroho lakini akichukua nafasi hiyo waliyompa, baada ya muda anaiona mzigo au ni kero kwake na kuacha, kwa sababu tu amepewa wito na wanadamu.
Kuna watu wa makanisani huteuliwa na viongozi wa kanisa husika kwenda kusimamia makanisa au huduma mpya na huko badala kuendeleza kazi ya MUNGU wao huiua kazi ya MUNGU ile kwa sababu hawana mzigo wala wito wa MUNGU ndani yao wa kazi ile, ila wana wito uliotokana na viwango na sifa za wanadamu.
Ndugu, nakuomba fanyia kazi wito wa MUNGU ndani yako na sio kuuacha wito wa MUNGU na kuanza kufanyia kazi wito wa kibinadamu.
Unaweza kukuta watu wanakuambia "Wewe ni mhubiri mzuri sana hivyo fungua kanisa lako"
Kama huna wito wa MUNGU yanaweza kukushinda mapema Kabisa.

Watu wanaweza kukuambia kwamba "Wewe una sauti nzuri sana hivyo record nyimbo zako na utakuwa mwimbaji mkubwa sana" Ukijaribu kuimba na kuona hufikii viwango ulivyoambiwa unaweza ukavunjika moyo mapema sana.
Ndugu inawezekana MUNGU amekuita katika kazi nyingine ya injili na wewe humtii yeye na sasa unasikiliza watu wanavyokuelekeza cha kufanya ambacho ni nje na wito wa MUNGU.
Ndugu hakikisha unaomba MUNGU ili akujulishe amekuita katika wito gani na karama gani katika injili ya KRISTO.

Hapa ROHO wa MUNGU alisema juu ya wito aliowaitia Barnaba na Mtume Paulo, hata wewe anaweza kukujulisha pia kwamba amekuitia katika nini, unahitaji tu kuomba
Matendo 13:2-3 “…..nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia

MUNGU anataka haya kwako wewe Mtumishi wake.
Kumb 28:1 '' Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;''
1. Je unaisikia sauti ya MUNGU?
MUNGU anataka uisikie sauti yake.
Sauti ya MUNGU ni Biblia pamoja na  Neno la ufunuo analokupa ROHO MTAKATIFU kutoka katika Neno la MUNGU yaani kutoka katika Biblia.
 
2. Je unafanya nini kwa MUNGU katika ulichokisikia kwa MUNGU?
MUNGU anataka ukifanyie kazi alichokueleza ulipoisikia sauti yake. 

3. Je unatembea katika kusudi la MUNGU?
Hakikisha unaisikia sauti ya MUNGU na fanyia kazi kile ulichokisikia kwa MUNGU ili utembee kwenye kusudi la MUNGU.
Kumbuka Amosi 3:7 Biblia inasema ''Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.'' 



MUNGU anapokuita katika KRISTO kwenye kazi yake huwa anahusika na haya yafuatayo yanayotokana na wewe kuisikia sauti yake.
 
1. Anakuokoa, kwa wewe kumpokea YESU KRISTO.

Yohana 3:16 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.''
 Kama wewe hujaokoka hakika wewe hujaanza kuwa mtumishi wa MUNGU. Hivyo mpokee kwanza YESU KRISTO kama Mwokozi wako na uache dhambi ndipo utaanza kuwa mtumishi wa MUNGU.

2. Anakuchagua kwa utumishi.
Mathayo 28:19-20 '' Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.'
''Enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu'' Huo ndio wito wa MUNGU kwako uliyechaguliwa. Ni MUNGU amekuchagua ili umtumikie.

3. Anakuhesabia haki kwa Wokovu.
Warumi 5:1-2  ''Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa MUNGU, kwa njia ya Bwana wetu YESU KRISTO, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa MUNGU.''
 
4. Anakutengeneza ili umtumikie.

 Zaburi 119:105 ''Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. ''
 
 MUNGU anakutengeneza kwa Neno lake.
Anakutengeneza kwa maisha yako kubadilishwa na Neno la MUNGU ili umfananae KRISTO.


5. Anakupa Neno lake la injili.

Yohana 17:14 '' Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.'' 
YESU ametupa Neno la MUNGU ambalo injili yake, hivyo mtumishi lazime utembee na injili ya YESU KRISTO siku zote.

6. Anakupa karama na kipawa.
1 Kor 12:4-7 ''Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule. Tena pana tofauti za huduma, na Bwana(YESU) ni yeye yule. Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.  Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana. '' 

7. Anakupa nguvu za ROHO MTAKATIFU.

Matendo 1:8 '' Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu ROHO MTAKATIFU; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.''
Kama huna nguvu za ROHO MTAKATIFU hakikisha unajifunza sana kuhusu ROHO MTAKATIFU na uwe muombaji hakika utapata nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Ndugu mtumikie MUNGU katika injili ya KRISTO YESU ya Wokovu wa milele.

Lakini pia kumbuka jambo hili ya kwamba huwezi kuwa mtumishi mzuri wa MUNGU kama
1. Mvivu wa kusoma Neno la MUNGU.

2. Mvivu wa kuomba.
3. Mvivu wa kuzingatia mambo ya MUNGU.
4. Mvivu wa kutii Kanuni za MUNGU.
5. Mvivu wa kufanya kazi ya MUNGU aliyokupa.
Ukiwa mtumishi mvivu katika hayo matano hakika huwezi kuwa mtumishi mzuri wa kuwasaidia watu waliopendwa na mbingu ili wamjie KRISTO na kuokolewa.
Waebrania 6:10-12 '' Maana MUNGU si dhalimu hata aisahau kazi yenu, na pendo lile mlilolidhihirisha kwa jina lake, kwa kuwa mmewahudumia watakatifu, na hata hivi sasa mngali mkiwahudumia. Nasi twataka sana kila mmoja wenu aidhihirishe bidii ile ile, kwa utimilifu wa matumaini hata mwisho; ili msiwe wavivu, bali mkawe wafuasi wa hao wazirithio ahadi kwa imani na uvumilivu.''
 
 Jambo la mwisho naomba nikushauri mtumishi mwenzangu wa YESU KRISTO.
Kumbuka hujaitwa peke yako ili umtumikie Bwana YESU.
Wapo watumishi wengi sana wa Bwana YESU hivyo usijione kwamba ni wewe tu ndio mtumishi sahihi wa MUNGU.
Usiwaseme vibaya watumishi wenzako wa Bwana YESU.
Kama kuna mtumishi anafundisha uongo huyo sio mtumishi wa Bwana YESU lakini kama yuko mtumishi wa kweli wa Bwana YESU na anaifundisha kweli ya MUNGU basi usikubali kumsema vibaya.
Muogope Mtumishi aliyeitwa na MUNGU.
Ukimsema vibaya ujue utamchukuza MUNGU aliyemwita.
Hata kama huyo mtumishi hukubaliani naye heri kukaa kimya kuliko kumzushia uongo. MUNGU anaweza kukupiga na ukashangaa wakati ulijiona una haki.

Haruni alikuwa kuhani mkuu na alipigwa ukoma kwa sababu ya kumsema vibaya mtumishi mwenzake MUNGU.
Miriamu alikuwa kiongozi wa kusifu na kuabudu na alikuwa mtumishi wa MUNGU lakini alipigwa ukoma kwa sababu ya kumsema mtumishi mwenzake Musa.
Sasa kama kuhani mkuu wa taifa zima anapata ukoma kwa kosa la kumsema mtumishi mwingine wa MUNGU aliyeitwa na MUNGU itakuaje kwa upande wako kama utamsema vibaya mchungaji wako kwa sababu tu unajiona una upako na unatumika kuliko Mchungaji wako?
Ndugu yazingatie haya katika utumishi wako.
Unajua akina Haruni na Miriamu walikosea nini katika utumishi wao?
Biblia inasema Katika Hesabu 12:3  '' Wakasema(Haruni na Miriamu), Je! Ni kweli BWANA amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? BWANA akasikia maneno yao.''
Biblia inaendelea kusema katika Mstari wa 9 hadi wa 11 wa hiyo Hesabu 11 kwamba ''Hasira za BWANA zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma. Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi.''
Ndugu usikubali kumsema vibaya mtumishi mwenzako wa kweli wa KRISTO.
Lakini pia  Mtumishi wa KRISTO aliyeitwa huisema kweli ya MUNGU na huyo kama kweli ameitwa na MUNGU basi usimzushie uongo, hata kama hakubariki wewe na hakufurahishi, ni heri kukaa kimya na sio kutaka kumzuia kufanya kazi ya MUNGU, MUNGU anaweza kukupiga maana unalizuia kusudi lake.

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments