IJUE TOFAUTI YA SADAKA, MSAADA NA ZAWADI KATIKA UTOAJI WAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

 Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu!
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Watu wengi sana hutoa matoleo yao  madhabahuni lakini matokeo ya baraka walizozihitaji huwa hayaji.
Kwanza ni makosa kudhani kwamba kazi ya matoleo ni baraka tu, hapana, matoleo yana kazi nyingi sana nje na baraka. Na baraka ni kipande tu katika hayo matokeo, na baraka hizo zitakuja kutegemea na mambo kama mannne au zaidi ambayo ni  mtoaji, utoaji wake, madhabahu husika, maombi, nia ya moyo na kumcha MUNGU.
Sasa wengi hawaelewi sana kuhusu sadaka ndio maana unatakiwa kujifunza somo kama hili.
Sadaka, msaada  na zawadi ni nini? kwa nini zitofautiane? je inawezekana huwa natoa zawadi au msaada na sio sadaka ndio maana matokeo ya utoaji siyaoni? Je maombi ni sahihi yanayoambatana na sadaka zangu?
Maswali kama hayo yanaweza kumsumbua mtu, ngoja tujifunze leo.

Sadaka ni nini?
Sadaka ni kitu au fedha ambayo hutolewa na mtu kanisani au kwa wanaostahili, kwa lengo la kupata thawabu kwa MUNGU.
Thawabu ni malipo  mema anayoyapata mtu  kutoka kwa MUNGU kwa sababu ya mtu huyo kutii maagizo ya MUNGU.

Msaada ni nini?
Msaada ni kitu anachotoa mtu ili kutimiza haja ya mtu aliyempa.

Zawadi ni nini?
Zawadi ni kitu atunukiwacho mtu  kama ishara ya upendo, wema au utendaji mzuri wa kazi au shughuli.
Ni muhimu sana wewe mtoaji wa sadaka utofautishe sadaka, msaada  na zawadi.
Inawezekana kabisa kila jumapili kanisani wewe huwa unatoa zawadi na sio sadaka.
Inawezekana kabisa wewe kila ukienda kwenye semina au mikutano ya injili au ibadani huwa unatoa msaada na  au zawadi na sio sadaka.
Kumbuka MUNGU hahitaji msaada au zawadi ya mwanadamu  ya aina yeyote.
Sasa hakikisha unatoa sadaka na sio zawadi au msaada.
Watoaji wengi hutoa zawadi na sio sadaka ndio maana hawayaoni matokeo ya utoaji wao, kwa sababu walitoa zawadi na sio sadaka.
Huwezi ukaweza kutoa zawadi kila siku ila unaweza ukawa unatoa sadaka au zaka kila mara.
Kumb 14:22 '' Usiache kutoa zaka ya fungu la kumi katika maongeo yote ya mbegu zako, yatokayo shamba mwaka baada ya mwaka.''

Watoaji wengi hutoa zawadi na sio sadaka.
Watoaji wengi hutoa pesa au vitu na sio kuvifanya vitu hivyo viwe sadaka.
Unapotoa pesa au kitu na ufahamu wako ukabaki umetoa pesa au kitu hakika hapo utakuwa umetoa msaada na sio Sadaka, utakuwa umetoa zawadi na sio sadaka.
Unatakiwa ujue kwamba Vitu vyote ulivyonavyo ni vya MUNGU.
Zaburi 24:1 '' Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake.''
  Hivyo MUNGU hahitaji msaada wala zawadi kutoka kwa mwanadamu ila anahitaji sadaka.
Hivyo Pesa yako au kitu chako unachokitoa kwa mtumishi wa MUNGU au kanisani  hakikisha vitu hivyo vinakuwa sadaka na sio zawadi.
Tamka kwa maneno yako kwa imani kwamba ''Natoa pesa hii kama sadaka mbele zako MUNGU Baba kupitia mtumishi huyu au huduma hii au madhabahu hii''
 Watu wengi sana wanaweza wakatoa sadaka nzuri au kitu kizuri sana na baada ya mwaka au miezi kadhaa anawasilimulia marafiki zake kwamba ''Nilitoa msaada katika huduma ya mtumishi fulani''
Hiyo ni kuonyesha kwamba alitoa msaada au zawadi na sio sadaka, na MUNGU anahitaji sadaka na zaka tu na sio msaaada au zawadi, Hapo ndipo wengi sana huishia kulalamika tu kwamba tangu aokoke mwaka wa 10 huu lakini hajabarikiwa japokuwa ni mtoaji mwaminifu. Ndugu Kanuni za MUNGU hazisemi kwamba tumtolee zawadi au msaada bali tutoe sadaka na zaka. Kanuni za MUNGU pia zinakutaka umtolee matoleo yako lakini pia ufanye kazi na katika hizo kazi ndipo utamuona MUNGU akikubariki sana sana na utayaona matokeo ya utoaji wako. Ukiwa huna kazi basi omba MUNGU atakupa kazi na atakufunulia jinsi ya kufanya biashara au kujiajiri na kwa sababu ya utoaji wako hakika utamuona MUNGU, ukiwa mtu wa kulala tu basi unahitaji msaada wa kiroho.
 Ili  usiwe mtu wa kutoa zawadi na msaada tu basi jifunza jinsi SADAKA YA MTEULE  WA MUNGU ILIVYO.
1. Ni sadaka inayoambatana na moyo wa mtoaji.
Luka 12:33-34 ''Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu. Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu.''

2. Ni sadaka inayotoka katika moyo wa upendo.
Kutoka 25:1-2 ''BWANA akanena na Musa, akamwambia, Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu.   '' 

3. Ni sadaka ya heshima na nzuri, sio kilema au sio isiyostahili au ziada ya mtoaji.
Kutoka 25:3 '' Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii; dhahabu, na fedha, na shaba,''

4. Ni sadaka iliyowekwa wakfu na mtoaji.
2 Nyakati 29:31-33 '' Ndipo Hezekia akajibu, akasema, Sasa mmejifanya wakfu kwa BWANA, karibuni mkalete dhabihu na matoleo ya shukrani nyumbani mwa BWANA. Basi kusanyiko wakaleta dhabihu na matoleo ya shukrani; na wote wenye moyo wa ukarimu, wakaleta sadaka za kuteketezwa. Na hesabu ya sadaka hizo za kuteketezwa walizozileta kusanyiko ikawa ng'ombe waume sabini, kondoo waume mia, na wana-kondoo mia mbili; hao wote walikuwa ni sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA. Na vitu vitakatifu vilikuwa ng'ombe mia sita, na kondoo elfu tatu.   ''
Labda tujue pia Neno ''Wakfu'' ni nini?
Wakfu ni mali iliyotengwa maalumu kwa ajili ya kazi ya MUNGU ambayo mtoaji  hana mamlaka nayo tena.
Jitakase na takasa matoleo yako kisha mtolee MUNGU kwa moyo wa upendo  na jiweke wakfu  na huku ukiweka wakfu sadaka yako.
Epuka bajeti ya sadaka bali msikilize ROHO wa MUNGU ndani yako katika utoaji.
Unaweza ukaitenga mapema sadaka yako na hakikisha mtumishi husika anaiombea sadaka yako.
Pesa yako ibadili ili isiwe pesa tu bali iwe sadaka takatifu mbele za MUNGU.
Unaweza ukaibadilisha kwa maombi tu na kujiweka wakfu na huku ukiiweka wakfu pia, mambo ya Ki MUNGU huenda kwa imani hivyo ondoa mazoelea bali toa kwa imani.
Sadaka ni ufunguo mkubwa sana katika ulimwengu wa roho.
Maombi ni Master key kabisa hivyo sadaka yako ikiambatana na maombi sahihi lazima uone matokeo sahihi yaliyokusudiwa kupitia sadaka yako.
Sadaka huleta matokeo ya haraka sana. Na Wewe Mtumishi wa MUNGU unayesoma somo hili nakuomba  kwamba unapopewa sadaka iombee na ikabidhi kwa MUNGU kama sadaka takatifu na sio msaada au zawadi.
Unapopewa msaada iwe wazi kwamba huo ni msaada.
Unapopewa zawadi iwe wazi kwamba ni zawadi. Siku moja kuna ndugu mmoja alinitumia kiasi fulani cha pesa na akanipigia simu akaniambia ni zawadi hiyo amenipa. Nikamuuliza mara ya pili na tatu kama ni zawadi tu au ni sadaka akasema hiyo sio sadaka ni zawadi, nikamuombea kwa ajili ya zawadi na sio kwa ajili ya sadaka. Zawadi zina thawabu yake na sadaka zina nguvu yake hivyo mtumishi ni muhimu uwasaidie watu kwamba wajue wanatoa nini, zawadi au sadaka. 
Penda watu watoe sadaka na sio zawadi tu, ila hata zawadi au misaada sio dhambi bali ni jambo jema sana ila hakikisha tu watu wale wanatambua kiroho hicho walichotoa. Kama wanamtolea MUNGU basi watoe sadaka au zaka. Lakini kama wanakupa wewe mtumishi zawadi au msaada basi wasiseme kwamba '' Wanamtolea MUNGU'' Maana MUNGU hatuwezi kumtolea zawadi au msaada.
2 Kor 9:1-8 ''Kwa habari za kuwahudumia watakatifu sina haja ya kuwaandikia.  Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu kwa Wamakedonia, kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu imewatia moyo wengi wao. Lakini naliwatuma hao ndugu, ili kujisifu kwetu kwa ajili yenu kusibatilike katika jambo hili; mpate kuwa tayari, kama nilivyosema; kusudi, wakija Wamakedonia pamoja nami, na kuwakuta hamjawa tayari, tusije tukatahayarika sisi, (tusiseme ninyi), katika hali hiyo ya kutumaini. Basi naliona ya kuwa ni lazima niwaonye ndugu hawa watangulie kufika kwenu, na kutengeneza mapema karama yenu mliyoahidi tangu zamani, ili iwe tayari, na hivi iwe kama kipawa, wala si kama kitu kitolewacho kwa unyimivu. Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.  Na MUNGU aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; ''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.

Comments