YAKATAE MAFUNDISHO YA UONGO YOTE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Tunaishi leo katika nyakati za mwisho ambazo ROHO MTAKATIFU kupitia Biblia anasema kwamba Kuna mambo matatu mabaya yatatokea ili kuwakosesha   uzima wa Milele baadhi ya watu.
Mambo hayo matatu ni;
1. Watu kujitenga na Wokovu wa KRISTO.
2. Watu kusikiliza roho zidanganyazo, roho hizo kazi yake ni kuwatoa watu katika Wokovu wa KRISTO.
3. Watu kufuata mafundisho ya mashetani.
 1 Timotheo 4:1-7  '' Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo MUNGU aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.  Kwa maana kila kiumbe cha MUNGU ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la MUNGU na kwa kuomba. Uwakumbushe ndugu mambo hayo, nawe utakuwa mtumishi mwema wa KRISTO YESU, na mzoevu wa maneno ya imani, na mafundisho mazuri yale uliyoyafuata. Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa.''
 
Mafundisho ya uongo ni mafundisho yanayowaondoa watu katika Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.
Wokovu ni mpango wa MUNGU wa kumwokoa Mwanadamu.
Wokovu wa KRISTO hutufundisha kuacha dhambi na mabaya yote.
Ukiona fundisho linasapoti dhambi ujue hilo ni fundisho la uongo.
Tito 2:11-13 " Maana neema ya MUNGU iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa KRISTO YESU, MUNGU mkuu na Mwokozi wetu;"


Injili ya KRISTO imefunuliwa ikikataza uovu.
Kila mtumishi wa MUNGU kipaombele chake cha kufundisha ni muhimu kiwe kweli ya MUNGU na utakatifu.
Biblia iko wazi kwamba siku hizi za mwisho yatakuwepo pia mafundisho mengi ya mashetani, hivyo ni kipindi cha kuwa makini sana.
Mafundisho ya mashetani ni mafundisho yanayowaondoa watu kwenye kumtegemea MUNGU na sasa wanategemea vitu, watu au majini na mizimu.

Walimu wengi wanaofundisha mafundisho ya uongo huwakataza wanafunzi wao kujifunza injili ya Wokovu wa YESU KRISTO.
Huwawekea mipaka waumini wao ili tu wasijifunze juu ya Wokovu wa KRISTO.
Mafundisho ya mashetani  ni mafundisho ya Mpinga Kristo na yanawazuilia watu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao.


1 Yohana 2:22-25 ''Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa YESU ni KRISTO? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba(MUNGU) na Mwana(YESU). Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia. Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya Baba. Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele.'' 

Mafundisho ya mashetani ni mafundisho yanayokataza watu kuokoka.
Mafundisho ya mashetani ni mafundisho yanayowatenga wanadamu na Mwokozi wao pekee YESU KRISTO.
Matendo 4:12 "Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo."

 
Mafundisho ya mashetani ni mafundisho ya kuyakimbia.
Mafundisho ya mashetani ni mafundisho yanayompinga MUNGU Baba, YESU KRISTO na ROHO MTAKATIFU.
Wahubiri wote wa Neno la MUNGU imewapasa sana kuhubiri Neno Kibiblia na sio kuhubiri kidini au kidhehebu.
  Baadhi ya wahubiri Leo huhubiri Neno la MUNGU kidhehebu.
Ndugu zangu ni muhimu kujua kwamba mafundisho ya mashetani yapo na hayo yanawazuilia watu kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao.
Hakikisha unajitenga na mafundisho ya uongo .
Leo pia kuna watumishi hucheza na akili za watu. Watumishi hao hukemea mafundisho ya uongo huku na wao wakifundisha mafundisho hayo ya uongo ila kwa njia nyingine.
Unaweza ukakuta mtumishi anakemea sana mafundisho ya uongo wakati na yeye anafundisha mafundisho ya uongo ila ni mafundisho tofauti na anayoyakemea.
Ndugu unahitaji kuwa makini sana.
Usikubali tu kusomewa Biblia Bali ithibitishe mwenyewe kwa kuisoma na kuielewa.

Biblia inasema ''Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa(Ucha MUNGU).-1 Timotheo 4:7 ''
 
Kumbuka Sumu ndicho kitu ambacho ni hatari zaidi kwa mwanadamu kukila.
Mafundisho yasiyo ya injili ya KRISTO YESU ni sumu Kali Sana.
Kazi ya sumu ni kuua au kudhuru, mtu wa MUNGU akianza kujifunza mafundisho ya kidini yaliyo kinyume na injili ya KRISTO anaweza akafa kiroho.
Mafundisho yeyote ya kidini yaliyo kinyume na injili ya Bwana YESU hayo hayafai na ni sumu Kali inayoweza kumuua mtu kiroho hata akakosa mbingu.
Ndugu uwe makini sana.

Kuna watu wamelishwa sumu na viongozi wao wa dini na kuzuiliwa kujifunza Neno la KRISTO la injili ya uzima wa milele.
Kuna watu wamelishwa sumu na muanzilishi wa dhehebu lao na kuzuiliwa kuwaamini wanaohubiri Wokovu.

Ndugu ulilishwa sumu ya mafundisho?
Umekatazwa kuokoka na kiongozi wako wa dini ?
Je unamtii kiongozi wako wa dini kuliko YESU KRISTO au kuliko Biblia?

Jikague kama umelishwa sumu ili utoke Leo katika utumwa wa sumu za wanadamu.
Kuna wengine walilishwa sumu mpaka leo huwa wanaomba wanadamu badala ya MUNGU, kuna wengine huomba mawe na kuyasujudia na kuyabusu, kuna ambao wanadhani MUNGU yuko ndani ya sanamu walizotengeneza wenyewe.
Kuna wengine wamekunywa sumu mbaya sana hadi kiongozi wao wa dini amewaambia wamwite Mungu na wao wanamwita Mungu hata Leo.
Kuna waliopokea neno kutoka kwa majini na wao wanalishika neno hilo wakidhani ni Neno la MUNGU. Ndugu nakuomba ujue kwamba Neno la MUNGU analo mmoja tu yaani YESU KRISTO aliyetoka juu mbinguni, wengine wote wametoka duniani tu hivyo hawana Neno la MUNGU.

Yohana 3:31 '' Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote. ''
Wengine wote wametokea duniani tu. YESU ni NENO juu ya Neno la MUNGU. Fundisho lolote lililo kinyume na injili ya YESU KRISTO, hilo fundisho ni sumu Kali na hakikisha unajitenga nalo.
Sumu inaweza ikakufanya ukabaki kuwa mwanafunzi wa majini tu na sio Mwanafunzi wa YESU KRISTO Mwokozi.

Sumu inaweza kukufanya ukabaki Mwanafunzi wa Mafundisho ya awali ya ulimwengu tu na usiweze kuwa Mwanafunzi wa YESU KRISTO.
Sumu inaweza ikakufanya ubaki kuwa Mwanafunzi wa nabii wako wa uongo tu na mbinguni usiende.
Sumu inaweza kukufanya uwe mtumwa unayeteseka duniani na mbinguni usiende.
Ndugu unahitaji sana kuambatana na Neno la KRISTO la Wokovu wa milele.
Kataa mafundisho yaliyo sumu na mkimbilie Bwana YESU mwenye Neno la uzima, nje na Neno la KRISTO kuna mafundisho yaliyo sumu na hayana msaada wa uzima wa milele.
2 Yohana 1:9-10 " Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba(MUNGU) na Mwana(YESU) pia. Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu."


Tambua neno hili muhimu kwamba mtu asiye na YESU huyo hana MUNGU.
Mtu anayemkataa YESU kuwa Mwokozi wake, huyo mtu anamkataa MUNGU aliyeumba mbingu na dunia.
Biblia iko wazi sana ikisema kwamba '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.-Yohana 3:16-18 ''
Usikubali kusema uongo kwa MUNGU aliye hai.
Usije ukakubali hata siku moja kusema uongo kwa MUNGU.
Akina Anania na Safira walikufa kwa sababu tu walisema uongo kwa MUNGU, hiyo iko Matendo 5:1-10
Usije ukakubali hata siku moja kusema uongo kwa MUNGU.
Ewe kiongozi wa dini na ewe unayetaka kuanzisha dhehebu au tawi la kanisa, usikubali kusema uongo katika mambo ya MUNGU.
Kumkataa YESU ni kuukataa uzima wa milele.
Kumkataa YESU ni kujipeleka mwenyewe jehanamu.
Ewe uliyedanganywa  na watu na ukamwacha YESU, nakuomba rudi leo kwa YESU utubu na kuanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu.
Ewe unayelazimishwa na ndugu zako au wazazi wako au jamii yako kwamba usiokoke, naomba tambua kwamba hao ndugu au wazazi hawana mbingu ya kukupeleka. Hao wazazi au ndugu ukaribu wako na wao unaishia kaburini baada ya kufa. Wengine hata kuigusa maiti yako wanaweza wakaona ni mkosi hivyo hao hawana msaada wako kuhusu milele ijayo kama wanakushauri umwache YESU au usikokoke hakika hao hawafai.
Usiwaogope wanadamu katika suala linaloamua hatima yako ya milele.
Ni leo ndugu nakuomba mkimbilie Bwana YESU.
Marafiki wasikudanganye kwamba YESU hawezi kukusamehe, tubu tu na anza kuishi maisha matakatifu hakika jina lako litakuwa katika kitabu cha uzima.
Nakuomba sana mume/mke wako asikuzuilie kwenda mbinguni kwa sababu tu yeye hataki kuokoka.
Wazazi wako au ndugu unaoishi nao usikubali wakakuzuilia kwenda mbinguni, kwa sababu tu wao wanaona kuokoka ni kujishusha hadhi.
Ndugu naomba utambue kwamba hata kama kibinadamu marafiki zako wataona kuokoka ni hasara, naomba utambue kwamba mbinguni ni furaha kuu sana mtu mmoja tu anapookoka na kutubu.
Luka 15:10  '' Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.''  
Malaika hushangilia sana sana mtu mmoja tu anapotubu. 
Kama Malaika wa MUNGU wanakupa heshima kubwa kwanini unawatazama wanadamu wanaokushusha?
Kama mbinguni zimekupa heshima baada ya kuokoka kwako, unaogopa nini?
Ndugu naomba utambue kwamba kwa MUNGU ukiokoka hakika wewe ni thamani sana sana.
Ni Muda tu wa wewe kufanya maamuzi sahihi katika maisha yako.
Biblia inasema '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa.  Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA.-Isaya 55:6-8''
  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments