HERI WENYE NJAA NA KIU YA HAKI

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU KRISTO atukuzwe.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Mkristo yeyote kokote aliko wakati wowote anatakiwa kuwa na kiu na njaa ya Neno la MUNGU.
Kimwili, kama huna njaa hutahitaji chakula.
Kimwili, kama huna kiu hutahitaji maji.
Kiroho, kiu na njaa ya neno la MUNGU haitakiwi kuwa ya muda tu kwa mkristo Bali ya kudumu.

Mathayo 5:6 "Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa."
Mimi Peter Nimeanza kububiri mtandaoni tangu mwishoni mwa mwaka 2012 baada ya ROHO MTAKATIFU kunisemesha na kunielekeza jukumu hilo. Hata somo hili unalojifunza muda huu ni la 768 tangu wakati huu achilia mbali masomo ambayo sikuyaweka kwenye blog yangu ya Maisha ya ushindi. Hata maana ya jina la Blog yangu Mwanzo lilikuwa ''Maisha ya ushindi dhidi ya dhambi-Mathayo 3:2'' lakini kwa sababu ya jina kuwa refu sana basi nikaita tu maisha ya ushindi. Mwanzoni upinzani ulikuwa mkubwa sana. Matukano yalikuwa mengi sana na hata vitisho pia vilikuwepo. Wakati mwingine Watu kunitukana ndiko kuliniongezea nguvu zaidi za kuandika Neno la MUNGU. Kuna kipindi nilipoona mambo yanakuwa magumu niliamua kuanzisha group langu nilililoliita Maisha ya ushindi lakini kwa mwaka mzima hata watu 200 hawakufika katika group, baadae nimamwomba MUNGU na kuanzisha group Nililoliita ''Neno la MUNGU'' Kwa neema ya MUNGU group hilo likapata kibali cha ajabu maana hadi leo group hilo lina Members Laki moja na nusu. Sitasahau matukio mawili ya vitisho. Tukio la kwanza ni baada ya kuandika somo linalokataza kuabudu sanamu na kitisho kingine ni baada ya kuandika somo la Biblia ya vitabu 66. Vitisho vile vilikuwa na nguvu sana kiasi kwamba unaweza ukawaza mara mbili mbili lakini ROHO wa MUNGU alikuwa mwaminifu kwangu maana vitisho vikizidi na ndivyo juhudi zaidi ya kuandika masomo inaongezeka. Wakati huo unaweza ukaandika somo na hata mtu mmoja asi-comment chochote wala ku-like. Rafiki yangu mmoja hata alinishauri kuacha kuandika masomo maana hakuna anayesoma hata mmoja na akaniambia ''Ukitaka ujue basi andiko somo zuri kisha angalia likes au comments'' . Kwangu mimi likes na Comments havikuwa kipaombele kabisa japokuwa napenda sana vitu hivyo na hunitia moyo sana. Miaka miwili ya mwanzo ilikuwa migumu mno lakini niliendelea mbele. Lakini kwa nini nakupa ushuhuda huu? Ni kwa sababu Neno la MUNGU li hai siku zote na ni jipya kila iitwapo leo.  Mwaka huu tu kuna watu hata idadi yao siikumbuki walionipigia simu na kumshukuru MUNGU kwa ajili ya masomo waliyosoma ya kwangu. Nimekuwa nikiwauliza ''Umesoma somo gani na likakubariki na kukufungua'' Ndugu yule cha ajabu sana anataja somo la  mwaka 2012 au 2013. Ndugu mmoja alitaja somo ambalo limembariki sana na kubadilisha maisha yake hata akaanza kulia kwenye simu juu ya kumshuru MUNGU kwa somo hilo, lakini aliponitajia nikashangaa sana sana maana somo hilo siku nalipost nilitukanwa hadi na wachungaji walioitana facebook ili wanipinge, ni somo lililohusu taji watakazopewa Wateule wa KRISTO. Mchungaji mmoja alinitukana sana na tangu siku hiyo wala sikuona akipost chochote, labda MUNGU alimpa u-busy mwingine nje na mtandao ili alipishe kusudi la MUNGU liendelee. Sasa swali la kujiuliza ni kwamba mtu anasoma somo la miaka mitano iliyopita na katika maelezo yake analiona kama ni somo lililofundishwa dakika chache zilizopita, ndugu yangu, Neno la MUNGU li hai na ni jipya kila leo hivyo Heri wenye njaa na kiu ya haki.
Neno la MUNGU ni chakula cha uzima.
Neno la MUNGU li hai kila siku.
Neno la MUNGU ni jipya kila siku hivyo kiu na njaa ya kulihitaji neno la MUNGU haitakiwi kukoma katika maisha ya Mteule wa MUNGU siku zote.

Kumbuka Neno la MUNGU ni jipya kila siku, ni kama fedha mpya iliyotolewa na serikali ili ianze kutumika, haijakunjwa popote na iko vizuri, ni mpya. Ndivyo lilivyo Neno la MUNGU maana ni jipya kila siku.
Zaburi 12:6 '' Maneno ya BWANA ni maneno safi, Ni fedha iliyojaribiwa kalibuni juu ya nchi; Iliyosafishwa mara saba.''
Ukiona umeanza kukosa kiu na njaa ya kujifunza Neno la MUNGU tambua umepatwa na vitu vifuatavyo;

1. Njaa na kiu ya kumtumikia shetani.

2. Njaa ya kuitumikia dunia na maovu.

3. Huishi maisha matakatifu wala hufanyi maombi.

4. Mapepo yamekuvamia na sasa yanakuongoza.

5. Uko katika vifungo vya kipepo.

Ndugu hakikisha una kiu ya haki na njaa ya haki.
Kiu ya haki na njaa ya haki ni kujifunza Neno la MUNGU na kulitii na kulifanyia kazi katika maisha yako.

Mwenye Neno lake anasema kwamba ''Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.-Mathayo 24:35''
Kama maisha yako ni ya duniani tu basi utashughulika na mambo ya dunia tu.
Kama maisha yako ni ya mbinguni basi utashughulika sana na mambo ya mbinguni. Kumpokea YESU kama Mwokozi,Utakatifu, Kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU na kufanya kila jambo la ki MUNGU katika kazi yake ndio kushughulika na mambo ya mbinguni, kumbuka Neno la MUNGU ndilo msingi na Mwongozo.
Kushughulika na mambo ya mbinguni ni kuutafuta ufalme wa MUNGU na kufanya mambo yaipasayo injili ya ufalme wa MUNGU.
Mathayo 6:33 ''Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.''


Biblia inashauri kila mwanadamu kuutafuta ufalme wa MUNGU.
Watu wengi huutafuta ufalme wa duniani na sio ufalme wa MUNGU.
Ni heri kushughulika na mambo ya ufalme wa MUNGU.
Kushughulika na mambo ya mbinguni ni Kuokoka na kujali ibada.
Kushughulika na mambo ua mbinguni ni kujifunza Neno la MUNGU kila mara la kuliishi Neno hilo katika utakatifu na haki, kuwa muombaji na kumwabudu MUNGU Baba katika Roho na kweli.

Ndugu hakikisha unashughulika na ufalme wa MUNGU na sio ufalme wa duniani.
Kumbuka ''Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele.-1 Yohana 2:17''

Mteule wa kweli wa KRISTO huwa halichoki Neno la MUNGU maana ana kiu ya haki na njaa ya haki.
Mkristo halisi ni lazima awe na kiu na njaa ya yafuatayo:
1. Kumwabudu MUNGU.
 Zaburi 29:2 '' Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu.''  
 

2. Kuomba katika ROHO MTAKATIFU.
Yuda 1:20-23 '' Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika ROHO MTAKATIFU, jilindeni katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu YESU KRISTO, hata mpate uzima wa milele. Wahurumieni wengine walio na shaka, na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili. ''

3. Kujifunza na kulitafakari Neno la MUNGU.
 Yoshua 1:8 ''Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.''
 
Kuna tofauti kati ya mtu aliyeshiba na mtu mwenye njaa katika kula chakula, mwenye njaa hula sana na kwa umakini mkubwa, aliyeshiba hula kidogo tu au kugusa tu chakula na kuacha.
Mkristo anatakiwa kubaki na kiu ya haki na njaa ya haki siku zote.
Neno la MUNGU haliwezi kumkinai mteule wa KRISTO, labda yeye alikinai Neno, lakini Neno huwa halikinai watu.
Ukiona unakinai Neno la MUNGU basi tambua kwamba unahitaji msaada wa kiroho.


1 Peter 2:2 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;''
 Mimi Peter nilipookoka nilianza kusoma Biblia nzima Neno kwa Neno. Kwa miezi minane niliimaliza kuisoma Biblia nzima neno kwa Neno. Nilifaidika sana sana kiroho lakini baada ya mwaka mmoja kupita ni nikaanza tena kuisoma upya Biblia yote Neno kwa Neno lakini cha ajabu Biblia ikawa mpya kwangu, kana kwamba sikuwahi kuisoma yote, kumbe nilitakiwa kufahamu kwamba Neno la MUNGU li hai siku zote na ni jipya kila siku kiasi huwezi kulikinai Neno la MUNGU kama kweli unaihitaji mbingu.
Ayubu 23:12 "Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,"

Ndugu, ukiona huna hamu ya kujifunza Neno la MUNGU Fanya yafuatayo;
1. Jilazimishe kulisoma Neno na jiwekee ratiba ya kulisoma kila Mara.
Na katika kusoma soma kwa malengo na soma kwa kusudi la kukujenga na kukusaidia na kukutakasa.

 2 Timotheo 2:15 '' Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.''

2. Fanya maombi ili Kama una kifungo cha kipepo kinachokuzuia kulisoma Neno la MUNGU na kulielewa basi kikuachie na uwe huru.
 Waebrania 4:12 ''Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.''

3. Soma kwa kutafuta kusudi la MUNGU.
 Zaburi 119:11 ''Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.''

Neno la MUNGU ni la muhimu sana kwako ndugu.
Yeremia 15:16 "Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee BWANA, Mungu wa majeshi."

Huwezi kuomba bila Neno la MUNGU.
Huwezi kulisoma Neno la MUNGU na kulielewa bila maombi.
Maombi na Neno la MUNGU ni vitu viwili ambavyo ili matokeo mazuri yatokee ni lazima hivyo viwili viambatane.
Hakuna aliye kama Bwana YESU.
Mimi nampenda sana Bwana YESU, wewe je?
Ona hapa anazungumza na roho yako uliyeokoka.

''Kama vile BABA alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu.Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za BABA yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa BABA yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo BABA kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana. Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia. -Yohana 15:9-19''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu
.

Comments