MKRISTO MWENYE MOYO WA UKUHANI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu!
Karibu tujifunze Neno la MUNGU. Je una moyo wa ukuhani?
Neno "Kuhani" Kibiblia lina maana zifuatazo.
Kuhani ni mtu anayezingatia mambo ya kiroho.
Kuhani ni mtu mtakatifu aliyetengwa ili kufanya kazi ya MUNGU.
Kuhani ni kiongozi wa taratibu za ibada.
Kuhani ni kiongozi anayewaongoza watu katika mambo yanayomhusu MUNGU.
Katika agano la kale ukuhani ulihusu kabila moja tu kati ya makabila 12 ya Israel yaani kabila la Lawi, lakini katika agano jipya wote waliookolewa na Bwana YESU ni Makuhani.

Ufunuo 5:9-10  '' Nao waimba wimbo mpya wakisema, Wastahili wewe kukitwaa hicho kitabu na kuzifungua muhuri zake; kwa kuwa ulichinjwa, ukamnunulia MUNGU kwa damu yako watu wa kila kabila na lugha na jamaa na taifa, ukawafanya kuwa ufalme na MAKUHANI  kwa MUNGU wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.''
Kumbe wale waliookoka ni makuhani wa MUNGU, Kumbe wateule wa KRISTO wanaoishi maisha matakatifu ni Makuhani wa MUNGU.
Kumbe wewe uliyeokoka ni kuhani wa MUNGU aliye hai.
Na tena katika agano jipya ambalo mimi na wewe tunaishi ni kwamba tuliookoka ni makuhani wa kifalme

1 Petro 2:9-10 ''Bali ninyi ni mzao mteule, UKUHANI WA KIFALME, taifa takatifu, watu wa milki ya MUNGU, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la MUNGU; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.''
Ufalme unawakilisha mamlaka na ukuhani unawakiliza utumishi.
Katika agano jipya Kuhani ni mteule wa KRISTO.
Kwa sababu ya mamlaka ya jina la YESU basi Kuhani ni mwenye uwezo wa kulitoa Neno katika ulimwengu wa roho na kulileta katika ulimwengu wa mwili.
Kitu kilicho katika ulimwengu wa roho kukipata ni lazima uwe rohoni na sio mwilini.
Wewe Mteule wa KRISTO Jitambue sasa kwamba wewe ni Kuhani wa MUNGU aliye hai

Ufunuo 1:5-6 ''tena zitokazo kwa YESU KRISTO, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na MAKUHANI kwa MUNGU, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.'
  Katika kujua juu ya ukuhani ni muhimu pia kutambua kwamba kuna makunani yaani wanaofanyia kazi katika ofisi ya ukuhani na sisi wengine ni makuhani kwa sababu tuna moyo wa ukuhani.
Wanaofanyia kazi ofisi ya ukuhani ni wachungaji au maaskofu n.k ambao ni viongozi wa kanisa tawi, huduma na waangalizi lakini wateule wote sisi lazima tuwe na moyo wa ukuhani maana ndivyo Biblia inatuzungumzia wateule wa KRISTO katika maandiko hapo juu.
Je wewe una moyo wa ukuhani?
Kama huna moyo wa ukuhani hakikisha unakuwa nao maana wateule wote wa MUNGU katika KRISTO YESU wanatakiwa kuwa na moyo wa ukuhani.
Inawezekana unajiuliza sasa nitajuaje kama Nina moyo wa ukuhani?
Wala usihofu maana Niko hapa kukujulisha juu ya hilo leo.
Wenye moyo wa ukuhani hufanya yafuatayo.
Jipime ili kama hutimizi katika wajibu wako kama Kuhani basi kuanzia Leo utimize.

Mteule mwenye moyo wa ukuhani hufanya kazi zote za ukuhani.
Na kazi hizo ndizo zitaonyesha kama wewe una moyo wa ukuhani.


Kazi ya Mteule wa KRISTO aliye na moyo wa ukuhani.

1.Kutunza mahali patakatifu.
 
Hesabu 3:38 ''
Na hao watakaopanga mbele ya maskani upande wa mashariki, mbele ya hema ya kukutania upande wa kuelekea maawio ya jua, watakuwa hawa, Musa na Haruni na wanawe, wenye kulinda ulinzi wa mahali patakatifu, yaani, huo ulinzi wa wana wa Israeli; na mgeni atakayekaribia atauawa.'
Kazi mojawapo ya mtu mwenye moyo wa ukuhani ni kutunza mahali patakatifu.
Katika andiko tunaona Musa, haruni na watoto wa Haruni ambao wote ni wa kabila la lawi  na hao ndio walikabidhiwa kazi ya ukuhani. Katika agano jipya Waliookolewa na KRISTO wote ni makuhani kwa MUNGU hivyo ndugu hakikisha una moyo wa ukuhani.
Tunza mahali patakatifu, tunza kanisa la MUNGU, tunza moyo wako, Tunza utakatifu na tunza mali za kanisa.
Huyo ndio Mteule mwenye moyo wa ukuhani.

2. Kuhakikisha taa haizimiki daima katika hema.
 
Kutoka 27:20-21 ''
Nawe waamuru wana wa Israeli wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya nuru, ili kufanya ile taa kuwaka daima. Ndani ya ile hema ya kukutania, nje ya hilo pazia, lililo mbele ya huo ushuhuda, Haruni na wanawe wataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele ya BWANA; itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyao vyote kwa ajili ya wana wa Israeli.''
Asubuhi hata jioni makuhani walihakikisha taa haizimiki kwenye hema ya kukutania.
Hata wewe Mteule wa KRISTO mwenye moyo wa ukuhani hakikisha taa haizimika katika Kanisa la MUNGU na katika maisha yako.
Kumbuka Neno la MUNGU ni taa ya kutuongoza.
Zaburi 119:105 ''
Neno lako(MUNGU) ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.''
Hivyo wewe mteule mwenye moyo wa ukuhani unatakiwa kuhakikisha Neno la MUNGU haliondoki maishani mwako na Kanisani kwako.
Huyo ndiye Mteule mwenye moyo wa ukuhani.

3. Kutoa dhabihu.
 
Walawi 1:2-3 ''
Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtu wa kwenu atakapomtolea BWANA matoleo, mtatoa matoleo yenu katika wanyama wa mifugo, katika ng'ombe na katika kondoo. Matoleo yake kwamba ni sadaka ya kuteketezwa ya ng'ombe, atatoa ng'ombe mume mkamilifu; ataleta mlangoni pa hema ya kukutania, ili akubaliwe mbele ya BWANA.''
Mteule  yeyote mwenye moyo wa ukuhani ni lazima awe na moyo wa utoaji vilevile.
Utoaji wa kwanza unaanzia hapa
Warumi 12:1 ''Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake MUNGU, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza MUNGU, ndiyo ibada yenu yenye maana.''
Kisha utoaji wa zaka na  sadaka, huyo ndiye mteule mwenye moyo wa ukuhani.
Lazima uwe mtoaji katika ujenzi wa kanisa au huduma, lazima uwe ni mmoja wa watu wanaotoa mali zao ili huduma ya injili iende mbele.
Lazima ujitoe katika kazi ya MUNGU, Lazima ujitoe dhabihu ili kushuhudia na kupeleka injili N.K
Huyo ndiye mteule mwenye moyo wa ukuhani.

4. Kuwapatanisha watu na MUNGU.
 
Hesabu 15:25 ''
Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya mkutano wote wa wana wa Israeli, nao watasamehewa; maana, lilikuwa ni kosa, nao wamekwisha leta matoleo yao, sadaka iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto, na sadaka yao ya dhambi pia wameileta mbele za BWANA kwa ajili ya kosa lao;''
Tunaona kabisa wakuhani wakiwapatanisha watu kwa MUNGU.
Katika wakati wetu, MUNGU ametupa huduma ya upatanisho.
2 kor 5:18 '' Lakini vyote pia vyatokana na MUNGU, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa KRISTO, naye alitupa huduma ya upatanisho;'' 
Huduma ya upatanisho ndio huduma ya Kanisa la MUNGU duniani.
Wewe uliyeokoka, ukimuongoza sala ya toba mtu uliyemshuhudia habari njema za ufalme wa MUNGU hakika mtu huyo anasamehewa na MUNGU na jina lake linaandikwa katika kitabu cha uzima, kinachofuata kwa mtu huyo ni kujiunga na kanisa na kuanza kujifunza Neno la MUNGU huku akiishi maisha matakatifu.
Kuwahubiria watu ili waokoke ni kufanya huduma ya upatanisho, yaani unawapatanisha watu na MUNGU kama watamkiri KRISTO na kuacha dhambi zao.
Sio kazi ya wachungaji tu au maaskofu kuwaongoza watu sala ya toba na kuwasaidia kuishi maisha matakatifu katika KRISTO, hiyo ni kazi ya kila mteule wa MUNGU anayeishi maisha matakatifu katika KRISTO. Lakini wenye moyo wa ukuhani tu ndio hufanya huduma hiyo ya upatanisho.
Ndugu, mimi sijui kama wewe una moyo wa ukuhani, ila nakuomba jipime katika mambo haya saba ndani ya somo hili yanayomthibitisha mtu kuwa ni Mteule wa KRISTO mwenye moyo wa ukuhani.
 

5. Kufundisha Neno la MUNGU.

Walawi 10:10-11 ''
kisha, mpate kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote, na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi; tena mpate kuwafundisha wana wa Israeli amri hizi zote ambazo BWANA amewaambia kwa mkono wa Musa.'
Makuhani waliamuriwa na MUNGU kuwafundisha wana wa Israeli Neno la MUNGU.
Kumb 24:8b ''kufanya mfano wa yote watakayowafundisha makuhani Walawi; tunzeni kwa kuyafanya vile vile kama nilivyowaamuru wao. ''
Moja ya makosa ya wateule wa MUNGU wengi ni kutokujua maana ya wao kujifunza Neno la MUNGU kanisani.
Tunafundishwa Neno la MUNGU kanisani ili Neno hilo tukawafundishe watu mitaani ili na wao wampokee Bwana YESU awe Mwokozi wao. Wateule wengi akijifunza Neno la MUNGU anataka apewe madhabahu kufundisha na kwa udhaifu huo wapo watu hugombania madhabahu Kanisani na wengine huhama makanisa kwa sababu tu wamekosa nafasi ya kusimama madhabahuni ili kuhubiri.
Ndugu yangu, Lengo la MUNGU ni kwamba wewe ufundishwe Neno la MUNGU na Mchungaji wako na hilo Neno wewe ukalifundishe mitaani au kazini kwako ili watu wa huko waokoke. Kama MUNGU atakupa mwito binafsi wa kwenda kufungua huduma au kwenda kuhubiri sehemu utaenda lakini awe ni MUNGU amekuambia, au kanisa limekutuma au kwa sababu ya kazi umehamia eneo hilo. Lakini kama upo kanisani basi tambua kwamba zipo madhabahuni nyingi sana zinakuhitaji  wewe uhubiri, kuna magereza, hospital, kwenye daladala, sokoni, kazini kwako na popote ulipo unaweza ukahubiri. Sio lazima uhubiri kwa sauti kubwa bali unaweza hata ukamshuhudia mtu mmoja kwa taratibu kazini na MUNGU akimpa Neema unamuongoza sala ya toba na kumwelekeza Kanisani, hapo unakuwa hakika umefanya kazi ya MUNGU.
Fundisha watoto wako, fundisha wazazi wako na ndugu zako na majirani zako na marafiki zako n.k
Huyo ndiye Mteule wa KRISTO mwenye moyo wa ukuhani.
 
6. Kutunza moto wa madhabahu.
 
Walawi 6:12-13 ''
Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake. Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike.''
Moto wa madhabahu ni nguvu ya madhabahu.
Biblia hapo juu inasema kwamba moto wa madhabahu hautakiwi kuzimika.
Moto wa madhabahu unachochewa kwa maombi.
Ni lazima uwe muombaji na wakati mwingine shiriki maombi ya kufunga ya kikanisa.
Kuna watu akifunga basi ujue anaombea mambo yake mwenyewe.
Akiambiwa afunge kwa ajili ya kuombea kanisa anaweza akatoa udhuru, ni mbaya.
Kanisa la MUNGU wote ni lazima tuwe waombaji.
Kufanya maombi ndio kuchochea kuni kwenye moto, ndio kuongeza moto au nguvu ya madhabahu husika.
Kuna baadhi ya makanisa ukienda kuabudu utakutana na nguvu kubwa ya MUNGU na kuna makanisa mengine ukienda ni pakavu sana.
Kwanini kutofautiane wakati MUNGU ni yule mmoja?
Ni kwa sababu kanisa moja ni waombaji na lingine wamelala.
Waombaji huchochea moto wa madhabahu.
Moto wa Madhabahu hutunzwa pia na vitu vifuatavyo pamoja na  Maombi.
a. Utakatifu.
b. Kujitoa kwa kazi ya MUNGU.
c. Umoja wa kweli.
d. Ushirika mzuri na ROHO MTAKATIFU.
e. Utoaji sahihi wa matoleo
f. Kutembea kwenye kusudi la MUNGU.
Ndugu unatakiwa ni wewe uwe hivyo.
Huyo ndiye Mteule wa KRISTO mwenye moyo wa ukuhani.

7. Kuwa mwaminifu.

1 Samweli 2:35 ''
Nami nitajiinulia kuhani mwaminifu, atakayefanya sawasawa na mambo yote niliyo nayo katika moyo wangu, na katika nia yangu; nami nitamjengea nyumba iliyo imara; naye atakwenda mbele ya masihi wangu milele. ''

Uaminifu ndio kipimo cha mteule wa kweli wa KRISTO.
Uaminifu ni vazi la wateule wa MUNGU.
Kila mteule wa MUNGU inampasa kuwa mwaminifu kwa MUNGU, kwa kanisa la kwa wanadamu.
Labda nikuulize ndugu, unampenda YESU wakati wote Au unampenda YESU wakati tu uko katika matatizo?
Unampenda YESU wakati wote au unampenda YESU wakati tu shetani amekupiga?
Unampenda YESU wakati wote au unampenda YESU wakati tu wachawi wamekufilisi?
Unampenda YESU wakati wote au unampenda YESU wakati tu unaumwa na hauna msaada?
Unampenda YESU wakati wote au unampenda YESU wakati tu umeishiwa?
Unampenda YESU wakati wote au unampenda YESU wakati tu ndoa yako ina mgogoro?
Unampenda YESU wakati wote au unampenda YESU wakati tu umeachwa na mchumba?
Unampenda YESU wakati wote au unampenda YESU wakati tu umefeli kimaisha?
Hebu jiulize na kujihoji ndugu kwamba unampenda YESU wakati gani.
Wengi humpenda YESU KRISTO wakati tu wa matatizo.
Ndugu naomba usiwe wewe mtu wa namna hiyo, Bali wewe mpende Bwana YESU wakati wote wa maisha yako.
Kithibitisho cha kwamba unampenda YESU ni pale tu unapoishi maisha matakatifu aliyokuagiza yeye.
Yeye Bwana YESU anasema katika Yohana 14:15 kwamba " Mkinipenda, mtazishika amri zangu."
Amri za KRISTO ni Neno la KRISTO, ni utakatifu.
Biblia inasema 1 Petro 1:15. " bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"

Ndugu hakikisha unampenda YESU KRISTO wakati wote kwa kuishi tu maisha matakatifu ya wokovu wake.
Huyo ndiye Mteule wa MUNGU aliye na moyo wa ukuhani.
 
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.

Comments