KUISOMA BIBLIA YOTE NI MUHIMU SANA KWA KILA MKRISTO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Somo la leo ni kuhusu umuhimu wa kila Mkristo kuisoma Biblia yote Neno kwa Neno, Aya kwa Aya na andiko kwa andiko.

Wakolosai 3:16 ''Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu.'' 

 Mimi Peter nilitumia miezi 8 kuisoma biblia yote neno kwa neno, hiyo ilikuwa mwaka. 2010.
Baada ya mwaka mmoja baadae kupita nilianza tena kuisoma tena biblia yote na wakati huu nilimshangaa sana MUNGU na neno lake maana wakati huu katika awamu ya pili ya kuisoma Biblia yote niliona Biblia kuwa ni ngeni kabisa kana Kwamba sikuwahi kuisoma kabisa yote yalikuwa mageni kwangu. Ni muhimu sana kila mkristo angalau Mara moja katika maisha yake ahakikishe anaisoma Biblia yote neno kwa neno.

MUNGU anataka tulisome Neno lake na kulielewa. Ona mfano huu hai ambapo ni MUNGU anamwagiza Joshua juu ya kuhakikisha Neno haliondoki kwake.
Yoshua 1:8 ''Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.''
ukiisoma Biblia yote utashangaa kuona umepata ufahamu wa ajabu juu ya neno la MUNGU.
Utajua kwa kina kila eneo la Biblia. Mfano watumishi  wengi katika mahubiri yao wakisoma kitabu cha Zaburi husema "Daudi anasema" kumbe sio kitabu chote cha Zaburi kaandika Daudi , Daudi kaandika Zaburi 74 tu hivyo mtu  akisema mfano kwamba "Daudi anasema katika Zaburi 121 kwamba atainua macho atazame milima " sio Zaburi yote kaandika daudi . kuna baadhi ya maandiko ya wana wa asafu na kuna baadhi ya maandiko kaandika mfalme Suleimani na wengine. kama umeisoma Biblia yote utajua.
Jambo jingine kuwa watu husema kwamba Biblia inasema "jisaidie nami nitakusaidia asema MUNGU" huo ni uongo na msoma Biblia tu ndio anaweza kugundua.
kuwa wahubiri wa dini nyingine hudai kwamba mitume wao wametajwa katika Biblia, ambaye hajaisoma Biblia yote anaweza akakubali mapema tu kumbe Biblia mitume hao inawatambua kwamba ni watoto wa shetani.
kuisoma Biblia yote ni faida kuu kwako mkristo.


Mithali 30:5-6 '' Kila neno la MUNGU limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio. Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo.'' 

 Kuna uongo mwingi sana husemwa juu ya Biblia lakini tuliowahi kuisoma Biblia huwa tunaubaini uongo huo mapema, Biblia inasema katika mwisho wa Mathayo 24:15 kwamba  ''Asomaye na afahamu'' Hivyo kuisoma Biblia inatakiwa kuwa ni ajenda yako ya kudumu.
Kumbuka ROHO MTAKATIFU hutumia Neno la MUNGU kukusaidia, kama Neno hilo halimu ndani yako hakika itakuwa kukusaidia katika kipengele ambacho kinahitaji Neno la MUNGU.
Nilipofunga maombi kwa mara ya kwanza mimi nilisikia sauti ikisema andiko la Mathayo 4:4, ikinielekeza kufunga. Kama Neno hilo lingekuwa sijawahi kulisoma nisingeelewa kwa usahihi ujumbe ule.
Ni muhimu sana kwa kila Mkristo kuisoma Biblia yote angalau mara yote katika maisha yake yote, yaani asome Neno kwa Neno kutoka Mwanzo hadi Ufunuo.

FAIDA SABA ZA KUISOMA BIBLIA YOTE.

1. Utapata ufahamu juu ya Neno la MUNGU.
 Matendo 17:11 '' Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo ''
Watu wa Beroya walipata ufahamu wa Neno la MUNGU kwa kulisoma na kuchunguza maandiko, hata wewe unatakiwa ulisome Neno la MUNGU ili ulielewe.


2. Utamjua MUNGU na mpango wake kwa mwanadamu.
 Danieli 9:2-42 ''katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu.''
Kupitia kusoma Biblia, Danieli alielewa mwisho wa Waisraeli kukaa utumwani Babeli ndio maana akachukua hatua za maombi na maana Maandiko aliyoyasoma ya Biblia ndiyo yalimjulisha hilo, baada ya muda walitoka utumwani kama Neno la MUNGU lilivyosema.
Hata wewe kwa kulisoma Neno la MUNGU unaweza ukajua mpango wa MUNGU na nini cha kufanya ili ufanikiwe katika jambo fulani maishani mwako.

3. Itakuwa ni rahisi sana wewe kuwajua wanaodanganya kuhusu Biblia.
1 Yohana 4:1 '' Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani.''
Waongo ni wengi sana, kama huna Neno thabiti la KRISTO rohoni mwako ulilojifunza wanaweza kukuteka hawa waongo kwa mafundisho yao. Nakuomba soma Neno la MUNGU kwa faida yako mwenyewe.

4. Utagundua kiini cha Biblia kwamba ni ukombozi wa MUNGU kwa mwanadamu.
Yohana 3:16-18 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.'
Kiini cha Biblia ni Wokovu wa MUNGU kwa wanadamu na wokovu huo uko pekee katika KRISTO YESU.
Usipoielewa Biblia utaweka msingi katika mambo ambayo hayakupeleki uzima wa milele.
Wapo walioweka msingi wao kwa Mariamu, wengine msingi wao ni sabato ya kiyahudi, wengine msingi wao ni kwa Musa, Wengine msingi wao ni kwa Eliya, Wengine Msingi wao ni kwa Nabii ajaye(asiyejulikana mbinguni), Wengine msingi wao ni kwenye mawe au sanamu. Lakini ukiisoma Biblia utagundua kwamba msingi pekee wa Wokovu kwa Mwanadamu ni YESU KRISTO, Misingi mingine yote ni mpango wa shetani kuwakosesha wanadamu uzima wa milele.
Biblia inasema '' Maana msingi mwingine(Wa wokovu kwa mwanadamu) hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, YESU KRISTO.-1 Kor 3:11''
 Biblia inawaita wengine wote ni kama wezi tu na wanyang'ani maana hawana msaada hata mmoja kwa mwanadamu kwa ajili ya uzima wake wa milele. Bwana YESU anasema
 ''Wote walionitangulia ni wevi na wanyang'anyi; lakini kondoo hawakuwasikia. Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.-Yohana 10:8-9 ''
Biblia inaweka muhuri wa kimbingu juu ya hilo kwa kusema kwamba ''Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya KRISTO.  Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe. Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.-Wagalatia 1:7-9''
Kulisoma Neno la MUNGU kutakufanya uuelewe mpango wa MUNGU wa uzima wa milele.

5. Hutashitushwa na maneno mengi ambayo watu huyatamka kwa watu na kusema ni Biblia inasema.
 Yuda 1:17-21 ''Bali ninyi, wapenzi, yakumbukeni maneno yaliyonenwa zamani na mitume wa Bwana wetu YESU KRISTO,
 ya kwamba waliwaambia ya kuwa, Wakati wa mwisho watakuwako watu wenye kudhihaki, wakizifuata tamaa zao wenyewe za upotevu. Watu hao ndio waletao matengano, watu wa dunia hii tu, wasio na ROHO. Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU, jilindeni katika upendo wa MUNGU, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu YESU KRISTO, hata mpate uzima wa milele.'
'

 ''yakumbukeni maneno yaliyonenwa zamani na mitume wa Bwana wetu YESU KRISTO''=Hayo maneno yaliyosemwa na mitume utayapata kwa kuisoma Biblia.
''Wakati wa mwisho watakuwako watu wenye kudhihaki''= Hawa ndio wanaopotoa Biblia, utawajua kwa kujifunza Neno la MUNGU.
 

 7. Ukisoma Biblia katika kusudi la MUNGU utapata cha kuwafundisha wengine.
2 Timotheo 2:14 '' Uwakumbushe mambo hayo, ukiwaonya machoni pa MUNGU , wasiwe na mashindano ya maneno, ambayo hayana faida, bali huwaharibu wasikiao.''
Timotheo asingefundisha Neno la MUNGU kama hajalisoma na kujifunza hilo Neno la MUNGU.
Hata wewe inakupasa kulisoma Neno la MUNGU ndipo utaweza kufundisha wengine Neno la MUNGU.

6. Utajua kwanini wewe unaishi duniani.
 '' Afadhali, heri walisikiao neno la MUNGU na kulishika.-Luka 11:28 ''
Ukilisoma Neno la MUNGU litakufanya ujitambue kwamba, wewe ni nani(ni Mteule au ni mdhambi), ufanyeje ili umpendeze MUNGU(Utubu au uongeze maombi n.k)
Biblia kulisoma Neno la MUNGU na kujifunza huwezi kujitambua.
 Zaburi 119:72 ''Sheria ya kinywa chako(Neno la MUNGU) ni njema kwangu, Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.''

7. Utaujua Wokovu na mwenye Wokovu ambaye ni Bwana YESU.
Waefeso 4:12-14 '' kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa KRISTO ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na KUMFAHAMU SANA  MWANA wa MUNGU, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa KRISTO; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. ''

Hii inajieleza vyema kabisa juu ya kuujua wokovu na mleta Wokovu.

Kuna baadhi ya watu husema wanashindwa kuielewa Biblia, ukweli ni hivyi  mtu ambaye anaona anashindwa kuielewa biblia kutokana na baadhi ya misamiati migumu,kwanza kabisa unapoanza kusoma neno la MUNGU lazima umuombe MUNGU na umwambie ROHO MTAKATIFU  akuongoze katika kulisoma neno la MUNGU maana yeye ndiye mwalimu pekee anayeweza kukufafanulia Kwa mapana zaidi ya upeo wa mwanadamu, pia ukiona haujaelewa bado waweza rudia hicho kipengele zaidi ya Mara tatu au nne utashangaa unapata ufahamu wa ajabu sana kuhusu neno la MUNGU, pia Kwa msaada zaidI waweza nunua Biblia aina ya ITIFAKI, hiyo imefafanua sana baadhi ya maneno magumu yaliyoandikwa kwenye Biblia,au kamusi ya Biblia pia inaweza kukusaidia Kwa viwango vikubwa sana wewe uliye na kiu ya kujifunza maneno ya MUNGU.
ni vizuri sana kusoma Biblia na kujua kusudi lako la kuja duniani mana MUNGU alikuwa na kusudi na mpango kwa mwanadamuu,
Usisome Biblia kama gazeti.
Unaweza kulisoma sana Neno la MUNGU lakini kama hulitendei kazi haitakusaidia lolote.
Nakuomba usiache kulisoma lakini pia nakuomba fanyia kazi hilo neno la KRISTO ulilolisoma.

Kumbuka ,Tumeokolewa na Bwana YESU kwa imani.
Tunapona magonjwa kwa maombi ya imani kupitia jina la YESU.
Tunapatanishwa na MUNGU kwa imani.
Tunapata baraka za MUNGU kwa imani.
Tumesamehewa na MUNGU kwa imani.
Tunatakaswa na damu ya YESU kwa imani.
Tunahesabiwa haki na MUNGU kwa imani.
Tunamshinda shetani kwa imani katika kupitia jina la YESU.
Tunawashinda wachawi na wakuu wa giza kwa imani.
Tumekombolewa kwa damu ya YESU kwa imani.
Imani yetu ni ile tu ambayo chanzo chake ni kulisikia neno la KRISTO na kulitii.

Warimi 10:17 "Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO"
Lazima uhusike na Neno la MUNGU sana
Imani yetu huambatana na matendo mema na matakatifu katika KRISTO YESU Bwana wetu.
Ni imani hii pekee inayoweza kuushinda uoga ndani yetu.
Ni imani hii pekee inayompendeza MUNGU Muumba wetu.
Ndugu, nakuomba ishi kwa imani katika KRISTO YESU huku ukimtii yeye siku zote na ukijitenga na uovu wote.
Imani sahihi ikiambatanishwa na maombi sahihi katika jina la YESU huleta majibu ya haraka na mapema, huleta majibu sahihi.
 Na ishi kwa imani na utakatifu katika KRISTO YESU siku zote.

Unaweza ukaielewa vizuri Biblia ikiwa tu ROHO wa MUNGU atakuangazia.
Watu wengi sana wamekuwa tu kazi yao kubishana juu ya maandiko Fulani ya Biblia.
Wengi hushindwa kuielewa Biblia kwa sababu wanasoma maandiko huku wakitaka Biblia iwe jinsi wao wanavyopendelea.

Inawezekana wewe ni mmoja wa watu wanaoisoma Biblia huku wakiwa na misimamo yao binafsi au msimamo wa tabaka Fulani, hivyo huwezi kuielewa Biblia.
Inawezekana wewe ni mmoja wa wanaoisoma Biblia kama kitabu na sio kama Neno la MUNGU, huwezi ukaielewa Biblia.

Ukitaka uielewe Biblia kwa wakati huu unahitaji kuweka mbali mambo haya.
1. Udini.
Udini utakufanya uhusike na baadhi tu ya maandiko na sio kuhusika na lile kusudi la MUNGU la injili ya KRISTO kwa wakati huu.


2. Udhehebu.
Udhehebu utakufanya uhusike ndani ya Biblia na kile tu ambacho dhehebu lako linataka au kuelekeza.


3. Misimamo binafsi au misimamo ya tabaka lako.
Misimamo Binafsi itamfanya ROHO MTAKATIFU asikusaidie kuielewa Biblia.


4. Dhambi.
Dhambi ni uasi kwa MUNGU, dhambi ni kikwazo cha kila jambo la ki MUNGU.
Dhambi hufungulia mlango wa shetani kukutumia wewe na kukuelekeza kinyume kabisa na maagizo ya ROHO MTAKATIFU.


5. Mazoelea ya Neno la MUNGU.
Mazoelea yanaweza kukujengea tabia ya kupuuzia ujumbe wa Neno la MUNGU.


6. Akili na elimu za kidunia.
Kumcha MUNGU ndio chanzo cha maarifa sahihi. Kama humchi MUNGU ujue maarifa yako shetani atayatumia kukuhamisha kwenye kusudi la MUNGU. Ukitaka kuielewa Biblia unahitaji akili ya ki MUNGU na sio akili za darasani.


7. Kumpinga YESU KRISTO.
Kumpinga YESU ni kumpinga MUNGU.
Kulipinga Neno la KRISTO ni kumpinga ROHO MTAKATIFU, na KRISTO ndio Neno juu ya Neno la MUNGU.
Roho ya MpingaKristo ikikuvaa hutaielewa Biblia katika kusudi la MUNGU, utakalia kubishana asubuhi hadi usiku na bado huelewi.
Unamhitaji sana ROHO MTAKATIFU ili uielewe Biblia takatifu.


Bwana YESU anasema  '' Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba(MUNGU) kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana. Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. LIKUMBUKENI LILE NENO  nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu. '' Yohana 15:16-20 '' 

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments