ITUMIE VIZURI NEEMA YA MUNGU ULIYOPEWA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Umeingia mwaka mwingine inakupasa kujua wakati uliopita ulikosea wapi, ili wakati huu  utengeneze kwa MUNGU.

Ni muhimu kujua kwamba Wateule wa KRISTO tumeokolewa kwa Neema ya MUNGU, tunaishi kwa Neema ya MUNGU, tutaenda uzimani kwa Neema ya MUNGU, tupo hai Leo kwa Neema ya MUNGU, tumekuwa watu wa KRISTO kwa Neema ya MUNGU.
Waefeso 2:8 " Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU;"

Lakini sasa baadhi ya watu huitumia vibaya neema ya MUNGU waliyopewa.
Neema ya MUNGU haitakiwi kuambatana na maovu wala dhambi.
Tunatakiwa kuitumia vizuri Neema ya MUNGU tuliyopewa
Tukitaka tuishi vyema na neema ya MUNGU ni vyema tukajifunza Neema ya MUNGU imebeba nini na inataka nini?
Hapa nataka tuangalie kitu muhimu sana kwamba neema ya MUNGU inataka nini.
Biblia inatusaidia.
Tito 2:11-13 " Maana neema ya MUNGU iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa KRISTO YESU, MUNGU mkuu na Mwokozi wetu;"


1. Neema ya MUNGU inatutaka kuacha dhambi, uovu na makosa

2 Timotheo 2:19 " Lakini msingi wa MUNGU ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, BWANA awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la BWANA na auache uovu."

2. Neema ya MUNGU inatutaka kukataa mambo ya kidunia yaliyo machukizo.

1 Yohana 2:15-17 " Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele."

3. Neema ya MUNGU inatutaka tuwe na kiasi na tuishi maisha ya haki.
 
Tito 2:12 "........ tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa;"


4. Neema ya MUNGU inatutaka tuwe watauwa.
 
Zaburi 37:28 '' Kwa kuwa BWANA hupenda haki, Wala hawaachi watauwa wake. Wao hulindwa milele, Bali mzao wa wasio haki ataharibiwa.''


Utauwa maana yake ni ucha MUNGU.
Mtauwa maana yake ni mtu anayemcha MUNGU kwa moyo wote na kwa dhati.


5. Neema ya MUNGU inatutaka kumtazamia Mwokozi YESU KRISTO.

Waebrania 12:2" tukimtazama YESU, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha MUNGU."

  Neema ya MUNGU inaweza ikahusisha maeneo mengi  sana lakini sio wote wanafanyia kazi neema ya MUNGU.
Kuna watu wanapewa nafasi za kumtumikia MUNGU lakini wanakataa. 
Kisha nafasi hiyo ikiondoka watu hao hujaribu kuitafuta nafasi hiyo ya kumtumikia MUNGU lakini hawaipati.
Ndugu, ukipewa rohoni msukumo wa kumtumikia Bwana YESU unaanza kumtumikia. 

Nafasi hiyo ikipita unaweza kuja kuitafuta sana na usiipate.
Ukipewa nafasi ya kumtumikia MUNGU hakikisha unamtumikia kwa uaminifu na juhudi maana ukiiachia nafasi hiyo, unaweza kuja kuitafuta sana baadae na usiipate.
Nwasaliana na watu wengi, wengi katika hao husema kwamba waliwahi kumtumikia Bwana YESU zamani lakini kwa sasa kila wakijaribu wanashindwa. Wengi husema "Natamani niwe kama wewe lakini sijui nianzie wapi na sijui nianzeje".
Ndugu mmoja akiwa na miaka 76 baada ya kufunguliwa na kujua kwamba ataulizwa mbinguni ya kwamba alifanya mambo gani ili kuupa faida ufalme wa MUNGU ikamsumbua sana, ndipo akatangaza kwa uchungu huku akilia akisema kwamba " Sasa naanza kumtumikia Bwana YESU maisha Yangu yote"

Mtu kama yule hata akitumika ni vyema sana lakini hawezi kufika maeneo ambayo angefika akiwa kijana wa miaka 30. Mfano awe mhubiri au mwinjilisti naamini kabisa asingeweza kufanya kazi ya MUNGU kwa nguvu ukilinganisha na angekuwa kijana.
Kama sasa anaweza kushuhudia Nyumba 4 anachoka nahakika angekua kijana angeshuhudia Nyumba 10 bila kuchoka.
Ndugu Yangu, ukipewa nafasi Leo ya kumtumikia Bwana YESU hakikisha unaanza kumtumikia, ukidharau hakika unaweza kuja kuitafuta baadae nafasi ya kumtumikia MUNGU na usiipate.

Wakorintho 15:58 " Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."

Ndugu itumie vizuri Neema ya MUNGU.
Hata katika maisha yako ya kila siku hakikisha unaitumia vizuri Neema ya MUNGU.
Nakukumbusha tu kwamba kila aliye katika safari ya mbinguni hujitakasa katika KRISTO.
1 Yohana 3:2-3 ''Wapenzi, sasa tu wana wa MUNGU, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa(YESU), tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo. Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu.''

 
Biblia inaposema kwamba ujitakase haina maana kwamba uendelee na dhambi kwa sababu nafasi ya kujitakasa utakuwa nayo.
Biblia inakutaka uache dhambi na uishi maisha ya utakaso.
1 Petro 1:14-15 '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''

 
Maisha ya waenda mbinguni ni maisha ya utakaso.
Utakaso maana yake ni hali ya kupata baraka ya MUNGU ya kusafishwa dhambi, ni hali ya kutakaswa.
Maisha ya wateule wa KRISTO ni maisha ya utakaso.
Ndugu, husika zaidi na toba katika maisha yako na usikubali kufanya dhambi tena.

Hata kama wewe ni kiongozi wa kiroho ni muhimu kutambua kwamba Kiongozi mzuri wa kiroho ni lazima ajue kujitambua kwanza ni vipi yeye awe, ndipo atapata nguvu kuwaambia wengine ni vipi wanatakiwa kuwa.
Kiongozi aliyezoelea dhambi itakuwa sio sawa kuwaambia wengine waache dhambi.
Kiongozi anatakiwa kujitambua kwamba anatakiwa kuziacha dhambi zote ndipo apate nguvu za kuwakataza wengine kutenda dhambi.

Ndugu usiichezee Neema ya MUNGU.
Usiidharau Neema ya MUNGU kwako.
Umepata Neema ya uzima ili umtumikie KRISTO YESU.
Umepata Neema ya MUNGU ya baraka ili umtolee MUNGU sadaka na fungu la kumi sahihi.
Umepata Neema ya MUNGU ya kuwa hai leo ili ulitumikie sasa kusudi la MUNGU ambalo ni kuokoka.
Ndugu itumie Vyema Neema ya MUNGU ya Wokovu na usikubali Neema ya wewe kuokoka ikupite katika maisha yako yote.
 Hata kama ndugu zako hawataki uokoke, ndugu hakuna ndugu yako hata mmoja atakayekwenda na wewe siku ukiondoka duniani. Uzima wa milele una kuhusu wewe binafsi hivyo usiangalie watu wanavyokubeza juu ya uamuzi wako wa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
Kumbuka kama  kuna watu wanakupenda basi hata wanaokuchukia wapo muhimu timiza wajibu wako kama mtoto wa MUNGU uliyeokolewa kwa neema. na hayo mengine mwachie JEHOVAH MUNGU.
Ndugu nakuomba usiishi kwa sababu tu unaishi bali ishi kwa sababu YESU KRISTO anaishi ndani yako.
Yeye Bwana YESU anasema kwamba kama ukimpokea kama Mwokozi na ukatubu hakika yeye YESU na BABA yake watakuja na kufanya makao katika maisha yako.
Yohana 14:23 ''YESU akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na BABA yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. ''
 Ndugu, zinagtia sana points 5 hapo juu ambazo zinazungumzia Neema ya MUNGU inakutaka ufanyeje.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments