MAOMBI YA KUFUTA AGANO LA KIPEPO LA MUDA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
  Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze kisha tuombe maombi ya ushindi.
Agano maana yake ni patano.
Maagano ya muda ni mapatano yaliyoelekeza katika muda fulani tu.
Kuna aina mbili za maagano.
Kuna agano jema yaani agano la ki MUNGU na kuna agano baya yaani agano la kipepo.
Katika ulimwengu wa roho kila jambo lina majira yake, muda wake, wakati wake.
Mhubiri 3:1 '' Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''
 Kuhusu agano la ki MUNGU, Kama ulifanya agano fulani kwa MUNGU kwa wakati fulani basi unatakiwa kutimiza agano hilo.
Kama muda wa kutimiza jambo hilo umepita unatakiwa kutubu kwa MUNGU kisha timiza agano hilo.
Kama uliahidi kitu kwa kanisa au kwa mtumishi fulani wa MUNGU inakupasa kutimiza nadhiri hiyo uliyojiwekea wewe mwenyewe.
Nimegusia kwa sehemu juu ya agano jema ambalo wewe umeweka kwa MUNGU, Lakini kiini cha somo langu ni kufuta maagano ya muda ya kipepo.
Hosea 10:4 ''Hunena maneno yasiyo na maana; huapa kwa uongo wafanyapo maagano; basi ndipo hukumu huchipuka kama mbaruti katika matuta ya shamba.''
 Nilipopata ufunuo wa somo hili niliona kwenye maono Mwanamke  mmoja anateswa na ugonjwa fulani, mwanamke huyo ana miaka 33. Niliona katika maono hayo ugonjwa kama huo huo ulimtesa  mama yake mzazi kipindi akiwa na miaka 33,
 Kisha nikaona ugonjwa kama huo ulimpata bibi yake alipokuwa na miaka 33, niliona hadi bibi wa tatu wa Mwanamke huyo.
Hayo ni maagano urithi ya kipepo yaliyofungwa katika muda fulani kwenye maisha.
Kuna Binti  mmoja rafiki yangu alipewa  jina la bibi yake wa kambo kipindi anazaliwa, Bibi huyo wa kambo hakuzaa katika maisha yake yote. Binti huyu naye  baada ya kuolewa hata yeye uzao uligoma hadi miaka zaidi ya minne ikapita tangu baada ya kufunga ndoa, alikuja kufanikiwa baada ya kufuta maagano ya urithi kwa maombi.
Mawakala wa shetani wanaweza wakapanga jambo kwa mtu  ili ukifika muda walioupanga  basi mabaya hayo yanampata.
Inawezekana kabisa ratiba ya kipepo kukuhusu wewe ni kwamba wamekuwekea agano la kipepo la muda kwamba huruhusiwi kuoa/kuolewa katika umri kati ya 20 na 30, wengine wamewekewa agano la hivyo katika umri wa miaka 30 hadi 40. Unaweza ukashangaa mtu anapanga kuoa tangu akiwa na miaka 24 lakini anakuja kufunga ndoa akiwa na miaka 42, yuko ndugu yalimkuta hayo na alinisimulia.
Kuna baadhi ya matatizo uwe unachunguza ili kujua kama yaliwapata wazazi wako na babu zako katika umri huo ili kama ni maagano ya kipepo ya muda basi uyafute kwa damu ya YESU KRISTO.
YESU anaweza hakika kukuweka huru na kukutenga mbali na magano ya giza.
Ngoja nikushuhudie jambo hili ambalo mimi Peter nilifunuliwa kuombea kwa sababu ya hila za shetani. Baba yangu mzazi mzee Marko Mabula alifariki akiwa na miaka 30, Babu yangu mzaa Baba ambaye ni Mzee Mabula alifariki katika umri daraja sawa na la Baba mzazi hata Babu yake Baba yangu. Kuna kipindi nilipata msukumo mkubwa sana wa kuharibu hila za kishetani za kukatisha umri kwenye ukoo wangu, Nimeshavuka sasa huo umri wa Baba yangu lakini Nilipokuwa nakaribia kufikisha miaka 30 nilipata ajali mbaya ya gari nikiwa Zanzibar, hata madaktari walisema sitapona lakini kwa Neema yake Bwana YESU akaniponya na kunipa kazi ya kumtumikia.
Ndugu kuna vitu vingine vinaweza kumpata mtu kwa sababu ya maagano ya kipepo ya muda. Lakini ashukuriwe MUNGU maana kwa YESU KRISTO tunashinda na zaidi ya kushinda.
Inawezekana uliandikiwa kufa ukifikisha miaka fulani, leo lifute agano hilo la kipepo, Bwana YESU yuko tayari kukushindia hakika, Neno lake linamthibitisha na kusema kwamba 
 '' Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa.-Zaburi 102:20''
 Inawezekana uliandikiwa kufa lakini ukimtegemea Bwana YESU hakika wanaweza kufa wao hao mawakala wa shetani huku wewe ukisonga mbele.
Wakati tukiwa wadogo kijijini kulikuwa na Baba mmoja ambaye ilibidi asioe maana kila akiona mke wake anakufa mwaka wa kwanza wa ndoa, kwa sababu kijijini watu wengi walimjua basi ilibidi akaoe mbali lakini cha ajabu hata huyo mwanamke akafariki mwaka wa kwanza wa ndoa. Ndugu zangu shetani ni mbaya sana na leo futa kwa damu ya YESU KRISTO kila maagano ya shetani ya muda.
Kama walipanga kipepo kwamba ukioa/Ukiolewa tu mwenzi wako afe mwaka wa kwanza au wa pili wa ndoa, leo futa agano hilo la muda, lifute kwa damu ya YESU KRISTO Mwokozi aliye hai milele.
 Kama walipanga kila mtoto wa kwanza au wa mwisho katika familia yenu au ukoo wenu awe anakufa mapema tena bila kuumwa, leo futa agano hilo la muda la kipepo.
Chunguza katika ukoo wenu au familia yenu au jamii yako kama yako matatizo aina moja na ambayo huwapata wahusika katika majira ya aina moja, kama ni agano la kipepo futa kwa damu ya YESU KRISTO.
Haiwezekani iwe katika ukoo wenu tu kwamba kila mtu akifikisha miaka 40 anaumwa kisukari na kupoooza na Pressure.
Nimewahi kumuombea Baba mmoja wa miaka 40 ambaye alikuwa anaumwa Bp na akaniambia kwamba Baba yake mzazi alikufa kwa bp na babu yake pia alikufa kwa bp, ndugu mengine huwa ni maagano ya kishetani ya muda.
Hakikisha Bwana YESU  anakuweka huru leo mbali na maagano ya kipepo ya muda.
Yohana 8:36 '' Basi Mwana(YESU) akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. '' 
Juhudi yako kwa YESU ndio itakufanya uwekwe huru mbali na vifungo vya giza.
Dada mmoja ambaye tulikuwa tunaabudu naye kanisani alikuwa na ugonjwa wa ajabu. Yeye kila akiingia kwenye siku zake anaumwa na kuwa katika hali ya mahututi, wakati mwingine anazimia, yeye alidhani ni jambo la kawaida kabisa kwake maana lilimtokea kila mwezi. Siku moja katika ibada ya jioni tulipomaliza ibada akazidiwa pale kanisani, nilipomuuliza hakujibu lolote bali akamwambia mke wangu, na mke wangu ndiye akanijulisha. Ikabidi tumuombee na katika kuomba akalipuka mapepo na tulipozidi kuomba mapepo yakamtoka na tangu siku hiyo kila akiingia katika siku zake yuko salama hadi ilibidi ashuhudie kanisani, ndugu sio kila tatizo ni kawaida tu, chunguza na kama ni agano la kipepo la muda ambalo linakupata wewe katika muda fulani tu basi lifute agano hilo kwa damu ya YESU KRISTO.
Kama ni wewe mwenyewe ulingia agano la kipepo la muda hakikisha unalifuta kwa damu ya YESU. 
Kama wachawi walikufunga agano la kupata mabaya muda fulani wa maisha yako hakikisha unafuta mipango hiyo ya giza kwa maombi,  ukipata msukumo wa sadaka hiyo nayo ni muhimu sana maana Sadaka njema kwa MUNGU hutengeneza agano na MUNGU hivyo kuwa ni rahisi sana maagano ya giza kukuacha, Hakikisha tu sadaka yako inaambatana na maombi ya Mtumishi wa MUNGU.
Zaburi 50:5 ''Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu.''

KAZI ZA AGANO LA MUDA LA KIPEPO.

 1. Matatizo au uharibufu uliokusudiwa vinakupata katika muda huo wa agano.
Isaya 28:15 '' Kwa sababu mmesema, Tumefanya agano na mauti, tumepatana na kuzimu; pigo lifurikalo litakapopita, halitatufikia sisi; kwa maana tumefanya maneno ya uongo kuwa kimbilio letu, tumejificha chini ya maneno yasiyo kweli; ''
Agano na mauti ni agano na uharibifu, lazima uharibifu huo ukupate usipojua kukaa vizuri kwa MUNGU.

2. Kukufanya ufeli kila jambo muda huo wa agano ukifika.
 Yohana 10:10a  '' Mwivi(Shetani) haji ila aibe na kuchinja na kuharibu;''
 Kazi moja wapo ya shetani ni kukufanya usifanikiwe katika kila jambo, huko ndiko kufelishwa kipepo.

3. Kukufanya ulitumikie kusudi la shetani 
Kutoka 23:32 ''Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao. '' 
Tangu zamani MUNGU anawaonya watu wake kujiepusha kufanya agano la kipepo, maana agano la kipepo linaweza kukufanya ulitumikie kusudi la shetani.

4. Kuteswa na vifungo vya  kila namna katika muda huo.
Isaya 42:22 ''Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.''
 Kuibiwa kipepo, kutekwa na shetani, kunaswa kwenye mashimo, kufichwa gerezani, hivyo ni vifungo vya aina mbalimbali vya kipepo ambavyo mtu asiyejitambua anaweza kufungwa vifungo hivyo, kumbuka kujitambua ni kumkimbilia Bwana YESU ili akuweke huru.

JINSI YA KUFUTA AGANO LA MUDA LA KIPEPO.

1. Tubu juu ya chanzo kilichosababisha agano la kipepo kukupata.
Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''

2. Omba maombi ukitumia damu ya YESU KRISTO kufuta maagano hayo ya muda.
Ufunuo 12:11 '' Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.''
 Utamshinda shetani kwa damu ya YESU KRISTO na kwa Neno la MUNGU.

3. Haribu madhabahu za giza zilizotengeneza agano la kipepo la muda, haribu na watenda kazi wa kipepo
Kumb 7:5 '' Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata
na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni 
MAOMBI YA KUFUTA AGANO LA KIPEPO LA MUDA ULILOFUNGWA KIPEPO.
Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea.


 MAOMBI YA KUFUTA AGANO LA KIPEPO LA MUDA.

 JEHOVAH MUNGU Unayeishi pokea sifa, heshima, utukufu, sifa na adhama yote.
Ninakushukuru MUNGU Baba maana uliniumba ili nikuabudu.
Ninakushukuru MUNGU Baba kwa ajili ya ufunuo wa leo na naomba ee BWANA kwa msaada wako leo nimshinde shetani na kazi zake zote.
Mawakala wa shetani hawakujua kama nitajua siri yao waliyonifunga nayo, lakini leo nimegundua na maagano yao yote ya muda kunihusu mimi nayafuta kwa damu ya YESU KRISTO.
MUNGU Baba ninatubu mbele zako BWANA kwa kila jambo ambalo ni mimi nilisababisha hadi nikafungwa maagano ya kipepo ya muda, naomba unisamehe BWANA na naomba hati za mashitaka katika ulimwengu wa roho kunihusu mimi zifutike kwa jina la YESU KRISTO.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai sasa ninafuta kila agano la kipepo la muda lililoelekezwa kwenye maisha yangu.
Agano la kipepo la muda la kunifunga ufahamu, ninalifuta agano hilo la muda la giza, nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO katika, jina la YESU KRISTO.
 Agano  la giza lililofunga ndoa yangu ili kila muda fulani ukifika amani isiwepo, ninalifuta agano hilo la muda la giza, nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO katika, jina la YESU KRISTO.
Agano la muda la kufilisika kila kipindi fulani kikifika,ninalifuta agano hilo la muda la giza, nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO katika, jina la YESU KRISTO.
Agano la muda la ajali na balaa na majanga,ninalifuta agano hilo la muda la giza, nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO katika, jina la YESU KRISTO.
Agano la kipepo la kuzuia uzao, ninalifuta agano hilo la muda la giza, nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO katika, jina la YESU KRISTO.
Agano la kipepo la kuzuia kuoa/kuolewa,ninalifuta agano hilo la muda la giza, nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO katika, jina la YESU KRISTO.
Agano la kipepo la muda la kunizuia kupata kazi, ninalifuta agano hilo la muda la giza, nalifuta kwa damu ya YESU KRISTO katika, jina la YESU KRISTO.
Kila agano la kipepo la muda lililowekwa na mawakala wa shetani nalifuta agano hilo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Kila agano la mchawi, mganga, mshirikina, mwanga au mkuu wa giza ninalifuta agano hilo kwa damu ya YESU KRISTO katika jina la YESU KRISTO.
Sasa naharibu kila madhabahu ya giza iliyotengeneza agano la kishetani la muda ili kunidhuru au kuniharibia, naibomoa na kuivunja madhabahu hiyo, kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO na iharibike hiyo madhabahu.
Madhabahu ya kwa mganga au kwa mchawi ninaiharibu kwa jina la YESU KRISTO.
Ninaziangusha madhabahu zote za giza kama Neno la MUNGU linavyosema katika Kumbu 7:5 kwamba ''Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.''
Sasa naangusha ngome zote za giza na naharibu madhabahu zote za giza.
Kuanzia sasa niko huru kwa jina la YESU KRISTO.
Ndoa yangu iko huru kwa jina la YESU KRISTO.
Maisha yangu yako huru, kwa jina la YESU KRISTO.
Ndugu zangu na familia yangu ipo huru, kwa jina la YESU KRISTO.
Ufahamu wangu uko huru,kwa jina la YESU KRISTO.
Afya yangu iko huru,kwa jina la YESU KRISTO.
Bishara yangu iko huru, kwa jina la YESU KRISTO.
Ndoa yangu iko huru, kwa jina la YESU KRISTO.
Uchumba wangu uko huru, kwa jina la YESU KRISTO.
Kila kitu changu kiko huru kuanzia leo, katika jina la YESU KRISTO aliye hai
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda.
Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 3 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri ikiambatana na maombi kutoka kwako na kwa mtumishi hai wa Bwana YESU juu ya ukomo wa kuteswa na maadui katika ulimwengu wa roho
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa BWANA YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.


Comments