UMEITWA NA MUNGU KUFANYA NINI?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU atukukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kama Mtumshi wa MUNGU ni muhimu sana kujua umeitwa katika nini.
1 Kor 4:1-2 ''Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU. Hapo tena inayohitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.''
Hebu jifunze kupitia ujumbe huu wenye shuhuda kidogo za kihuduma upate mwanga na kuijua huduma yako na ujue utumikeje kwa YESU KRISTO Mwokozi.
1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA.''
 
Ukishajua umeitwa katika nini.
 
1. Ijue huduma yako.
 
2 Timotheo 4:5 '' Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.''
Mimi Peter Mwaka fulani tarehe 2 mwezi wa 4 ROHO wa MUNGU aliniambia kwamba ameniita kuwa mwalimu wa Neno la MUNGU, na hata somo hili unalojifunza leo ni la 772 tangu mwishoni mwa mwaka 2012.
Hapo nikaijua huduma yangu hata kama sikupenda sana huduma ya ualimu lakini aliyenipa anajua hiyo tu ndio inanistahili na sio zile huduma ninazozitamani mimi.
Inawezekana wewe umeitwa katika huduma nyingine tofauti na mimi, Ndugu hakikisha unaijua huduma yako

2. Ijue vita inayopinga huduma yako.
 
2 Timotheo 4:1-2 ''Nakuagiza mbele za MUNGU, na mbele za KRISTO YESU, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake;  lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho.''
 
Katika huduma yako lazima uijue vita yako.
Inawezekana vita yako ni kusemwa vibaya.
Inawezekana una maono makubwa lakini ukiwashilikisha watu wanakucheka na kukusharau.
Inawezekana wewe ni mwimbaji na vita yako ni kwamba shetani anataka uimbe kidunia ndio maana sasa uko nusu kwa nusu. Wakati mwingine unaweza kuwa na vita kubwa kiroho kutokana na huduma yako, lakini kama ni MUNGU alikupa huduma hiyo hakikisha unasonga mbele.
Mfano mimi kama Mwalimu wa Neno la MUNGU vita yangu kubwa inahusiana na Neno la MUNGU.
Kwa jinsi hiyo nimewahi kutukanwa hadi na watumishi mbalimbali wa MUNGU. Nimeshawahi kuambiwa sana mambo ambayo natakiwa kufundisha ambayo ROHO wa MUNGU hanipi kufundisha kwa sasa. Mfano masomo kuhusu nyota, mafuta ya upako n.k nimejikuta siwezi kufundisha maana rohoni sipewi kufundisha japokuwa watumishi wengi hufundisha.
Mwimbaji anaweza akaangaliwa katika sauti, nyimbo, style za kucheza na mwonekano wake kwa ujumla kama kweli ana hofu ya MUNGU sahihi.
Mwalimu nitaangaliwa katika Neno la MUNGU zaidi.
Kumbuka kuna watu kazi yao sio kujifunza bali kazi yao ni kukosoa hata ambapo hapastahili.
Wengine kwa sababu ya kuzoezwa na watumishi na wengine kwa sababu ya kushika mafundisho ya dhehebu na sio mafundisho injili ya KRISTO ni lazima kama Mwalimu ukutane na vita kali. Hata wewe ndugu una huduma hivyo hakikisha unaijua vita yako hata kabla haijaja.

3. Vijue vipaombele ulivyopewa na ROHO MTAKATIFU katika huduma yako.
 
1 Kor 12:4-11 ''Basi pana tofauti za karama; bali ROHO ni yeye yule.  Tena pana tofauti za huduma, na Bwana(YESU) ni yeye yule.  Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali MUNGU ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa ROHO kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa ROHO apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo ROHO yeye yule; mwingine imani katika ROHO yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika ROHO yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda ROHO huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye. ''
 
Hata katika karama moja pekee unaweza ukakuta kila mtu amepewa vipaombele vyake.
Mfano kwa walimu wa Neno la MUNGU.
Kuna ambao wamepewa kuweka misingi.
Mfano kuna mwingine amepewa kuweka msingi wa maombi, mwingine utakatifu, mwingine utoaji, mwingine nguvu za ROHO MTAKATIFU na Mwingine toba.
Kuna wengine wala sio walimu wa kuweka misingi bali ni walimu waendelezaji wa misingi ambayo ilikwisha kuweka na wengine.
Mimi kwa mfano nimepewa vipaombele hivi; kufundisha watu wamjua MUNGU wa kweli, waokoke, wafunguliwe na waishi maisha matakatifu.
Kila somo langu huwa natamani ''Awemo YESU akifungua na kuokoa''. Siku moja nilisikia sauti ikisema ''Usiishi kwa sababu tu unaishi bali ishi kwa sababu YESU KRISTO anaishi ndani yako.''
Inawezekana wewe ni kihuduma ni Mchungaji au mtume na vipaombele vyako ni kufungua makanisa.
Wapo watu wamepewa kufundisha kuhusu ROHO MTAKATIFU, Hata kama wanafundisha mambo mengine lakini kiini ni ujumbe kuhusu ROHO MTAKATIFU.
Wapo watu wamepewa Neno la siku za mwisho, hata kama anguhubiri ni lakini bado angekutahadhalisha juu ya siku hizi za mwisho.
Kuna Mwingine ameitwa kufufua vipawa katika watu wa MUNGU.
Kila mmoja kuna kipaombele chake alichopewa.
Inawezekana wewe ni mwimbaji na vipaombele vyako ni watu waijue njia ya kweli kupitia mahubiri yako kwa njia ya uimbaji. Changamoto ni pale ambapo unakuwa mwimbaji na kipaombele chako ni kimoja tu yaani kurekodi, hiyo ni hatari. 
Kuna Nyimbo za baadhi ya waimbaji maarufu kabisa lakini wamesema maneno wakidai ni Biblia inasema , Kwa sababu hawasomi Biblia basi wanakuwa wanafundisha kitu cha uongo. Unatakiwa uijue huduma yako na ujue kwamba Msingi wa kila huduma na kipawa katika KRISTO ni Wokovu, toba na utakatifu na yote hayo yako katika Biblia, ukiwa mbali na Biblia unaweza ukadanganya.

4. Yajue mambo ya kuyaepuka ili yasiue huduma yako.
 
Zaburi 34:14 ''Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. ''
Vijue vikwazo vikuu vya kukwamisha huduma yako
Mfano Mwalimu epuka kujiona wewe unajua kila kitu hata ambacho hujui, Uwe makini na maswali, Vita yako wakati mwingine inaweza kutokea kwa baadhi ya  watumishi, ikiwa wewe  unasimamia Neno na wao wanasimamia taratibu za dhehebu.
Mwimbaji epuka mashindano na mitindo ya kidunia. Epuka dhambi, epuka kiburi, kumbuka hata yaliyomwangusha shetani ambaye naye alikuwa mwimbaji.
Mchungaji Epuka kuwasema vibaya wachungaji wenzako, epuka kujiona ni wewe tu uliyeitwa, wewe hubiri injili basi.
Mtume epuka kujiona wewe ndio kaka yao akina Mchungaji, walimu, mwinjilist na nabii.
Nabii epuka kusema jambo kutoka kwenye akili zako tu n.k
Inawezekana kabisa kuna mambo zaidi ya kumi unayotakiwa kuyaepuka katika huduma yako. Hakikisha unayajua na ujue jinsi ya kuyaepuka.

5. Mtii ROHO MTAKATIFU na Neno la MUNGU kuliko chochote.
 
Yohana 14:26 '' Lakini huyo Msaidizi, huyo ROHO MTAKATIFU, ambaye Baba(MUNGU) atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. ''
Hata karama tulizonazo zinaitwa zawadi za Neema hivyo mtoaji ni ROHO MTAKATIFU na yeye humgawia kila mtu kama apendavyo yeye ROHO MTAKATIFU.
Tungekuwa tunachagua sisi kama basi inawezekana kabisa kuna baadhi ya karama na huduma zisingekuwepo japokuwa kwa Kanisa zinatakiwa karama zote na huduma zote zifanye kazi.
Bila ROHO MTAKATIFU ujue wewe huwezi. Ukimkataa ROHO MTAKATIFU wewe umemkataa YESU KRISTO na Umemkataa MUNGU Baba hivyo hufai kuitwa mtumishi wa MUNGU.
Zaburi 32:8 '' Nitakufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea; Nitakushauri, jicho langu likikutazama.''
Kubali ROHO MTAKATIFU akuonyeshe njia.
Kubali ROHO MTAKATIFU akushauri huku akikutazama na kukusimamia.

6. Uwe mtu wa Neno la MUNGU muda wote.
 
Zaburi 119:130 '' Kufafanusha maneno yako kwatia nuru, Na kumfahamisha mjinga.''
Neno la MUNGU ndilo hukupa ufahamu sahihi.
Neno la MUNGU ndilo huleta nuru ya KRISTO ndani yako na kuondoa giza ndani yako.
Neno la MUNGU ndilo hukufanya usiwe mjinga katika mambo ya kiroho.
Mjinga ni mtu yule ambaye hajui kitu ila akijulishwa anaelewa, hata wewe kuna mambo unahitaji kujulishwa na Neno la MUNGU ndipo utaelewa vyema.
Jifunze na tafakari sana Neno la MUNGU.
Hata katika karama yako au huduma yako uliyopewa na MUNGU hakikisha unakuwa ni mtu wa Neno la MUNGU.
2 Timotheo 2:15 '' ''Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na MUNGU, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli.''

7. Lijue Neno kuu la Biblia kwamba ni ''Wokovu wa KRISTO''
 
Katika ulichoitwa kwacho hakikija mada kuu ni kwamba YESU KRISTO anaokoa na kufungua kwa wanaoamua kumpokea Kama Mwokozi wao.
Tambua kwamba shabaha ya Biblia ni MUNGU kumleta YESU KRISTO duniani kwa ajili ya kazi moja tu yaani kuwaokoa wanadamu.
Yohana 3:16-18 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''
Hivyo katika utumishi wako hakikisha kwa hali zote unawapeleka watu kwenye kuokolewa na Bwana YESU KRISTO.
 YESU hakuja kukufanya uwe maarufu au kukufanya watu wakunyenyekee  bali alikuja kuokoa wanadamu
Luka 19:10 '' Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.''
Hivyo timiza huduma yako katika Wokovu wa KRISTO YESU.
Kumbuka ukijifanya unajua kila jambo utageuka falisayo.
 
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292.
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments