FAIDA NA HASARA ZA MARAFIKI ZAKO

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ujumbe huu umekuwa rohoni mwangu kwa zaidi ya mwaka sasa, na namshukuru MUNGU maana ni leo nakuletea ujumbe huu kuhusu hasara na faida za marafiki zako.
Neno ''Rafiki'' lina maana gani?
Rafiki ni mtu anayependana na kuaminiana na mwingine.
Ni ni mtu wa kweli wa kumtegemea katika wazo, ushauri au msaada wakati mwingine.
Ni mtu  wa kutumainiwa unayempenda.

Kuna aina Mbili(2) za marafiki.
Mithali 18:24 ''Ajifanyiaye rafiki wengi ni kwa uangamivu wake mwenyewe; Lakini yuko rafiki aambatanaye na mtu kuliko ndugu. ''

1. Kuna marafiki wema.
Yohana 13:34-35 ''Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.''
Wateule wa KRISTO ni marafiki wanaopaswa kupendana kwa upendo wa Ki MUNGU, hao ni marafiki wema.

2. Kuna marafiki wabaya.

 Yakobo 4:4 '' Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa MUNGU? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa MUNGU.''
Kuwa rafiki wa dunia ni kuwa mtu wa dhambi na mtu wa kushirikiana na matendo mabaya yaliyomo katika dunia. Mdau mkubwa wa kukufanya uwe rafiki wa dunia ni rafiki mbaya.
Wapenda dunia ni marafiki wabaya.


Biblia inatoa tahadhari juu ya marafiki.
Mika 7;5 ''Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari.''
 
Kuna aina Mbili(2) za marafiki wema.

1. Marafiki waliobeba baraka au Kusudi la MUNGU.
Mwanzo 39:2-3 '' BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. BWANA wake akaona ya kwamba Bwana yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake.''
Watu wa kundi hili ni marafiki kweli lakini ni zaidi ya rafiki wa kawaida.
Mfano wa marafiki hawa ni Mke wako/ Mume wako, Watumishi wa MUNGU waliolibeba kusudi la MUNGU, Wazazi wako au ndugu zako  n.k

2. Marafiki wema wasiobeba baraka zako.

Mithali 17:17 '' Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.''
Hwa ni marafiki wazuri sana lakini hawana kitu cha zaidi au ziada kwako. Jukumu lao linaishia kwenye urafiki tu.

Sifa za Marafiki wema.

1. Wabebeba baraka na hana hila dhidi yako.
Mwanzo 30:27 '' Labani akamwambia, Iwapo nimeona fadhili machoni pako, kaa, maana nimetambua ya kwamba BWANA amenibariki kwa ajili yako.''
Yakobo alikuwa Ni kama rafiki kwa Labani Mjomba wake lakini Yakobo alikuwa amebeba baraka. Ukitaka kujua ni kwa jinsi gani Yakobo alibeba Baraka kubwa katika maisha ya Labani Msikilize Labani anachosema katika andiko hapo juu.

2. Anayaona mambo yako mema kuwa bora zaidi kuliko ya kwake.

Wafilipi 2:3 '' Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. ''
 
3. Ana upendo kwako na anakuwazia mema.

Mithali 27:17 ''Chuma hunoa chuma; Ndivyo mtu aunoavyo uso wa rafiki yake.''

4. Anakuombea na
Hukushauri mambo mema.
Yakobo 5:16 '' Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii. ''
 
5. Ni mcha MUNGU halisi.

Mitthali 13:20 ''Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. ''

Unahitaji kuwa makini sana na marafiki zako.
Hakikisha unakuwa na marafiki wema na sio marafiki wabaya.
Wako watu wamewahi kuumizwa sana na marafiki.
Wapo marafiki kwa sababu ya kujua siri zako wanaweza kuwa mtego na tanzi mbaya kwako.
Uwe makini sana na marafiki zako, kama rafiki haeleweki vunja urafiki. Kama rafiki hataki kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO hakikisha unavunja urafiki huo.
Mimi Peter Leo nataka kupitia somo hili utafakari marafiki zako ili wasikupeleke kubaya.
Zamani kabla sijaokoka kuna rafiki yangu sana alinishauri twende kwa mganga wa kienyeji ili tuwe na maisha mazuri, siku hiyo ambayo angenipitia, kwa neema ya MUNGU nikatumwa na wazazi kwenda sehemu hivyo safari ya kwa mganga ikaishia hapo. Huko kwa mganga kungetengeneza vifungo vya giza, maagano, kutoa sadaka za damu na kutumiwa majini, ni hatari sana na chanzo ni rafiki asiyemcha MUNGU.
Ayubu 17:5 ''Awafitiniye rafiki zake wawe mawindo, .................''
Ndugu,Wapo marafiki ndio kilikuwa chanzo cha baadhi ya watu kupata mimba za utotoni, kuuguwa Ukimwi,  kufukuzwa shule,Kuna watu wako jela kwa sababu ya utapeli wa marafiki, kuvunjika ndoa au uchumba n.k Hivyo uwe makini sana na marafiki zako.
Najua kabisa mwanadamu hawezi kukaa bila rafiki lakini uwe makini na marafiki zako.
Kama rafiki zako hawajaokoka hakika hata wewe kusimama katika Wokovu itakuwa ngumu sana, hao sio marafiki wazuri hivyo uwe makini sana sana maana marafiki wengine wamebeba vifungo vya giza kwako.
Kumbuka hata hii ili ujue umuhimu wa kuwa makini na marafiki.
Zaburi 55:12-13 '' Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione. Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. ''

Sifa  za marafiki wabaya.

1. Hutafuta faida yao kupitia wewe na hutaka kujua siri zako ili wazitumie baadae.
Mithali 19:4 ''Utajiri huongeza rafiki wengi; Bali maskini hutengwa na rafiki yake.''

2. Hukushauri vibaya na  ni waongo na wasaliti.

Kumb 13:6-8 '' Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako;  katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia; usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche;''
 
3. Hutamani uangamie au uharibikiwe japokua haonyeshi hivyo ukimtazama kimwili.

 Zaburi 38:11'' Wanipendao na rafiki zangu wanasimama mbali na pigo langu; Naam, karibu zangu wamesimama mbali. ''
 
4. Hukukimbia wakati wa matatizo
na hawana hofu ya MUNGU ndani yao.
Mithli 19:7 ''Ndugu zote wa maskini humchukia; Jinsi gani rafiki zake huzidi kujitenga naye! Huwafuata kwa maneno, lakini wametoweka. ''

5. Ni marafiki wa muda kisha hugeuka maadui.
 Mombolezo 1:2 ''Hulia sana wakati wa usiku, Na machozi yake yapo mashavuni; Miongoni mwa wote waliompenda Hakuna hata mmoja amfarijiye; Rafiki zake wote wamemtenda hila, Wamekuwa adui zake. ''
  Je utamjuaje rafiki mzuri na mwenye baraka?
Muombe MUNGU akujulishe na Msikilize ROHO MTAKATIFU.
Je utamjuaje rafiki mzuri ila amebeba laana?

Jifunze Neno la MUNGU na kulitafakari utapata ufahamu wa kujua.
Je utamjuaje rafiki mbaya kwako?

1. Msikilize ROHO MTAKATIFU  na Kumtii yeye ROHO.
2. Wasikilize watumishi wa MUNGU au waulize juu ya huyo rafiki.
3. Utamjua huyo rafiki mbaya kwa matendo yake na kazi zake.
 Ayubu 16:20 ''Rafiki zangu hunidharau; Lakini jicho langu humwagia MUNGU machozi;''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.


Comments