LIFAHAMU JINA YESU KRISTO. .

Na Mtumishi Alex Simion.

Shalom Shalom Mtu wa Mungu
Ninakusalimia katika jina lile lipitalo majina yote yaani jina la Kristo Yesu.
Karibu sana mtu wa Mungu ili tujifunze kuhusu JINA LA YESU.

Jina YESU ni jina la Mungu mwenyewe yaani ni jina la Mungu Baba ambalo alimpa mwenae YESU KRISTO. Hili jina YESU sio jina halisi la Bwana wetu Yesu Kristo katika asili yake bali ni jina ambalo alirithi kutoka kwa Baba yake yaani Mungu Baba.
  Waebrania 1:4
"Amefanyika bora kupita malaika kwa kadri jina alilorithi lilivyo tukufu kuliko lao"


  Wafilipi 2:9
"Kwa hiyo Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lipitalo kila jina".

Biblia inasema kwamba YESU amefanyika bora kupita malaika.
Je ni nini kinachomfanya awe bora kupita malaika?
Kinachomfanya awe bora kupita malaika ni JINA AMBALO NI TUKUFU, na hilo jina amerithi sio la kwake, kwa lugha nyepesi amepewa au amekirimiws na Baba yake na ni jina la Mungu Baba mwenyewe na hilo jina ndilo jina ambalo linapita kila jina, yaani ni jina linalopita majina yote.

Pengine unaweza ukajiuliza hilo jina ni lipi?
Hilo jina ni jina ni Tukufu na ambalo ni jina lipitalo majina yote linaitwa jina YESU ndilo hilo jina ambalo tumezoea kuliita jina la Yesu.


Mathayo 1:21
"Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana yeye ndiye atakaye waokoa watu wake na dhambi zao"

Tunaona Bwana wetu Yesu Kristo anapewa jina YESU kwa kumaanisha kwamba ni jina ambalo hakuwa nalo tangia mwanzo, baada ya kuzaliwa hapa duniani ndipo tunaona anapewa jina hilo YESU.
Kabla ya kuja hapa duniani alijulikana kwa jina la NENO LA MUNGU na pia alikuwa ni Mwana wa Mungu.
Na hilo Neno la Mungu/Mwana wa Mungu ndiye aliyefanyika mwili, yaani hilo Neno lililokaa kwetu nasi tukauona utukufu wake, utukufu wa Mwana pekee atokaye kwa Baba amejaa Neema na kweli.
Baada ya huyo Neno/Mwana wa Mungu kufanyika mwili na kuzaliwa hapa duniani ndipo alipewa jina hilo YESU.

Hebu tuangalie YESU mwenyewe anavyosema kuhusu hilo jina kwamba ni la nani.
Yohana 17:6
"Jina lako nimewadhihilishia watu wale ulionipa katika ulimwengu, walikuwa wako ukanipa mimi, na Neno lako wamelishika, sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako".

YOHANA 17:26
Anasema;
"Mimi naliwajulisha jina lako tena nitawajulisha hilo, ili pendo lile ulilonipenda liwe ndani yao nami niwe ndani yao".

Hebu ona tena hapa anavyosema;
YOHANA 17:11b
"Baba mtakatifu kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa ili wawe na umoja kama sisi tulivyo, nilipokuwa pamoja nao niliwalinda kwa jina lako ulilonipa, ila yule mwana wa mpotevu ili andiko litimie".

Ukisoma vizuri katika mistari hiyo utakutana na maneno haya;
√JINA LAKO NIMEWADHIHILISHIA
√MIMI NALIWAJULISHA JINA LAKO
√KWA JINA LAKO ULILONIPA UWALINDE HAWA.

Hapa tunaona Bwana YESU akisema KWA JINA LAKO au JINA LAKO Kwa kumaanisha kwamba hilo jina ni la Baba yake yaani hilo jina YESU ni la Mungu Baba na hilo jina ndilo jina ambalo Bwana wetu Yesu Kristo alilidhihilisha kwetu, akisha kulidhihilisha akatujulisha hilo jina na sio hivyo tu bali katika hilo jina YESU tunalindwa kwalo.
Ndio maana baada ya kutujulisha jina hilo na kulidhihilisha pia, INJILI ilianza kuhubiliwa kwa hilo jina YESU au kwa jina la YESU, Wagonjwa, viwete, vipofu, vziwi waliponywa kupitia hilo jina YESU au hilojina la YESU.

Hebu tusome hapa; Matendo 5:27-29
"Walipowaleta wakawaweka katika balaza, kuhani mkuu akawauliza akisema je hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa Jina hili?,.nanyi tazameni mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuleta damu ya mtu huyu juu yetu".

Angalia na hapa;
Matendo  3:1-16
Lakini hebu tuangalie msatari wa 6 na 7.
"Lakini Petro akasema, mimi sina fedha wala dhahabu lakini nilichonacho ndicho nikupocho,Kwa jila la Yesu Kristo  wa nazareti simama uende, akamshika mkono wa kuume akamwinua mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu".

Hiyo ni baadhi ya mistari ambayo inaonyesha kwamba Injili ilihubiliwa kwa hilo jina la Yesu na wasioweza waliponywa kwa jina la Yesu.
*Hili jina YESU au jina la YESU ndilo kila kitu nasema hivyo kwa sababu hata kuokolewa tunaokolewa kwa jina hilo la YESU~ #Mdo 4:12.
*Kama ni kuomba ni lazima tuombe kupitia hilo jina la YESU~ YOHANA 14:12, YOHANA 16:23.
*Kama ni kutoa mapepo yanatolewa kwa hilo jina la YESU~ 
Marko 16:17.
Bwana wetu YESU KRISTO alipoondoka hapa duniani alituachia hilo jina ila kwa bahati mbaya wengine wamelipuuza hili jina na wamejaribu kutengeneza vitu mbadala.
Niliwahi kuona mapepo yanatolewa kwe kutumia maji ya upako, sasa sijui hili agizo la kutoa pepo kwa kutumia maji yaupako limetoka wapi ila mimi ninachojua ni kwamba YESU alisema kwamba KWA JINA LANGU MTATOA PEPO.

Ibada yeyote ile ambayo jina la YESU halihusiki katika ibada hiyo ibada hiyo haiwezi kuwa ya kweli.
Ibada yeyote ile inayobeba vitu mbadala badala ya jina la YESU kuhusika hiyo sio ibada ya kweli.

Sio kila mtu anaweza kulitumia jina la YESU likaleta matokeo, ni kweli jina la YESU lina nguvu na mamlaka pia, lakini ili uweze kuona hiyo nguvu na mamlaka inavyotenda kazi ni lazima uwe na uhalali katika ulimwengu wa roho wa Mungu aliye hai katika kulitumia jina hilo, kuna wengine hawana uhalali wa kulitumia jina hilo la YESU.
Ngoja nikupe mfano ili uweze kunielewa vizuri.
  Matendo 19:13-16.
Ukisoma vizuri hiyo habari unaona Wayahudi wapunga pepo maana yake walikuwa ni watu wa kuyatuliza mapepo yaliyomvagaa mtu ili yatulie sio kwamba walikuwa wanayatoa hapana.
Sasa hebu angalia hawa wana wa SKEWA nao walikuwa ni wapunga pepo, sasa wakajaribukutoa pepo kwa kutumia jina la YESU kwa sababu walimwona mtume Paulo akitoa mapepo kwa jina la Yesu nao wakajaribu kuiga.

Hebu cheki walichojibiwa;
Mstari wa 15
"Yule pepo mchafu akawajibu akawambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakinani ninyi ni nani?".

Sijui kama ulishawahi kujiuliza ni kwa nini YULE PEPO ALIWAHOJI WANA WA SKEWA KWAMBA NINYI NI NANI.
Ni kwa sababu wale wana wa skewa walikuwa hawana uhalali katika ulimwengu wa roho wa Mungu aliye hai kwa kulitumia jina la Yesu yaani kwa lugha nyepesi ni kwamba walikuwa hawana uhalali wa kumtoa yule pepo kwa kutumia jina la Yesu.
Hivyo basi Yesu Kristo ni Kuhani mkuu na kama ni kuhani mkuu ametufanya na sisi tuliomwamini kuwa makuhani kwa Mungu wetu.
Na kama sisi ni makuhani tunao ujasiri na uhalali kwa Imani katika ulimwengu wa roho kama makuhani kwa kulitumia jina la Yesu ili kumwadhibu adui shetani pamoja na kazi zake.

Kwa leo naishia hapo ila Mungu akipenda tutajifunza tena.
Kama hujampokea Bwana Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako, wakati ni sasa usisubiri kesho, Wakati wa Wokovu ni sasa maana baada ya kifo ni hukumu.

Mungu akubariki sana kwa kujifunza.
By Alex Simion.
0768140422
alexsimion931@gmail.com

Comments