PIGANA VITA KIROHO NA SIO KIMWILI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Naamini wewe ni muombaji unayeishi maisha matakatifu katika KRISTO. Kama ni ndio nisikilize na leo nina ujumbe kwa ajili yako.
Ewe mtu wa MUNGU nakuomba usikubali kufanya vita kimwili.
Ukifanya vita ya kimwili hutashinda lakini ukifanya vita ya kiroho utashinda kirahisi Kabisa haijalishi maadui ni wengi kiasi gani.
Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

Vita yetu ni kwa njia ya maombi na sio fimbo, visu au jiwe.
Kuna madhara kama mtu wa MUNGU utaamua kupigana kimwili vita ya kiroho.


1 Yohana 5:5 ''Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba YESU ni Mwana wa MUNGU? ''
Kumwamini YESU inahusisha vitu viwili.
1. Kumkubali YESU kama Mwokozi wako.
2. Kumpokea kama Mwokozi wako.
Sasa Biblia inasema ya kwamba mtu mwenye kuushinda ulimwengu ni yule tu anayemwamini YESU KRISTO.
Kama unamwamini YESU hakika utaomba katika yeye na kushinda.
Ni kweli wakati mwingine unaweza ukapitia vita kubwa sana lakini nakuomba ndugu kwamba ili ushinde vita inakupasa kupigana kiroho ndipo utashinda.
Kupigana kiroho ili ushinde inakupasa kuwa muombaji na mtoaji wa sadaka yenye kusudi, ndipo utakuwa mshindi kila leo.
Vita yako ipigane kwa maombi na kutoa sadaka yenye kusudi. 
Kumbuka MUNGU anaweza akakumbuka sadaka zako na kukujaalia kwa kadri ya haja(Mahitaji) yako.
Zaburi 20:3-4 '' Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote.''  
Maadui zako wanaweza wakafanya vita na wewe kwa kupeleka sadaka(kafara) kwa waganga. Wewe toa sadaka kwa MUNGU aliye hai huku ukiomba.
 Fanya vita kiroho na sio kimwili.
Kitu kilicho katika ulimwengu wa roho, kukipata ni lazima uwe rohoni na sio mwilini.
Hiyo ni kanuni ya kiroho ambayo unatakiwa kuifuata.
Ukiufuata ufalme wa MUNGU inakupasa kuenenda kama ufalme huo uendavyo.

Mathayo 6:33  '' Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.''
Huhitaji kwenda kimwili bali enenda kiroho huku ukimsikiliza ROHO MTAKATIFU ambaye yuko rohoni siku zote. 
 
Madhara ya kufanya vita kimwili:

1. MUNGU hatakuwa upande wako katika hiyo vita.

 Yohana 18:10-11 ''Basi Simoni Petro alikuwa na upanga, akaufuta, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio la kuume. Na yule mtumwa jina lake ni Malko. Basi YESU akamwambia Petro, Rudisha upanga alani mwake; ....''
-Petro alitaka kwenda kinyume na kanuni ya ufalme wa MUNGU kwa kutaka kupigana vita kimwili lakini Bwana YESU akamkataza, hata leo Bwana YESU anakukataza wewe mtumishi wake kupigana vita kimwili.
  Unaweza kuishia tu wewe mwenyewe kujeruhiwa kimwili na kudhurika.
 Utashindwa vibaya sana.


2. Utatenda dhambi.
 Zaburi 34:13-15 '' Uuzuie ulimi wako na mabaya, Na midomo yako na kusema hila. Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. ''



3. Utakuwa umeenda kinyume na sheria ya ufalme wa MUNGU na silaha za MUNGU hazitafanya kazi na wewe.

2 Wakorinto 10: 3-4 ''Maana ingawa tunaenenda kaitka mwili hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili  (maana silaha za vita vyetu si za mwili,bali zina uwezo katika MUNGU hata kuangusha ngome)''
  Silaha za MUNGU za vita hazitakuwa upande wako.
 Utadhalilisha Kanisa na Wokovu kwa ujumla.
 Kumbuka adui wa kipepo hupigana kiroho na kimwili. 
Ukipigana kimwili ujue adui yako atakuja kimwili na kiroho hivyo utashindwa.
Ndugu unahitaji sana kupigana kiroho na sio kimwili.
Ukipigana kiroho ujue Malaika wa MUNGU watakuwa pamoja na wewe ili kuwaharibu maadui zako wa kishetani.
Zaburi 34:7" Malaika wa BWANA hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa."

Ukipigana kiroho utaweza kuwapiga maadui zaidi ya 1000 kwa muda mfupi sana.
Yoshua 23:10" Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana BWANA, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia."

Hebu jiulize kama una maadui 1000 na unauwezo wa kuwapiga kiroho kwa saa moja wote na wakakimbia, je kuna haja gani ya kutaka kupigana nao kimwili?
Kwanza adui 1000 unaweza kupigana nao kimwili mwaka mzima na hujawamaliza na watakuumiza.

Kwanini basi maombi ni muhimu sana katika maisha yote ya mteule wa KRISTO.
Ni kwa sababu kupitia maombi utamruhusu MUNGU kukushindia kila vita inayoletwa kwako na wakuu wa Giza, wachawi, majini, waganga na washirikina wote na kila mwanadamu anayetumika kipepo dhidi yako.
Silaha za MUNGU kwenye ulimwengu wa roho ni Kali kuliko shetani na wapambe wake wote.
Ukiamua kupigana kiroho ujue utakuwa na jina la YESU KRISTO na mamlaka yake haijawahi kushindwa.

Ukipigana kiroho ujue damu ya YESU KRISTO itakuwa upande wako, na damu hiyo haijawahi kushindwa kukifuta chochote cha kishetani.
Ukipigana vita ya kiroho ujue nguvu za ROHO MTAKATIFU zitakuwa na wewe tena zitakuwa upande wako, nguvu za ROHO MTAKATIFU hazijawahi kushindwa na chochote cha kishetani.
Ukipigana vita ya kiroho utaomba katika Neno la MUNGU au kwa Neno la MUNGU. Na Neno la MUNGU ni silaha ambayo haijawahi kushindwa na shetani au mawakala wa shetani.


Kwa kukusaidia tu ni kwamba Neno la MUNGU ni silaha Kali mno;

1. Neno la MUNGU ni zaidi ya upanga mkali wenye makali kuwili.
"Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.-
Waebrania 4:12.

2. Ni kama Moto mkali na ni kama nyundo kubwa yenye uwezo wa kupasua mawe makubwa.
Yeremia 23:29Je! Neno langu si kama moto? Asema BWANA; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?"

Ndugu hakikisha unapigana vita ya kiroho.
Ondoa chuki ndani yako ndipo utamruhusu MUNGU kukushindia, usichukie watu Bali chukia mashetani yao na uchawi wao ndipo utawashinda.
Omba hata maombi ya kufunga na Kirahisi Kabisa utashinda.
Hakikisha tu unaishi maisha matakatifu katika Wokovu wa Bwana YESU.
Utashinda hakika.
"Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi. -Zaburi 2:9


Hakikisha kwa maombi yako roho ya uchawi ndani ya ndugu yako inamwacha ndipo atakuwa mtu mzuri, hiyo ni tanzi mbaya kama isipothibitiwa, ni mwiba ambao inapaswa udhibitiwe.
kuna uchawi wa aina mbili.
1. Kuna watu ni wachawi na wanajitambua kwamba ni wachawi.
2. Kundi la pili kuna wenye roho ya uchawi ila wao hawajijui kama ni wachawi, hawa hutimiza kusudi la shetani kichawi bila wao kujijua. Mtu wa jinsi hii ndoto zake nyingi anaweza kuwa anaota. Mara yeye mwenyewe anageuka na kuwa mdudu Fulani au mnyama, Mara aote ana mapembe, Mara aote anabadilika na kuwa ndege na kupaa, Mara maadui zake waje kisha wasimuone kwa sababu amebadilika na kuwa kiumbe kingine.
Ndoto inaweza ikajulisha mtu alivyo.
Kuna watu wamepandikiziwa roho za uchawi ndio maana wao kuua kwa kutumia nguvu za Giza sio jambo gumu kwamba.
Ndugu hakikisha unaharibu roho za uchawi kwa wote wanaokuhusu na unaoshirikiana nao.

Yeremia 1;19 '' Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema BWANA, ili nikuokoe. ''

MUNGU ni MUNGU wa karibu sana, endelea na maombi na utakatifu na iko siku waliokucheka watajicheka wao kwanini walikucheka.
Yeremia 23:23 " Mimi ni MUNGU aliye karibu, asema BWANA, mimi si MUNGU aliye mbali."


Mawakala wa shetani ndio huwa wasimamizi wa matatizo yako.
Ukitaka kuyashinda matatizo yako usipambane tu na matatizo Bali haribu kwa jina la YESU KRISTO
1. Mleta tatizo wa kipepo.

2. Msimamizi wa tatizo.
3. Tatizo lenyewe.
Wengi sana hupambana na tatizo tu ndio maana tatizo huisha kwa muda kisha linarudi maana mleta tatizo na msimamizi wa tatizo hujamgusa.
Ngoja nikupe mfano ili unielewe vyema.
Mfanya kazi mwenzako anaweza akakuendea kwa mganga wa kienyeji ili tu ufukuzwe kazi.
Maadui zako hapo ni;
1. Tatizo lenyewe.
2. Mleta tatizo ni yule aliyekupekeka kwa mganga.
3. Msimamizi wa tatizo lako ni mganga wa kienyeji.

Ndugu mteule wa KRISTO hakikisha unapambana kimaombi na wote watatu ndipo watapondwa na kujua kwamba wewe una BABA yako mbinguni aliye mtetezi wako wa milele.
Unataka kujua zaidi wewe muombaji?
Biblia inasema Zaburi 40:14 " Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu."


Hakikisha kwa maombi yako wanafedheheshwa na kuabishwa wao.
Na ndio maana nakuambia kwamba " MUNGU kwetu sisi ni MUNGU wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.-Zaburi 68:20"


 Kumbuka pia kwamba taarifa za madaktari sio taarifa za MUNGU.
Taarifa ya madaktari inaweza ikaonyesha kwamba hutapona lakini ukipata taarifa ya MUNGU iliyo na YESU KRISTO utapona na kusonga mbele.
Kama kweli Umeokolewa na Bwana YESU basi usimfanye Mwanadamu kuwa ndio msemaji wa mwisho wa maisha yako.
Msemaji wa mwisho wa maisha yako anatakiwa awe ni JEHOVAH MUNGU aliye hai.
Endelea na maombi katika ROHO MTAKATIFU na MUNGU akubariki sana

Kumbuka pia kwamba inakupasa Mteule wa KRISTO  utembee katika hali ya kujilinda.
Yakobo 4:7-8 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.''
 
Jilinde kwa kukaa mbali na shetani.
Jilinde kwa kukaa mbali na anasa za dunia.
Jilinde kwa kukaa mbali na kila kitu kinachoweza kukuondoa katika kumpendeza MUNGU.

Jilinde katika usemi.
Jilinde katika matendo.
Jilinde kwa kukaa mbali na kila unajisi
Jilinde kwa kukaa mbali na watu wabaya wanaokuzunguka.


Njia za mteule wa MUNGU kujilinda na machukizo.

1. Kujilinda kwa kulitii Neno la MUNGU.
 Zaburi 119:11 '' Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.''

2. Kujilinda kwa kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.
 Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''

3. Kujilinda kwa kuwa mtu wa maombi kila siku.
 Mathayo 7:7 '' Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; ''

4. Kujilinda kwa kuweka tumaini kwa MUNGU tu.
 Yeremia. 17:7 “Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana ambaye Bwana na tumaini lake”
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments