KWANINI BWANA YESU KRISTO ALIAMUA KUTOKA MBINGUNI NA KUJA DUNIANI?

Na Peter & Scholar Mabula.
Watenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Heri ya Christmas, sherekea katika utakatifu.
Mimi na Mke wangu Scholar Tunawatakia sikukuu njema sana ya kukumbuka kuzaliwa kwa Mwokozi wetu YESU KRISTO.
Kabla ya yote ngoja nikukumbushe jambo hili; Maana ya CHRISTMASS ni maneno mawili yaani
1. CHRIST(Mesiah au mpakwa mafuta au aliyetengwa kwa kazi maalum)
2.MASS yaani kusanyiko (group of .....) Kwa hiyo maana ya CHRISTMASS ni kusanyiko la KRISTO
Ujumbe wangu wa Christmas mwaka huu ni huu


KWANINI BWANA YESU KRISTO ALIAMUA KUTOKA MBINGUNI NA KUJA DUNIANI?

Maswali mawili muhimu;
Swali la kwanza, Kama mtu atakuuliza kwanini MUNGU aliamua kumleta YESU KRISTO duniani.
Majibu ni haya kwamba MUNGU aliwapenda wanadamu na kuwaletea Wokovu pekee kupitia YESU KRISTO.
Yohana 3:16-18 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''

 
MUNGU alipoupenda ulimwengu wala hakupenda majengo au wala milima bali aliwapenda wanadamu na kuwahurumia hivyo kuwaletea wokovu mmoja tu wa milele kupitia YESU KRISTO.
Swali la pili; Kwanini Bwana YESU aliamua kuja duniani?
Majibu yake ndio ujumbe wa Christmass mwaka huu.


Sababu hizo ni nyingi sana lakini chake katika hizo ambazo zilimleta Bwana YESU duniani ni hizi.


1. YESU alikuja Ili tupate uzima sasa kisha uzima wa milele.

 
Yohana 10:10b '' mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.''

 
Uzima wa sasa aliotupa Bwana YESU sisi tuliompokea kama Mwkozi na tunaliishi Neno lake ni ushindi dhidi ya kila mipango ya giza inayoweza kuondoa uzima wa miili yetu, lakini baada ya kuondoka ni uzima wa milele.
Ndugu, Usisherekee tu sikukuu ya kukumbuka kuja kwa ukombozi duniani bali husika na Mkombozi ili upate uzima sasa kisha uzima wa milele.


2. YESU alikuja Ili kuanzisha Kanisa la waenda mbinguni, Yeye katika Kanisa lake ndiye Mchungaji mkuu na sisi wengine wote ni kondoo wa malisho yake.

Yohana 10:11 ''Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.''

 
Ndugu usihusike na kanisa ambalo hawahubiri injili ya KRISTO YESU iokoayo, maana kanisa la hivyo sio kanisa la MUNGU bali ni kanisa tu la dini na kibinadamu. Kanisa la MUNGU ni lazima KRISTO awe ndiye Mchungaji mkuu, ukiona Kanisa linampinga KRISTO kwa jambo lolote lile ujue hilo ni Kanisa la Shetani.
Hivyo usisherekee tu sikukuu huku wewe sio sehemu ya Kanisa hai la MUNGU aliye hai na Kanisa hilo ni Kanisa la KRISTO YESU. Hili Kanisa sio dhehebu fulani bali nin jumuiko la waabudui halisi waliookolewa na Bwana YESU na wanaliishi Neno lake la injili ya Milele, bila kujichanganya na maomvu ya dunia.


3. YESU alikuja ili aziharibu kazi zote za shetani zinazotesa watu.
 
1 Yohana 3:8b ''Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi.''

 
Hakuna kazi ya shetani inayoweza ikabaki maishani mwako kama kweli utamwamini YESU KRISTO na kumwomba MUNGU katika yeye huku ukiishi maisha matakatifu, huku ukilitii Neno la MUNGU na Kanuni zake.
Ndugu, usiishie kusherekea tu bali kubali YESU akufungue vifungo vyote vya shetani na mawakala zake, Kazi moja wapo iliyomleta Bwana YESU ni kuziharibu kazi zote za shetani. Hakuna ugonjwa usiopona na hakuna tatizo ambalo damu ya YESU haiwezi kulifuta. Kaa tu vizuri na MUNGU na husika na maombezi utafunguliwa hakika.
Kumbuka hakuna ugonjwa wowote ukiwemo na huo unaoujua wewe ambao YESU hawezi kuponya, Ona andiko hili likionyesha kwamba YESU anaponya magonjwa yote hata leo, kama alivyofanya tangu mwanzo wa injili.
Mathayo 9:35 ''Naye YESU alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.''

 
Katika maisha yangu mimi Peter nimehusika kuomba watu wanne na wakapona Ukimwi ambao ndio inawezekana ndio ugonjwa hatari zaidi, YESU huyu tunayemhubiri hakika aliwaponya. Hata wewe ukimwamini na kuhusika na yeye hakika utapona. Kila kifungo cha kichawi kinafutika kwa damu ya YESU KRISTO.katika jina la YESU KRISTO.


4.YESU alikuja kutupa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU.
 
Yohana 1:12-13 ''Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.''

 
Ukiwa mtoto wa MUNGU unakuwa unasehemu ya kuurithi/Kuupata uzima wa milele.
Kuwa mtoto wa MUNGU kunarudisha mahusiano yako na Muumbaji wako.
Kuwa mtoto wa MUNGU ina maana kubwa sana, hatuwezi kueleza yote hapa tukamaliza ila ni muhimu sana kuwa mtoto wa MUNGU.
Ndugu usisherekee tu bali hakikika unasherekea huku ukiwa mtoto wa MUNGU kupitia YESU KRISTO.


5. YESU alikuja kutafuta na kuokoka kila mwanadamu aliyekuwa amepotea.
 
Luka 19:10 '' Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. ''

 
Ukweli ni kwamba hakuna mwanadamu hata mmoja ambaye alikuwa hajapotea, hivyo YESU alipokuja kutafuta na kuokoa waliokuwa wamepotea maana yake kila mwanadamu anamwitaji Bwana YESU ili amuokoe.
Kumbuka kumpokea YESU kama Mwokozi wako ndio mwanzo wa kuabudu MUNGU katika kweli, hivyo kabla mtu hajampokea YESU kama Bwana Na Mwokozi wake hakika mtu huyo hata kama ana dini nzuri lakini kwa MUNGU aliye hai hakika mtu huyo amepotea.
Kumpokea YESU ndio kuutafuta uzima wa milele.
Ndugu, Usisherekee tu sikukuu huku umepotea maana YESU KRISTO sio Mwokozi wako, hakikisha kwanza unampokea YESU KRISTO kama Mwkozi wako na anza kuliishi Neno la MUNGU sasa.


6. YESU alikuja ili kutupa Mamlaka ya kumshinda shetani na mawakala zake.
 
Luka 10:19 ''Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.''

 
Mamlaka hata leo inajithihilisha ndani ya wateule wa KRISTO wenye imani, tunaweza tukaomba nguvu za giza zikakimbia, tunaweza tukaombea watu magonjwa yakawaacha, Kwanini nguvu za giza zikimbie? au kwanini magonjwa yatoke katika miili ya watu?
Ni kwa sababu YESU alikuja tukupa mamlaka na mamlaka hiyo iko ndani ya wateule wa MUNGU wote ambao wana imani na ni waombaji wanaoishi katika kusudi la MUNGU.
Ndugu, Usisherekee tu bali hakikisha una mamlaka ya kuwakimbiza wachawi, majini na wakuu wa giza wote. YESU KRISTO ndiye mwezeshaji wako, mpokee kama Mwokozi na anza kumsikiliza ROHO MTAKATIFU ili akuongoze kukufikisha katika kila kweli unayoihitaji, iwe ni kweli ya kuomba, iwe ni kweli ya kufanikiwa na kweli ya kila kirtu cha ki MUNGU ambacho ni stahiki yako.


7. YESU alikuja ili tusamehewe dhambi katika yeye.
 
1 Yohana 1:7-8 '' bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote''

 
Ni damu ya YESU KRISTO pekee inayoweza kufuta dhambi zako zote.
Ndugu, usisherekee tu huku hujampokea YESU kama Mwokozi wako na hujatubu dhambi zako na uovu wako na wala hujaacha hizo dhambi na uovu.
Ndugu tubu kwa MUNGU na hakika damu ya YESU KRISTO itazifuta dhambi zako zote hata kama ni dhambi mbaya sana. Baada ya kutubu hakikisha unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU Mwokozi.

Hizi ni baadhi tu ya sababu za Bwana YESU kuja duniani, nimesema kwa ufupi lakini ziko nyingi zaidi na za muhimu sana. Kama Kuja kwa ROHO MTAKATIFU, MUNGU aanze kuishi ndani yetu pamoja na kutimiza unabii wote wa tangu zamani.
Baada ya hayo nakutakia sikukuu njema.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments