JINSI YA KUIJUA NDOTO ILI UPATE KUOMBA UKIHUSIKA NA KILICHO NDANI YA NDOTO HIYO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo nazungumzia ndoto.
Somo la ndoto ni pana sana sana na nimewahi kuandika masomo zaidi ya matano kuhusu ndoto, na kuna siku nitaandaa somo la Jinsi ya kuombea ndoto uliyoiota.
Leo nataka tujifunze jinsi ya kuijua ndoto na kujua kilichomo ndani ya ndoto hiyo.
Natambua kabisa kwamba kuna ndoto zingine ni za ujumbe wa moja kwa moja, yaani kama ulivyoona ndotoni ndivyo itakuwa. Na watu wengi sana wamebaki hawaelewi baada ya kuota ndoto ambayo haina fumbo bali iko kama itakavyokuwa katika hali halisi.
Lakini ndoto zilizo nyingi ni kama fumbo, kwa sababu ndoto ni lugha ya rohoni hivyo kwa akili za kimwili unaweza ukashindwa kuielewa.
Ndoto ni nini?
Ndoto ni taarifa ya rohoni inayojulisha mambo yaliyotokea, yatakayotokea au yanayotokea sasa.
Siku moja niliota ndoto napewa Pesa Tsh  45,000/= na watu fulani Wakristo, ila pesa hizo ndotoni niliziona zikiwa nyeusi nyeusi, yaani Noti 4 za 10000 na noti moja ya 5000 lakini zina rangi nyeusi hata kama zinaonekana kwamba ni 10000 na 5000. Nilipoamka asubuhi nilikumbuka ndoto hiyo lakini sikuelewa. Nikaomba MUNGU anisaidie ili kama kuna mpango wa kipepo kupitia pesa ambayo labda itapitia mikononi mwangu basi MUNGU afute mpango huo mbaya dhidi yangu. Baadae siku hiyo hiyo muda kama saa tano asubuhi nilipigiwa simu na kwenda sehemu fulani kukutana na watu fulani. Tuliongea mambo mengi sana ya kiroho mazuri kabisa lakini mwisho wakatoa Tsh. 45,000 kunipatia, ghafla ROHO wa MUNGU akanikumbusha ndoto ya usiku kumkia siku hiyo. Nikajikuta nakataa kupokea pesa hiyo, walinishangaa sana watu wote pale maana tulikuwa kama watu zaidi ya 7. Walinibembeleza lakini nilikataa, wakasema sasa watakuwa wananipa 45,000 kila mwezi kama posho ya utumishi wangu kwa MUNGU, Bado nikakataa. 
Baadae niligundua kwamba pesa zile zingeleta lawama kubwa baadae na zingesababisha baadhi ya watu kususia kazi ya MUNGU. Ukweli nilikuwa nauhitaji sana wa pesa na siku hiyo sikumbuki kama nilikuwa  hata na pesa ya chakula, lakini kwa Neema ya MUNGU niliukataa mtego ule wa shetani kupitia pesa. Nisingeota ndoto ile ningepokea pesa ile kwa furaha na kicheko kikubwa lakini kumbe kulikuwa na pando la shetani.

Chanzo cha ndoto kinaweza kuwa.

1. Ulimwengu wa wa roho wa nuru. 

Hapana ndugu tunahusika zaidi maana MUNGU husema sana na watu wake na ahadi ya MUNGU kwa wanadamu katika wakati wetu huu ni pamoja na kusema na sisi kwa ndoto.
Yoeli 2:28 ''Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; '
Ndoto kutoka ulimwengu wa roho wa nuru inaweza ikahusika na.
A. Kukujulisha lile lililoko mbele yako linalotoka ulimwengu wa roho wa nuru.
B. Kukujulisha lile lililoko mbele yako linalotoka ulimwengu wa roho wa giza.
Hapa ndipo watu wengi sana hukwama maana anaweza akaona mfano mbwa anamfukuza, sasa yeye anadhani ni ndoto ya shetani hivyo hafanyii kazi, wakati ni ndoto ya MUNGU inayokujulisha analokuandalia shetani, umeona ili uwe makini na ujue namna ya kuomba na kuliepusha jambo hilo la giza.

Vyanzo vingine vya ndoto ni 

2. Ulimwengu wa giza.

Zakaria 2:10 ''Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure  ........... '
Vinyago vinamwakilisha shetani.
Wengi wamekuwa waganga wa kienyeji na kukosa mbingu kwa sababu tu majini yalisema na wao kwa ndoto kuhusu uganga na uchwai.

3. Mwanadamu mwenyewe kutokana na kile anachowaza sana au kinachompotezea sana muda.
Unampenda mtu na unamuwaza kila muda kisha usiku unamuona kwamba atakuwa mumeo au mkeo, kumbe ni fikra zako zinakupoteza.
Unawaza pesa sana na unaziota, umeona filamu kisha unaona matukio uliyoyaona kwa filamu.
 Mhubiri 5:3 '' Kwa maana ndoto huja kwa sababu ya shughuli nyingi; na sauti ya mpumbavu kwa njia ya wingi wa maneno. ''

 Baada ya kukujulisha hayo sasa nataka tuendelee kujifunza juu ya ndoto kama sehemu ya MUNGU kuzungumza na Mwanadamu.
Kwenye ndoto kunaweza kuwa na kusudi fulani, unajulishwa na unapewa njia za kushinda.
Mathayo 2:13,14,19,20,21  '', malaika wa BWANA alimtokea Yusufu katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize. Akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; Hata alipofariki Herode, tazama, malaika wa BWANA alimtokea Yusufu katika ndoto huko Misri, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mamaye, ushike njia kwenda nchi ya Israeli; kwa maana wamekufa walioitafuta roho ya mtoto. Akaondoka akamchukua mtoto na mamaye, akafika nchi ya Israeli.''
 Hapa tunapata kuona kusudi la ajabu sana lililokuwa ndani ya ujumbe wa ndoto ya Yusufu, kama ambavyo wewe unaweza ukapewa ujumbe kwa ndoto leo.
Yusufu alifanyia kazi maagizo ya ujumbe wa MUNGU kwenye ndoto na kila kitu kilienda vyema kinyume kabisa na mipango ya wanadamu wabaya. Ndugu usidharau ndoto bali husika na maombi kulingana na ulichokiona kwenye ndoto.

Mambo ya kuzingatia ukiota ndoto ni haya;
1. Kwenye ndoto unaweza ukajulishwa juu ya eneo ulilopo, tabia za watu wa eneo hilo, madhabahu gani za giza zinatesa watu eneo hilo na kuna tishio gani, hali ya ardhi kiroho na unatakiwa ufanyeje wewe kama mteule wa KRISTO.
Hesabu 12:6 '' Kisha akawaambia,Sikizeni basi maneno yangu;Akiwapo nabii kati yenu,Mimi,BWANA,nitajifunua kwake katika maono,Nitasema naye katika ndoto.''

 Siku moja nilienda eneo fulani kwa muda wa wiki moja. Usiku wa siku ya kwanza niliota ndoto juu ya sehemu ya kununua chakula, nilielekezwa hadi sehemu husika kwa ndoto. Kesho yake nilienda na kukutana na sehemu nyingi wakiuza chakula lakini nilienda nipoelekezwa. Baadae niligundua rohoni kwamba wale wengine hufanya maagano ya giza kwenye vyakula ili wavute wateja kipepo.

2. Kwenye ndoto unaweza ukajulishwa nini cha kufanya, ukajulishwa kuongeza juhudi katika unachokifanya wakati huu.
Mfano ni mimi nilijulishwa juu ya nini cha kufanya juu ya zile Pesa 45,000
Yusufu alijulishwa jinsi ya kumfanya adui aishiwe pozi na huyo adui asijue nini cha kufanya, hadi akafa huyo adui bila kutimiza mpange wake wa kipepo.
 
3. Kwenye ndoto unaweza ukajulishwa ni wapi ulikwama na ni wapi ulifungwa kipepo.
Wakati mwingine unaweza ukawa kila ndoto unaota eneo fulani ambalo uliwahi kuishi zamani, kumbe labda unajulishwa juu ya ni wapi ulikwama au ulifungwa.
Nakuomba ndugu kwamba, kwenye ndoto usihusike tu na uliyemuona kwa sura bali husika zaidi na yafuatayo;
1. Husika na Maneno yaliyokuwa yanatamkwa, hayo ndio yamebeba ujumbe wa ndoto husika.
Danieli 7:1 '' Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danielii aliona ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo.''
 Siku moja niliota ndoto Mtumishi mmoja wa MUNGU akiniambia niombe sana, niliamka na kuomba na ajabu wiki hiyo ilikuwa ni ngumu sana kwangu maana shetani alijaribu kuniharibia, lakini kwa maombi nilishinda. Ilikuwa ni wiki ya ngumu kuanzia jumatatu hadi jumapili.

2. Husika na mazingira ya kwenye ndoto, hayo yana maana sana na hujulishwa kusudi la ndoto.
Yeremia 23:28 '' Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema BWANA. ''
 Siku moja niliota ndoto nikiona picha yangu lakini ikiwa haina rangi. Nikaambiwa huko huko ndotoni kwamba huyo sio wewe ila ni watu wanabadili masomo yako na wengine wameandika vitabu kwa kutumia masomo yako, wengine wanadanganya watu kwamba wao ndiyo wewe. Msemaji wa ujumbe huo aliwaita watu wale kwa jina la ''Akina Peter Mabula wadogo'' Nilipoamka nilijisikia vibaya sana sana, niliona hadi vitabu walivyoandika wakitumia masomo yangu. Niliumia sana lakini nilijulishwa pia nini cha kufanya.
Ndio maana kuna siku niliandika post kwa uchungu nikiwakataza watu kuyabadilisha masomo yangu, nikiwakataza watu kuyaweka kwenye vitabu na nilikataza mtu kujiita jina langu, nikiwashauri kwamba wamtumikie Bwana YESU sio kwa utapeli na uongo. Niliwaambia kwamba nawaruhusu kutumia masomo yangu kufundisha makanisani, kwenye semina au mikutano ya injili, kwenye mitandao ya kijamii ila kama ni maandishi basi wasiyabadili bali wayapost kama nilivyopost. Namshukuru MUNGU sana maana kila mara wengine hunijulisha kwamba wanataka kutumia masomo yangu ibadani au mtandaoni na mimi nawaruhusu maana ndio injili itakavyo.

 3. Husika na vitu maana vitu, maana vitu hukuonyesha ni tukio la lini na limefungwa katika muda gani.
Unaweza mfano ukaona mazingira ya zamani sana kipindi uko mtoto, unaweza ukaona shuleni wakati ulimaliza shule miaka hata zaidi ya 20. Unaweza ukaona vyungu, matope au chochotena hicho ndicho kikawa kinaonyesha tukio la ndoto unalitakiwa kulifanyia kazi kimamombi.
MUNGU akupe ufahamu juu ya ndoto yako.
Danieli 1:17 '' Basi, kwa habari za hao vijana wanne, Mungu aliwapa maarifa na ujuzi katika elimu na hekima; Danielii naye alikuwa na ufahamu katika maono yote, na ndoto. ''

 4. Omba maombi kulingana na ulivyoona kwenye ndoto.
Ayubu 33:14-18 ''Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao, Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi; Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni, Na uhai wake usiangamie kwa upanga.''
 Kumbuka pia kuna baadhi ya ndoto hazihitaji maombi tu bali maombi na kuchukua hatua.
Mfano umeota ukiambiwa kuna mtu atakuja ofisini kwako ni wakala wa shetani, usikubali atakayokuambia. Ndoto kama hiyo maombi ni muhimu lakini ndoto imekupa ufahamu kwamba huyo wakala wa shetani usikubali akushawishi chochote.

5. Mwambie MUNGU akupe kushirikiana na majira yake ya baraka uliyoiona kwenye ndoto.
Mwanzo 37:56 ''Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota.''
 Huu ni mfano hai kwetu kwamba unaweza ukaota ndoto lakini kutimia kwake ni miaka mingi ijayo, Nimewahi kuota hadi ndoto ikionyesha tukio la mwaka 2096 Tanzania. MUNGU anaweza akajulisha jambo hata la miezi mingi ijayo au la miaka mingi ijayo.
Ndoto zingine unaweza kujulishwa tu  hata kama hutakuwepo ila unajulishwa ili uombe ili wakati huo ukifika kama liko jambo baya litazuiliwa kwa watoto wako au wajukuu zako.
Kwa yale ambayo umeona kabisa ni katika wakati wako basi
Omba MUNGU akupe kushirikiana na majira yako ya baraka kama ulivyoona kwenye ndoto.
Kuna mtu aliota ndoto inafika siku ya harusi yake lakini akiwa kanisani na Mchumba wake na ni mbele ya mchungaji anakuja mtu pale kumnong'oneza kuhusu sehemu ya kuwaweka wageni na sehemu ya ukumbi. Ndugu yule baada ya kuota ndoto hiyo alikemea wakati alikuwa anajulishwa kwamba suala la kufunga ndoa akizubaa litakuja kabla hajajiandaa, na kweli ikaja kuwa hivyo. Huyo alitakiwa baada ya kuota ndoto aanze kujiandaa kwa tukio la kufunga ndoa. Dada mmoja aliota ndoto anafunga ndoa na Mchumba wake lakini yeye(Huyo dada) hana shela, hiyo ilikuwa ni taarifa kwamba wajiandae vizuri. Ni kweli suala la kufunga ndoa lilikuja ghafla sana bila kuzuilika na hadi bado siku moja ndoa ifungwe shela hata ya kukodi au kuaziwa ilikuwa haijapatikana, Kwa Neema ya MUNGU kutoka katika kamati mtu mmoja alifanya mpango kwa kutumia gharama nyingi kukodi shela ndipo yule dada akapata shela masaa mawili kabla ya kuingia kanisani kufunga ndoa.
Ndugu usidharau ndoto na zingatia  huku ukiomba maana zingine ni ujumbe wa moja kwa moja kwako, na ujumbe huo unatakutaka utengeneze.
ndugu kama ndoto inakujulisha nini cha kufanya ili mabaya yakupupate basi zingatia. Na kama inahitajika toba basi fanya haraka sana.
Nimewahi kukutana na watu wengi wakisema kwamba wameota ndoto wanaenda jehanamu. Maana ya ntoto hiyo ni kwamba kama wakati huu YESU akirudi wao wanaachwa maana njia zao sio sawa mbele za MUNGU. Maana ya ndoto hiyo ni kwamba wakifa sasa kabla hawajatubu wanaweza wakapishana na uzima wa Milele ulio pekee katika Bwana YESU.
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.


Comments