UKISEMA NA MUNGU ATAKUPA NAFASI MPYA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ukisema na MUNGU kwamba akupe nafasi mpya ya kuishi maisha ya Wokovu hakika atakupa..
Ukisema na MUNGU hakika atakupa nafasi mpya.
Ukisema na MUNGU kwa toba na kurejea hakika atakupa nafasi mpya.
Inawezekana zamani wewe ulikuwa Mcha MUNGU sahihi aliyeokoka lakini ukaamua kuufuata uongo ukamwacha YESU.
Ulipomwacha YESU na MUNGU alikuacha wewe ila sasa anakupa nafasi utubu na urejee ili MUNGU akupe nafasi mpya.
Matendo 3:19 " Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"

Dada mmoja alikuwa ni Mtumishi mzuri Kanisani, alikuwa alikuwa mwimbaji na kiongozi mzuri lakini baadae katika harakati za kutafuta Mchumba akapata mwanaume mpagani, yule dada alionywa na watumishi wa MUNGU lakini alishupaza shingo na kuanza kuwatukana watumishi wa MUNGU kwamba wanataka asiolewe. Watumishi wakanyamaza kimya na Dada yule akaanza kufanya mapenzi na Baba yule kabla ya ndoa. Wakiwa katika mahusiano hayo kabla ya ndoa yule Dada akapata mimba na kuondoka Kanisani kwa aibu. Yule Mwanaume kumbe hakuwa na nia ya kumuoa ila kutembea naye tu hivyo akamwacha akiwa Mjamzito, yule Dada akawa akikutana na mtu wa kanisani anajificha kwa aibu. Baadae alipoenda Hospital alijikuta ana ukimwi, akawa kama amechanganyikiwa. Jambo la ajabu ni kwamba akawa anatamani kwenda Kanisani kutubu lakini anaogopa kwa jinsi alivyowatukana watumishi wa MUNGU. Baadae katika hali ya kuzidiwa na ugonjwa akawa hoi na siku moja akakutana na Mtumishi mmoja waliyekuwa wanatumika wote Kwenye huduma Kanisani, ikabidi amweleze ukweli. Yule Mtumishi alilia sana na kumsihi tu kwamba arejee na MUNGU atamsamehe. Yule Dada alikataa kurejea akiangalia heshima aliyokuwa nayo Kanisani.

Ndugu kama na wewe uliharibu kanisani na sasa unaogopa kurudi nakuomba rudi tu ili upatanishwe na MUNGU na uendelee mbele na KRISTO.
Kumbuka Biblia inasema '' Kuwaogopa wanadamu huleta mtego; Bali amtumainiye BWANA atakuwa salama.-Mithali 29:25''

MUNGU yuko tayari kukupa nafasi mpya kama utaamua kumpokea YESU KRISTO upya, ukatubu na kuacha uovu wote.
YESU anakuita Leo wewe ndugu uliyemwacha.
YESU anakuita Leo wewe ambaye unaitaka mbingu.
YESU anakuita Leo kwa ajili ya uzima wa milele.
Inawezekana ulidanganywa na mawakala wa shetani ili umwache YESU na ukamwacha.

1 Timotheo 4:1-3 '' Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;  kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo MUNGU aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli.''
 
Ndugu kumbuka kwamba ulipomwacha YESU uliiacha njia pekee ya uzima wa milele, rejea Leo ndugu kwa na utakatifu hakika atakusamehe na kuliandika jina lako katika kitabu cha uzima.
Hata kama umefanya dhambi nyingi sana na kubwa sana hata hudhani kama anaweza kukusamehe, ndugu mpokee YESU Leo atakusamehe na kukupa nafasi mpya ya kumtumikia na kuishi maisha matakatifu.

Kumbuka hakuna pa kukimbilia kama kweli unautaka uzima wa milele, bali ni kwa YESU tu.
Hakuna pa kukimbilia kama kweli huitaji jehanamu ya moto, bali kimbilia kwa YESU.
Ndugu wala hujachelewa, Fanya hima Leo kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.

Ndugu mmoja alikuwa Kanisani lakini hajaokoka maana alikuwa ni mtu wa michanganyo mingi, baadae akadanganywa na Wapinga Kristo ili amwache YESU na wao hao watampa nafasi ya kwenda kusoma uarabuni mambo ya dini ili wampe nafasi katika dini yao ya uongozi. Yule ndugu kwa tamaa ya ukubwa  na heshima na mali za uongo akaamua kuwa mpinga Kristo. Alienda huko huku akijua kabisa kwamba hakuna uzima wa milele bila YESU KRISTO. Akiwa kule alikuwa ana maumivu moyoni yasiyoisha maana alijua kabisa amepotea. Alidumu katika hiyo dini mpya kwa miaka kadhaa, alitumika kuzusha uongo dhidi ya watumishi wa Kanisa ili apewe nafasi katika dini mpya, alijaribu hata kufanya mikutano ya kupinga Ukristo. Baadae aliona maono ya kwamba shetani aliyempokea anataka amtumie kwa muda kisha amuue. Yule ndugu alijikuta anakimbilia kanisani na kuombewa, mapepo yakamtoka na ndipo akaokoka upya na kuanza kumtumikia MUNGU.
Ndugu, hata wewe uliyemwacha YESU kwa sababu ya tamaa ya mali au tamaa ya ndoa nakuomba rejea kwa YESU, Usiwaangalie wanadamu bali mwangalie YESU KRISTO Mwokozi.
Kuanzia leo usiwe adui na Kanisa wala huwezi usiwe adui na ibada.
Ni saa ya kurejea kwako kwa MUNGU aliye hai, itumie saa hii kuokoka.

Isaya 55:6-7 " Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa."
Ujumbe wa Leo nimesema na wewe uliyerudi nyuma kiroho kwa sababu ya dhambi au mambo ya kidunia na nimesema na wewe ambaye hujaokoka.
Nimewahi kukutana na watu ambao zamani walikuwa watumishi wa MUNGU lakini wakaukubali uongo wa shetani na kujipoteza, baadae mambo yaliwaharibikia wakabaki wanatamani kurejea kwa YESU lakini wanaogopa, ndugu kumbuka hakuna mwanadamu anayeweza kukusaidia bali usimwogope mwanadamu bali mtii MUNGU na Neno lake.
 Najua unajua kabisa kwamba bila YESU hutaweza kuupata uzima wa milele, hivyo hata kama hujaamua kumrudia YESU basi usikubali tena usikubali kabisaaa  kusema uongo kwa MUNGU aliye hai.
Kumbuka Biblia inasema ''Mizani ya hadaa ni chukizo kwa BWANA; Bali vipimo vilivyo sawasawa humpendeza. Ukamilifu wao wenye haki utawaongoza Bali ukaidi wao wenye fitina utawaangamiza.-Mithali 11:1-3''
Usije ukakubali hata siku moja kusema uongo kwa MUNGU.
Ulikosea sana kumwacha YESU lakini leo anakuhitaji ili akusamehe na kukurudishia karama na vipawa ulivyokuwa navyo Mwanzo.

Nimewahi kukutana na watu wengi sana ambao walichobakiza ni kusema tu '' Mimi nilikuwaga mtumishi mmzuri sana kanisani'' Anakuambia haya kipindi akiwa amelewa na huku ameshikilia chupa ya Bia mkononi, hali ni mbaya sana.
Anakuambia haya akiwa amekongoroka kwa sababu ya utumwa wa dhambi, anakuambia haya akiwa gerezani baada ya kuiba, anakumbia haya akiwa yuko katika mateso makali sana ya ndoa yake.
Kumwacha YESU kuna hasara nyingi mno mno.
Ndugu ni kweli kabisa ulikosea sana kumwacha YESU lakini leo anakuhitaji ili akupe neema mpya. Biblia inasema juu yako kwamba '' bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.  Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.-1 Yohana 1: 7-10''

 Ndugu jinsi ya kurejea kwa YESU, Fanya yafuatayo.

1. Mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako kwa upya huku ukiacha njia mbaya iliyokuangusha.
Luka 19:10 '' Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.''

2. Tubu na anza kushikiana na kanisa la MUNGU katika kazi ya MUNGU.
Ufunuo 2:5A '' Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu,''

3. Acha dhambi zote 
1 Petro 1:13-14 ''Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake YESU KRISTO.
14 Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; ''

 
4. Mtumikie Bwana YESU kwa kuwasaidia wengine kurudi kwa YESU Mwokozi.
1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''

5 Jitenge na mawakala za shetani wote.
2 Yohana 1:7-8 '' Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa YESU KRISTO yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga KRISTO. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu.''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments