PICHA YA NJE ITHIBITISHE KWA PICHA YA NDANI ILI UJUE KUFANYA MAAMUZI SAHIHI

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Picha ni taswira ya mtu au kitu inayotokana na kitu husika.
Taswira ni picha ya mambo au vitu inayomjia mtu akilini mwake.
Kuna mtu nje na kuna mtu ndani.
Wakati mtu alivyo nje inaweza kuwa tofauti na alivyo ndani.
Mara nyingi tunaviona vitu kwa nje tu na kuamua lakini baadae matokeo ya maamuzi Yale yanasumbua sana.
Sio kila picha ya kitu kwa nje ndio picha halisi ya kitu hicho kwa ndani.
Picha zingine za nje ni photocopy tu na sio picha original.
Ahabu kwa picha ya nje alimuona Yezebeli ni mwanamke mzuri sana ndio maana akamuoa, lakini kwa picha ya ndani Yezebeli halisi alikuwa mleta vifungo vya kipepo kwa Ahabu na kwa taifa zima la Israel.
1 Wafalme 16:30-33 ''
Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kuliko wote waliomtangulia. Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia. Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria. Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia. ''
Ndugu, picha ya nje ithibitishe kwa picha ya ndani ili ujue jinsi ya kufanya maamuzi sahihi.

Katika kumtia mafuta mtoto wa Yese ili aje awe mfalme, picha ya nje ya Samweli na Yese hazikumuona Daudi kama ndiye mteuliwa wa MUNGU, ndio maana Daudi alisahaulika hadi MUNGU aliposema kwamba katika waliokuwepo pale hakukuwa na aliyetakiwa kuja kuwa mfalme.
1 Samweli 16:7 ''
Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo. ''
 
Picha ya nje ya mafalisayo juu ya YESU ilikuwa tofauti na picha ya ndani aliyoiona Simeoni juu ya YESU KRISTO.
Mafalisayo walimuona kwa picha ya nje YESU kuwa ni mwanadamu wa kawaida tu, Mathayo 13:54-56 ''
Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii?  Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? ''
Lakini Simeoni kwa picha ya ndani alimuona YESU kuwa ni mwokozi wa ulimwengu wote.
Luka 2:28-32 ''
yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru MUNGU, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. ''
Ndugu, usiishie kukijua kitu kwa picha ya nje tu, Bali kijue kitu hicho hata na kwa picha ya ndani ili ikusaidie katika maamuzi.
Usiishie kumfahamu mtu kwa nje tu Bali muulize ROHO MTAKATIFU ili akujulishe juu ya picha ya ndani ya mtu huyo.



Picha ya nje unaweza ukaona kushidwa lakini picha ya ndani ukaona ushindi na kweli ukaja kuupata ushindi kwa maombi na tumaini lako kwa MUNGU.
Sio picha zote za vitu au watu kwa nje ni mbaya lakini wakati mwingine katika baadhi ya maamuzi unahitaji kuthibitisha picha ya nje kwa picha ya ndani. Dada mmoja aliyeokoka alifuatwa na kijana mmoja akitaka amuoe. Yule Dada akamwambia atamjibu yule kijana siku inayofuata. Usiku wa siku hiyo hiyo yule Dada akaota ndoto kwamba yule kama ana mke na watoto, alipojiridhisha kwamba ni MUNGU amemjulisha hakumkubalia yule kaka na siku chache baadae ikagundulika kwamba yule kaka ana mke na watoto na alikuwa ameikimbia familia yake iliyokuwa mkoa wa mbali.
Mtu kwa nje anaweza kuwa tofauti kabisa na uhalisia alioubeba, inakupasa kuwa makini sana, omba sana na msikilize sana ROHO MTAKATIFU ili usiangukie pabaya.

Mama mmoja alifuatwa na Baba mmoja akitaka kumuoa na yule Mama akakubali lakini usiku wa siku hiyo hiyo yule mama kwenye maono akamuona yule Baba kwamba ni mchawi gwiji, akaamua kumkataa maana aliona hadi madhara ambayo angeyapata kama angemkubalia.
Ndugu, picha ya nje ya mtu inaweza kuwa nzuri sana lakini picha ya ndani ikakataa kwamba yule sio mtu mzuri.
Ndugu unahitaji kuwa makini na hakikisha unakuwa muombaji.



Picha ya nje inaweza ikabeba.
1. Vitu vizuri kwa macho lakini ndani ya vitu vibaya au Vitu vibaya kwa nje lakini kwa uhalisia ni vitu vizuri.1 Yohana 4:1 ''Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; ............''

2. Vitu vizuri kwa nje na kwa ndani vikawa ni vitu vizuri pia.
 Mathayo 7:17 ''Vivyo hivyo kila mti mwema huzaa matunda mazuri; .............''
 
3. Vitu vibaya kwa nje na ndani ni vitu vibaya pia.
 Mathayo 7:18 ''Mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mwovu kuzaa matunda mazuri.''
 
4. Vitu vizuri nje na ndani lakini sio vyako au havikufai wewe.
Mwanzo 2:9 ''
Bwana MUNGU akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.'' 
Mti wa katikati ya Bustani ambao ni mti wa uzima ulikuwa ni mtu mzuri sana lakini hawakuruhusiwa kula matunda yake.
Vipo vitu vingi tu ni vizuri sana lakini havikufai wewe.
Vitu hivyo vinaweza kuwa vizuri lakini sio fungu lako.
Ni vitu vizuri lakini havibebi kusudi la MUNGU kwako.

Ndugu unahitaji tu kuwa muombaji na unayemsikiliza ROHO MTAKATIFU na kumtii.


Njia za kiroho za kukusadia kujua picha ya ndani ya kitu au ya mtu, ili uamue vyema ukiwa na ROHO MTAKATIFU(Zaburi 32:8 ''Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.'')

1. Amani ya KRISTO.
Wakolosai 3:15 ''
Na amani ya KRISTO iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.''

2. Uhuru wa KRISTO.
2 Kor 3:17 ''
Basi ndiye ROHO; walakini alipo ROHO wa BWANA, hapo ndipo penye uhuru.''

3. Neno la MUNGU la ufunuo
Zaburi 107:20 ''
Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao. ''
 
4. Kujulishwa kwa ndoto au maono.
Ayubu 33:14-16 ''
Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao, ''
 
5. Mtumishi wa MUNGU kukujulisha.
Amosi 3:7 ''
Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.''
 
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu

Comments