MTUMISHI USIKUBALI KUJIONA WEWE NI BORA KULIKO WATUMISHI WENGINE WA KRISTO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mteule wa KRISRO nisikilize kwa makini mimi Mtenda kazi mwenzako katika shamba la Bwana YESU Mwokozi.
Moja ya kosa kubwa analoweza kulifanya Mtumishi wa MUNGU ni kujiona kwamba ni yeye tu aliyeitwa huku wengine wamejiita, hivyo anataka wawe chini yake
Mtumishi wa MUNGU akijiona yeye ni bora kuliko wengine ni makosa makubwa.
Biblia inasema kwako Mtumishi hai wa KRISTO unayeishi maisha matakatifu huku ukimtumikia MUNGU kwamba " Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.-Wafilipi 2:3-4"


Hivyo Mtumishi mmoja wa MUNGU akijiona kwamba ni yeye tu aliyeitwa ni makosa makubwa.
Nimewahi kusikia kwa sauti kadhaa watumishi Fulani kila mmoja akisema kwamba yeye ndiye nabii pekee Tanzania. Huo ni uongo.
Mtumishi mwingine akasema yeye ndiye nabii mkubwa pekee, huo ni uongo.
Kwa hali hiyo inaweza ikatokea siku moja mtu mmoja akasema yeye ndiye Mchungaji au Askofu pekee Tanzania au Kenya au Congo, au Uganda au popote pale, huo ndugu zangu ni uongo.
Hakuna nabii pekee, mtume pekee, mwalimu pekee, Mchungaji pekee wala mwinjilisti pekee.

Leo kuna maeneo majengo ya Kanisa yanazuiliwa kujengwa katika baadhi ya maeneo na mzuiaji mkuu  ni Mtumishi wa MUNGU aliye na kanisa kijiji hicho muda mrefu..
Mchungaji mmoja ambaye ni rafiki yangu aliomba MUNGU ampe pesa za kununua kiwanja cha kujenga Kanisa. Alipata Eneo na kulipia kisha kujenga Kanisa dogo la muda yaani la miti na bati basi, kama mita 100 kutoka pale kwenye Kanisa jipya kuna Kanisa lingine na Mchungaji alipoona katika mtaa huo kuna Kanisa limeanzishwa akawa ndio wa kwanza kulipiga vita, akafika hatua hadi anafundisha waumini wake kwamba vikanisa vidogo inabidi waombe maombi ya kuvifuta na kuvifunga.Kanisa lililojengwa ni kutoka madhehebu ya kiroho kabisa yanayofanya vizuri Tanzania. Hakika kama ni hivyo tunakoelekea ni kubaya. Kwa sababu huyu naye ni Mtumishi wa MUNGU na hajajipeleka hapo ili kuanzisha Kanisa jipya bali ni MUNGU amempa hapo hakika ni hatari kama MUNGU akiingilia kati. Yaani watu wa Kanisa ndio hao hao wanakuwa chanzo cha kuzuia kanisa kuenea na huku wakihubiri kwamba injili lazima iendelee mbele, hilo ni tatizo.
Kuna wachungaji hutunga hata uongo ili kuwazushia wachungaji katika maemeo yao ili wakimbiwe na washirika, anayezushiwa ni Mtumishi halisi wa Bwana YESU na anahubiri injili halisi ya Wokovu na utakatifu, chuki na kugombea washirika kumeharibu kuongezeka kwa Kanisa la KRISTO katika baadhi ya maeneo.
Siku moja nilimsikia Mtumishi mmoja ambaye ni Mchungaji Maarufu alisema kwenye mahubiri yake kwa njia ya Tv kwamba katika eneo liliko kanisa lake vimakanisa vidogo vimeshafungwa na ambavyo bado vipo viko mahututi, hayo ni mahubiri ya Mtumishi wa MUNGU anayetaka kanisa liongezeke, hilo ni tatizo kubwa.
Leo kuna vijana na mabinti wanahangaika sana kuhusu suala la kufunga ndoa kwa sababu tu watumishi ndio kikwazo. Mtumishi mmoja alimkataza mwimbaji wa Kanisani kwake asiolewe na kijana wa Kanisa jirani, ni makanisa ya Wokovu yote. Katika watumishi kabisa baadhi ya maeneo kuna changamoto sana na ambazo mimi naziona kama pando la shetani kulivuruga Kanisa la MUNGU duniani. Mchungaji naweza akamvuruga mshirika kwa sababu tu ya chuki au hampendi, Mshirika yule mwaminifu kwa KRISTO anapohama kanisa wanamtangaza kwamba ameasi na mbinguni haendi, hiyo sio kibiblia na kujifurahisa nafsi tu isivyo sahihi.
Mtumishi mmoja maarufu nilimsikia siku moja katika mahubiri yake kwenye TV akisema kwamba Yeye ndio Mchungaji na wengine watabaki kuwa wainjilisti tu, hiyo sio kibiblia bali ni sifa za kijinga.

Biblia inasema kwamba kwa wote tuliookoka na tunaishi maisha matakatifu mtu atuhesabu kwamba sisi wote tu watumishi wa MUNGU.

1 Wakorintho 4:1-2 " Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu."

Wote tuliookolewa na Bwana YESU tu watumishi wa MUNGU na kazi yetu ni kuupa faida ufalme wa MUNGU.
Mteule wa MUNGU usikubali kuwa mtukanaji.
Leo kuna watu wa kanisa hutukana sana na watu hao huona matusi kuwa ni jambo la kawaida kabisa.
Ndugu, matusi hayatakiwi kuwapo katika wateule wa KRISTO.
Kuna watu wengine ni vielelezo kabisa lakini hata wao wamejaa matusi hivyo kuwafanya na walio chini yao kuwa watukanaji.
Mwenyekiti wa kwaya ukiwa mtu wa matusi hakika unaweza ukaifanya kwaya kujaa matusi, na chungeni msije mkaimba matusi na mipasho.
Mzee wa kanisa kuwa mtukanajj inaweza kuwafanya baadhi ya watu kanisani kuona kutukana ni jambo la kawaida tu.
Mama Mchungaji kuwa mtukanaji unaweza kuwafanya wamama kujaa matusi na umbea tu.
Mchungaji, Askofu, Mwinjilisti n.k hakikisha huwi mtukanaji.
Biblia inasema kwamba wateule wa MUNGU haipasi kuwa watukanaji .

Tito 3:2-4 "wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote. Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana. Lakini wema wake Mwokozi wetu MUNGU, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, alituokoa;"


 Ndugu, Kuna vikao vingine wewe uliyeokoka hutakiwi kukaa.
Ukikaa vikao kama hivyo kitakutoa katika uwepo wa MUNGU.
Ukikaa kikao kama hicho utashiriki dhambi na unaweza kupata madhara mengi sana.
Mfano jiulize ofisini kwenu kuna kikao cha siri ili kumfukuza kazi mfanyakazi mwenzenu ambaye hana kosa hata moja ila ni chuki tu za wanadamu, mtu kama huyo akifukuzwa kazi na akalia mbele za MUNGU huponi.
Mtu kama huyo akimkumbusha MUNGU juu ya uaminifu wake kazini na kanisani na jinsi alivyokuwa anamtolea MUNGU zaka na sadaka na kutoa michango yake kupeleka kazi ya MUNGU hakika huponi, unaweza wewe ukapata majanga na umasikini mkubwa ukiwa kazini kuliko yeye uliyeshiriki kumuondoa kazini na sasa yuko nje ya kazi.
Kuna vikao vingine wewe mteule usishiriki maana kesi inaweza kukugeukia wewe kumbe wewe ulikuwa ni mgeni mwalikwa tu ila hajitambui.
Mnaweza mkakaa kikao kuwasema vibaya wazazi wenu kabisa, ni hatari sana.
Mimi binafsi huwa najiuliza Mara mbili mbili juu ya vikao vya baadhi tu ya watu na sio watu wote.
Mnaweza mkakaa kikao ili kumuondoa Mchungaji, Askofu au kiongozi fulani wa serikalini lakini kama mtu huyo amewekwa hapo na MUNGU na kwa kusudi la MUNGU huku akiishi maisha safi mbele ya MUNGU hakika kikao hicho ulichoshiriki wote mnaweza kupata ukoma na wewe ukiwemo.
Kumbuka akina Haruni na Miriamu walipata ukoma kwa sababu ya kuitamani nafasi ya Musa aliyopewa na MUNGU.
Viko vikao vingi sana na vingi vimejaa chuki, upendeleo, kuoneana na ushetani. Unaweza ukashirikisha ili ufanyike sehemu ya tatizo.
Ndugu hudhuria vikao kwa kusudi la MUNGU na sio la wanadamu au la shetani.

1 Petro 1:13-15 '' Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake YESU KRISTO. Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''

Usimdharau aliye chini yako sasa maana baadae anaweza kuwa juu kuliko wewe.
Mfano hai ni Yusufu, yeye alikuwa mtumwa wa Potifa na Potifa hadi aliamua kumfunga Yusufu Gerezani kutokana na uongo wa mkewe Potifa. Lakini ghafla Yusufu akawa bosi wa Potifa maana Yusufu alitoka Gerezani na kwenda Ikulu kuwa makamu wa Rais wa nchi.
Jifunze kitu kwa mfano huu kwamba Yusufu alikuwa Mtumwa wa Potifa na kwa ghafla sana yaani kwa siku moja akawa bosi wa Potifa.
Pia ajabu ni kwamba Yusufu alipoinuliwa hakumfunga Gerezani Potifa wale mkewe Potifa.
Ndugu usimdharau aliye chini yako Leo maana inawezekana ni huyo huyo akaja kuwa juu yako sana baadae.
Na wewe uliye chini Leo siku ukiwa juu ya wanaokutesa Leo usikubali kulipiza kisasi au kuwaonea.
Biblia inakuonya kwamba " Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya MUNGU; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena BWANA.-Warumi 12:19
Inawezekana kitendo cha wewe kuwa juu yao waliokutesa zamani tayari hicho ni kisasi cha MUNGU kwao na kitawatesa miaka miaka mingi.
Ndugu wewe hakikisha hulipizi kisasi.
Na kumbuka unaweza pia ukapandishwa lakini usipomtii MUNGU na Neno lake hakika unaweza ukashushwa kuliko Mwanzo hivyo mche MUNGU wakati wote kuanzia Leo.
Mtii KRISTO Nyakati zote kuanzia Leo.
Usidhani utabaki chini tu siku zote, na wewe uliye juu sasa usimdharau aliye chini yako sasa maana ghafla unaweza kushangaa amekuwa juu yako.

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments