MAOMBI YA KUITA UTISHO WA MUNGU UKUZUNGUKE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu, tena karibu sana tujifunze Neno la MUNGU na tuombe maombi ya ushindi mkuu.
Tunaishi katika kipindi ambacho kuna hila nyingi za shetani na mawakala zake zidi yetu sisi wateule wa KRISTO. Ni kweli sisi ni waombaji na tunaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU, lakini shetani naye hujaribu kuleta vitisho vyake. 
Kuna kipindi fulani mimi nilikuwa kila nikiota ndoto na kumuona adui akijaribu kufanya kazi zake, nilikuwa nafurahi baada ya kuota hiyo ndoto kwa sababu nilijua ana bahati mbaya huyo adui niliyemuona ndotoni, kwa sababu kwa maombi ambayo nitaomba kumhusu yeye, huyo atajua kabisa ya kwamba kushindana na mtu aliye katika ulimwengu wa Nuru ya KRISTO huleta madhara makubwa katika ulimwengu wa roho wa giza. Nilikuwa nikiona adui wa aina yeyote awe amejigeuza kuwa wanyama au vitu au chochote nilikuwa najua kabisa kwamba MUNGU amenifunulia kumjua adui huyo na sasa lazima kwa maombi yangu nihakikishe anapata madhara ambayo hajawahi kuyaona. 
Sijui ndugu yangu unayejifunza somo hili, huwa ukiota mfano unafukuzwa na nyoka au unamezwa na nyoka huwa unaombaje, sijui wewe ukiota kuna mtu anataka kukutumbukiza shimoni huwa unaombaje. Mimi sijui maadui zako huwa unawaona wanakushambulia katika nini. Ndugu unahitaji kuomba na unahitaji sana kumpendeza MUNGU ili uwe katika mikono salama.
Moja ya vitu muhimu kuwa navyo Mteule wa KRISTO ni utisho wa MUNGU.
Utisho wa MUNGU humtisha kila anayetumika kipepo dhidi yako.
Utisho wa MUNGU huzifanya silaha za shetani zisifanye kazi hata kama zimetumwa kwako.
Waisraeli walipokuwa wanatoka Misri walipita katika mataifa mengi lakini ajabu kila taifa walimopita , taifa hilo liliwaogopa sana kwa sababu utisho wa MUNGU uliwatangulia.
Kutoka 23:27 ''Nitatuma utisho wangu utangulie mbele yako, nami nitawafadhaisha watu wote utakaowafikilia, nami nitawafanya hao adui zako wote wakuonyeshe maungo yao.''

 Utisho wa MUNGU uliwafanya hadi adui zao kuwapa siri zao na hata mipango yao kabla hata wateule wa MUNGU hawajafika katika ile nchi. Leo waliookolewa na Bwana YESU ndio Wateule wa MUNGU lakini ajabu leo baadhi ya wateule wa MUNGU  tena wengi hawana utisho wa MUNGU.
Leo kuna watu wa Kanisa hukabwa na majinamizi na majini.
Leo  mara utasikia Mtumishi fulani ameota anafanya mapenzi na majini.
Ndugu yangu, omba maombi ya kumwambia MUNGU Baba akupe utisho dhidi ya nguvu zote za giza.
Waisraeli kama Wateule wa MUNGU walikuwa na utisho wa MUNGU.
Yeremia  32:21-22 '' ukawatoa watu wako, Israeli, katika nchi ya Misri, kwa ishara, na kwa ajabu, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na KWA UTISHO MKUU; ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kwamba utawapa, nchi iliyojaa maziwa na asali;''

Leo kuna wateule hutegewa hata uchawi kazini kwao, lakini kama ana utisho wa MUNGU basi kazi hizo za shetani hazitafanya kazi.

Ndugu ukiwa na utisho wa MUNGU hata kama utapita njiani ambako wachawi walitega majini ili atakayepita pale njiani yamwingie na lakini Mteule  wa MUNGU ukipita pale yale majini yatakupisha njia ili upite maana yatatambua kwamba wewe una utisho wa MUNGU na kwa njia hiyo hawawezi kukukaribia.
Ndugu mmoja alienda beach na kumbe huko beach kulikuwa kuna kitu cha kipepo kimetegwa ili atakayekikanyaga adhulike. Ndugu yule kwa bahati mbaya alikikanyaga kitu kile na pale pale akavimba mkuu na kuumwa sana kiasi kwamba mguu wake kwa jinsi ulivyovimba ukawa unatisha. Alihangaika sana hospitalini lakini hakupona hadi alipokimbilia maombezi kanisani.
Ndugu inawezekana kabisa njia panda ambako unapita pametegeshwa majini lakini ukiwa na utisho wa MUNGU wale majini watakuwa kama wamepigwa na shoti ya umeme na hawatafanya kazi yao hadi utakapoondoka eneo hilo.
Ndugu unahitaji sana kuwa na utisho wa MUNGU.
Kumb 2:24-25 '' Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama, nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake; anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano. Hivi leo nitaanza mimi kutia utisho wako na kuhofiwa kwako juu ya watu walio chini ya mbingu kila mahali, watakaosikia uvumi wako, na kutetemeka, na kuingiwa na uchungu kwa sababu yako.'

 Je unataka kumiliki baraka gani?
Je baraka ya mchumba? Je baraka ya kupata kazi? N.k
Kama huna utisho wa MUNGU hata baraka yako unaweza kupokonywa na anayetumika kipepo. Usipokuwa na utisho wa MUNGU hata mchumba wako mnayekaribia kufunga ndoa anaweza akachukuliwa na mtu mwingine aliyeenda kwenye madhabahu za shetani ili ampate.
Ndugu unahitaji sana utisho wa MUNGU.
Katika maandiko hapo juu unaona jinsi ambavyo MUNGU aliwamilikisha I
sraeli na utisho wake ulikuwa kwao.
Kila taifa walianza kuwahofia Israeli maana walijua Wakishindana na Taifa la MUNGU watapigwa.
Kila taifa walitetemeka na kuwa na hofu na kuingiwa na uchungu.
Hivyo ndivyo anavyotakiwa kuwa leo Mteule wa KRISTO dhidi ya mawakala wa shetani wote.
Inawsezekana kabisa una kesi mahakamani na unayemshitaki kwa kukudhulumu anatumia uchawi au rushwa. Ndugu ukiwa na utisho wa MUNGU yaliyopangwa kipepo ili uonewe hakika watayasahau ukifika wewe mahakamani na haki yako stahiki utaipata.
Kumb 11:25 '' Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama mbele yenu; BWANA, Mungu wenu, ataweka utisho wenu na kuhofiwa kwenu juu ya nchi yote mtakayoikanyaga, kama alivyowaambia.''

Mwanadamu alipoumbwa na MUNGU aliumbiwa utisho kwa viumbe wengine wote. Ndio maana Adamu na Eva waliwatawala hata wanyama wakali wote bila kudhurika.
Mwanzo 1:28 '' MUNGU akawabarikia, MUNGU akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.''
 Baada ya dhambi kuingia kwa wanadamu ndipo utisho wa MUNGU ukaondoka, ndio maana leo mwanadamu anaogopa wanyama wakali, hayo ni madhara ya dhambi yaani kuondoa utisho wa MUNGU kwa mtu. Wateule wa MUNGU leo kwa 
Neema ya MUNGU  alikuja kwa Bwana YESU KRISTO kuja kutuokoa.
Sasa tunalo jina la YESU KTISTO lenye utisho mkuu kwa kila nguvu za giza. Sasa inatupasa tutembee na utisho wa MUNGU.
Kumbuka pia kwamba leo wapo watu wana utisho wa kipepo badala ya utisho wa MUNGU.
Lakini ukiwa na utisho wa MUNGU hakika mwenye utisho wa kipepo atakukimbia.
Ndugu unatakiwa ufikie mahali wachawi wakuogope maana una utisho wa MUNGU.
Inatakiwa majini/mashetani wakutoe katika kundi la watu wa kuonea, kwa sababu sasa wewe unaishi maisha matakatifu katika KRISTO na hayo huambatana na utisho wa MUNGU.
Isaya  8:13 '' BWANA wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu.''

Uzuri wa utisho wa MUNGU ni kwamba utisho huo hauwezi kuwatisha wanadamu wema bali utisho huo huwatisha wanaotumika kipepo tu.
Ndugu unahitaji sana kuhakikisha una utisho wa MUNGU.
Leo kuna watu badala ya kuwa na utisho wa MUNGU wao wamewekewa na mawakala za shetani utisho wa kishetani.
Watu ambao wana utisho wa kishetani hata kuchumiwa au kupata mchumba haiwezekani, maana huyo anaogopwa au familia yake inaogopwa.
Ndugu unahitaji kufuta utisho wa kipepo na kisha omba  MUNGU akupe utisho wake dhidi ya mawakala wa shetani.

JINSI YA KUWA NA UTISHO WA MUNGU.

1. Kuokoka na kuishi maisha matakatifu ya Wokovu.

2 Kor 5:17 ''Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.''

2. Kuishi na ROHO MTAKATIFU.

1 Yohana 4:4 ''Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye aliye ndani yenu(ROHO MTAKATIFU) ni mkuu kuliko yeye(shetani) aliye katika dunia.''

3. Kuomba maombi ya kupokea utisho wa MUNGU.

Yohana 14:13 ''Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba)MUNGU0 atukuzwe ndani ya Mwana(YESU).''

4. Kuhudumiwa na Malaika wa MUNGU.

Zaburi 91: 11 '' Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.''

Kumbuka Malaika ni roho watumikao wakitumwa na MUNGU ili kuwahudumia wateule wa KRISTO.
Waebrania 1:14 '' Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu? ''

5. Kuwa na Neno la MUNGU Moyoni na kulitumia.

Ufunuo 12:11 '' Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.''

Hakika kwa Mteule wa MUNGU anayejitambua yaani anaishi maisha matakatifu na ni muombaji hakika maadui watamkimbia,
Zaburi 73:19 '' Namna gani wamekuwa ukiwa mara! Wametokomea na kutoweshwa kwa utisho.''

UOMBE MAOMBI GANI KATIKA SUALA LA UTISHO?

1. Omba maombi ya kufuta utisho wa kipepo kama unahisi unao, ili kutoa nafasi ya utisho wa MUNGU kuja kwako.

2. Ita utisho wa MUNGU uambatane na wewe kila uendako.

3. Kila ukitaka kwenda sehemu omba maombi ya kumwambia MUNGU akutangulie na aharibu kila hila za shetani na mawakala zake.

4. Omba maombi ya kuwapiga na kuwaharibu wanaotumika kipepo dhidi yako.


Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni MAOMBI YA KUITA UTISHO WA MUNGU UKUZUNGUKE.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea.


 MAOMBI YA KUITA UTISHO WA MUNGU UKUZUNGUKE.

YAHWEH MUNGU mwenye enzi yote, ninakushukuru kwa uzima ulionipa MUNGU wangu.
Niko mbele zako BWANA kwa ajili ya maombi kuhusu utisho.
Kwanza kabisa katika jina la YESU KRISTO ninaufuta utisho wa kipepo wa aina yeyote ambao shetani na mawakala zake waliuweka kwangu.
Wateja wanaogopa kuja katika biashara yangu kwa sababu ya utisho wa kipepo uliowekwa kwangu na wachawi, Sasa naufuta utisho huo wa kipepo, naufuta kwa damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO.
Wachumba wananikimbia na tatizo ni utisho wa kipepo uliowekwa kwangu hata mwanzo sikujia, Sasa naufuta utisho huo wa kipepo, naufuta kwa damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO.
 Ndugu zangu sasa wananiogopa bila kosa lolote,  sasa mwenzi wangu wa ndoa hana amani akiwa karibu yangu na kumbe ni utisho wa kipepo, Sasa naufuta utisho huoutisho  wa kipepo, naufuta kwa damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO.
 Kila nikiwa na rafiki hunikimbia kwa sababu ya utisho wa kipepo ambao sikuujua mwanzo, kazini kwangu kila mtu ananichukia na kunihofu vibaya kumbe sababu ni utisho wa kipepo, Sasa naufuta utisho huo wa kipepo, naufuta kwa damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO.
 Katika jambo lolote ambalo shetani na mawakala zake wameweka utisho wa kipepo ili nitengwe, nikataliwe, nionewe au ninyanyasike,
Sasa naufuta utisho huo wa kipepo, naufuta kwa damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO.
 Ee MUNGU Baba sasa baada ya kuufuta utisho wa giza naomba wewe ndiye unipe utisho wako mtakatifu ambao wanaotumika kipepo wote ndio wanikimbie wao na wala kazi zao za kipepo hazitayagusa maisha yangu kuanzia sasa.
Kama ni dhambi zangu ndizo ziliondoa utisho wako kwangu, ee MUNGU Muumbaji wangu naomba unisamehe dhambi zangu zote na naomba sasa niishi maisha matakatifu katika Wokovu wako ili utisho wako uendelee kuwa na mimi daima.
ROHO MTAKATIFU wa MUNGU nakuomba kwa neema yako BWANA uwe unanikumbusha kuomba kila ninapotaka kwenda sehemu yeyote ili utisho wa MUNGU Baba unitangulie na ili mawakala wa shetani wote wapigwe na wakimbie mbele yangu.
Ninaomba pia ROHO MTAKATIFU kwa neema yako unifundishe jinsi ya kuombea safari zangu na unipe ufunuo wa jinsi ya kuomba maana wewe hata kabla sijaondoka nyumbani unajua yaliyoko mbele yangu. Nakuomba Ee BWANA unifundishe kuomba sawasawa na kusudi lako na ili wachawi na kila mawakala za shetani wakimbie mbele yangu siku zote.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO sasa ninawapiga maadui wote wanaotumika kipepo dhidi yangu, nawapiga kwa jina la YESU KRISTO aliye hai.
Kila adui anayefuatilia uchumi wangu, kazi yangu na kipato changu, ninampiga katika ulimwengu wa roho na kuharibu kazi zake zote, ninaharibu kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
Kila adui anayefuatilia kibali changu na baraka zangu, ninamharibu kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
 Kila wakala wa shetani anayefuatilia afya yangu akitaka niwe na maisha ya kuumwa kila mara, ninamharibu kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
Kila adui anayefuatilia uzao wangu na ndoa yangu,ninamharibu kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
Kila adui anayeleta uvamizi wake katika uchumba wangu/ ndoa yangu, ninamharibu kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
Kila adui anyefuatilia familia yangu na kazi yangu,ninamharibu kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu aliye hai.
 Nakushukuru MUNGU Baba wa mbinguni maana katika wewe nimeshinda.
Nakushukuru Bwana YESU maana kwa neema yako mimi kuanzia leo ni mshindi dhidi ya kila wakala wa shetani.
Nakushukuru ROHO MTAKATIFU maana wewe uko pamoja na mimi na nikiwa na wewe mimi nitashinda.
Katika Jina la YESU KRISTO nimeomba na kushukuru.
Amen, Amen, Ameeeeeeeeeeeen
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
+255714252292.

mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments