UKIOKOKA MHITAJI SANA ROHO MTAKATIFU

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU asifiwe wateule wa MUNGU.
Tunalo jambo la kumshukuru MUNGU kwa Uzima aliotupa katika siku mpya aliyotupa.
Nakutakia siku njema na MUNGU aliyekulinda Jana akulinde na Leo na kesho.

Nimewahi kuzungumzia sana kuhusu ROHO MTAKATIFU lakini hata leo nataka kugusia mambo kadhaa kuhusu ROHO MTAKATIFU maana Bibla ROHO MTAKATIFU Kanisa linakuwa sio kanisa la MUNGU tena.
Kama Kuna mafundisho ya muhimu sana katika kanisa na yanayotakiwa kusisitizwa sana na watumishi wa KRISTO ni mafundisho kuhusu utakatifu, maombi na kuhusu ROHO MTAKATIFU.
ROHO MTAKATIFU ndiye msimamizi wa Kanisa la KRISTO duniani.
Yohana 14:26 ''Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye BABA atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.''

 YESU alipoondoka alimkabidhi kanisa ROHO MTAKATIFU ili alisimamie.
Katika andiko hapo juu ni Bwana YESU anamzungumzia ROHO MTAKATIFU kwamba huyo akija ndiye atakuwa mwalimu wetu mkuu maana ndiye aliyeiandika pia Biblia, hivyo hakuna anayeijua Biblia kuliko ROHO MTAKATIFU.
ROHO MTAKATIFU ndiye hutukumbusha na kutujulisha yote sisi kama wateule wa KRISTO tunaongoja uzima wa milele.

ROHO MTAKATIFU huleta umoja kati ya waamini na MUNGU wao.
ROHO MTAKATIFU hutufanya tuwe na ushirika na MUNGU Muumba wetu.
Wateule wa KRISTO ni watu wa rohoni kwa sababu wanaye ROHO MTAKATIFU.
Kama huna ROHO MTAKATIFU hakika roho feki zitaendelea kukudanganya.
Kama unataka kumjua MUNGU aliye hai basi husika na ROHO MTAKATIFU atakusaidia ili ujue.
ROHO MTAKATIFU hutufundisha jinsi ambavyo MUNGU anataka.
ROHO MTAKATIFU hutupa nia ya KRISTO ndani yetu.

Bwana YESU alisema hivi ''Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa BABA, huyo ROHO wa kweli atokaye kwa BABA, yeye atanishuhudia.-Yohana 15:26''

Watu wengi sana hawamjua Bwana YESU vyema kwa sababu tu hawana ROHO MTAKATIFU, Biblia inasema kwamba ROHO MTAKATIFU ndiye anayemshuhudia YESU KRISTO ndani yetu.
Mkristo ambaye hana ROHO MTAKATIFU ni mwoga.
Mkristo ambaye hana ROHO MTAKATIFU kutekwa na dunia ni haraka sana.
Mkristo ambaye hana ROHO MTAKATIFU kutenda dhambi ni rahisi.

Ndugu yangu, kitu muhimu unachohitaji katika maisha yako ya kiroho ni kuwa na ROHO wa MUNGU ndani yako.
Aliye na ROHO MTAKATIFU huisikia sauti ya MUNGU.
Aliye na ROHO MTAKATIFU huishi maisha matakatifu.
ROHO MTAKATIFU ndiye hutupatia ujasiri wa kusonga mbele kwa ushindi na hutuombea kwa MUNGU.

Warumi 8:26-27 ''Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.  Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya ROHO ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo MUNGU.''


ROHO MTAKATIFU hutupa matunda tisa ndani yetu.
Matunda tisa ya ROHO MTAKATIFU yakikaa ndani ya mtu, mtu huyo utu wake wa ndani umekamilika.
Wagalatia 5:22-23 " Lakini tunda la ROHO ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.''
Hayo ndio matunda Tisa ya ROHO MTAKATIFU ambayo mteule akiwa nayo hakika mteule huyo utu wake wa ndani umekamilika.
Ndugu hakikisha utu wako wa ndani unakamilika kwa wewe kuwa na matunda 9 ya ROHO MTAKATIFU na kuyaishi.
Ukimuona mteule hana upendo, huyo utu wake wa ndani haujakamilika.
Ukiona mtu hana furaha, amani au uvumilivu ujue Kabisa utu wake wa ndani huyo ndugu una tatizo.
Ukimuona si Mtu mwema na wala hawezi kuwafadhili wengine na tena sio mwaminifu kwa MUNGU na kwa Kanisa, huyo ndugu hana tunda la ROHO MTAKATIFU na utu wake wa ndani haujakamilika.
Ukimuona mtu hana upole na kiasi katika maisha yake ya Wokovu huyo utu wake wa ndani haujakamilika.

Matunda 9 ya ROHO MTAKATIFU ni lazima yawe sehemu ya maisha yetu kama wateule wa MUNGU tuliozaliwa Mara ya pili.
Ukiwa huna ROHO MTAKATIFU tambua pia kwamba huwezi kuwa na karama za ROHO MTAKATIFU zikifanya kazi na huwezi kuwa na matunda Tisa ya ROHO MTAKATIFU ndani yako.
Kama kuna kitu muhimu sana kwa mwenda mbinguni basi ni kuongozwa na kuenenda katika ROHO MTAKATIFU.

Ukifanya kinyume na matunda 9 ya ROHO MTAKATIFU utu wako wa ndani utakuwa na matatizo makubwa sana.
Hakikisha unalinda utu wako wa ndani.
Ulinde utu wako wa ndani kwa kuyaishi matunda Tisa ya ROHO MTAKATIFU.

Wagalatia 5:25 ''Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.''
 
Tunza sana matunda Tisa ya ROHO MTAKATIFU

 Kaa Na ROHO MTAKATIFU Siku Zote Za Maisha Yako Maana Yeye Ana Kazi Kubwa Kwako.
Thamani Ya Kuokolewa Kwako Na Bwana YESU Anaijua ROHO MTAKATIFU Hivyo Usimwache Hata Siku Moja.

ROHO MTAKATIFU hutoa pia karama kwa Kanisa la MUNGU.
 Karama za ROHO MTAKATIFU tunapewa na MUNGU kama zawadi ili kumtumikia Mwokozi wetu YESU KRISTO kwa usahihi.
1 Kor 12:4-11 '' Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule.  Tena pana tofauti za huduma, na Bwana(YESU) ni yeye yule.  Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.  Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana.  Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. ''

Kuna baadhi ya watu wa MUNGU au watumishi hukosea kutimiza wajibu wao, kwa sababu hawamtii ROHO MTAKATIFU.
Sisi Waliookoka  ni mashahidi wa KRISTO wala sio mashahidi wa kitu kingine chochote.
Shahidi wa KRISTO husema habari za KRISTO na sio za vitu vingine.
Ndugu, Kama wewe ni shahidi wa YESU KRISTO mbona unatangaza tu habari za siasa?
Mbona kazi yako ni kuwasema tu vibaya watumishi bila uthibitisho?
Mbona kazi yako ni kulipigia debe tu dhehebu lako?
Kazi yako ni kuhubiri mambo ya Mpira wa miguu, mieleka na masumbwi?

Kama wewe ni wakili wa siri za ufalme wa MUNGU mbona humtangazi Mfalme wa ufalme wa MUNGU?
1 Yohana 5:10 "Yeye amwaminiye Mwana wa MUNGU anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini MUNGU amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao MUNGU amemshuhudia Mwanawe. Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanaye(YESU) Yeye aliye naye Mwana(YESU), anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa MUNGU."

Uuliyezaliwa Mara ya pili ni lazima uwe na ushuhuda na ushuhuda huo ni injili ya KRISTO unayopaswa kuipeleka.
Wewe uliyezaliwa kwa Neno na kwa ROHO lazima uwe na ushuhuda wa YESU KRISTO.

Aliyezaliwa ROHO na kwa Neno hawezi kunyamaza, bali atausema ushuhuda wa YESU KRISTO.
Ushuhuda wa YESU KRISTO ni Neno la MUNGU, ni injili  iponyayo.

Kama shahidi wa KRISTO na wakili wa siri za ufalme wa MUNGU basi hakikisha unaupeleka ushuhuda wa YESU KRISTO ambao ni injili yake.
ROHO MTAKATIFU ndiye kiongozi wa safari ya wateule wa MUNGU, Unamhitaji ROHO MTAKATIFU.

Waefeso 2:18-22 '' Kwa maana kwa yeye(YESU) sisi sote tumepata njia ya kumkaribia BABA katika ROHO mmoja. Basi tangu sasa ninyi si wageni wala wapitaji, bali ninyi ni wenyeji pamoja na watakatifu, watu wa nyumbani mwake MUNGU. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye KRISTO YESU mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika BWANA. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya MUNGU katika ROHO.''
  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments