MUNGU AKIKUPA NENO KUSEMA HAKIKISHA UNASEMA.



 Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze neno la MUNGU.

Biblia ni Neno la MUNGU, na ndani ya Biblia kuna sehemu MUNGU alisema na watumishi wake, na wao wakasema kwa watu waliokusudiwa, na hicho kulichosemwa kiliwasaidia waliokisikia lakini pia hicho kilichosemwa hata na sisi leo kinatusaidia.
MUNGU huzungumza sana na watu wake, ona mfano huu ambao MUNGU alimpa Eliya Neno Kusema.

2 Wafalme 1:3-4 '' Lakini malaika wa BWANA akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, BWANA asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka. ''

MUNGU husema sana na watu wake.

Mtu mmoja anaweza akaliponya Kanisa zima au taifa zima kwa sababu tu MUNGU alipomsemesha na yeye hakunyamaza bali alienda kusema hicho ambacho MUNGU alimwambia.

Yona 1:1-3 ''Basi neno la BWANA lilimjia Yona, mwana wa Amitai, kusema,  Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukapige kelele juu yake; kwa maana uovu wao umepanda juu mbele zangu.  Lakini Yona akaondoka akimbilie Tarshishi, apate kujiepusha na uso wa BWANA; akatelemka hata Yafa, akaona merikebu inayokwenda Tarshishi; basi, akatoa nauli, akapanda merikebuni, aende pamoja nao Tarshishi, ajiepushe na uso wa BWANA.''

Unaweza ukawasaidia watu ili wasiingie kwenye uharibifu kwa sababu tu MUNGU alipokusemesha hukunyamaza.

Kumbuka MUNGU hatafanya jambo lolote bila kuwaambia watumishi wake.

Amosi  3:7 ''Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake. ''



Wewe Mteule wa KRISTO ndiye Nabii wa leo unayeweza kupokea ujumbe kwa MUNGU na kuiambia jamii yako, Kanisa au popote pale ambapo ROHO MTAKATIFU atakuelekeza kwenda kusema.

Hata kama wewe sio Mchungaji au Mtumishi Mkubwa kanisani, MUNGU anaweza kukupa Neno lake ili ulipeleke panapohusika.

Amosi 7:14-15 '' Ndipo Amosii akajibu akamwambia Amazia, Mimi sikuwa nabii, wala sikuwa mwana wa nabii; bali nalikuwa mchungaji, na mtunza mikuyu; naye BWANA  akanitwaa, katika kufuatana na kundi; BWANA akaniambia, Enenda uwatabirie watu wangu Israeli.''
 

Hezekia alikuwa katika kufa kwa sababu ya ugonjwa

Isaya 38:1-2 ''Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA,''

Lakini Isaya alipewa Neno kumwambia Hezekia na Neno hilo Hezekia alipolifanyia kazi aliponywa na kuongezewa miaka 15 ya kuishi, Lisingeenda lile Neno la MUNGU kwake hakika angekufa na tena angekufa bila kutengeneza na MUNGU.

Lakini alipolisikia Neno la MUNGU alitengeneza.

Ndugu ukipewa Neno na MUNGU kusema kwa ndugu zako hakikisha unasema.

Ndugu ukipewa Neno na MUNGU kusema kwa marafiki Kanisa  hakikisha unasema.

Ndugu ukipewa Neno na MUNGU kusema kwa  taifa lako hakikisha unasema.

Japokuwa Waisraeli walikuwa Misri lakini ROHO MTAKATIFU alimjulisha Yusufu na kumwambia kwamba siku moja watatoka Misri.

Mwanzo 50:24-25 '' Yusufu akawaambia nduguze, Mimi ninakufa, lakini MUNGU atawajia ninyi bila shaka, atawapandisha toka nchi hii, mpaka nchi aliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. Yusufu akawaapisha wana wa Israeli, akasema, Bila shaka MUNGU atawajia ninyi, nanyi mtaipandisha huko mifupa yangu. ''

Ndio maana majira yao ya kuondoka Misri yalipofika waliomba kwa MUNGU na MUNGU akakumbuka agano lake na Ibrahimu hivyo akawatoa Misri

Kutoka 3:7-8 ''BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. ''
 

UKISEMA ALICHOKUAMBIA ROHO MTAKATIFU UTAKUWA  UMEWASAIDIA YAFUATAYO.



     1.  Utakuwa umewasaidia watu kujua jinsi ya kuiepuka adhabu ya MUNGU, Kama jambo husika linahusisha adhabu ya MUNGU.  

 Yona 3:1-10 ''Neno la BWANA likamjia Yona mara ya pili, kusema,  Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru.  Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu.  Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa.  Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo.  Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu.  Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji;  bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba MUNGU hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? MUNGU akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi MUNGU akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.''

Majira ya adhabu kwa ajili ya dhambi za Ninawi yalikuwa yamefika hivyo Yona asingewaambia Neno la MUNGU wangeadhibiwa na MUNGU.

Yako mambo mabaya Mtu/watu wanaweza wakatenda haki kikombe cha ghadhabu ya MUNGU kikajaa, kinachofuata ni adhabu mbaya, MUNGU anaweza akakupa Neno ulipeleke  na wao wakitii na kutubu na kuacha njia zao mbaya hakika MUNGU anaweza akaghairi kuwaadhibu,

Hata kama ni Mtu mkubwa kiasi gani, kama MUNGU amekupa Neno lipeleke ndugu.



    2.  Utawapa watu mbinu za kushinda vita wanayopitia.

2 Nyakati 20:1-17  Utasoma yote lakini baadhi ya maandiko hapo ni haya ''Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya MUNGU. Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa BWANA ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa BWANA yu pamoja nanyi. ''

Watu hawa walikuwa katika maombi mazito ili baada ya maombi waende vitani, Neno la MUNGU likawajia kusema ‘’Hamtahitaji kupigana vita(Mstari wa 17) na ni kweli maana walishinda vita ile kubwa bila kupigana vita,  kumtegemea MUNGU hakika kuna faida kuu.

Maadui walijikuta wanapigana na wana wa Amoni na sio kupigana na Israeli hivyo Israeli aliyekuwa vitani alishinda vita bila kupigana vita kwa sababu ya Neno la MUNGU.

Hata Hezekia aliishinda roho ya mauti kwa nsababu ya Neno la MUNGU alililoambiwa.

Sasa ingekuwaje kwa Waisraeli kwenda vitani wakati walitakiwa kushinda vita bila kupigana vita?

Neno la MUNGU lina maana sana kwa wanaopelekewa Neno hilo.


3.  Neno la MUNGU litaonyesha usahihi, hivyo Mijadala na maswali kukoma.

1 Samweli 16:8-13 Utasoma yote lakini baadhi ya maandiko hapo yanasema ''Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, BWANA hakumchagua huyu.
 Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala
BWANA hakumchagua huyu. Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, BWANA hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku.   ''

Yamkini Yese alipokuwa anawaleta watoto wake wakubwa aliamini moyoni mwake kwamba mmoja katika hao angekuwa ndiye ameteuliwa na MUNGU aje awe Mfalme wa Israeli.

Inawezekana hata Samweli alikuwa na mtu wake moyoni katika wale watoto wa  Yese ili aje awe Mfalme, ndio maana  MUNGU alisema kwamba yeye haangalii kama wanadamu wanavyoangalia, MUNGU aliwakataa hao watoto wakubwa wa Yese na inawezekana alipowakataa na mijadala na maswali kichwani mwa waliokuwepo ikakoma maana hata wao walidhani mmoja katika wale vijana wakubwa wa Yese  angekuwa Mfalme wa Israeli.

Lakini kumbe MUNGU alikuwa amemchagua kijana mdogo ambaye hata wakati huo hakuwepo nyumbani.

Ndugu, Neno la MUNGU linaweza kukujulisha juu ya Mke/Mume ambaye mtafunga ndoa, hivyo maswali na mjadala kichwani kwako kukoma.

Neno la MUNGU  linaweza kukujulisha juu ya Kazi n.k.

Ngoja nikupe ushuhuda kidogo.

Mimi Peter Niliwahi kuishi Zanzibar kwa miaka Minne(4) kati ya mwaka 2008 hadi 2012.

Nilinunua vitu vingi na kila kitu kilikuwa sawa. Siku moja Neno la MUNGU lilinijia kwa njia ya ndoto kwamba mwaka mmoja kama na nusu unaofuata ningehama Zanzibar na kuja Hapa Dar es salaam. Nilifurahia ufunuo huo lakini sikufanyia kazi Neno hilo maana Uhamisho wa kutoka Zanzibar ulikuja ghafla na hivyo nikashindwa kusafirisha vitu vyangu nilivyokuwa nimenunua Zanzibar nilipata hasara kubwa sana maana ilibidi vitu vingi nigawe na vingine niliwauzia watu kwa bei ya hasara na kwa ahadi tu na hizo ahadi zaidi ya asilimia 60 hawakutimiza.

Nilijikuta natoka Zanzibar nikiwa na redio na Begi za nguo tu maana gharama za kusafirisha vitu kama friji, vitanda, na vingine vyote sikuweza hivyo nikajikuta nawagawia marafiki hata kama rohoni sipendi na vingine niliwapa kwa ahadi kwamba watakapopata pesa watanitumia, lakini zaidi ya nusu walinidhulumu. Kwanini nasema nilikosea?

Ni kwa sababu nilipolipokea Neno la MUNGU la kuhama kwangu huko nilitakiwa kujiandaa kwa kutokununua vitu ambavyo vitanisumbua kubeba, kwa kuuza taratibu vitu hivyo, kwa kutokulipia pesa ya kupanga vyumba, kwa kusafilisha taratibu. Sasa ndani ya siku 4 nilitakiwa niwe Dar es salaam. Lilikuwa jambo gumu sana.

Ndugu ukipewa Neno na ROHO MTAKATIFU lifanyie  kazi ili usipate hasara ambayo hukuitarajia.

Mimi nilipopewa Neno nilifurahia lakini nikasahau kwamba Neno hilo limenijulisha ili nijiandae na ndio maana nikapata hasara ambayo kuirudisha ilichukua muda mrefu.

Ndugu, ukipewa Neno na ROHO MTAKATIFU kulipeleka hakikisha unalipeleka.

Ukipewa Neno na Bwana YESU kulipeleka hakikisha unalipeleka.

Ukipewa Neno Binafsi kwa ajili ya maisha yako hakikisha unalifanyia kazi Neno hilo, ni kwa faida yako.

Daudi aliambiwa kwa habari ya kuwa Mfalme, wewe unaweza kuambiwa na MUNGU kupitia watu jambo lolote na mpeleka ujumbe wa MUNGU inampasa sana kuupeleka sehemu sahihi na muda sahihi.

Usiambiwe leo Neno na ROHO MTAKATIFU ili ulipeleke kisha wewe upange kulipeleka mwakani, ndugu watu wanaweza kufa kabla hawajalipokea hilo Neno na kabla hawajatengeneza  kwa Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

Yusufu alifunuliwa na ROHO MTAKATIFU juu ya miaka 7 ya Neema na miaka 7 ya njaa, asingesema hakika maelfu ya watu wangekufa kwa njaa, hata ndugu zake wangedhulika kwa sababu Yusufu alijulishwa na MUNGU lakini hakusema.

Ndugu, ukipewa Neno na Bwana YESU kusema hakikisha unasema.



MAKOSA YA BAADHI YA WATU WANAOPEWA NENO NA MUNGU KUSEMA.



1.  Kutafuta umaarufu wao na heshima.

Mtu wa aina hiyo anaweza kupewa Neno na ROHO MTAKATIFU ili akuambie lakini anaweza kukuambia nusu tu ya Neno hilo na kukupa mashariti mengi ambayo wala hakuambiwa na ROHO MTAKATIFU.

Anaweza kutangazia watu ili aonekane yeye hupewa ujumbe na MUNGU, hutafuta thawabu za wanadamu.

Mathayo 6:1 ''Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.''



2.  Kuogopa kusema au kumuonea aibu mtu wanayetakiwa kumwambia hilo Neno la MUNGU waliojulishwa.

Isaya 58:1 ''Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao. ''
Sasa kuna watu hupewa Neno na MUNGU kusema lakini huogopa au kuwaonea aibu wanaotakiwa kuwaambia, hayo ni makosa. 
MUNGU anataka kwamba anachokuambia sirini wewe kakiseme nurini mbele za watu tena usiwaogope watu hao.

Mathayo 10:27-28 ''Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba. Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. ''



3.  Kuhukumu wao na kusubiria adhabu kama jambo husika linahusu adhabu.

Mfano hai ni Yona ambaye hakujua kwamba watu wale wakitubu MUNGU anaweza kuwasamehe hivyo adhabu ikazuiliwa. Yona alihubiri Neno la MUNGU aliloambiwa lakini baada ya kuhubiri alikwenda nje ya mji akisubiri watu wale waangamie kwa moto kutoka mbinguni. Ni kweli moto ulikusudiwa lakini walipotubu MUNGU aliwasamehe na kuwapa nafasi mpya, Yona ni kama alitaka wateketee hata kama amewaonya.

Yona 4:1-2 '' Lakini jambo hili lilimchukiza Yona sana, naye akakasirika.  Akamwomba BWANA, akasema, Nakuomba, Ee BWANA; sivyo hivyo nilivyosema, hapo nilipokuwa katika nchi yangu? Hii ndiyo sababu nalifanya haraka kukimbilia Tarshishi; kwa maana nalijua ya kuwa wewe u MUNGU mwenye neema, umejaa huruma, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, nawe waghairi mabaya. ''



4.  Kuchelewa kupeleka ujumbe.

Madhara yanaweza yakatokea kabla ujumbe haujafika maana kwa kila jambo kuna majira yake.

Mhubiri 3:1 '' Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''.

Sasa ukichelewa kupeleka ujumbe unakuwa unakosea sana kama majira ya tukio husika ni sasa.



5.  Kutokuombea jambo hilo kama maombi yanahitajika.

Kutoka 32:9-14 '' Tena BWANA akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize, nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana BWANA, Mungu wake, na kusema, BWANA, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka, na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, Nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu nao watairithi milele. Na BWANA akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake. ''

Musa aliambiwa Neno la MUNGU akaanza kuwaombea wahusika kwa MUNGU ili wasamehewe, hata wewe unaweza kupewa Neno na ROHO MTAKATIFU na jambo la kwanza ni wewe kuwaombea wahusika ili mabaya yaliyokusudiwa yasiwapate.

 Ufunuo 3:22 ''Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments