NJIA TATU(3) ZA PEKEE ZA KUMPATA MKE/MUME MWEMA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.

Bwana YESU atukuzwe sana ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mimi Peter Nimeshawahi kuulizwa sana kuhusu jinsi ya kumpata Mke Mwema au mume mwema. Namshukuru ROHO MTAKATIFU maana ni leo najibu swali hilo kwa wote, vijana na mabinti.
Kabla sijaendelea ngoja nikuwekee msingi mzuri wewe unayetaka kuoa au kuolewa.
Kumcha MUNGU ndio chanzo cha kumfanya mwanaume awe mume mwema.
Mitathali 1:7 ''Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu.''
Kumcha MUNGU ndio chanzo cha kumfanya mwanamke awe mke mwema. Wewe unayetaka kuoa/Kuolewa tafakari hilo kwanza kabla ya mengine yote.

Kumbuka kama anataka mfanye dhambi mkiwa wachumba tu basi hapo ucha MUNGU ni 0%.
Anayetaka muonjane kwanza kabla ya ndoa huyo hakupendi, mwambie wewe sio mchuzi hata uonjwe kabla ya ndoa. Wengi sana wameachwa kwa sababu ya kukubali ujinga huo ambao shetani huutumia kupanda mapando ambayo kuyang'oa hushindikana. Japokuwa ni mzuri wa sura lakini kama story zake ni za uovu tu hakika huyo sio mcha MUNGU.
Kumbuka pia kwamba kumpokea YESU KRISTO kama BWANA na Mwokozi ndio mwanzo wa kuabudu katika kweli.

Warumi 10:13 '' kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la Bwana(YESU) ataokoka. '' 
Jambo jingine ni kwamba Yale yasiyowezekana kwa wanadamu, kwa MUNGU yanawezekana.
Wapo watu wanaishi kwa mashaka na wasiwasi sana juu ya labda hawataolewa kabisa maishani mwao na wanaume wanasumbuka labda hawatapata mke wa kuoa kabisa maishani mwao.
Ndugu, Nimeyaona mengi yalishindikana kwa wanadamu lakini hayo yote kwa MUNGU yaliwezekana kupitia maombi na maisha safi ya Wokovu wa KRISTO.
Yeremia 32:27 ''Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza? ''
Ndugu endelea kuomba na kuishi maisha matakatifu hakika yasiyowezekana kwa wanadamu, kwa MUNGU yanawezekana.
Binafsi mimi sidhani kama MUNGU aweza kutushushia wenza kama embe. Hivyo baada ya maombi si mbaya hata binti kuweka mawasiliano mazuri na vijana wenye kumpenda MUNGU huku akimuomba MUNGU kwa bidii japo si vema amuweke kichwani kana kwamba anataka ndio awe huyo huyo...... Laweza kuwa chaguo lake sasa. Lakini ni muhimu kujua vijana kwamba hata kama unasugua goti ili upate mwenzi kama utabaki umejifungia Nyumbani huyo mchumba hutampata. Mabinti walioomba sana kuhusu wachumba na hawajafanikiwa naomba kuwashauri: Binti ni Hapana kupeleka application kwa kijana ila ni lazima wakati mwingine uonekane kwenye macho hao vijana.
Kuonekana kwako kwao sio ukajionyeshe kwamba upo bali ni kwa kufanya kazi za MUNGU na matendo mema.
hiyo ndio application yako. 
Kwa sababu umeomba hakika kibali kilichozaliwa kwa maombi yako ndicho kitaongea na sio wewe ila atakayefanikiwa ni wewe, naamini binti amenielewa.
Hakuna ushindi bila mapambano. Hiyo ndio application ya binti, sio wale wa nimeonyeshwa ila hajui alionyesha muda gani na hana uhakika alionyeshwa na nani
Kuna wengine kwa ujinga wao hujiingiza kwenye dhambi ya uasherati. Hao Wanaojiingiza kwenye uzinifu ni kwa sababu ya kutokujitambua tu maana 
Mwenye hofu ya MUNGU hakika atatenda kwa akili na utakatifu


Kwa ambaye una mpango wa kumtumikia MUNGU na bado hujaoa au kuolewa naomba kukushauri yafuatayo.
 
1. Mke/ Mume wako ni wa thamani sana katika kuyafanya maono yako yakafika katika ubora sahihi.

 1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''
Mke wako au mume wako anatakiwa kuwa muendelezaji wa maono yako na sio mtu wa kuyaua.
Omba MUNGU akupe mtu ambaye atayabeba maono yako ya kumtumikia Bwana YESU na sio kumpata mtu wa kuyaua maono yako.


2. Ukimpata mke/ Mume ambaye hatalibeba kusudi la MUNGU la kuitwa kwako katika Wokovu wa KRISTO basi utambue kwamba huduma yako itashindwa kusonga mbele.
 1 Timotheo 2:3-4 ''Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu; ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.''
 
Leo wapo waliokuwa waimbaji wazuri kabla hawajaolewa au kuoa lakini baada tu ya kuingia kwenye ndoa huduma waliacha maana waliwapata wenzi ambao hawaiendelezi huduma bali wanaiua.
Wapo waliokuwa wanahubiri na wapo waliokuwa wanamtumikia MUNGU kwa juhudi kubwa sana kipindi hawajaingia katika ndoa. Lakini baada ya ndoa hata kuwahi kanisani kunafutika na hata huduma inafutika, ni hatari sana sana.


3. Ndoa yenye amani na furahi itasaidia sana kuwafanya mtimize huduma zenu.

2 Kor 7:1 '' Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha MUNGU.'' 

Hivyo MUNGU akupe mtu ambaye anajua kumcha BWANA ni nini.

4. Omba MUNGU akupe mtu ambaye anatambua wewe ni nani na unatakiwa ufanye nini katika kazi ya MUNGU.
 1 Kor 4:1 ''Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU.''

Ukimpata mtu wa hivyo hakika atakuhimiza na kukukumbusha ili utekeleze wajibu wako kwa Bwana YESU.


Mimi Peter Naamini utapata ndoa njema na, wewe ambaye uko katika ndoa naamini uko sehemu sahihi na kama unaona hauko sehemu sahihi basi unaweza ukamwomba MUNGU aitengeneze ndoa yako ili iwe sahihi maana kwa maombi ya imani katika KRISTO YESU kila kitu kinawezekana.

Tatizo lingine kubwa ni mabinti na vijana wengi hawajikubali.
Ndugu, Wewe mwenyewe hujikubali.
Je nani akukubali?.
Wewe mwenyewe hujipendi,
Je nani akupende?.
Kila alichokiumba MUNGU ni chema sana(Mwanzo 2:19) Wasiwasi wa nini?

Kama wewe umejidharau, itakuwa ngumu watu kukuheshimu.
Kama wewe umejikataa, itakuwa vigumu watu kukukubali.
Kama umejidharau tambua kwamba hakuna atakayekuheshimu maana wewe mwenyewe umejidharau.
Kama umejikataa hakuna mtu atakukubali maana wewe mwenyewe umejikataa.
Ndugu, unahitaji kujiheshimu kwa kuishi maisha matakatifu ndipo na watu watakuheshimu.

Unaweza usiolewe kwa sababu tu wewe mwenyewe hujikubali kama unafaa kuwa mke mwema wa mtu.
Unaweza usipate wa kumuoa kwa sababu wewe mwenyewe hujielewi wala kujikubali kama unafaa kuwa mume mwema wa mtu.
Zaburi 96:7-9 '' Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, Mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake, Leteni sadaka mkaziingie nyua zake. Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu, Tetemekeni mbele zake, nchi yote.''

Sasa ajabu unaweza kukuta mtu amekubali Kuchezewa akitarajia Kuolewa?
Kama ni wewe nakupa  Pole Sana Maana Unaweza Ukakosa Ndoa Na Ukakosa Na Mbingu Pia.

Ndugu unahitaji kujikubali huku ukimcha MUNGU kwa usahihi wote ndipo na watu watakukubali.
Baada ya hayo niliyokueleza ya muhimu sana sasa naingia katika kiini cha somo langu la leo.

 Njia 3 pekee za kumpata mke/Mume Mwema.


1. Kupenda.
Mwanzo 29:17-18 ''Naye Lea macho yake yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso.
18 Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo.'
'

Katika andiko hili hatuoni Yakobo akiambia na watu jinsi ya kumpenda Raheli, hatuoni Yakobo akiota ndoto kwamba Raheli atakuwa mkewe ndipo ampende. Yakobo alimpenda Raheli automatic na likawa ni kusudi la MUNGU kabisa. Kuna watu hujulishwa watu sahihi wa kuwaoa au wa kuolewa nao kwa njia ya kuwekewa tu upendo kuwahusu.
Tatizo kubwa la vijana wengi ni kumwekea MUNGU mashariti kwamba hadi waone kwa ndoto ndipo wataamini kwamba waliowaona kwenye ndoto ni watu sahihi.
Ndugu nisikilize itakusaidia, kuna vyanzo vitatu vya ndoto. Kuna ndoto ambayo chanzo chake ni MUNGU, Kuna ndoto ambayo chanzo chake ni shetani na kuna ndoto inayotokana na unayoyawaza sana na kuyafikiri, ndoto hii chanzo chake ni Binadamu. Ndoto yab kundi moja tu ndio huwa ndoto sahihi, ni ile ambayo chanzo chake ni MUNGU. Sasa wewe unayesuburi ndoto ndipo uthibitishe kwamba huyo kijana au huyo binti ndio wa kwako una uhakika gani kama ndoto hiyo ni ya MUNGU?
Ni kweli MUNGU anasema sana kwa njia ya ndoto lakini usimlazimishe MUNGU kusema kwa ndoto, wakati mwingine upendo tu unatosha kukujulisha kwamba huyo mtu ni sahihi. Wengi sana wakati wakingoja MUNGU awasemeshe kwa ndoto shetani huwani kuwaletea ndoto na kuwachanganya, wakati mwingine hujikuta wanaota ndoto kwa sababu kila mara wanawazia watu hao wanaowahitaji kwa ajili ya uchumba kisha ndoa.
Ndugu yangu, upendo tu unaweza kuamua kama ni kweli huyo Mchumba ni sahihi kwako au sio sahihi.
Kumbuka ni lazima uoe unayempenda au uolewe na unayempenda 
Hesabu 36:6 ''BWANA ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila ya baba zao.''
Biblia haijasema kwamba waolewe na waliowaota ndotoni bali waolewe na wanaowapenda.
Ndugu yangu, kama ulikuwa hujui siri naomba utambue leo kwamba Upendo tu unaweza kukujulisha kwamba huyo mchumba anakufaa.
Jiulize kuna wanawake wangapi wazuri kuliko yeye na wenye sifa kuliko yeye, lakini wewe umempenda yeye tu?
Jiulize kuna vijana wangapi wazuri na wana sifa nyingi kuliko huyo kijana lakini wewe moyo wako uko kwake tu?
Wakati mwingine upendo tu hujulisha kwamba huyo ni mtu sahihi kwako.
Muhimu tu chunguza chanzo chako cha upendo kwake.
Isiwe unampenda sana lakini kwa sababu ya sura, umbo, mali, elimu n.k
Kuna somo nitalileta lina kichwa cha somo kinachosema UMEMPENDEA NINI HUYO MCHUMBA WAKO?
Kuna ufafanuzi mrefu huo na utaelewa zaidi juu ya kipengele cha upendo.
Nakufundisha haya kwa sababu nimepitia haya, mimi nilikuwa naomba na najitamkia kabisa kwamba ''Leo MUNGU atanijulisha kwa ndoto kuhusu ni nani anafaa kuwa mke wangu''
Nilisubiri ndoto lakini wakati huo hazikuja, na wakati huo kuna mabinti zaidi ya watatu ambao tumejuana mtandaoni tu wala hawajawahi kuniona live lakini walinijulisha wamefunuliwa kwa ndoto kwamba mimi ni Mume kwao, nilijua kabisa huo ni uongo wa shetani maana haiwezekani MUNGU aseme na watu watatub tofauti kwa mwezi mmoja. Sikuwakatisha tamaa lakini niliwaambia kwamba mimi ninaye tayari mchumba nimpendaye sana, lakini nilikuwa sina, ila sikutaka wanifuatilie kwa sababu nilijua ni waongo.
Kwa Neema ya MUNGU nilikuja kumuoa mrembo wangu Scholar na hadi tunachumbiana nilishangaa maana MUNGU alisema nasi kwa njia ya tofauti kabisa na nilivyodhani.
Ndugu ni muhimu ujue kwamba upendo unaweza kuwa njia ya kukujulisha usahihi wa huyo unayemtarajia. Kuna mtu alijikuta anampenda ghafla kijana mmoja wanayeabudu naye kanisani, alijaribu mno kukemea na wakati mwingine alifunga na kuomba ili kufuta upendo ndani yake kuhusu huyo kijana lakini alishindwa, na baadae walikuja kufunga ndoa na hadi leo ni wanandoa wanaopendana sana sana na ndoa yao ni nzuri sana.
Naamini umenielewe katika kipengele hiki.


2. Amani ya KRISTO.

Wakolosai 3:15 ''Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.''
Amani ya KRISTO ni moja ya njia ambazo ROHO MTAKATIFU hutumia kutujulisha sisi wateule wake.
Unaweza ukampenda sana binti fulani au kijana fulani na ukajua kabisa upendo huo sio wa kawaida kwa hiyo kulingana na njia ya kwanza tuliyojifunza unaweza ukadhani kwamba hakika huyo ni wa kwako, lakini ukiona amani moyoni mwako inaondoka kuhusu mtu huyo au kuhusu jambo hilo hakikisha unasitisha kwanza kuendelea na taratibu za uchumba kuelekea ndoa.
Amani ya KRISTO lazima iamue ndani yako hivyo ikiondoka amani ya KRISTO kila wakati ukiliwazia jambo hilo kuhusu mtu huyo unayetaka kuingia naye katika ndoa naomba utambue yafuatayo.
a. Inawezekana mtu huyo sio sahihi kwako hata kama unampenda, hivyo amani inaondoka kama njia ya kukujulisha kwamba huyo hakufai.

b. Inawezekana kuna uharibifu utakupata kama ukimkubalia huyo, hivyo amani inaondoka ndani yako ili ujue kwamba hautakiwi kuendelea na mtu huyo.

c. Inawezekana mtu huyo ni wakala wa shetani ili kukuharibia maisha yako au kiroho chako, hivyo japokuwa kwa jinsi ya kawaida hana tatizo, lakini msema kweli ambaye ni amani ya KRISTO anaondoka ndani yako kama sehemu ya kutaka ujue kwamba mtu huyo hakufai.

d. Inawezekana MUNGU hayuko pamoja na wewe katika suala hilo, ndio maana amani yake inaondoka kama sehemu ya wewe ujue kwamba jambo hilo halikufai.

e. Inawezekana mtu huyo ni sahihi kwako na atakuja kuwa mkeo au mumeo lakini kwa sasa hutakiwi kuanzisha uchumba na yeye, hivyo amani ya KRISTO inaondoka ndani yako wakati huo ili kukujulisha kwamba unatakiwa uachane na jambo hilo kwa sasa au uingie kwenye maombi ya kufunga kwanza.


Kama kweli wewe unammcha MUNGU Baba, umeokoka na ROHO MTAKATIFU yuko ndani yako hakika ukimpenda mtu fulani na  ukatamani mfunge ndoa hakika unapoanza tu kumuwazia amani ya KRISTO itaamua ndani yako, ukiona una amani na jambo hilo endelea nalo na ukiona huna amani achana nalo.
Amani ya KRISTO lazima iamue ndani yako.
Amani ya KRISTO kwa jina jingine inaitwa amani ya MUNGU.
Wafilipi 4:7 ''Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU.'' 
 
Wewe sasa ni mali ya KRISTO hivyo hawezi kukuacha uingie sehemu mbaya, muhimu tu msikilize yeye na Neno lake na amani yake iamue ndani yako.
Ni mambo mengi tu ambayo baadhi ya watu wameniuliza au wameniambia lakini rohoni kwa njia ya amani ya KRISTO niligundua  hila  hivyo sikushughulika. Siku moja kuna mtu alinipigia simu rohoni nikakosa amani na wakati huo huo nikajua ananirekodi huku akiniuliza maswali ya mitego, nilichokifanya kwa sababu nimetahadharishwa hakika nilikuwa namjibu kwa maandiko tu huku siongei sana hadi akakata simu.
Amani ya KRISTO ni lazima iamue ndani ya wateule wa MUNGU katika kila jambo.
Hata katika kumthibitisha mchumba hakika amani ya KRISTO tu inaweza kukujulisha kwa usahihi kabisa.
Muhimu tu chunguza amani inayoamua ndani yako ni amani gani, maana wengine amani ya kibinadamu ndani yao ndio inaamua na sio amani ya KRISTO.
Mfano, Unaweza ukakuta Binti anasema hana amani na kijana fulani anayetaka kumchumbia kumbe amani haipo kwa sababu kijana yule hana pesa au sio msomi.
Hivyo unatakiwa pia kuchunguza  ni amani gani inaamua ndani yako, kama ni amani ya KRISTO hakika hiyo inajua jambo mwisho kabla ya mwanzo hivyo izingatie sana.

3. Ufunuo.

Ufunuo ni kitu kilichokuwa kimefichwa na sasa unakijua na kukifanyia kazi.
1 Kor 2:10 ''Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.''
Kazi mojawapo ya ROHO MTAKATIFU ni kutufunulia mafumbo.
Kuna mambo ili ujue ni lazima ROHO wa MUNGU akujulishe.
Kuna njia nyingi  ambazo ROHO MTAKATIFU anaweza kukujulisha ili ujue.
Baadhi ya njia hizo ni ndoto, maono, mazingira, Neno la MUNGU la ufunuo, Watumishi wa MUNGU kukujulisha na Sauti ya moja kwa moja ya ROHO MTAKATIFU.
Hata katika kumfahamu mtu sahihi kwako, MUNGU anaweza kukujulisha kwa ndoto au kwa maono, huo ni ufunuo kwako ili ujue.
MUNGU anaweza akakusemesha   kwa sauti ya moja kwa moja ya ROHO MTAKATIFU.
MUNGU anaweza akakusemesha kwa njia ya mazingira tu uliyopo, mazingira tu yanaweza kukujulisha kwamba sasa unatakiwa uolewe, uoe na katika mazingira hayo unaweza kujikuta unampenda mtu na ukawa na amani moyoni hivyo mnafunga ndoa takatifu.
MUNGU anaweza akawatumia watumishi wake kukujulisha na kukufumbulia mafumbo ya nani ni sahihi kwako.
Unaweza ukapewa andiko la Biblia na hilo likakujulisha kabisav juu ya nani ni sahihi kwako, unaweza ukasoma somo kama hili na ukajikuta unaamua vyema.
Kufunuliwa ni njia mojawapo ya MUNGU kukuthibitishia jambo hivyo usidharau kile ambacho MUNGU anakuambia kupitia njia hizo nilizokutajia.
Jilidhishe kwamba ni MUNGU amesema na wewe.
Hizo ndizo njia tatu za pekee za kumjua mke/mume mwema wako.

Nakupa kanuni hii na nakuomba uizingatie na utafanikiwa.;
=MUNGU anatembea kwa upendo.
=MUNGU anatembea kupitia amani ya KRISTO.
=MUNGU anatembea kwa ufunuo kutoka kwake

Endelea kufuatilia na kwa Neema ya MUNGU utafaidika sana na injili ya mahali hapa.
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments

Unknown said…
barikiwa sana,
Unknown said…
Njia ya kwanza umesema kumpenda na ukimpenda lakini yeye kwako hana muda na wewe?