MTEULE ALIYE NURU YA ULIMWENGU NA CHUMVI YA DUNIA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Wewe uliyeokolewa na Bwana YESU ni Nuru ya ulimwengu na tena ni chumvi ya dunia.
Wewe Mteule uliye Nuru ya ulimwengu inakupasa uonekana, maana nuru ni mwanga, na mwanga huonekana. Usijionyeshe bali onekana kutokana na KRISTO kuwa ndani yako na Onekana kwa kuishi maisha matakatifu ayaagizayo MUNGU Baba.
Mathayo 5:14-16 '' Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima. Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.'

Wewe Mteule uliye chumvi ya dunia inakupasa utoe radha takatifu inayotokana na kubadilishwa kwako na Neno la injili ulilohubiriwa.
Wewe Mteule uliye Nuru ya ulimwengu inakupasa ung'ae/Uonekane kwa matendo mema yanayowapasa wamwaminio Bwana YESU.
Mathayo 5:13-14" Ninyi ni chumvi ya dunia; lakini chumvi ikiwa imeharibika itatiwa nini hata ikolee? Haifai tena kabisa, ila kutupwa nje na kukanyagwa na watu. Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima."

Kuna wakristo ni chumvi ya ulimwengu na ni Nuru ya ulimwengu maana wanaishi maisha matakatifu ayatakayo MUNGU Baba.
Lakini kuna wakristo pia sio Nuru ya ulimwengu na wala sio chumvi kwa sababu hawana tofauti na watu wa dunia na hutenda dhambi kama watu wa dunia, wana tabia ambazo ni sawa tu na watu wa dunia.

Ndugu, hakikisha imani yako  inathibitishwa na matendo yako.
Yakobo 2:17-20 '' Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake. Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami nitakuonyesha imani yangu kwa njia ya matendo yangu.
 Wewe waamini ya kuwa MUNGU ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. Lakini wataka kujua, wewe mwanadamu usiye kitu, kwamba imani pasipo matendo haizai?''
Wapo Wakristo wanahudhuria kanisani lakini hawajawahi kuliruhusu Neno la KRISTO liwabadilishe na kwa kulitii wawe Nuru njema ya ulimwengu na wawe chumvi njema ya ulimwengu.
Ndugu Mimi sijui kama wewe ni Nuru na chumvi ya ulimwengu au wewe sio Nuru wala chumvi ya dunia.
Kumbuka Neno la MUNGU ndiye kiwanda cha kutengeneza nuru kwa mteule.
Ndugu ni heri ukakubali kubadilishwa na Neno la MUNGU.

 Kumbuka kwamba Mtu aliyeokolewa na Bwana YESU huyo ni kiongozi, na kwa sababu ni kiongozi basi inampasa kuwa shujaa.
Katika uaminifu ni shujaa, katika kuisema kweli ya MUNGU inampasa kuwa shujaa.
Katika kazi ya MUNGU Fanya kwa juhudi na kwa ushujaa.
Kiongozi mzuri wa kiroho lazima aambatane na ushujaa ndani yake katika kuitimiza kazi ya MUNGU.

Fanya connection na MUNGU huku ukifuta connection na shetani.
Kuna watu wana connection na madhabahu za Giza.
Kuna watu wana connection na mapepo.
Kuna watu wana connection na sanamu.
Kuna watu wana connection na mizimu.
Kuna watu wana connection na majini mahaba.
Kuna watu wana connection na kuzimu.
Kuna watu wana connection na mauti ya kipepo.
Kuna watu wana connection na hawara.
Kuna watu wana connection na waganga wa kienyeji.
Kuna watu wanateswa na magonjwa kila Mara kwa sababu tu wana connection na magonjwa yaliyotumwa kichawi.
Kwa jina la YESU KRISTO ndugu hakikisha unafuta connection za kishetani na sasa weka connection na MUNGU Baba katika YESU KRISTO.
Kuweka connection na MUNGU ni kumpokea YESU KRISTO, kutubu na kisha kujazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU kisha unakuwa mtu wa maombi na kuishi maisha matakatifu safi ya wokovu wa Bwana YESU.

1 Petro 1:14-16 ''Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye(MUNGU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. ''
Weka connection na MUNGU aliye hai.
Ukijiunganisha na MUNGU utakuwa rafiki wa MUNGU.
Hakikisha kwa maombi yako unafuta connection zote za kishetani ulizoungwa nazo.
Futa connection za mgonjwa.
Futa connection za ajali.
Weka connection na Bwana YESU mwenye uzima wako wa milele.

Mteule aliye nuru ya ulimwengu na ni chumvi ya dunia hujua kanuni za MUNGU za kumfanya awe mshindi duniani.
Kanuni hizo ni pamoja na kuishi maisha matakatifu, kuishi maisha ya maombi, kuenenda katika ROHO MTAKATIFU pamoja na kuwa mtoaji mzuri wa zaka na sadaka. Sadaka njema uitoayo inaweza kusababisha jambo kubwa sana kwako katika ulimwengu wa roho.
Ibrahimu hakuizuilia sauti yake ya kipekee Isaka.
Mwanzo 22:15-18 '' Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.   ''

  Wewe kama mteule uliye nuru na chumvi inakupasa pia ujitambue katika mambo mengi sana, mojawapo ni hili; ni kosa kubwa sana kufikilia kuwa uwepo wa MUNGU katika ibada unaletwa na mtu mmoja tu yaani mchungaji, Mhubiri au kiongozi yeyote, bali kila mtu anachangia kuleta uwepo wa MUNGU, na kama umetenda dhambi ujue kuwa unaleta uwepo wa dhambi yako.

 Mteule aliye nuru humtumikia Bwana YESU.
 Ikiwepo Huduma basi tuwemo katika Huduma.
Hakikisha wakati au muda wa Huduma uliyopewa na MUNGU unakuwa katika Huduma hiyo.
Wakati wa Huduma uliyopewa na MUNGU hakikisha unauzingatia muda huo na timiza Huduma yako.
Muda wako wa kuwa kwenye uimbaji hakikisha unakuwepo.
Muda wako wa kuhubiri hakikisha unakuwepo.
Muda wako wa kushuhudia mitaani hakikisha unakuwepo.
Muda wako wa kumtolea MUNGU hakikisha unakuwepo.
Muda wako wa kufanya kazi ya MUNGU ya aina yeyote hakikisha unakuwepo.

Wakolosai  4:5-6 '' Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.  Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu. ''
Mteule uliye nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia hakikisha unang'aa kwenye ulimwengu wa roho ili ujue uonekane kwenye ulimwengu wa mwili, nuru huonekana kwa kung'aa kwake.
Kutoka 34:29-30 ''
Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling'aa kwa sababu amesema naye. Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake iling'aa; nao wakaogopa kumkaribia.'

MUNGU alipokuwa katika uwepo wa MUNGU kwa muda mrefu aling'aa sana, hata wewe inakupasa ung'ae  na ndio maana Biblia inasema '' Nuru ya mwenye haki yang'aa sana; Bali taa ya mtu mbaya itazimika.   -Mithali 13:9''
 
Usipong'aa kwenye ulimwengu wa roho maana yake hutaonekana kwenye ulimwengu wa mwili.
MUNGU anataka ung'ae ili yeye atukuzwe.
Yakobo aling'aa katika nyumba ya Labani(Mwanzo 30-26-45)
Yusufu aling'aa kwa Potifa na kwa taifa zima la Misri,

Mwanzo 39:2-3 ''BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri.  Bwana  wake(Mmisri) akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake(Yusufu). ''
 
Ndugu mteule inakupasa uonekane.
Inuka uangaze yaani uonekane maana YESU KRISTO ndio nuru yako.

Isaya 60:1 ''Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa BWANA umekuzukia.'' 
Hata katika mahitaji yako unahitaji kung'aa ili MUNGU atukuzwe.
Haiwezekani mteule uingie katika uchaguzi na mtu anayetumia uchawi akushinde kwa sababu hujaonekana.
Haiwezekani wanaotumia mkorogo ndio wampate mchumba wako huku wewe huonekani kwa mchumba huyo.

Ndugu hakikisha unang'aa kwenye ulimwengu wa roho ili uonekane kwenye ulimwengu wa mwili.
Jinsi ya mteule kung'aa katika ulimwengu wa roho.
 
1. Kuishi maisha matakatifu.

1 Petro 1:15 ''bali kama yeye(MUNGU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''
 
2. Maombi katika ROHO MTAKATIFU.
Yuda 1:20-21 '' Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU, jilindeni katika upendo wa MUNGU, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu YESU KRISTO, hata mpate uzima wa milele.''
 
3. Kutii Neno la MUNGU na maagizo ya MUNGU.
Kumb 28:1 '' Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; ''
 
4. Kujua wakati wa MUNGU wa ushindi kwako.
Mhubiri 3:1 ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. '' 

Katika kung'aa tambua kwamba;
1. Usipong'aa katika ulimwengu wa roho hutaonekana katika ulimwengu wa mwili.

2. Using'aa utafunikwa na wanaotumika kipepo.
3. Usipong'aa utashindwa katika mambo mengi sana.
Hakikisha unang'aa ndugu.

 Mwanzo 29:16-17 '' Labani alikuwa na binti wawili, jina la mkubwa ni Lea, na jina la mdogo ni Raheli. Naye Lea macho yake yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso.''
Raheli aling'aa kwa Yakobo kuliko Leo, hata wewe ng'aa mbele za watu wasio na Muda na YESU Mwokozi, Ng'aa katika kazi yako, biashara yako, masomo yako na katika huduma ya Kazi ya MUNGU.


Katika maisha yako zingatia sana haya.
1. Vunja mipango ya wanadamu na weka mipango ya MUNGU juu ya maisha yako.
2. Usiishi kwa sababu tu unaishi Bali ishi kwa sababu YESU KRISTO anaishi ndani yako.
3. Enenda kwa ROHO MTAKATIFU siku zote na mtii yeye daima.
4. Ishi maisha ya maombi siku zote.
5. Mpende JEHOVAH MUNGU wako kuliko vyote upendavyo.
6. Kataa dhambi, ipinge dhambi, ikimbie dhambi, iondoe dhambi na usitende dhambi tena.
7. Wekeza kwa YESU KRISTO.
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments