MAMBO YALIYOTOKEA BAADA YA YESU KRISTO KUPANDISHWA MSALABANI.


Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe sana.
Karibu tujifunze ujumbe mfupi huu.


Luka 19:10 '' Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. ''

 
Hilo ndilo kusudi kuu la Bwana YESU kuja duniani.


Yohana 3:16-21 ''Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU.''

 
Najua unajua mambo mengi sana kuhusu safari ya wokovu wetu, leo niko msalabani tu nikitaka ujue yaliyotokea siku ile kuu na ya kipekee ya Bwana YESU kutukamilishia wokovu sisi tunaomtii.


Mambo gani yalitokea Baada ya YESU kupandishwa Msalabani ?

1. Pazia la hekalu lilipasuka ;
 
Mathayo 27:51a '' Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; ''

 
Hii inamaanisha ushindi mkubwa wa mkristo.
Pazia kupasuka kunamaanisha kuwekwa huru.
Kuondolewa kwa vizuwizi vyote mbele yako.
Ikumbukwe kuwa, pazia, liliwekwa kuwazuwia watu wasiingie wala hata wasiweze kupaona patakatifu pa patakatifu. Mahali hapa,aliingia kuhani peke yake. Baada ya pazia kupasuka, kizuwizi kiliondolewa kwa yeyote kufika hapo. Kifo cha Yesu msalabani, kimeondoa dhambi zako, kama ukimpokea na kutubu, kimekupa kibali cha kunena kwa lugha kwa raha zako.


2. Tetemekeo kubwa; 
 
Mathayo 27:51b ''nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka; ''

 
Tetemeko hili,liliambatana na giza nene,ikiwa ni ishara ya nguvu kubwa yenye utisho wa ajabu sana. Tetemeko hili, lilionesha uwezo ulio juu ya uwezo wote,nguvu inayozidi nguvu zote. tetemeko hili, lilidhihirisha kuwa kweli YESU ni mwana wa MUNGU, na yule mlinzi alishuhudia kwa kinywa chake.
Mathayo 27:54 '' Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda YESU, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa MUNGU. ''
Hata leo, maisha ya mtu aliyeokoka, yanapaswa kudhihirika mbele za watu wote, kuwa kweli kuna nguvu mpya na uweza wa ziada ndani ya mtu aliyeokoka.


3. Makaburi yalifunguliwa ;
 
Mathayo 27:52-53 ''makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala; nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.''

 
Baada ya YESU kushuka kuzimu, watakatifu walio lala, wote wakaamka, wakatangaziwa uzima upya, ndio maana Biblia inasema watakatifu hao wakauingia mji mtakatifu yaani wakaenda mbinguni, Wakawa katika uzima wa milele pamoja na YESU; baada ya YESU kumnyang’anya funguo za kuzimu ibilisi, akawa hana mamlaka tena, uwezo wake wote na mamlaka yote akawa amenyeng’anywa.
Nguvu ya msalaba, ni nguvu inayoshinda mauti. YESU ni zaidi ya mateso yote, ni zaidi ya kifo, ni zaidi ya magonjwa, ni zaidi ya kukata tamaa, ni zaidi ya umasikini, nguvu ya msalaba iko juu ya laana na vifungo vyote.


4. Tamko la Ushindi likatolewa ;
 
Yohana 19:30 ''alisema, IMEKWISHA. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake. ''

 
Tamko la ushindi lilitolewa rasmi YESU aliposema (Imekwisha). Kauli ya YESU iliashilia kufikia mwisho kwa mateso yote, uonevu, laana, mikosi na vifungo vyote. Kauli ya YESU inatufundisha nini aliposema Imekwisha? Kwa mtazamo wa ndani zaidi, ilimaanisha, kukamiliaka kwa kazi yake iliyomleta duniani ambayo ilikuwa ni ukombozi. Kumweka huru kila mtu ili asipotee, bali awe na uzima wa milele. Kwa maelezo mengine tuseme kuwa, Msalaba wa YESU, ulibadirisha Historia ya Ulimwengu wote na kuweka utamaduni mpya.


5. Msamaha wa dhambi ulitolewa; 
 
Kupitia mauti ya msalaba wa YESU, msamaha wa dunia ulitangazwa, hivyo kila anayeitii hakika anapokea msamaha wa dhambi bure. Mfano ni huu ambao ulitokea palepale msalabani.
Luka 23;42-43 '' Kisha(Mfungwa) akasema, Ee YESU, nikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. YESU akamwambia, Amin, nakuambia, leo hivi utakuwa pamoja nami peponi. ''

 
Kupitia kifo cha msalaba, toba kwa ulimwengu ilipatikana. Kifo cha msalabani, kinatupa maji ya uzima, kinatupa pumziko la kweli, kina tuhesabia haki. Wakati wayahudi walidhani wanamkomesha, kumbe agano la MUNGU linatimia kwa ulimwengu, kuwa Mtu hatafika mbinguni ila kwa njia ya YESU KRISTO. Kupitia kifo cha YESU, mlango wa kuiendea mbingu Ulifunguliwa wazi kwa wote wampokeao na makao yao yakaanza kuandaliwa tangu hapo. Hata leo, ukiokoka, makao yako yanaanza kuandaliwa leo.
Yohana 14:1-3 ''Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini MUNGU, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.''

 
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments