SABABU YA MTU KUSHINDWA KUFANIKIWA KIROHO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Nafasi ya wewe kuwa katika mambo ya MUNGU muda mwingi ni moja ya faida kuu kwako inayoweza kukufanya kufanikiwa sana kiroho.
Nafasi ni ya muhimu sana.
Ni muhimu pia kujua kwamba nafasi inatafutwa hivyo itumie vyema nafasi yako uliyopewa na MUNGU.
Umepewa nafasi ya kuokoka, itumie vyema.
Umepewa nafasi ya kuomba, itumie vyema.
Umepewa nafasi ya kuhubiri na kufundisha, itumie vyema.
Umepewa nafasi ya kushuhudia, itumie vyema.
Kila nafasi uliyopewa na MUNGU itumie vyema kwa utukufu wa MUNGU.
Kumbuka ukimtumikia MUNGU zaidi utapata zaidi na utapata upendeleo.
MUNGU ukimtumikia kwa uaminifu atakupeleka panapo nafasi.
Zaburi 18:18-21 " Walinikabili siku ya msiba wangu, Lakini BWANA alikuwa tegemeo langu. Akanitoa akanipeleka panapo nafasi, Aliniponya kwa kuwa alipendezwa nami. BWANA alinitendea sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu akanilipa. Maana nimezishika njia za BWANA, Wala sikumwasi MUNGU wangu."


Usikubali kuifanya kazi ya MUNGU hovyo Bali ifanye kazi ya MUNGU vizuri na kwa moyo wa unyenyekevu kwa MUNGU.
Baada ya utangulizi huo sasa nakuletea kiini cha ujumbe wangu wa leo.

SABABU YA MTU KUSHINDWA KUFANIKIWA KIROHO.

1. Dhambi.

1 Yohana 3:4-10 ''Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. Nanyi mnajua ya kuwa yeye(YESU) alidhihirishwa, ili aziondoe dhambi; na dhambi haimo ndani yake. Kila akaaye ndani yake hatendi dhambi; kila atendaye dhambi hakumwona yeye, wala hakumtambua. Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. Kila mtu aliyezaliwa na MUNGU hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na MUNGU. Katika hili watoto wa MUNGU ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na MUNGU, wala yeye asiyempenda ndugu yake. '' 
Dhambi ndio kikwazo cha kila kitu katika maisha ya Mwanadamu, dhambi pia ni sababu kuu inayoweza kumzuia mtu kufanikiwa kiroho.
Mtu akitawaliwa na dhambi atakuwa ni mtu wa kiburi, kujihesabia haki, hasira na kila hila inayomfanya awe mbali na utii kwa Neno la MUNGU.
 

2. Kusubiri mtu mwingine akufanyie maamuzi yako kiroho.

Ezra 10:4 ''Inuka; maana shughuli hii yakuhusu wewe; na sisi tu pamoja nawe; uwe na moyo mkuu, ukaitende.'' 
Andiko hili ni mfano hai wa Mtu anayetakiwa kufanya majukumu ya  ki MUNGU yeye binafsi na sio kutegemea wengine.
Hata wewe kusubiri mwingine afunge maombi kwa ajili yako kutamfanya yeye akue kiroho na sio wewe.
Kama unasubiri hadi Baba au Mama yako akushauri kuachana na marafiki wabaya, hakika utakuwa unajichelewesha wenyewe kukua kiroho.
Watu wengine wanatakiwa kuwa mashahidi tu lakini mtendaji ni wewe.
Inawezekana ROHO wa MUNGU hukusemesha mambo mengi lakini huwa mpaka watu fulani wakushauri kuhusu hayo ndipo utende, ndugu kuna majukumu yanakuhusu wewe binafsi hivyo kukuwa kiroho tambua kwamba kunatokana na wewe kumtii MUNGU na Neno lake tu.
Biblia inasema '' Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari.-Mika 7:5''
Maamuzi ya kiroho unapaswa uyafanye wewe mwenyewe binafsi na sio wengine wakufanyie maamuzi.
Kwanini watu wengi husubiri watu wengine wawafanyie maamuzi yao ya kiroho?
Ni kwa sababu wao hawajiamini, ndugu jiamini sasa.
Ni kwa sababu wao hawajielewi, ndugu jielewe sasa.
Ni kwa sababu wao hawajitambui, ndugu jitambue sasa.
 Ni kwa sababu Wao wanajitambua kwamba hawana mamlaka ya kiroho sahihi wakati sio kweli.
Wana matatizo ya kiroho ndio maana wao hawawezi. 
Hawamjui MUNGU vyema na kanuni zake.
Hawajui nafasi zao kiroho.
Ndugu, Kusubiri mtu mwingine akufanyie maamuzi yako kiroho ni kujichelewesha mwenyewe kufanikiwa kiroho.
Watu wa aina hii ni  waoga wa kuthubutu ndio maana hawafanikiwi kiroho.

3. Kutokulifanyia kazi Neno la MUNGU.

Yakobo 1:22-24 '' Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.''
Ni muhimu sana kulifanyia kazi Neno la MUNGU kama kweli unataka kukua kiroho na kufanikiwa kiroho.
 
Kwanini ulifanyie kazi Neno la MUNGU?
Ili utembee kwenye kusudi la MUNGU na ufanikiwe kiroho.
Ili usihame kutoka kusudi la MUNGU.
Ili likuongezee Imani ya ushindi wako.
Ili kwa hilo umshinde shetani.
Ili umpendeze MUNGU
Kwa sababu ROHO MTAKATIFU analitumia Neno la MUNGU kukusaidia kiroho ili ufanikiwe na kustawi.
Ili upate kushinda na zaidi ya kushinda.

4. Kukata tamaa mapema.

Luka 18:1 '' Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba MUNGU sikuzote, wala wasikate tamaa.'' 
Watu wengi sana hukata tamaa mapema sana ndio maana hawafanikiwi kiroho.
Unapokata tamaa maana yake humwamini MUNGU.
Ukitaka kufanikiwa kiroho hakika usikubali kukata tamaa.
Dada mmoja aliniambia kwamba amevumilia sana kuhusu kupata mchumba lakini hakufanikiwa hivyo rafiki yake amemshauri kwenda kwa mganga. Niliumia sana baada ya kusikia maneno hayo kwa sababu kwa mganga alienda kupata vifungo vya kipepo ambavyo vinaweza kumtesa kuliko hata angeamua tu kuvumilia.
Ndugu, kumbuka MUNGU hukupa unachostahili na sio kila unachoomba.
Kila jambo na majira yake hivyo ni heri kusubiri majira yako huku ukiwa zizini mwa Bwana YESU na sio kutaka kwenda kuyatafuta majira yako kwenye mbwa mwitu wakali na simba porini huku wewe ukiwa ni kondoo, hakika mbwa mwitu hao na simba watakutafuna, hapo ndipo unasikia kuna mtu amekufa kiroho hadi akiona watu wa kanisani anajificha.
Vyanzo vya mtu wa MUNGU kukata tamaa.
Kutokumjua MUNGU na nguvu zake.
Kutokumtegemea MUNGU.
Kutegemea akili zako.
Kukosa maombi sahihi.
Kutolizingatia Neno la MUNGU.


5. Kuridhika mapema na kujiona hahitaji msaada.
 
1 Kor 8:2-3 '' Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote bado, kama impasavyo kujua.  Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo amejulikana naye.''
Hapa napo ni watu wengi sana wamekwama na kushindwa kabisa kufanikiwa kiroho.
Kuna mtu imefika kipindi hata kanisani haendi na Biblia na wala habebi Daftari ya kuandika hasa aikimjua Mhubiri wa siku hiyo, mtu kama huyu anajiona anajua lakini ukweli ni kwamba hakuna anayelijua Neno la MUNGU zaidi ya ROHO MTAKATIFU hivyo ukijiona unajua na huhitaji msaasa hakika kuna maeneo kufanikiwa kiroho hutaweza.
Kuna watu makanisani kwao huwa hawaendi ibadani hadi wasikie kuna mhubiri mgeni kaja, huko ni kujizuia mwenyewe kufanikiwa kiroho.
Sisi tuliookoka wote Biblia inatuita ni wanafunzi wa YESU, tunajifunza kwa YESU na kwa jinsi hiyo maisha yetu yote sisi ni wa kujifunza kwa Bwana YESU hivyo mtu kujiona ametosheka hata hahitaji tena kitu kutoka kwenye Injili hakika huyo anajipoteza taratibu taratibu.
Ndugu, usikubali kuridhika mapema na wala usijione kwamba huhitaji msaada kutoka kwa wateule wenzako.
 
6. Kushindwa kuzitumia mbinu za kiroho na mafanikio.

Waefeso 6:10-13 '' Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika BWANA na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za MUNGU, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.''
Kuna mbinu nyingi sana za kiroho ambazo zinaweza kukufanya umshinde shetani na wapambe wake wote hata imani yako ikaongezeka na kukua sana kiroho.
Mbinu zote za kiroho ziko na ROHO MTAKATIFU tu kupitia Neno la MUNGU hivyo ukitaka uzijue mbinu za kiroho za kukufanya ufanikiwe kiroho hakikisha  unamtii ROHO MTAKATIFU na kuenenda katika yeye huku ukilisoma na kulitafakari sana Neno la MUNGU.
Kwa mfano hai ni kwamba kuna mamlaka nne za Mteule wa MUNGU ambazo kwa hizo mtu huyo lazima ashinde kila nguvu za giza na kwa hizo afanikiwe kiroho na kukua sana kiroho.
Mamlaka hizo ni;
a. Jina la YESU KRISTO
b. Damu ya YESU KRISTO.
c. Neno la MUNGU.
d. Nguvu za ROHO MTAKATIFU. 
Je unajua nini juu ya kila kilichomo ndani ya kila mamlaka katika hizo nne hata uweze kufanikiwa kiroho?
Ndugu unahitaji sana kujua kila mbinu za kiroho ili ushinde na kufanikiwa kiroho.
Ndugu mmoja alikuwa na vita kubwa sana na kila mwaka katika familia yao walikuwa wanazika, kwa miaka minane mfululizo ndugu wanane wa tumbo moja walikuwa wamefariki na walikuwa wamebaki wanne tu lakini ndugu huyo akaamua kutoa sadaka na kuombewa ili kusitishwa kwa mpango huo wa shetani wa kuua familia hiyo kila mwaka, hakika baada ya pale vita ile ikakoma, hiyo ni mbinu ya kiroho ambayo yeye binafsi aliipaa kwa ufunuo na akashinda.
Ndugu mmoja yeye alijua kabisa yuko hatarini kwa sababu ya maagano ya madhabahu za giza ambazo zilikuwa zinawafuatilia, yeye akaamua kumtumikia MUNGU kwa juhudi akijua kabisa ya kwamba MUNGU atamlinda na kila hatari maana anamtumikia. Hakika MUNGU alimlinda maana anamtumikia kwa uaminifu, hiyo nin mbinu mojawapo katika mbinu maelfu. Ndugu unahitaji kujua mbinu za kiroho ili ushinde.
 Mbinu ni kanuni kwa jina lingine. Jua kanuni  za kubarikiwa kwako, jua kanuni za wewe kulindwa na MUNGU, jua kanuni za kutunza nguvu za ROHO MTAKATIFU ndani yako n.k
 
7. Kukosa maombi au kuomba vibaya

Yakobo 4:3 'Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. ''
Watu wengi sana hawafanikiwi kiroho kwa sababu ya kukosa maombi, inawezekana hata wewe hujafanikiwa kiroho kwa sababu wewe sio muombaji.
1 Thesalonike 5:17 ''  ombeni bila kukoma; ''
Na wengine japo ni waombaji lakini huomba vibaya.
Hawamsikilizi ROHO wa MUNGU katika maombi yao.
Wanaomba kwa tamaa zao n.k

 
8. Kuna wateule wana mamlaka lakini hawana nguvu, ndio maana mamlaka yao haifanyi kazi.

 Waefeso 3:20-21 " Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika KRISTO YESU hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina."
Labda hujaelewa, ngoja nifafanue.
Iko hivi Kuna Wakristo hawana nguvu za rohoni ndio maana mamlaka yao haifanyi kazi vyema.
Nguvu za mteule ni maombi, maisha matakatifu, kulijua Neno la MUNGU na kulitumia katika kusudi la MUNGU.
Mamlaka ya KRISTO ndani ya mwamini ni kuu sana lakini inaweza isifanye kazi kama mwamini huyo hana maombi, utakatifu na Neno la MUNGU.
Ukiwa na nguvu hakika mamlaka yako itafanya kazi.
Ukiwa hauna nguvu basi mamlaka yako hata kama ni kubwa haitafanya kazi.
Kama hauna maombi hakika mamlaka ya MUNGU ndani yako haitafanya kazi vyema.
Kama hauishi maisha matakatifu tambua kwamba dhambi usifanyazo zinaiondoa nguvu ya MUNGU ndani yako.
Tambua kwamba unahitaji kuliishi Neno la MUNGU, kulitafakari na kulitumia ili mamlaka ya MUNGU ndani yako ifanye kazi.
Ndugu Yangu, kama moyo wako hauna Neno la MUNGU basi hakika nguvu ya MUNGU ndani yako itakuwa vigumu kufanya kazi.


Jambo lingine ni hili,Usipofurahi wengine wakitendewa muujiza na MUNGU, hata wewe itakuwa vigumu kupata miujiza ya MUNGU.
Kuna watu akisikia wengine wanashuhudia matendo makuu ya MUNGU waliyotendewa, wao huchukia.
Kama unachukia wengine wakitendewa muujiza na MUNGU maana yake hukutaka wapate miujiza hiyo, au wewe ndio ulikuwa kizuizi cha wao kupokea lakini wamekazana na maombi ndio maana wamepokea.
Mimi nasema hivi; kama huwa una tabia ya kuchukia wenzako wakishuhudia miujiza yao basi hakika itakuwa vigumu na wewe kupata miujiza ya MUNGU hata kama wewe ni muombaji mzuri.
MUNGU anajua maisha ya kila mmoja wetu.
Ndugu hakikisha unaishi katika mema maana MUNGU anakuona na hakuna siri mbele zake.

Leo nataka nikushauri uwe unamtegemea MUNGU asilimia zote.
Kwa mfano kama unaumwa usimpe daktari au hospital fulani nafasi kwenye moyo wako hata kama wanakutibu, bali mpe MUNGU nafasi moyoni mwako ndipo utapona.

Jambo Jingine ni kwamba ukishughulika juu ya kazi ya MUNGU na MUNGU atashughulika na mambo yako.
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments