UKIOKOKA FANYA MATENDO YANAYOKUTHIBITISHWA KWAMBA KWELI UMEOKOKA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuokoka ni nini?
Kuokoka ni kumwamini Bwana YESU kama Mwokozi wako kisha unampokea kwa imani moyoni mwako kama Mwokozi wako kisha unaanza kuishi sawa sawa na Neno lake.
Hayo matatu yaani Kumwamini, kumpokea na kuanza kuliishi Neno la MUNGU ndio humkamilisha mtu kwamba anamwamini YESU.
Na huko ndiko kuokoka.

Yohana 3:18 " Amwaminiye yeye(YESU) hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."
Kwanini aliyemwamini yesu yaani aliyempokea hahukumiwi?
Ni kwa sababu ameshaokoka tayari hivyo hawezi kuhukumiwa.
Neno lenyewe "Aaminiye" maana yake ni "Anamkubali YESU kama Mwokozi na kisha kumfuata ili amwokoe na kuliishi Neno la MUNGU"

Mtu unakuwa ameokoka baada ya kufanyaje?
Mtu anakuwa ameokoka baada ya kumwamini YESU kama Mwokozi na kisha kumpokea, tukio hilo tu humfanya mtu kuwa ameokoka.
Yohana 1:12-13 "Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."


Baada ya kumpokea YESU kama Mwokozi kinachofuata ni kuishi maisha matakatifu katika yeye ili kuuthibitisha Wokovu wako uliyeokolewa kwa neema ya MUNGU.
1 Petro 1:15 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"

 
Ukimpokea YESU na kuishi maisha matakatifu yanayoagizwa na Biblia hakika umeokoka.

ROHO MTAKATIFU hufanya kazi ya kumsaidia mteule kutunza Wokovu wake, kwa kumfundisha, kumkumbusha na kumjulishi ni nini MUNGU anataka kwa wateule wake.
Kuokoka ni kitu cha muda mfupi kabisa lakini kulifuata Neno la MUNGU huku ukiongozwa na ROHO MTAKATIFU hukufanya uokoke kila Leo maana MUNGU hulituma Neno ili kukufanya uokoke zaidi na ili usinaswe na kamba za shetani na mambo ya kwanza maovu uliyoyaacha.
Zaburi 107:20-21 " Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. Na wamshukuru BWANA kwa fadhili zake, Na maajabu yake kwa wanadamu."

Je tunaweza tukasimama hadharani na kusema TUMEOKOKA?
Ni kweli hakika tunaweza tukasimama hadharani na kusema tumeokolewa na Bwana YESU yaani tumeokoka.
Ona maandiko haya

Waefeso 2:8-10 " Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika KRISTO YESU, tutende matendo mema, ambayo tokea awali MUNGU aliyatengeneza ili tuenende nayo."

Biblia inasema tumeokolewa maana yake kuna aliyetuokoa ambaye ni Bwana YESU baada ya sisi kumkubali na kumpokea kama Mwokozi hivyo ni hakika tumeokoka.
Na yeye YESU alisema " Wala Yeyote Ajaye Kwangu Sitamtupa Nje Kamwe- Yohana 6:37."

Ajaye kwa YESU ni yule aliyemkubali YESU kisha akampokea na kuanza kuliishi Neno la MUNGU.
Kumbukapia hili ambalo Bwana YESU alisema
Luka 6:47 "Kila mtu ajaye kwangu, na kuyasikia maneno yangu na kuyatenda, nitawaonyesha mfano wake."

Ndugu umeokoka?
Mtu akiokoka inatakiwa afuate yafuatayo ndipo yatamthibitisha kwamba ni Mkristo Kamili.
1. Kuishi maisha matakatifu yanayoagizwa na Neno la MUNGU.

Wakolosai 1:21-22 '' Na ninyi, mliokuwa hapo kwanza mmefarikishwa, tena adui katika nia zenu, kwa matendo yenu mabaya, amewapatanisha sasa(YESU);katika mwili wa nyama yake, kwa kufa kwake, ili awalete ninyi mbele zake, WATAKATIFU, wasio na mawaa wala lawama; ''

  2. Kuacha dhambi na kuacha kila kilicho cha shetani ndani yake.
 
Mfano, kutambika,ibada za wafu na kutoa sadaka kwa mizimu, kwenda kwa waganga wa kienyeji, kujihusisha na mizimu N.k

 Zaburi 34:14 ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. ''
 
3. Kumtegemea MUNGU kwa maombi.

  Thesalonike 5:17-18. ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya MUNGU kwenu katika KRISTO YESU. 

4. Kuwa na maisha ya ushuhuda mzuri kwa watu wote.

 1 Petro 2:11-12 ''Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho. Mwe na mwenendo  mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze MUNGU siku ya kujiliwa. ''

5. Kumtumikia Bwana YESU KRISTO.

1 Kor  15:58 '' Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.'' 

6.  Kumkiri mbele za watu wote kwa ujasiri.

 Mathayo 10:32-33 '' Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za BABA yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za BABA yangu aliye mbinguni.''

7. Kuwa na umoja kama Kanisa  la MUNGU na Kushirikiana katika yaliyo ya MUNGU.

 Waefeso 4:1-3 ''Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika BWANA, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa;  kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo;  na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa ROHO katika kifungo cha amani. ''
 
8. Kuwa na ushirika na ROHO MTAKATIFU.

2 Kor 13:14 '' Neema ya Bwana YESU KRISTO , na pendo la MUNGU, na ushirika wa ROHO MTAKATIFU  ukae nanyi nyote.''

Hayo mambo manane ni muhimu sana katika kukuthibitisha mteule kwamba kweli umeokoka.
Kuokoka ni jambo la muhimu sana na la laxima kwa mtu anayetaka kwenda mbinguni.
Wote waliokufa katika Wokovu wa Bwana YESU tukifika mbinguni tutawaona. Najua tukifika tutatamani kwanza kumwona Mwokozi YESU.
Ndugu Yangu unayesoma Ujumbe huu jitahidi ufike mbinguni kwa MUNGU muumbaji wetu.
Dhambi isikukwamishe. Uzinzi na uasherati usikukwamishe.
Dini isikukwamishe. Unamhitaji YESU KRISTO na Wokovu wake tu. Kutokusamehe kusikukwamishe.
Kuabudu sanamu kusikukwamishe. Mazoelea mabaya yasikukwamishe. Tamaa za Mali zisikukwamishe.
Wizi na uongo usikukwamishe. Unamwitaji YESU KRISTO ili upone. Kwenda kwa waganga kusikukwamishe.
Kushirikiana na mizimu kusikukwamishe. MUNGU Baba atupe kufika uzima wake wa milele.

 Bwana YESU atupe kufika uzima wa milele.
ROHO MTAKATIFU atuongoze kufika uzima wa milele.

Wakolosai 2:6-10 '' Basi kama mlivyompokea KRISTO YESU, BWANA, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya KRISTO. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa MUNGU, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka. ''.

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments