USIMFUNGULIE SHETANI MLANGO KATIKA MAISHA YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Ujumbe wa leo unasema kwamba Usimfungulie mlango shetani katika maisha yako.
Jambo la kwanza kujua ni kwamba Shetani hana nguvu hata moja labda tu wewe umfungulie mlango kwenye maisha yako.
Biblia inakuambia kwamba usimpe shetani nafasi hata moja katika maisha yako.
Waefeso 2:27-32 '' wala msimpe Ibilisi nafasi. Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji. Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. Wala msimhuzunishe yule ROHO MTAKATIFU  wa MUNGU; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi.''

Shetani anaweza akaonekana ana nguvu sana katika sehemu ambayo atafunguliwa mlango.
Eva alikubali uongo wa shetani na kwa tendo hilo la Eva kutokumwamini MUNGU aliyewakataza kula matunda ya mti wa Ujuzi wa mema na mabaya, shetani alikuwa na nguvu katika wanadamu maana amefunguliwa mlango na kuingia.

Mwanzo 3:4,6,8,13 ''Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,  Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Kisha wakasikia sauti ya BWANA Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, BWANA Mungu asiwaone. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.''

Ni neema ya MUNGU kwamba YESU KRISTO alikuja ili kutufanya tuwe na nguvu kuliko shetani na maajenti wake wote.
1 Yohana 3:8 ''atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.''
 
Ndugu hakika shetani hana nguvu mbele yako uliyeokolewa na Bwana YESU, labda tu wewe mwenyewe umfungulie mlango katika maisha yako ndipo atakuwa na nguvu.
Lakini kama hujamfungulia mlango hakika shetani hana nguvu hata moja kwako.
Kwanini watu wengi wanateswa na shetani?
Ni kwa sababu walimfungulia shetani mlango katika maisha yao.
Lakini shetani wala hana nguvu mbele ya mteule wa KRISTO.
Biblia inasema tukimpinga shetani hakika atatukimbia(Yakobo 4:7B ''
Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. '')
Kama ana uwezo wa kutukimbia basi hana nguvu na kama hana nguvu basi hatuwezoi sisi tulio na YESU KRISTO.

Kwa jinsi gani unaweza kumfungulia shetani mlango kwenye maisha yako na akaonekana ana nguvu kubwa kwako?
1. Kukataa kuokolewa na Bwana YESU na  kuishi maisha matakatifu.

Yohana 3:18-20 ''Amwaminiye yeye(YESU) hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. ''
 
2. Kutokumwamini MUNGU.
1 Nyakati 20:20 ''  ........ mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.''
 
3. Kuwategemea watu au vitu na sio MUNGU.
Yeremia 17:5-6 '' BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.''
 
4. Kuacha maombi.
1 Thesalonike 5:17 '' ombeni bila kukoma; ''
 
5. Kuacha kulifanyia kazi Neno la MUNGU.
Yakobo 1:22 '' Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.'' 
 
6. Kupenda mambo ya dunia kuliko kumpenda MUNGU.
 1 Yohana 2:15 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake.'' 

7. Kujiunganisha na mawakala wa shetani.
Kutoka 23:32-33 '' Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao. Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni tanzi kwako.''
Mawakala wa shetani ni pamoja na wachawi, washirikina, waganga wa kienyeji, wanajimu, majini, wakuu wa Giza, mizimu na kila kazi ya shetani.


8. Tamaa mbaya.
Yakobo 1:14 '' Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. '' 
 
9. Dhambi zote.
Zaburi 34:14 ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. '' 
 
10. Kutokumtii ROHO MTAKATIFU
Warumi 8:14 ''Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU. '' 
Ukikataa kuongozwa na ROHO MTAKATIFU unakuwa unakataa kuwa mtoto wa MUNGU, ni hatari sana sana kwako ukiwa mtu wa hivyo.

  Mengineyo ni pamoja na Kufanya kazi ya shetani na kuwa na Upofu wa kiroho.
Ndugu usikubali kumfungulia shetani mlango hata akawa na nguvu wakati kiuhalisia hana nguvu.
Naamini sasa hautamfungulia shetani mlango.
Wapo wengine waliwahiwa na mawakala za shetani na kuharibiwa ufahamu kabisa ili wasiipokee Neema ya MUNGU ya Wokovu wa KRISTO. Ni kweli wakati mwingine kuubadili moyo wa mtu kama huyo wakati mwingine ni jambo gumu sana.
Kuubadili moyo wa mtu kutoka katika mitazamo mibaya ni kazi sana wakati mwingine.
Imani ya kweli ipo moja tu na hiyo chanzo chake ni kusikia Neno la KRISTO kama hili la leo(Warumi 10:17,
Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO. )
lakini wapo watu waliosikia mambo mabaya na wakajenga imani katika hayo mabaya kiasi kwamba kuwageuza ili waje kwenye ukweli wa MUNGU ni kazi kubwa sana.
Ukweli wa MUNGU ni YESU KRISTO akiokoa.
Wako watu walisikia kwa mizimu na majini na wakajenga imani katika hayo kiasi kwamba kuwabadili inakuwa ngumu sana.
Ndugu ukitaka umpendeze MUNGU basi imani yako iwe na chanzo kimoja tu yaani Injili ya Wokovu ya YESU KRISTO.
Wengi sana wamedanganywa na wafanyakazi wa shetani na mioyo yao ikawa na mitazamo ya kishetani kiasi kwamba kuwabadili inahitaji Neema ya MUNGU.

Wengine wamekalia kuipenda tu dunia, hawana habari na Kuokoka.
Biblia inatukataza kuipenda dunia na mambo mabaya yaliyomo duniani.
1 Yohana 2:15-17 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba(MUNGU), bali vyatokana na dunia.Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.''
Baadhi ya dalili za Mkristo anayeipenda dunia.
1. Kujitenga na waliookoka.
2. Lugha za matusi.
3. Hapendi Kusoma Neno la MUNGU wala kulitafakari.
4. Anakunywa pombe.
5. Kujipenda mwenyewe kuliko kumpenda MUNGU.
6. Kupenda starehe na anasa za dunia, kama kwenda disko.
7. Kuiga taratibu mbaya za watu wengine.
8. Kukubaliana na mitindo isiyofaa.
9. Kuwa mtu wa mizaha hata pasipohitaji mizaha.
10. Kuwa kinyume na Neno la MUNGU.
11.Kuwa mtu wa majungu, uongo na kauli mbaya za mitaani.
12.Kufanya kazi za shetani.
13. Kupenda pesa kupitiliza.
14. Kukosa hofu ya MUNGU.
15. Kwenda kwa mazoelea katika mambo ya MUNGU.

Ndugu unahitaji kutengeneza.
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.

Comments