MAKUNDI MATATU(3) YA DHAMBI AMBAZO KILA MWANADAMU ANATAKIWA KUZIEPUKA.


Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU la msaada sana.
Dhambi ni nini?
=Dhambi ni mabaya yote ayatendayo mtu yaliyokatazwa na Neno la MUNGU.
Warumi 6:12 '' Basi, dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake; ''
 
=Dhambi ni uasi kwa MUNGU
1 Yohana 3:4 '' Kila atendaye dhambi, afanya uasi; kwa kuwa dhambi ni uasi. ''
 
=Hakuna dhambi ya mwanadamu ambayo MUNGU haioni
Mithali 15:3 ''Macho ya BWANA yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema.''
 
=Mshahara au malipo ya dhambi ni mauti
Warumi 6:23 '' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU Bwana wetu.''
 
=MUNGU anamsihi kila mwanadamu kuacha mabaya yote na kuanza kutenda mema siku zote.
Zaburi 34:14 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie.''
 
=MUNGU anataka tuwe watakatifu waliookolewa na YESU KRISTO na kutakaswa dhambi zote kwa damu ya YESU KRISTO.
1 Petro 1:15 ''bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''
 
=Kumbuka YESU KRISTO alikuja kuokoa wenye dhambi ili dhambi zao zifutwe na wakubaliwe sasa na MUNGU Muumbaji wao.
1 Timotheo 1:15 '' Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa, ya kwamba KRISTO YESU alikuja ulimwenguni awaokoe wenye dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi.''
 
=Ni muhimu sana ndugu kuacha dhambi, kujitenga mabli na dhambi na kuzikimbia dhambi maana kuna hukumu ya kutisha kwa  wenye dhambi wasiopata neema ya kutubu kwa Bwana YESU Mwokozi.
Obadia 1:15 '' Kwa maana hiyo siku ya BWANA i karibu juu ya mataifa yote; kama ulivyotenda, ndivyo utakavyotendwa; malipo yako yatakurudia juu ya kichwa chako mwenyewe.''
 
Sasa makundi matatu ya dhambi ni haya ambayo ndugu inakupasa uyaepuke sana katika maisha yako yote ya Wokovu.

   1. Dhambi za dhamiri.

Hizi ni dhambi zisizoonekana kwa macho.
Ni dhambi za ndani kwa ndani kwenye moyo wa mhusika.
Dhambi hizi hukaa katika nafsi ya mhusika.
Baadhi ni hizi.
A. Uchungu.
Waebrania 12:15 ''mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya MUNGU; shina la UCHUNGU lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.'' ''
Uchungu ni masikitiko au masononeko ya ndani moyo wa mtu ambayo hayana mwisho wa haraka.
Mfano hai ni huyu ndugu aliyeambiwa na Mtume Paulo.
Mtendo 8:23 ''Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu. ''
 
B. Kutokusamehe
Waefeso 4:32 '' tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi. '' 
MUNGU anatutaka tuwe watu wa kusamehe, kama ambavyo yeye hutusamehe kama tukitubu.
Kuna madhara makubwa katika kutokusamehe.
Mathayo 6:14-15 '' Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.''

C.  Chuki
1 Yohana 3:15 '' Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake. ''
Chuki ni nini?
Chuki ni tabia ya kutokuwapenda watu au ni tabia ya kuwa na roho mbaya.
Mithali 10:18 '' Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.''

D.Kinyongo
Walawi 19:18 ''Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi BWANA.''
Kinyongo ni nini?
Kinyongo ni hasira za ndani kwa ndani.

E.  Hasira
Mathayo 5:21-22 ''Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto.''
Hasira ni nini?
 Hasira ni kuwa na ghadhabu au fundo moyoni na inakuelekeza kuchukua hatua mbaya. Hivyo kwa mawazo tu kutokana na hasira unaweza ukaamua mabaya moyoni mengi tu.

F.   Kuhukumu moyoni
Luka 6:37 '' Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. ''
 
G. Mawazo mabaya yote
Mathayo 15:19 ''Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano; ''
Mawazo mabaya yanaweza yakahusisha wivu, kutunga uongo,kukusudia mabaya, tamaa mbaya n.k

H.Hila
1 Petro 2:1-3 ''Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote.  Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;  ikiwa mmeonja ya kwamba BWANA ni mwenye fadhili. ''

     2. Dhambi  za kinywa.
Dhambi hizi zinajumuisha.
A. Uongo
Waefeso 4:25 '' Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.''
Uongo ni tabia ya kudanganya.
Kutoka 23:1 ''Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu. ''
Uongo unahusisha Pia.

               I.  Kusema uongo 
Kumb 5:20 '' Wala usimshuhudie jirani yako uongo. ''
 
               II. Kufundisha uongo 
 Mithali 10:19-20 ''Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili. Ulimi wa mwenye haki ni kama fedha teule; Moyo wa mtu mbaya haufai kitu.''

B. Kuhukumu kwa kinywa 
Luka 6:37 '' Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. ''

C.  Kusingizia 
Zaburi 101:5 '' Amsingiziaye jirani yake kwa siri, Huyo nitamharibu. Mwenye macho ya kiburi na moyo wa majivuno, Huyo sitavumilia naye.''
 
D.Kusema yasiyokupasa 
Yakobo 1:19 '' Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika;''

E.  Kulaani watu wa MUNGU
 Yakobo 3:8-10 ''Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo twamhimidi MUNGU Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa MUNGU. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo.''
 
F.   Kutukana na majivuno
 2 Kor 12:20 ''Maana nachelea, nisije nikawakuta si kama vile nitakavyo kuwakuta, nikaonekana kwenu si kama vile mtakavyo; nisije nikakuta labda fitina na wivu, na ghadhabu, na ugomvi, na masingizio, na manong'onezo, na majivuno, na ghasia;''
 
G. Kusengenya.
 Zaburi 50:20 ''Umekaa na kumsengenya ndugu yako, Na mwana wa mama yako umemsingizia.''
 
H.Kujipendekeza kwa maeno yasiyo maana.
 Mithali 26:28 '' Ulimi unenao uongo huwachukia wale uliowajeruhi; Na kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu. ''
 
I.     Kufitini.
  Mithali 26:20 ''Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma. ''
 
    3.  Dhambi za matendo.
Inawezekana dhambi hizi ndizo huonekana zaidi maana matendo huzionyesha.
Biblia inasema kwa Neno au kwa tendo tufanye katika MUNGU maana yake matendo yetu yanatakiwa kuwa ni matendo safi tu na sio matendo mabaya. 
Wakolosai 3:17 '' Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye.''
Matendo ya mtu huonekana zaidi na hata kama atafanya dhambi bila kuonekana na watu basi MUNGU huona dhambi hiyo na hakuna kificho mbele zake.
Jambo muhimu sana kukumbuka ni, Ufunuo 22:12 '' Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. ''
Kumbe Bwana YESU atakuja ili kumlipa kila mtu sawasawa na matendo yake. Kama ulikuwa mtu wa dhambi malipo ni jehanamu. Kama uliokoka na kuishi maisha matakatifu malipo ni uzima wa milele.
Kumbuka kila tendo baya lina hukumu yake
Mhubiri 12:14 '' Kwa maana MUNGU ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya. ''
Matendo yote ayatendayo  mtu yaliyo kinyume na Neno la MUNGU ni dhambi.
Biblia inakushauri kwamba 
Amosi 5:15 ''Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba BWANA, Mungu wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu.''
Matendo ambayo ni dhambi yako mengi mno baadhi tu ni haya.
A. Uzinzi na uasherati
B. Kuiba
C.  Kuua
D. Kuokuwa mwaminifu
 Zaburi  37:3 ''Umtumaini BWANA ukatende mema, Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu. ''
Kuna dhambi zingine pia  ziko katika makundi mawili moja kwa moja maana yake ilikuwa dhambi moyoni kisha inadhihilika katika matendo.
Mfano unakusudia kufanya uasherati au kubaka, hiyo ni dhambi na ukifanya huo uasherati ni dhambi pia hivyo ni dhambi juu ya dhambi na madhara yake ni makubwa.
Ndugu yangu, katika maisha yako hakikisha unaacha dhambi zote.
Na dhambi kuu kabisa ambayo wanadamu wanaifanya walio wengi ni kumkataa YESU KRISTO kuwa Mwokozi wao.
Yohana 3:16-18 ''Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''
Asiyemwamini YESU kama Mwokozi yuko katika hukumu tayari, ni lazima ampokee YESU na atimize utakatifu autakao YESU ndipo atafanyika mwana wa MUNGU.
Ndugu, ni muhimu sana kuacha dhambi zote.
Warumi 12:17-21 ''Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya MUNGU; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena BWANA. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema. ''
Hii dhambi huwezi kusamehewa hadi umpokee YESU KRISTO  kama Mwokozi wako na uanze kuishi maisha matakatifu katika yeye,
  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments