UNAFANYIA KAZI WAZO LA NANI?


Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Je wewe binafsi huwa unafanyia kazi wazo la nani?
Neno ''Wazo" ni mpango,pendekezo au picha inayoingia moyoni mwa mtu kama ramani ya kufanya jambo fulani na kufanikiwa.
Kuna makundi matatu ya mawazo yanayoweza kuingia moyoni mwako.
1. Wazo kutoka kwa MUNGU.
Yeremia 29:11 '' Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho. ''
 
2. Wazo kutoka kwa shetani.

2 Kor 4:4 '' ambao ndani yao mungu(shetani) wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU.''
 
3.Wazo kutoka kwako Binafsi au kutoka kwa wanadamu wengine.

Isaya 65:2 '' Nitazameni, nitazameni. Mchana kutwa nimewanyoshea mikono yangu watu walioasi, watu waendao katika njia isiyo njema, wakifuata mawazo yao wenyewe; ''
 
Kwanini ni lazima uwe makini sana na mawazo unayofanyia kazi?
Ni kwa sababu shetani naye hujihudhulishwa katika kati ya watu wa MUNGU ili kuwapoteza.
2 Kor 11:12-15 '' Lakini nifanyalo nitalifanya, ili niwapinge hao watafutao nafasi wasipate nafasi; ili kwamba katika neno hilo wajisifialo waonekane kuwa kama sisi. Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa KRISTO. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru. Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.''
 Kuna watu walianzisha dini kwa wazo la shetani na hao kuwajua ni rahisi sana, wanamkataa YESU KRISTO kuwa Mwokozi wao.
ROHO wa MUNGU aliyaona haya kabla dini nyingine yeyote haijakuwepo duniani, ndio maana Biblia iko wazi sana juu ya hilo.
2 Yohana 1:7-9 '' Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa YESU KRISTO yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya KRISTO, yeye hana MUNGU. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba(MUNGU) na Mwana(YESU KRISTO) pia.''
 Kuna watu leo ni waganga wa kienyeji kwa sababu walifanyia kazi wazo la shetani kupitia ndoto za kipepo walizoota.
Kuna watu leo wanateseka na vifungo vya kishetani kwa sababu tu walifanyia kazi wawazo ya rafiki zao wanaoabudu shetani.
Kuna watu wenaabudu sanamu, mawe, miti au wanyama, kwa sababu tu walikubali kufanyia kazi wazo la shetani lililoletwa na mawakala wa shetani.
Kuna watu wanateseka katika maisha yao kwa sababu tu walimpinga MUNGU na Neno lake, Baada ya wao kukubali ushawishi wa kipepo kutoka kwa marafiki zao.
Ndugu, kumbuka Mawazo mema  ni mawazo kutoka kwa MUNGU, Na mengine kutoka kwa watu.
MUNGU anakuwazia mema na MUNGU anataka uokoke ili usiende jehanamu, lakini wengine hukataa kuokoka baada ya marafiki zao au ndugu zao kuwaambia kwamba wasiokoke bali wataokoka uzeeni. Mtu kama huyo anaweza akapishana na mbingu kwa sababu tu amekubali kufanyia kazi wazo la mwanadamu aliyejikinai, na sio kufanyia kazi wazo la MUNGU.
Kuna watu maisha yao yamevurugwa au yamevurugika sana kwa sababu tu walikubali kufanyia kazi wazo la kipepo kutoka kwa watu wao wa karibu. Mfano mwanafunzi unakubali kufanyia kazi wazo la rafiki yako mzinzi na unajikuta umeingia kwenye dhambi ya uasherati, na shule inaishia hapo hapo na huku ukiwapa mzigo wazazi wako kukulea wewe na mimba yako.
Dada mmoja alionywa sana na watumishi wa MUNGU na wazazi kwamba asikubali kufanya dhambi ya uasherati. Yule dada alidharau na akaendelea na dhambi yake ya uasherati. Alitoa mimba kadhaa lakini baadae alibeba mimba ambayo iligoma kutoka. Alijaribu nusura afe hivyo akaamua kutokuitoa. Baadae alizaa lakini jambo hilo likawa kama sababisho la yeye kutokuolewa. Kila Mwanaume akitaka kumchumbia, akiambiwa kwamba ana mtoto yule mwanaume anatokomea kusikojulikana. Jambo hilo limemtesa sana kwa miaka mingi sana na sasa ana zaidi ya miaka 40 huku amekata tamaa ya kuolewa, amebaki akijuta tu na kulia na kujilaumu kwamba kwanini hakuwasikiliza watumishi wa MUNGU. Chanzo cha yote hayo ni yeye kufanyia kazi wazi la kishetani, huku akidharau wazi la MUNGU na wazo la wanadamu wema.
Ndugu unahitaji kuwa makini sana na wazo unalofanyia kazi.
Kuna mawazo mabaya ambayo ni kutoka kwa shetani na mengine kutoka kwa watu

Zaburi 41:7 '' Wote wanaonichukia wananinong'ona, Wananiwazia mabaya.''
Kuna mawazo ambayo watu wanakuwazia lakini pia kuna mawazo ambayo wewe unajiwazia na kuna mawazo ambayo ni wengine waliwaza lakini wewe unafanyia kazi mawazo hayo, muhimu chunguza vyanzo vya mawazo yako maana shetani naye hushawishi sana watu ili wawaze mabaya na kuyatenda, ili wamkosee MUNGU Mwenyezi.
Kuna watu leo ni walevi wanaojinyea hovyo hovyo kwa sababu ya pombe, chanzo cha yote hayo ni kwa sababu walifanyia kazi wazo la kipepo lililowataka kunywa kidogo ila wasilewe. Sasa walijaribu kunywa hicho kidogo lakini baadae huyo kidogo akazaa kingi na sasa hali ni mbaya sana, wanatamani kutoka katika utumwa huo wa dhambi lakini imeshindikana maana shetani bado ana nguvu mionyoni mwao.
Kuna watu wako gerezani leo kwa sababu tu ya kufanyia kazi wazo la kipepo.
Kuna watu leo hawana amani wala furaha katika ndoa zao kwa sababu tu walikubali kufanyia kazi wazo la kipepo. Ndugu, kumbuka  kuna Mawazo kutoka kwa watu au kwa mtu Binafsi yapo katika kundi la mema na kundi la mabaya. Nakuomba katika maisha yako fanyia kazi mawazo mema.
1 Wafalme 8:18 '' Lakini BWANA akamwambia Daudi baba yangu, Kwa kuwa ilikuwa moyoni mwako kujenga nyumba kwa jina langu, ulifanya vema kuwaza hivi moyoni mwako.''
 
Muhimu kujua kuhusu Mawazo.
1. Upo hapo kwa sababu ya ulivyowaza.
2. Usiridhike na hali yako ya sasa ambayo imetokana na kuwaza kwako.
3. Tafuta wazo la MUNGU kwenye Biblia ili utembee katika hilo.
4. Yapime kwa Neno la MUNGU mawazo yote yanayokujia.

Mimi sijui ndugu yangu wewe huwa unafanyia kazi wazo la nani.
Mimi nakushauri fanyia kazi wazo la MUNGU.
Wazo la MUNGU ni Neno la MUNGU.

Waebrania 4:12 ''Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.''
 Wazo la MUNGU analo ROHO MTAKATIFU, Msikilize yeye na kumtii ndipo utakuwa umefanyia kazi wazo la MUNGU.
1 Kor 2:10 '' Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.''
 
Fanyia kazi pia mawazo ya watu mema lakini uyachunguze mawazo hayo kwa kuyapima katika Neno la MUNGU ili yasiwe mawazo yanayokupeleka katika dhambi na yanayokupeleka katika vifungo vya kipepo.

Kama ulifanyia kazi wazo la kipepo hata likakuharibia sasa nakuomba tubu juu ya wazo hilo baya, livute na usilifanyie kazi tena. 
Tubu na mkimbilie Bwana YESU ili akuondolee vifungo vya giza vilivyokukamata kwa sababu ya wewe kukubali kufanyia kazi wazo la kipepo.
Okoka sasa na ishi  maisha matakatifu ya wokovu sasa.

Unahitaji kuwa na muda wa kuomba juu ya mawazo maana ni muhimu sana.

Katika maombi.
1. Futa mawazo mabaya wanayokuwazia kwa hila watu wabaya au mawakala wa shetani.
Zaburi 10:2 ''
Kwa kiburi chake asiye haki mnyonge anafuatiwa kwa ukali; Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.''
 
Wao ndio wanaswe na hila wanazoziwaza.


2. Futa mawazo mabaya uliyojiwazia wewe na kujipangia weweMwanzo 6:5-6 '' BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo'' 

3. Ombea kuwaza mema
Isaya 32:8 ''
Bali mwungwana huwaza mambo ya kiungwana, naye hushika sana mambo ya kiungwana. ''
 
4. Ombea wazo la MUNGU litimie juu ya maisha yako.
Nahumu 1:9 ''
Mnawaza nini juu ya BWANA? Yeye atakomesha kabisa; mateso hayatainuka mara ya pili. ''
 
5. Omba MUNGU akupe kuwaza sawasawa na Neno lake.
  Zaburi 19:14''
Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.

Comments