KAZI KUMI(10) ZA MUNGU KAMA MTETEZI WAKO IKIWA UNA SIFA ZA KUTETEWA NA YEYE.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunaangalia baadhi ya kazi za MUNGU akiwa kama mtetezi wako, lakini tu ukiwa na sifa za yeye MUNGU kukutetea wewe.
Siku moja wachawi walikuja katika eneo ambalo nilikuwa nimelala, ghafla ROHO wa MUNGU akaniondolea usingizi nikajikuta nimeamka na nikagundua kabisa natakiwa niombe japokuwa nilikuwa sijaona chochote. Niliomba kidogo kisha nikalala, baada ya muda nikasikia sauti tena ikisema ''Amka uombe'' nikaamka na kuomba kidogo kisha nikalala, baadae tena nikasikia sauti ikisema ''Amka uombe, nikaamka na na kujikuta naangalia nje ya dirisha maana lilikuwa dirisha la wazi kiasi unaweza kuona kila kitu nje. Nilipotazama niliona wachawi wawili wanaume na wananirushia moto lakini moto ule kila wakirusha unatoka mwingi kisha kabla haujanifikia unazima, wanakazana na huku wakiongea maneno ya kunifunga na kuchochea moto. Hapo ndipo nilipogundua ya kwamba kwa Neema ya tu ROHO MTAKATIFU alinijulisha kuomba kwa sababu yeye huona jambo mwisho kabla ya mwanzo. Baada ya hapo nikatoka kwenye Net(Chandarua) ili nipambane nao live lakini waliponiona tu kwamba kwa Neema MUNGU amenipa macho ya kuwaona na kuona vitendo vyao walikimbia. Ndugu, Yuko MUNGU anayeweza yote.
Biblia inajulisha kwamba MUNGU ni Mtetezi aliye hai.
Ayubu 19:25 '' Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.''
 MUNGU anaweza kukutetea dhidi ya adui zako wenye nguvu, lakini je una sifa za hadi MUNGU akutetee?
Nini maana ya mtetezi?
Mtetezi ni yule anayesimamia mtu ili kumkinga na mabaya yaliyokusudiwa au kumkinga na yale ambayo hasitahili.
Kwa upande wa BABA yetu wa mbinguni, hakika yeye ni Mtetezi aliye hai milele.
Bwana YESU ni mtetezi aliye hai milele.
ROHO MTAKATIFU ni mtetezi aliye na mbinu zote za ushindi.
 Je wewe una sifa za MUNGU kukutetea?
Je YESU ni Mwokozi wako hata akuokoe mbele ya adui wabaya?
Je una ROHO MTAKATIFU hata akusaidie kushinda kila adui anayekatisha mbele yako?
Je unamwamini ROHO MTAKATIFU au bado umemezwa na taratibu za dini zinazompinga ROHO MTAKATIFU ndio maana hakusaidii?. Ndugu, majibu sahihi yako moyoni mwako, mimi Peter Mabula kama mwalimu wa Neno la MUNGU, Kazi yangu ni kukujulisha tu kazi za MUNGU kama mtetezi wako kama ambavyo ROHO wa MUNGU alinifunulia.

Kazi za MUNGU kama Mtetezi wako ikiwa una sifa za MUNGU kukutetea.

1. Kukuokoa na mitego ya mauti ya maadui zako, ikiwa  una sifa za kutetewa na yeye.
Zaburi 91:3  ''Maana Yeye(MUNGU) atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo.''
 Mwenye sifa za kuokolewa na mitego ya shetani ya mauti ni.  Anayeishi maisha matakatifu,  Anayemwamini MUNGU na  anayehitaji msaada wa MUNGU kwa njia ya maombi katika KRISTO YESUI, Anayeishi katika kusudi la MUNGU.
Hizo ni sifa muhimu sana.
Kumbuka MUNGU kwetu sisi ni MUNGU wa kuokoa. Kwetu sisi akina nani? Ni kwetu sisi tunaomtii na kumwamini na kuomba mbele zake
Zaburi 68:20 ''MUNGU kwetu sisi ni MUNGU wa kuokoa; Na njia za kutoka mautini zina YEHOVA Bwana.'' 
Jambo muhimu ni kumwita kwa njia ya maombi ili atuokoe, kama humwiti unaweza kubaki ukiteswa na mitego ya mwingaji yaani shetani na mawakala zake, ukijitambua kwa kumwita MUNGU hakika unashinda.
Zaburi 50:15 '' Ukaniite siku ya mateso; Nitakuokoa, na wewe utanitukuza. ''

2. Kumkemea adui anayeiba na kula baraka zako.
Malaki 3:11  ''Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi.''
Ukisoma Sula hiyo ya Malaki utagundua kwamba MUNGU atawakemewa maadui wanaotafuna baraka zako ikiwa tu wewe ni mtoaji sahihi wa Zaka, sadaka na dhabihu.
Sifa za Mtu anayehitaji MUNGU awakemee maadui zake wanaotafuna uchumi wake ni Kuwa mtoaji sahihi na anayetoa kilicho bora tena anatoa kwa upendo.
YESU KRISTO hakika anaweza kuwakemea adui zako wote na wakaondoka kwako.
Inawezekana umefaulu sana katika mambo mengine ya kiroho lakini MUNGU anaweza akashindwa kukutetea kwenye suala la kazi, kipato, uchumi, biashara na kila chanzo chako cha pesa, kwa sababu tu wewe sio mwaminifu katika zaka, sadaka na dhabihu
 Hakikisha unakuwa na sifa ya MUNGU kuwakemea adui zako wanaofuatilia uchumi wako, Kama ni mtoaji hakika ukiomba tu utaona MUNGU akikusaidia kiajabu sana, MUNGU anapowakemea maana yake anawaondoa kwako ili wasikusumbue tena. Maadaui hao wanaweza kuwa magonjwa yanayopelekea pesa  yako iishie katika kutibu, maadui hao ni kukosa kazi, kudhulumiwa na watu wabaya, kuibiwa,  kurogwa kichawi ili biashara yako isifanikiwe au kuwekewa hila ili ufukuzwe kazi n.k
Hakikisha una sifa za MUNGU kukutetea katika masuala yanayohusu uchumi wako.

3. Kukupumzisha mizigo ambayo ni matatizo  yako.
Mathayo 11:28 ''Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.''
 Sifa hii ya kupumzishwa mizigo inawahusu watu ambao wanaamua kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao, wanamtambua YESU KRISTO kama Mwokozi wao, wanamkubali na kumtegemea kwa maombi, hakika hao yeye MUNGU atawapumzisha.
 Inawezekana una mizigo ya magonjwa, vifungo vya giza, laana, maagano ya kipepo, roho ya madeni, kiburi, hasira, tamaa mbaya,kuonewa, kuzuiliwa kipepo kupata baraka zako n.k
Itafute sifa hii muhimu ndipo utapumzishwa kupitia maombi na Kujifunza Neno la MUNGU na kulitii.

 4. Kuyakomesha mateso yaliyokuwa yanakutesa kwa muda mrefu.
Nahumu 1:9 '' Mnawaza nini juu ya BWANA? Yeye atakomesha kabisa; mateso hayatainuka mara ya pili.''
 Wenye sifa  hii ni wale wenye imani kubwa, Walioshiba Neno la MUNGU, waombaji wanaojitambua na wanaojua haki zao kwa MUNGU.
Hakika Bwana YESU anaweza kuyakomesha mateso kama alivyofanya katika maelfu ya watu kipindi akiwa kwenye huduma yake ya miaka mitatu. Soma kitabu cha Mathayo, marko, luka na Yohana Mtakatifu utaona watu wakifufuka, magonjwa sugu yakikoma, na kila tatizo likiondoka ndani ya watu.
Mfano ni hapa ambapo Biblia inasema YESU aliponya magonjwa yote na madhaifu yote, kama ambavyo anaweza kukuponya wewe leo magonjwa yote na madhaifu yote. Uwe na imani ya kupona hakika utapona kwa jina la YESU KRISTO.
Mathayo 9:35 ''Naye YESU alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, NA KUPONYA MAGONJWA YOTE NA UDHAIFU WA KILA NAMNA.''

5.Kukutia nguvu, kukusaidia na kukushika mkono.
Isaya 41:10 '' usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. ''
 Wenye sifa ni wale wateule wa MUNGU wasio waoga, ni waombaji, waomtegemea MUNGU na ambao tumaini lao ni kwa MUNGU tu hata wakiwa katika magumu sana.
ROHO MTAKATIFU anaweza kukutia nguvu, YESU KRISTO anaweza kukusaidia na MUNGU anaweza kukushika mkono na ukavuka salama hakika.
Mimi Peter hakika Bwana YESU ameshanishindia katika mambo mengi sana, hata nikishuhudia siku nzima inawezekana sitamaliza.
Watu walijua nimekufa baada ya kupata ajali lakini Bwana YESU alinitokea na kunipa neema na kuniponya kiajabu sana mbele ya watu waliodhani sitamaliza siku mbili nipo duniani.
Watu wa kundi hili Wanajua msaada wao ni kwa MUNGU tu.
Zaburi 121:2 '' Msaada wangu u katika BWANA, Aliyezifanya mbingu na nchi.''

 6. Kukuponya jeraha zako za moyoni na kukuponya magonjwa yako yote.
Yeremia 30:17 '' Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema BWANA, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa,  ....''
 MUNGU anaposema atakurudishia afya maana yake hiyo afya haikuwepo kabla, kama afya haikuwepo unadhani kulikuwa na nini? Ndugu mweshimu MUNGU katika maisha yako yote.
Tii Neno la MUNGU na mkimbilie Mwokozi YESU KRISTO daima.
Wenye sifa ni watu ambao wanaamini MUNGU anaweza kuponya kila ugonjwa, haijalishi ni ukimwi au ebola, watu wa kundi hili lazima wawe waombaji na wanaojitoa katika kazi yangu huku tumaini na tegemeo lao ni kwa MUNGU.

 7. Kupaharibu mahali pa kidunia palipoinuka.
Mika 1:2-3 '' Sikilizeni, enyi watu wa kabila zote; sikiliza, Ee dunia, na vyote vilivyomo; Bwana MUNGU na ashuhudie juu yenu, yeye BWANA kutoka hekalu lake takatifu. Kwa maana, angalieni, BWANA anakuja akitoka mahali pake, naye atashuka, na kupakanyaga mahali pa dunia palipoinuka.''
 MUNGU anapokuja kupaharibub mahali pa kidunia palipoinuka maana yake anakuja kuwaharibu maadui zako walioinuka.
Mchawi aliyekuinukia anaweza akafedheheshwa tu ghafla kwa sababu ya MUNGU kama mtetezi wako amekuja kukutetea.
Nani anataka kukuchukulia mume wako?
Nani anataka ufe?, nani anataka uwe kichaa?, nani ataka kukutesa kwa madawa yake?
 MUNGU kama mtetezi wako anaweza kuja na kuua maadui zako wote ili wasiwepo tena maishani mwako.
Isaya 41:11-12 '' Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. ''
 Lakini ni lazima uwe na sifa za kumfanya MUNGU akutetee katika hili.
Wenye sifa ni watu waliookoka, wanaishi maisha matakatifu na ya haki, waombaji, wanamtumikia Bwana YESU na wanaishi kwa kusudi la MUNGU huku wamejitenga mbali na machukizo ya kidunia.

 8. Kukulinda na kuyakataza mabaya yasije kwako.
Zaburi 91:9-11 ''Kwa kuwa Wewe BWANA ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.''
 Yako mabaya mengi hupangwa na maadui zako, wachawi, waganga, washirikina, wakuu wa giza na majini. Na ni hatari sana kama mabaya hayo yakikupata wewe.
Lakini MUNGU akiwa mtetezi wako hakika mabaya ya wabaya wako hao yatawapata wao maana Bwana YESU anakulinda na kukushindia.
 Wenye sifa za kutetewa na MUNGU katika kundi hili ni Wateule wa KRISTO walioweka kimbilio lao kwa MUNGU na kwa MUNGU kuwa ndio ngome yao na makao yao ya kudumu. Wanaamini nguvu za MUNGU na uwezoo wa MUNGU. Wanaamini jina la YESU KRISTO, Damu ya YESU KRISTO, Neno la MUNGU na nguvu za ROHO MTAKATIFU na pia wanaamini njia za MUNGU za kuwasaidia ikiwepo MUNGU kutuma malaika kwao.

 9. Kukubariki.
Hesabu 6:24-26 ''BWANA akubarikie, na kukulinda; BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani.''
 Inawezekana kabisa kuna watu wanafanya mbinu ufilisike au uwe chini yao, MUNGU anaweza akaja kukutetea kwa njia ya kukubariki tu.
Wachawi wanajaribu kukuroga lakini wakisema mwaka huu huyu kwisha kazi wewe ndio unabarikiwa zaidi na MUNGU.
MUNGU ana njia nyingi sana za kukutetea. Watu wanavyokusema vibaya au kukusema vibaya juu ya kazi yako unashangaa MUNGU anakuja kukutetea kwa kukubariki sana.
Wenye sifa ni watu wale wenye faida katika kazi ya MUNGU, Wanatumia mali zao kwa ajili ya kazi za injili na kuhudumia watumishi wa MUNGU, Ni wacha MUNGU na wanaishi maisha matakatifu na ya haki huku wakiwa wanamtegemea MUNGU katika maisha yao.

10.  Kuziharibu silaha za adui zako.
Isaya 54:17 '' Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa BWANA, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema BWANA.''
 Wenye sifa ni watumishi wa MUNGU yaani wateule wa KRISTO wanaotimiza kusudi la MUNGU la wito wao, wanaotambua haki zao kwa MUNGU, watauwa, waombaji na wanaotumia muda wao kumhubiri KRISTO kwa watu wote na kwa njia mbalimbali.
Kumbuka waliookoka wote ni watumishi wa MUNGU hivyo ndugu timiza wajibu wako kwa MUNGU.
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments