MBINU SITA(6) ZA SHETANI KUMKAMATA MTU WA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
MBINU SITA(6) ZA SHETANI KUMKAMATA MTU WA MUNGU.

Bwana YESU atukuzwe mtu wa MUNGU.
Karibu tijfunze Neno la MUNGU.
Samsoni alikuwa mnadhiri wa MUNGU kama ambavyo wewe Uliyeokoka ulivyo mnadhiri wa MUNGU.
Waamuzi 13:3-5 ''
Malaika wa BWANA akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume. Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi;  kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa MUNGU tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.''
Kitendo cha kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi ni kuwa pia mnadhiri wa MUNGU kupitia tendo hilo, maana jina lako limeandikwa katika kitabu cha uzima .
Kama mnadhiri wa MUNGU inakupasa kuishi maisha aliyokuagiza MUNGU.
Kuyajua maisha hayo aliyokuagiza MUNGU ni rahisi sana, ni haya

1. MUNGU amekuagiza uishi maisha matakatifu.
1 Petrol 1:15-16 ''
bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. ''
 
2. MUNGU amekuagiza uenende kwa ROHO MTAKATIFU.
Wagalatia 5:16 ''
Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. ''
 
3. MUNGU amekuagiza umtumikie.
1 Kor 15:58 ''
mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana. ''
 
4. MUNGU amekuagiza umwabudu katika Roho na kweli.
Yohana 4:24 ''
Mungu ni ROHO, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. ''
 
5. MUNGU amekuagiza uache dhambi na mabaya yote, na sasa utende mema tu.
Zaburi 34:14 ''
Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. ''
 
Ndugu unahitaji kutimiza maagizo hayo ya MUNGU wewe kama mnadhiri wa MUNGU.

Inaweza Kabisa umezingatia maagizo ya MUNGU yote.
Lakini ni muhimu kutambua kwamba yuko shetani ambaye ni adui yako unayetakiwa kumshinda siku zote.
1 Petri 5:8-9 ''
Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.''
Kwa kulijua hilo sasa ni muhimu kujifunza mbinu za shetani ambazo zinaweza kumfanya mteule wa MUNGU akamatwe na shetani.
Mbinu hizo zinapatikana katika Waamuzi Sura ya 16

 
Ngoja nikufafanulie njia hizo 6 za shetani anazozitumia kumkamata Mtu wa MUNGU.


1. Anakulaza usingizi wa kiroho.

''..... Naye akamlaza usingizi .... ''- Waamuzi 16:19. 
Shetani anapokuwa amekulaza usingizi dalili hizi utaziona.
Unaacha ibada, unaacha maombi, unaacha kusoma Neno la MUNGU wala kulitafakari.
Ukiona uko katika hayo ujue shetani yuko katika kukulaza usingizi wa kiroho.
Delila ni mfano wa nguvu za Giza zilizomlaza Samsoni usingizi ili wamkamate.

  1 Thesalonike 5:6-8 ''Basi tusilale usingizi kama wengine, bali tukeshe, na kuwa na kiasi.  Maana walalao usingizi hulala usiku, pia na walewao hulewa usiku. Lakini sisi tulio wa mchana, tuwe na kiasi, hali tukijivika kifuani imani na upendo, na chapeo yetu iwe tumaini la wokovu.''


2. Anatafuta sababu ya nguvu zako.

Waamuzi 16:5 ''......  Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi ......'' 
Baada ya shetani kukulaza usingizi wa kiroho kinachofuata ni kutafuta asili ya nguvu zako.
Kila Mteule wa KRISTO amepewa nguvu na MUNGU katika utumishi ili nguvu hizo zimfanye kuwa karibu na MUNGU.
Kuna wenye nguvu za maombi.
Kuna wenye nguvu za kufunga.
Kuna wenye nguvu za utoaji.
Kuna wenye nguvu za uimbaji.
Kuna wenye nguvu za kuombea watu.
Kuna wenye nguvu za kusaidia yatima, wajane na wahitaji.
Ziko nguvu nyingi sana ambazo kwa hizo mtu anaweza kuzitumia nguvu hizo kumtumikia MUNGU.
Hata wewe kuna eneo la kiutumishi una nguvu sana maana kupitia utumishi huo utakuwa unazingatia mambo ya MUNGU.
Kuna wenye nguvu kufundisha.
Kuna wenye nguvu za kinywa.
Kuna wenye nguvu za ushawishi.
Shetani akijua asili ya nguvu zako, yaani akigundua unamtumikia sana MUNGU katika nini anafanya mbinu za kukukamata katika nguvu zako ili ubaki bila kumtumikia MUNGU.
Mfano nguvu zako ni katika uombaji, akikuzuia kuomba ujue utakwama sana.
Akikuzuia katika kumtumikia MUNGU ujue ni hatari sana kwako.
Biblia inatufundisha kwamba tusimpe shetani nafasi hata moja katika maisha yetu.
Waefeso 4:27 ''
wala msimpe Ibilisi nafasi. ''


3. Anakupofusha macho ya kiroho.

 Waamuzi 16:21'' ...  wakamng'oa macho ....'' 
Baada ya shetani kukulaza usingizi wa kiroho kisha kutafuta asili ya nguvu zako kinachofuata anakupofusha macho ya kiroho.
Hii ni hatua mbaya sana.
Ukiwa katika hatua hii utaanza kitenda dhambi na huoni kama ni dhambi.
Utaanza kumwogopa Mchungaji wako au viongozi wa Kanisa na sio MUNGU.
Utaacha huduma aliyokupa MUNGU na ukidhani sio makosa au utafanya huduma kwa mazoea tu huku ukichaganya mema na mabaya pamoja.
Hata ukionywa na watumishi utabaki kuwachukia tu wanaokuonya na utaendelea kujihesabia haki maana umepofushwa kipepo macho yako ya rohoni.

Bwana YESU katika  Yohana 12:40  Aanasema juu ya watu waliopofushwa macho ya kiroho na shetani kwamba ''Amewapofusha macho, Ameifanya mizito mioyo yao; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakafahamu kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.''
Kama uko katika hatua hii nakuomba geuka ndugu kwa toba.


4. Anakuhamisha sehemu yako yenye baraka na faida kwako zitokazo kwa MUNGU.

 Waamuzi 16:21 ''wakatelemka naye mpaka  ''
Baada ya shetani kukulaza usingizi, kutafuta asili ya nguvu zako, kukupofusha macho kinachofuata ni kukuhamisha kutoka kwenye eneo lako la baraka za MUNGU.
Samsoni baada ya kupofuliwa macho alipelekwa kwa wafilisti.
Kitendo cha mtu kupofuliwa kipepo macho ya rohoni kina maana ya kwamba mtu huyo anamilikiwa na shetani.
Shetani akikumiliki anakuondoa kanisani.
Anakuondoa kwa watu ambao wangekuonya au kukushauri.
Anakuondoa kwa watu ambao wangekuombea ili urejee katika utakatifu na maagizo ya MUNGU.
Hatua hiyo ndiyo ambayo Mara utasikia mtu ameacha kusali.
Mara amebadili dini kwa kumwacha YESU na kufuata wapingaKristo.
Hatua hii ndio ambayo utaona mtu husika anaenda kwa waganga wa kienyeji.
Mara utasikia mtu amekuwa mwimbaji wa nyimbo za kidunia.
Mara mtu amekuwa mlevi na mvuta bangi, Mara amekuwa kahaba na jambazi hatari.
Ni hatua mbaya sana sana.
MUNGU anasema juu ya waliotekwa na shetani  katika Isaya 42:22  kwamba ''
Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha. ''


5. Kufungwa vifungo vya kipepo.

Wamuzi 16:21 ''wakamfunga kwa vifungo vya shaba ''
Baada ya shetani kukulaza usingizi, kukuzuia kumtumikia MUNGU kukupofusha macho kiroho kisha anakuteka, kinachofuata ni vifungo vya kipepo.
Ni rahisi tu kwamba baada ya shetani kumkamata mtu na kumteka kinachofuata ni kumfunga mtu huyo vifungo vya kipepo ili asifanikiwe kurudi kwa YESU KRISTO hata apate uzima wa milele.
Kuna vifungo vingi sana mtu anaweza akafungwa kipepo baada ya mtu huyo kuwa Mali ya shetani.
Baadhi ya vifungo hivyo ni roho ya uzinzi, kiburi, matusi, wizi, uongo, uchawi, tamaa, fitina n.k
1 Kor 6:9-10 ''
Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. ''
Hatua hiyo ni mbaya Sana Sana


6. Shetani kukupa kazi ili umletee faida.

Waamuzi 16:21 ''naye alikuwa akisaga ngano katika gereza. ''
Hatua ya mwisho ya shetani akimkamata mtu wa MUNGU ni kumpa kazi mtu huyo ili amletee faida shetani.
Vifungo ambavyo mtu anavipata kwa shetani hivyo ni vitendea kazi tu vya shetani ili kumzalia matunda.
Vifungo hivyo vitakufanya utimize matakwa ya shetani.
Ukiwa na kifungo cha uzinzi au wizi kuua kwa kutoa mimba haitakuwa tatizo kwako au kuua watu katika wizi haitakuwa tatizo kwako.
Ukiwa na kifungo cha tamaa mbaya ujue kujeruhi watu kwa kuwaibia haitakuwa tatizo kwako.
Unapofanya uharibifu ujue umempatia faida shetani.
Samsoni alipewa na wafilisti kazi ya kusaga ngano kipindi akiwa gerezani(Kifungonj)
Wako watu makanisani wameshafikia hatua hii ya kutafutia shetani faida kupitia dhambi zao.
Wako watu wameshageuka mawakala wa shetani Kabisa katika kanisa ili kuwafanya Kanisa wasitimize kusudi la MUNGU Bali watimize kusudi la shetani.
Ndugu, hii ni hatua mbaya sana sana.
Wagalatia 2:4-5 ''
Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika KRISTO YESU, ili watutie utumwani;  ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi. ''
Naamini umenifuatilia tangu mwanzo na kuna kitu umejifunza.
Ndugu kama umefikia hatua yeyote katika hizo sita nakuomba tubu na acha dhambi.
Anza sasa kumtii MUNGU na acha mazoelea katika kazi ya MUNGU.
 Neema bado ipo hivyo unahitaji kutubu ndugu ili kazi yako isiwe bure.
Biblia inasema na roho yako ikisema '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa.  Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA.-Isaya 55:6-8'
Kama wewe kweli ni mtu wa ibada lakini uko katika makundi haya, ndugu Biblia inasema ''Na hii ndiyo habari tuliyoisikia kwake, na kuihubiri kwenu, ya kwamba MUNGU ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye(MUNGU) ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu. -1 Yohana 1:5-10 '

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments