MUNGU ANAWEZA AKAKUMBUKA SADAKA ZAKO NA KUKUTENDEA MEMA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
MUNGU anaweza kukumbuka sadaka zako na kukutendea mema.
Zaburi 20:3-4 " Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote."

 
Sadaka inabeba ushindi mkubwa sana kama imetoka katika moyo wa upendo.
Kuna kazi nyingi za sadaka kiroho hivyo utoaji wa sadaka ni muhimu sana kwa wateule wa MUNGU.
Biblia inasema kwamba MUNGU akikumbuka sadaka zako anaweza kukutendea mema, lakini uwe umetoa sadaka kwa Imani na kwa moyo wa kupenda.
Sadaka yako inaweza ikaongea mema kwa MUNGU ili utendewe.

Kwanini MUNGU akumbuke  sadaka zako na kukutendea mema?
MUNGU atakumbuka sadaka yako kwa sababu sadaka unazotoa kwake huwa zinatengeneza agano(Patano) na MUNGU.
Zaburi 50:5 " Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu."

Sadaka yako inaweza ikatengeneza agano la ushindi kwako.
Sadaka katika jina la YESU KRISTO hutengeneza agano.
Pia sadaka huenda kwenye hazina yako mbinguni.

Mathayo 6:19-21 '' Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.''

Sadaka inaweza ikawa sababisho la kubarikiwa kwako na MUNGU.
Nakuomba usitegee kutoa sadaka.
Nakuomba inenee mema sadaka yako na toa kwa Imani.
Ukisikia msukumo juu ya kutoa sadaka toa maana ushindi wake ni mkubwa sana.
Inawezekana kuna mtu alikuendea kwa waganga na huko akatoa sadaka na kuweka maagano ya kukufunga.
Wewe kwa ufunuo wa ROHO wa MUNGU unaweza ukatoa sadaka yako kwa MUNGU aliye hai na hiyo ikanena kinyume na maagano ya kipepo ya kwa mganga hivyo wakashangaa kuona ukiendelea kushinda na hauzuiliki kwa sababu tu umemtolea MUNGU aliye hai na kutengeneza agano na damu ya YESU KRISTO linalovunja maagano ya kipepo yote.

Lakini ni muhimu sana kujua kwamba sio kila sadaka utoayo inaweza kutengeneza ukumbusho kwa MUNGU hata utendewe mema.
Kuna watu hutoa zawadi na sio sadaka.
Hakikisha unatoa sadaka na sio zawadi(Nimewahi kufafanua katika somo lingine linaloitwa TOFAUTI YA SADAKA NA ZAWADI).
Pia toa katika uwepo wa MUNGU na toa katika madhabahu hai ya MUNGU au kwa mtumishi sahihi wa Bwana YESU.
Toa kwa watu wanaostahili na sio kwa wasio stahili.
Sadaka yako sahihi ni lazima iambatane na maombi sahihi ndipo italeta matokeo sahihi yaliyotokana na ahadi ya MUNGU kwako.
Hivyo hakikisha sadaka yako inakuwa ukumbusho mbele za MUNGU, Sadaka yako sahihi ikiambatana na maombi sahihi kutoka kwa mtumishi sahihi hakika ipo siku utaona matokeo sahihi ya utoaji wako kwa MUNGU.
Sadaka za Kornelio zilikuwa ukumbusho kwa MUNGU, Jifunze kitu hapa.
Matendo 10:1-4 ''Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,  mtu mtauwa, mchaji wa MUNGU, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba MUNGU daima.  Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa MUNGU, akimjia na kumwambia, Kornelio! Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za MUNGU.''
Kupitia Kornelio tunajifunza kwamba;
1. Sadaka na maombi yake viliambatana na kuwa ukumbusho kwa MUNGU 
Malaika alipomtokea Kornelio alimwambia mambo haya ''Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za MUNGU.''
Wengi wanatoa bila matoleo hayo kuombewa, wengi pia kuomba sana bila kuwa watoaji, tofauti ya wao na Kornelio kuhusu sadaka kuwa ukumbusho kwa MUNGU na kuleta matokeo sahihi ya baraka za MUNGU kulingana na utoaji ni kwamba sadaka za Kornelio ziliambatana na maombi.
 
2. Kornelio hakuwa tu mtoaji wa matoleo bali alikuwa ''Mcha MUNGU mtoaji''
Wengi leo ni watoaji lakini sio wacha MUNGU.
Wengine wengi leo ni wacha MUNGU lakini sio watoaji, Mambo hayao ndiyo yanayoweza kukutenganisha wewe na Kornelio kuhusu matokeo sahihi ya baraka za MUNGU kutokana na utoaji. Biblia imemzungumzia Kornelio ikisema ''Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,  mtu mtauwa, mchaji wa MUNGU'

3. Kornelio alikuwa anawapa watu sadaka nyingi na kumuomba MUNGU daima.
Inawezekana wewe unatoa sadaka kidogo ndio maana huoni mafanikio sahihi, inawezekana wewe wakati mwingine hutoi kabisa hata kama rohoni umejulishwa utoe.
Inawezekana wewe hutoa kidogo na huombi daima kama Kornelio.
Biblia inasema juu ya Kornelio kwamba ''naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba MUNGU daima  ''
 Hakutoa kidogo na wala hakuacha kuomba, naomba na wewe uwe mtu wa hivyo.
Aliwapa watu wanaostahili, hilo kumbuka siku zote maana kuna watu waliwahi kupeleka sadaka zao kwenye madhabahu ya kishetani na sadaka hiyo ikatengeneza vifungo kwao.
Kama Mtumishi Hamhubiri KRISTO YESU kwa usahihi huyo usimpe sadaka yako haya kama anakusisitiza na kukulazimisha utoe sadaka.
Kuna watumishi wengine madhabahuni  huwatisha watu na kuwawekea viwango vya sadaka tena kwa lazima huku wakikagua, huo sio utaratibu wa Kibiblia.
Kumbuka mizani halisi ya kiwango chako cha matoleo anacho MUNGU, Hivyo ukitoa vichache ni kwa hasara yako mwenyewe.
Lakini vichache vinapimwa na MUNGU na sio macho ya kibinadamu.
 Jifunze kwa hayo matatu ya Kornelio ndipo utafanikiwa.
 Kama unapata msukumo wa kumpa sadaka yako mtumishi fulani hakikisha unajilidhisha kama kweli ni Mtumishi wa KRISTO anayeishi maisha matakatifu na ana hofu ya MUNGU, Kisha timisha hicho ulichokusudia maana wakati mwingine jambo hilo kutokana na maombi ya mtumishu huyo sahihi wa MUNGU maisha yako yanaweza kubadilika hata ukamtukuza MUNGU kila siku.
Mama mmoja alikuwa ni tasa na yuko katika ndoa kwa miaka mingi bila mtoto lakini sadaka zake kwa mtumishi sahihi wa MUNGU zilisababisha apate uzao.
 2 Wafalme 4:16-17 ''Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa MUNGU, usiniambie mimi mjakazi wako uongo. Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia.''
Huyu mwanamke hata alipoambiwa na Mtumishi wa MUNGU kwamba mwaka unaofuata atapata mtoto katika ndoa yake, yeye hakuamini lakini kwa sababu ya matoleo aliyokuwa ameyafanya kwa watumishi wa MUNGU na ikapelekea Mtumishi Elisha kutamka hivyo katika Roho hakika yule mama alipata mtoto wa kiume hata kama hakuamini, utoaji una nguvu sana.
Utoaji wake ulikuwaje hata ukasababisha kubarikiwa uzao?
Biblia inasema hivi '' Hata ikawa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; naye akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula. Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa MUNGU. Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo. Ikawa siku moja akafika huko, akaingia katika chumba kile akalala. Akamwambia Gehazi mtumishi wake, Mwite yule Mshunami. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mbele yake. Akamwambia, Sema naye sasa, Tazama, wewe umetutunza sana namna hii; utendewe nini basi?-2 Wafalme 4:8-13''
Mwanamke huyo alito matoleo aina ya chakula, kama ambavyo wewe unaweza ukampa Mchungaji wako au Mtumishi Sadaka ya chakula au sadaka ya pesa ya kununua chakula.
Baadae yule mama akaamua kuwatengenezea chumba cha kulala kabisa watumishi wa MUNGU, Na mengine mengi aliyafanya ili tu watumishi wale wakiwa katika huduma mambo yote yaende vizuri.
Utoaji wako unaweza ukasababisha MUNGU akubariki ndugu.
Kumbuka pia kwamba sadaka haileti muujiza ila sadaka ikiambatana na maombi husababisha miujiza mikubwa na ulinzi mkubwa juu ya baraka zako. 
Sadaka njema uitoayo inaweza kusababisha jambo kubwa sana kwako katika ulimwengu wa roho.
Ibrahimu baada ya sadaka yake ya ajabu alikutana na ahadi za MUNGU za baraka za ajabu sana, baraka ya Ibrahimu iliyotengenezwa na sadaka yake iliyohitaji utii mkubwa ndipo itolewe, ipo hata leo.
Mwanzo 22:15-18 ''
Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu. ''

Ndugu, ukisikia msukumo rohoni kutoa sadaka hakikisha unatimiza.
Sadaka zingine hutengeneza ushindi wa ajabu sana sana kama maombi sahihi kutoka kwa mtumishi yataambatana na sadaka hiyo.
Wakati mwingine hakikisha unamsikiliza Mtumishi akiiombea sadaka yako ili ujue hakika imeombewa, maana haitakiwi kwenda bila maombi.
Kama umempa sadaka kibinafsi na sio kundi basi mweleze aiombee sadaka hiyo, ni haki yako na wajibu kuhakikisha sadaka hiyo imeombewa maana matokeo ya sadaka iliyoambatana na maombi ni makubwa sana.
Wachawi wanaweza wakakuogopa sana kwa sababu tu sadaka zako nzuri huwa zinaombewa na ulinzi kwako kwa neema ya MUNGU unakuwa mkubwa sana.
Mimi binafsi ninazo shuhuda nyingi sana zilizotokana na sadaka kwangu mwenyewe na kwa wateule wengine ila nafasi haitoshi kuziweka hapa, ila kuna faida kubwa sana katika utoaji unaoambatana na maombi ya mtumishi na utakatifu kwa mtoaji.
Watumishi wengine hawaombei sadaka mara moja tu bali Roho wa MUNGU huwakumbusha hata baada ya muda mrefu waombee sadaka walizopokea kwa watu, hivyo ukisikia msukumo wa kutoa sadaka hakikisha unatimiza maana wakati mwingine miaka michache ijayo unaweza ukakutana na muujiza mkubwa wa MUNGU kwa sababu tu ya utoaji wako.
Dorkasi alifufuka kwa sababu tu ya matoleo yake.
Hata wewe uchumi wako au afya yako au uzao wako au ndoa yako au kibali chako vinaweza kufufuka ghafla hata kama wachawi walijua walishavizika
Matendo 9"36-42 ''Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao.  Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai. Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini BWANA. ''
Narudia tena hata wewe uchumi wako au afya yako au uzao wako au ndoa yako au kibali chako vinaweza kufufuka ghafla hata kama wachawi walijua walishavizika.
Hebu jiulize sadaka yako ukitoa itapeleka injili na usipotoa kuna watu watakufa bila kuokoka, hivyo kwa utoaji wa sadaka nzuri namna hiyo ni lazima tu MUNGU akukumbuke na kukutendea mema maana umesababisha watu waokolewe na Bwana YESU.
Kupeleka injili ni gharama sana na wengi hata kama wana wito lakini wamekimbia kupeleka injili kwa sababu walikosa pesa ya kuwezesha, sasa wewe unayesababisha watu waokoke kwa sababu ya utoaji wako mzuri hakika lazia MUNGU wa mbinguni akubariki sana.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.

Comments