KWANINI KITABU CHA KUMBUKUMBU LA TORATI?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

 Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo ninazungumzia Kitabu cha Kumbukumbu la torati.
Tunafahamu kwamba kitabu cha Mwanzo kinazungmzia historia ya uumbaji pamoja na matukio ya awali ya wanadamu na jinsi  walivyokuwa na uhusiano na Muumba wao, pia Kitabu cha Mwanzo kinazungumzia jinsi wanadamu walivyoanza kukengeuka na kufuata uovu badala ya utakatifu. Lakini pia kitabu hicho kinazungumzia Mwanzo wa taifa la Israeli na jinsi walivyokwenda Misri.
Tunafahamu kuhusu kitabu cha Kutoka kwamba kinazungumzia Waisraeli kutoka utumwani Misri na katika Kutoka huko Misri walipewa Sheria na taratibu za kutembea nazo  ili mataifa wengine  wajifunze kwa Israeli  jinsi ya Kumcha MUNGU.
Kitabu cha Mambo ya walawi kinazungumzia ukuhani na jinsi ya kufanya mapenzi ya MUNGU.
Kitabu cha Hesabu kinaendeleza safari ya Waisraeli ya Miaka 40 Jangwani kikianza na kuhesabiwa kwao idadi kulingana na kila kabila.
Baada ya kitabu cha Hesabu kinafuata Kitabu cha Kumbukumbu la torati.
Kitabu hiki kimeandikwa na Musa kama ilivyo kwa vitabu vinne vya kwanza vya Biblia, lakini Mwishoni mwa kitabu hicho  hajaandika Musa bali wateule wa MUNGU walioishi na Musa katika kipindi chake cha Mwisho cha uhai Duniani, inawezekana ni Joshua au wengine waliofuata.
 Musa katika kitabu cha Kumbukumbu la torati alikuwa anaongea na kizazi kipya, maana waliotoka Misri wakiwa watu wazima wakati huu walikuwa wameshakufa(Kwa kosa la kuabudu ndama, wakati Musa amepanda Mlimani kukutana na MUNGU',Angalia Kutoka 32:1........)
 Wakati huu watu waliotoka Misri wakiwa watu wazima walikuwa ni Musa, Joshua na Kalebu tu. Kipindi hiki wallikuwa jirani na Mto Yordani ili wakivuka wanafika Kaanani(Hata Musa hakuvuka Yordani kwa kosa la kutokumwamini MUNGU. angalia Hesabu 20:12)
Musa anaanza kwa kusema hivyo '' BWANA, Mungu wetu, alituambia huko Horebu, akasema, Mlivyokaa katika mlima huu vyatosha;  geukeni mshike safari yenu mwende nchi ya milima ya Waamori, na mahali pote palipo karibu ya hapo, katika hiyo Araba, na nchi ya vilima-vilima, na huko Shefela, na Negebu, na pwani-pwani, nchi ya Wakanaani, na Lebanoni, mpaka mto huo mkubwa, mto wa Frati.  Angalieni, nimewawekea nchi mbele yenu, ingieni mkaimiliki nchi BWANA aliyowaapia baba zenu, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kwamba atawapa na uzao wao baada yao. Nami wakati ule niliwaambia, nikasema, Siwezi mimi mwenyewe kuwachukua peke yangu. BWANA, Mungu wenu, amewafanya kuwa wengi, nanyi, angalieni, mmekuwa leo mfano wa nyota za mbinguni kwa wingi. BWANA, Mungu wa baba zenu, na awafanye kuwa wengi mara elfu kuliko mlivyo, na kuwabarikia, kama alivyowaahidi.-Hesabu 1:6-11''
Huu sasa ulikuwa ni mwaka wa 40 tangu Watoke Misri
 Kumb 1:3 '' Ikawa mwaka wa arobaini, mwezi wa kumi na moja, siku ya kwanza ya mwezi, Musa akawaambia wana wa Israeli kama yote aliyopewa na BWANA ya kuwaamuru; ''
 Kwanini kinaitwa kitabu cha Kumbukumbu la torati?
Ni kwa sababu kinazungumzia mambo yote pamoja ya tangu Waisraeli wanatoka Misri hadi mto Yordani, ili wakivuka wanaangia nchi yao.
Kitabu cha Kumbukumbu la torati kinarudia  yaliyofanyika  kutokea kitabu cha Kutoka, Mambo ya Walawi na Hesabu.
Maana yake yanayozungumzwa katika kitabu cha kumbukumbu la torati yana chanzo chake kutoka vitabu vitatu vya kabla yake na mengine ni ufunuo wa wakati huo huo.
Ujumbe huu mimi Peter nilipewa na ROHO wa MUNGU kama ufunuo  na sasa ndio nataka ujue kiini cha somo la leo.
 Tunafahamu kwamba Waisraeli zaidi ya Milioni 2 walitoka Misri lakini watu wazima waliotoka Misri hadi kuingia  Kaanani  walikuwa wawili tu yaani Joshua na Kalebu.
Safari ya Wana wa Isareli kutoka Misri kwenda Kaanani inafananishwa na safari ya wateule wa MUNGU waliookolewa na Bwana YESU ya kutoka duniani kwenda uzima wa milele.
Waisraeli waiotoka Misri hadi Kaanani walikuwa wawili tu, naamini Wateule wa MUNGU watakaofika uzima wa milele ni wengi sana lakini ni muhimu sana tukajifunza vyanzo vilivyosababisha Waisraeli waliokoka kutoka Misri wakashindwa kufika nchi ya ahadi.
Andika kwa makini katika moyo wako mambo haya ili wewe katika safari ya uzima wa milele usiishie njiani.
Kuna mambo mengi yaliyosababisha waisraeli wasifike Kaanani isipokuwa hao wawili.
Biblia imeyaweka vizuri sana mambo hayo yaliyosababisha waisraeli japokuwa wameokoka kama wewe lakini hawakufika kaanani.
Biblia inatujulisha  katika 1 Kor 10:1-12 mambo yaliyosababisha Waisraeli wasifike Kaanani, mambo kama hayo yanaweza yakasababisha baadhi ya wateule wa MUNGU wasiingie uzima wa milele. Jifunze kwa makosa haya ili usiyatenda katika maisha yako ya safari ya kwenda uzima wa milele.

SABABU ZILIZOSABABISHA WAISRAELI WALIOTOKA MISRI WASIFIKE KAANANI.

1. Kutamani mabaya.
1 Kor 10:6 '' Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale(Waisraeli) nao walivyotamani.''
Ndugu usikubali kutamani mabaya ya zamani kabla hujaokoka, ishi maisha matakatifu sasa na usikubali kujihusisha na dhambi za zamani kabla hujampokea YESU kama Mwokozi wako.

2. Kuabudu Sanamu.
1 Kor 10:7 '' Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa;''
Ndugu usiabudu sanamu, kuiheshimu wala kuisujudia.
 
3. Uasherati na uzinzi.
1 Kor 10:8 ''Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu.''
Kufanya uzinzi na uasherati huko ni kuitafuta jehanamu, ndugu usikubali kufanya dhambi hiyo mbaya.
 

4. Kumjaribu MUNGU.
1 Kor 10:9 '' Wala tusimjaribu BWANA, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka.''
Ndugu usikubali kumjaribu MUNGU bali mtii na kutii Neno lake la Wokovu wa YESU KRISTO.

5. Kunung'unika
1 Kor 10:10 '' Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu.''
Manung'uniko ni silaha ya shetani kuwatesa Kanisa,  na Manung'uniko ni dhambi kwa MUNGU hivyo ndugu kataa kunung'unika katika maisha yako ya Wokovu.

 Kumbuka Kaanani ya Waisraeli ni mfano wa uzima wa milele kwetu hivyo inapasa kuishi maisha matakatifu siku zote huku tukikataa mambo 5 hapo juu yaliyowaponza waisraeli.
Kitabu cha Kumbukumbu la torati kiliandikwa kipindi ambacho waasi walikuwa wameshakufa kwa sababu ya uovu wao na dhambi zao.
Musa katika kumbukumbu la torati alikuwa anawasaidia waisraeli  abao wakati maagizo ya kwanza yanatolewa walikuwa watoto wadogo na wengine walikuwa hawajazaliwa.
Sisi mambo ya Torati yanatusaidia nini?
1 Kor 10:11-12 '' Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.''
 Hatuko chini ya torati leo lakini ukiisoma Biblia kwa jinsi ya KRISTO utajifunza mambo mengi muhimu sana katika Wokovu wako leo.
Ninafurahishwa na Neno la Mwisho la Musa katika Biblia ambalo linatoka Kumb 33:29 Kwamba '' U heri, Israeli. Ni nani aliye kama wewe, taifa lililookolewa na BWANA! Ndiye ngao ya msaada wako, Na upanga wa utukufu wako; Na adui zako watajitiisha chini yako, Nawe utapakanyaga mahali pao pa juu.''
Kumbuka Hajawahi kutokea nabii kama Musa katika Israeli na manabii wote wa Biblia walitokea Israeli.
Kumb 34:10 ''Wala hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye BWANA alimjua uso kwa uso;''

Nimelipenda Neno la Musa la Mwisho. Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.

Comments