EPUKA DHAMBI, UOVU NA MAKOSA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kuhusu dhambi, uovu na makosa..
Kwanza kabla ya yote nakuomba sana epuka dhambi, uovu na makosa.

Uovu ni nini?
=Uovu ni hali ya kutenda mabaya, ni hali inayoondoa uzuri.
Isaya 1:16-17 '' Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. ''
 
Maovu/uovu ni dhambi iliyokomaa na kuwa ya kujirudiarudia kwa mhusika
Isaya 59:2 " lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."

Makosa ni nini?
=Makosa ni kufanya jambo lisilo sahihi au lisilokubalika.
Makosa ni kukosea  au kufanya kosa.
 Warumi 5:18-19 '' Basi tena, kama kwa kosa moja(la Adamu) watu wote walihukumiwa adhabu, kadhalika kwa tendo moja la haki(YESU kufa msalabani) watu wote\(wanaotii) walihesabiwa haki yenye uzima. Kwa sababu kama kwa kuasi kwake mtu mmoja(Adamu) watu wengi waliingizwa katika hali ya wenye dhambi, kadhalika kwa kutii kwake mmoja(YESU ) watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki.''
 Makosa ni kutenda mabaya kwa kukusudia au kutokukusudia,kwa kutokujua au kwa kutokujua.

Dhambi ni nini?
=Dhambi ni uasi kwa MUNGU au ni kufanya jambo linalokatazwa na Biblia.
1 Yohana 3:4 ''Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi.''
Katika maombi yako ya toba nakushauri kutubia uovu, dhambi na makosa na jitahidi usitende tena uovu, makosa na dhambi. 
Kuna makosa Mengine ni dhambi na kuna makosa mengine ni makosa tu na sio dhambi.
Mfano uliambiwa uende saa 11 wewe ukaenda Saa 11:05 hilo ni kosa lakini linaweza lisiwe dhambi kutegemea na hali na mazingira.
Uliambiwa na ROHO MTAKATIFU uombe na wewe hukuomba kisha mabaya yakakupata, kutokutii huko ni kosa na ni dhambi, hivyo ukitaka MUNGU akusaidie utatakiwa uanze na toba kwanza ya kutokutii kwako hata mabaya ya kipepo yamekupata.
Usugu wa dhambi hutengeneza uovu.
Uendelevu wa dhambi huzaa uovu.
Kama mtu ni mzinifu kila Mara huyo anafanya yote matatu yaani anafanya kosa tena dhambi na uovu kabisaa anahusika nao daima.

 Dhambi  ni uasi kwa MUNGU, Ni matendo yote yaliyo chukizo kwa MUNGU.
Zaburi 34:14 ''
Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''
Lakini habari njema ni kwamba mtu akitubu kwa MUNGU katika KRISTO YESU na kuacha anasamehewa.
Mtu akitubia dhambi zake anasamehewa.
Mtu akitubia uovu wake na kuuacha anasamehewa.
Mtu akitubia makosa yake anasamehewa.

Kutoka 34:6-7 "BWANA akapita mbele yake, akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe UOVU na MAKOSA na DHAMBI; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne."

Katika maandiko haya tunakutana pia na Neno kupatiliza uovu kutoka kwa wazazi kwenda kwa watoto, wengi wamewahi kuniuliza juu ya hili, naomba nitumie somo hili kujibu.
Hiyo iko Kutoka 34:7  Hapo juu,
Kuna maana 3 za kupatiliza maovu.
1. Kupatiliza maovu maana yake kuzungushia maovu.
2. Kupatiliza maovu maana yake ni kutilia maanani na kushugulikia maovu hayo.
3. Kupatiliza maovu maana yake kuadhibu kutokana na maovu hayo.

Maana mojawapo ya uovu ni hali ya kutenda mabaya. Hivyo MUNGU anapatiliza uovu kwa sababu uovu hasa  kwa sababu ya kuabudu miungu ndio maana MUNGU akaahidi kwamba atapatiliza wana uovu wa baba zao.
Kwa sababu uovu huo ungeingia kwenye system za kuabudu, kama baba anaabudu sanamu utakuwa rahisi pia watoto kuabudu sanamu.

Maana ya Pili ya kupatiliza uovu ni kwa sababu uovu huo ni dhambi tayari hivyo ukitaja uovu tu inatosha kuonyesha kwamba uovu huo ni dhambi nyingi na zinazoendelea
Uovu kama mtu ameufanya kwa MUNGU pia ni dhambi hiyo.

Katika wakati wetu, MUNGU hapatilizi tena maovu ya wazazi kwenda kwa watoto wao maana Biblia inasema ,
Ezekieli 18:20 '' Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake. ''

Hapo hakuna kupatiliza tena uovu.
Katika wakati wetu ni wajibu wa kila mtu kuokoka,kutubu na kuanza kuishi maisha matakatifu.

1 Yohana 1:9 ''Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. ''
Katika wakati wetu Biblia inasema mwanadamu anayefuata maovu hufuata mauti yake mwenyewe.
Mauti ni uharibifu hivyo mtu yeyote anayefuata maovu hufuata uharibifu wake mwenyewe.
Mithali 11:19 '' Haki huelekea uzima; Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe. ''

Leo kila mtu huhukumiwa kwa matendo yake na sio matendo ya babu zake.
Matendo ya babu zake yanaweza yakamwasithiri kama hatayafuta kwa damu ya YESU tu.
Mshahara wa dhambi ni mauti na mshahara wa utakatifu katika wokovu wa KRISTO ni uzima wa milele.

Kuna watu huwa wanajidanganya wenyewe.
Mimi sijui kama na wewe ni mmoja wa watu ambao wana tabia za kujidanganya wenyewe, yaani mtu Mmoja binafsi anajidanganya yeye mwenyewe binafsi.
Watu wa aina hii hujidanganya katika jambo moja tu, yaani kujiona wako sahihi mbele za MUNGU wakati kiuhalisia wao ni watenda dhambi wakubwa.
Wamejaa uovu sana lakini kwa akili zao wanajiona wako safi mbele za MUNGU.
Watu hawa Biblia inasema wanajidanganya wenyewe, hiyo iko 1 Yohana 1:8 " Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu."

Mtu ni mywa pombe siku zote(Hata Jana na Leo amekunywa) harafu anajiita mtakatifu.
Kila siku yeye ni uzinzi na uasherati harafu anajiita mteule wa MUNGU au Mtumishi wa MUNGU, huko ni kujidanganya mwenyewe.
Ametoa mimba kwa siri huku akijua ni dhambi, na wala hajatubu toba ya kweli, harafu bado anajiita mteule.
Kila siku anasema uongo na anaiba kila Mara harafu anasema yeye hana dhambi, ni mtakatifu, huko ni kujidanganya mwenyewe.
Ndugu nakuomba usiwe mmoja wa watu wanajidanganya wenyewe.

 Inawezekana jina lako liko katika vivywa vya watu wengi duniani kwa sababu ya umaarufu wako. Lakini licha ya umaarufu wako wewe huna jibu kama utaupata uzima wa milele.
Unaweza kuwa kiongozi mkubwa,
Unaweza kuwa tajiri mkubwa sana,
Unaweza kuwa msomi sana lakini licha ya sifa yako hiyo lakini wewe huna jibu moyoni mwako kama ukifa utakwenda uzima wa milele wa MUNGU katika YESU KRISTO.
Kama hujaokolewa na Bwana YESU hadi kifo chako ukweli hautaupata uzima wa milele na hapo ndipo utaanza kusema ni heri usingezaliwa, maana jehanamu ni mbaya na huko ni kilio na kusaga meno tu.
Ndugu ambaye hujaokoka nakuomba mpokee YESU KRISTO Leo ili uokoke.
Ndugu ambaye umeshampokea YESU ila bado unalegalega nakuomba amua sasa kumpendeza MUNGU.
Wewe ndugu ambaye kwa YESU upo na kwa shetani upo, nakuomba amua sasa kumtii MUNGU na neno lake.
Ndugu nakusihi amua kuishi maisha matakatifu na ya hakika katika wokovu wa KRISTO kuanzia Leo.
Bwana YESU anasema "Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?
Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake? Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.-Marko 7:36-38


Ndugu, Maisha sahihi ni kumjua MUNGU Baba na YESU KRISTO aliyemtuma kisha ukampokea na kuanza kuishi maisha matakatifu katika yeye.
Msiba mkubwa zaidi wa maisha ya mtu ni mtu huyo kumkosa YESU KRISTO maishani mwake.
Ndugu hakikisha humkosi YESU katika maisha yako.
Kumbuka pia kwamba 
Kama unawawazia wengine mema, na wewe kuna watu wanaokuwazia mema.
Kama unawawazia wengine mabaya, na wewe kuna watu wanakuwazia mabaya.
Kipi bora?
Uwaze mabaya au uwaze mema?
Mimi nakushauri waza mema itakuwa ni faida kwako na utakuwa mwana wa MUNGU.

Mathayo 5:8 "Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona MUNGU.''

Hakikisha huzoelei uovu, acha uovu, acha dhambi na epuka makosa.
Tukijifunza Neno la MUNGU na kulitii hakika tutayatambua makosa ili tuyaepuke, tutatambua dhambi ili tuzikimbie na tutatambua uovu ili tuuepuke.
Uking'ang'ania uovu hakika ni hatari kwako.
Mhubir 8:8b '' Wala uovu hautamwokoa yule aliyeuzoea.''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments