MUNGU AMEAGIZA MHUBIRI INJILI APATE RIZIKI KWA HIYO INJILI.


Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU


Bwana YESU KRISTO atukuzwe sana ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Somo hili nilipewa kama ufunuo kwa ajili ya kuwafundisha viongozi wa Kanisa ambao wamekuwa na vita na wachungaji wao kwa miaka mingi kwa sababu tu ya matoleo. Kuwapata wote kwangu ni jambo gumu hivyo  hata kwa nafasi hii najua maelfu ya viongozi Kanisani watajifunza kitu. Najua somo la namna hii ni moja ya masomo magumu sana kuyafundisha lakini MUNGU anaagiza nifundishe ndio maana sina budi kufundisha.
Nimewahi kuwasiliana kwa simu na watu wengi wakiwalalamikia wachungaji wao juu ya sadaka, rohoni mwangu nilishuhudiwa juu ya mara nyingi wanaolalamika ndio walikuwa wanahitaji kusaidiwa kiroho.
Mfano Kuna Mchungaji mmoja katika Kanisa lenye washirika 25 na katika washirika hao wanaotoa fungu la kumi ni chini ya watano na hilo fungu la kumi la wote halifiki hata Elfu 40 kwa Mwezi. Mchungaji wa Kanisa hilo kwa sababu ya vita na viongozi walio chini yake kanisani mara kadhaa ameshaacha uchungaji  lakini kwa sababu ya wito na maonyo ya MUNGU imembidi kurudi, viongozi kanisani hapo wamechachamaa wakimlaumu kwamba anatumia pesa yote inayopatikana, ambayo kwa mwezi jumla haifiki hata laki moja. Nilipopata habari hiyo rohoni mwangu  nilijikuta natafakari sana, na kuwaza kwamba inawezekana watumishi wa jinsi hiyo wako wengi.
Hata nilipopewa ufunuo huu nilikuwa bado nina maswali mengi sana. Mimi binafsi sio Mchungaji lakini ROHO MTAKATIFU alishanijulisha kwamba ameniita katika Huduma ya ualimu wa Neno la MUNGU. Uchungaji ni moja ya kazi ambazo naziogopa sana hata kama Bwana YESU akisema juu  ya kumtumikia katika uchungaji  hakuna mjadala lazima nifanye kazi hiyo.
Inawezekana pia  katika baadhi ya watumishi walioinuliwa kihuduma liko pia tatizo hivyo Kanisa la KRISTO  kwa sehemu linakuwa kama limevurugwa.
Lakini pia kuna wafundishaji wengi hasa wasio wachungaji makanisani hao hufundisha kwa juhudi sana juu ya kuwafanya kanisa lisiwategemeze wachungaji wao, Wafundishaji hawa wamejaa wivu juu ya wachungaji wao. 
Wakati mwingine mimi huwa natamani kila mwana kanisa ajue juu ya matoleo kila wiki ili kupunguza lawama mbalimbali ambazo labda zisingekuwepo.
Kwa sababu utoaji wa matoleo ni siri  ya mtoaji hivyo wakitoa Kanisa  zima mfano Kanisa la watu 100, mtu anaweza akadhani kwa kukadiria kwamba hapo jumla  ya matoleo hayo labda ni laki mbili lakini kumbe ukihesabu utakuta elfu 30 au 40. Kwa jinsi hiyo mitafaruku isiyohitajika inaweza kujitokeza  pasipo na sababu.
Na mara zote washirika Kanisani huwa hawana tatizo ila tatizo linakuwa  kutoka katika baadhi ya viongozi kanisani.
 Sasa nisikilize ndugu itakusaidia maana wapo pia walioambulia laana badala ya baraka kutokana na uongozi wao Kanisani.
Sasa nisikilize.
1 Kor 9:14 '' Na BWANA vivyo hivyo ameamuru kwamba wale waihubirio Injili wapate riziki kwa hiyo Injili. ''
Ni MUNGU ameamuru wahubiri injili wapate riziki katika hiyo injili.

Riziki ni nini?
Kuna maana mbili za Neno riziki.
   1. Riziki ni neema anayoipata mtu kutokana na uwezo wa MUNGU.

    2. Riziki ni kitu kinachopatikana kutokana na kazi ya mtu na hivyo kitu hicho kumwezesha kuishi.

Biblia imeagiza kwamba watumishi wanaochunga Kanisa la MUNGU duniani(Matendo 20:28) basi riziki zao wazipate katika kazi yao hiyo ya kuchunga kundi la MUNGU. 
Hiyo Matendo 20:28 Inasema '' Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo ROHO MTAKATIFU amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake MUNGU, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe. '' 
Kumbe ni muhimu pia Mtumishi kuwa amewekwa na ROHO MTAKATIFU na sio kujiweka kwa lengo la kujipatia pesa.
Kumbe Mtumishi huyo naye anatakiwa kuwa safi na sio Mchafu yaani mdhambi.
Watumishi hawa ni wale ambao wanafanya kazi ya MUNGU ya moja kwa moja siku zote na riziki hiyo wanaipata kutoka kwa watu wanaowachunga au kuwahudumia kiroho.
 Watumishi  hawa wanaweza kuwa wachungaji wa makanisa(Wanapata riziki kutokea Kanisani alipo)
Mitume na manabii wanapata riziki katika injili wanayoipeleka
Wainjilisti na walimu Wanaipata riziki katika semina au madarasa wanayofundisha
Biblia haimtaki Mtumishi kuidai riziki yake au kupanga mipango ya kuipata riziki hiyo kutoka kwa kundi la MUNGU. Mambo ya MUNGU hayana kulazimishana bali ni mtu mwenyewe rohoni anapata ufunuo au msukumo wa kutoa sadaka hivyo anatoa. Mambo ya MUNGU hayahitaji ushawishi wa namna yeyote bali kazi ya Mtumishi wa MUNGU ni kufundisha Neno sahihi la MUNGU hasa la kuwafanya watu waokoke,waache dhambi, waishi maisha matakatifu na wamtegemee MUNGU na kumwabudu MUNGU katika Roho na kweli.
Utoaji ni jambo la muhimu na lazima kwa wateule wa MUNGU. Biblia inasema 
''….. Mmeniibia Zaka na Dhabihu. Ninyi mmelaaniwa kwa laana;   maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote-Malaki 3:8b''

  Laana maana yake ni kutokufanikiwa, kutokustawi,kutofaulu, kukosa furaha, kukosa amani, na kukosa mwelekeo sahihi. Ni wazi kabisa kuwa Wakristo wengi  sana hawana furaha, hawana amani na hawafanikiwi katika maisha yao ya kila siku, kwa sababu hawamtolei MUNGU zaka na dhabihu. 
Utoaji ni agizo la MUNGU na hivyo kuna faida kubwa katika utoaji wa mtu.
2 Kor 9:7-8 '' Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na MUNGU aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; ''


Biblia inaendelea kusema '' Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya BWANA; ni takatifu kwa BWANA.- Kumb 27:30 ''
Kuna watu wengi pia hawapendi Watumishi kupewa funga la kumi, lakini maandiko yanasema  '' Tena utanena na Walawi, na kuwaambia, Hapo mtakapoitwaa zaka mkononi mwa wana wa Israeli niliyowapa ninyi kutoka kwao kuwa urithi wenu, ndipo mtakaposongeza sadaka ya kuinuliwa kwa BWANA katika hiyo, iwe zaka katika hiyo zaka.-Hesabu 18:26''
Ni kweli ni agizo la MUNGU kwamba wahubiri wa injili wapate riziki kutoka katika kazi yao ya injili, ni vyema pia tukajua kwamba riziki hizo sio zile anasa.
Sio kusudi la MUNGU mchungaji au mhubiri alazimishe kupewa pesa au watumie mbinu za kujipatia pesa, Hiyo ni dhambi na ni makosa.
Sio kusudi la MUNGU Mtumishi kuwapangia washirika pesa za kumpa, hayo ni makosa makubwa sana.
Riziki zinahusisha malazi na mavazi, hivyo ni heri kanisa au watu wa MUNGU wakamsaidia mhubiri riziki za vyakula na mahitaji mengine yaliyo ya lazima yatakayomwezesha aifanye kazi ya MUNGU vyema.
Mathayo 10:7-10 '' Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.  Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu; wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake.''
 
Lakini pia Mhubiri anatakiwa  kuwa na juhudi katika kazi yake mbele za MUNGU ili hata iwe sababu ya MUNGU kumwinulia watu wa kumpa riziki. Haiwezekani wewe ni Mchungaji wa Kanisa na hujawahi hujawahi kushuhudia watu hata 20 kwa mwaka  wakati ni wewe kazi yako ni kumtumikia MUNGU tu huku washirika wakifanya kazi zao za vipato ili katika hivyo na wewe wakupatie kidogo kwa agizo la MUNGU.
Unaweza ukawa ni mtumishi ambaye hutumizi wajibu wako hivyo riziki inaweza ikawa jaribu kwako kumbe ni wewe mzembe. Mimi naamini MUNGU ni rahisi zaidi kukuinulia watu kukupatia riziki kama wewe mwenyewe unatimiza wajibu wako kwa MUNGU.
Na zingatia sana kwamba hutakiwi kuhubiri Neno la MUNGU ili upate riziki, bali hubiri ni watu wampokee YESU KRISTO kama Mwokozi wao, hapo ndipo utakuwa mtumishi sahihi mbele za MUNGU.
Wewe umewekwa na MUNGU moja kwa moja katika kazi ya injili, kwanini huitendei haki kazi hiyo ya MUNGU.
Kazi yako ni kuwasaidia watu kiroho, kuwaombea na kutimiza kila wajibu wako kwa MUNGU.
Moja ya jambo la muhimu sana sana ni mtumishi wa MUNGU kujitambua.
Unaweza ukakabidhiwa funguo kiroho za maelfu ya watu ili uwapatie, usipojitambua utawafanya watu wasifunguliwe na hata riziki kwako inaweza kukosekana. Mfano mimi Binafsi ni mara kadhaa nimeombea watu kwa simu na MUNGU alipowafungua waliniambia mambo ya ajabu sana.
Mfano kuna Dada mmoja alikuwa anaumwa sana bna akadai ameombewa na watumishi wengi mno na ikafika kipindi akaacha kwenda kwenye maombezi, siku moja aliona somo langu mtandaoni akanipigia simu akijisemea huyu ni Mtumishi wa Mwisho kuniombea maana watumishi wameshashindwa, kwa Neema ya MUNGU akafunguliwa jioni ile ile na kuanza kusema mbona ameenda kuombewa sana lakini hakupona ila akapona kwa simu, nikamwambia amshukuru MUNGU. Watu wa aina hiyo ni wengi na baada ya maombezi husema mbona nimeombewa kwa watumishi wakubwa na nimeenda kwenye madhabahu kubwa sana lakini sikupona?
Nilichojifunza ni kwamba kila mtumishi wa KRISTO aliye sahihi anazo funguo za kufunga kazi za giza na kufungulia baraka kwa baadhi ya watu wa MUNGU(Mathayo 16:19 '' Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.'') ndio maana unaweza ukaombea watu wakapona na wengine wasipone na Mtumishi mwingine anaweza akaombea watu wakapona na wengine wasipone, labda ni kanuni ya MUNGU tusiyoijua, hata kama mimi naamini mtu akielekezwa kwenda kuombewa iwe ni Kanisa fulani, semina fulani, mkutano fulani au kwa Mtumishi fulani hakika funguo za uponyaji wake zinakuwa huko huko hivyo anaweza akafunguliwa. Hata kama ili mtu apone pia hasa magonjwa kunahitaji Mambo manne nanayofanya kazi, ndivyo ROHO MTAKATIFU aliniambia, ila akanitajia matatu kwanza na naamini siku moja jambo la nne nitalijua.
Aliniambia kwamba, katika maombi kuna hitajika
1.  Imani ya muombaji
2.   Imani ya muombewaji
3.  Mapenzi ya MUNGU
Jambo la 4 sikuambiwa ila naamini siku moja nitajulishwa, lakini hata haya matatu tu MUNGU amewaponya wengi. Hivyo mtu akienda kuombewa madhabahu fulani na asipone inawezekana tatizo sio la waombaji bali wakati mwingine tatizo ni lake na wakati mwingine ilihitajika kuyatafuta mapenzi ya MUNGU juu ya kupona kwa ndugu huyo. Mapenzi ya MUNGU kivipi?
Mfano Mtu husika alionywa sana juu ya kuacha uasherati, yeye akashupaza shingo na kuja kupata magonjwa mabaya, sasa kuomba tu apone kunaweza kusimsaidie bali mapenzi ya MUNGU atubu kwanza kwa sababu alipinga maonyo ya MUNGU.
Inawezekana mhusika alitamkiwa maneno ya kumfunga kwa ugonjwa na wachawi, sasa anaweza akafika kwa mtumishi akiomba aombewe ili apone, sasa mtumishi kuita uponyaji tu kunaweza kukapunguza tu tatizo na sio kuliondoa, mapenzi ya MUNGU katika hilo labda ni kuharibu madhabahu iliyomshikiria, kufuta agano la kipepo alilofungwa nalo n.k ukifanya hivyo kisha kwa dakika chache ukitamka apone kwa jina la YESU KRISTO hakika anapona. Mapenzi ya MUNGU anayo ROHO MTAKATIFU hivyo ni muhimu sana kumsikiliza ROHO MTAKATIFU katika maombi. Siku moja Kanisani kwetu alikuja dada mmoja kuombewa, kwa sababu waliokuwa wanaombewa walikuwa ni watu zaidi ya 5 basi Mchungaji akatugawa ili tuendelee kuwaombea. Mimi na wengine wawili tukuwa tunamuombea huyo dada, alianguka lakini tatizo lilikuwa halijatoka, Mchungaji alipofika alitamka jambo la ajabu sana na hapo hapo yule dada akafunguliwa na kupona. Mchungaji alipofika alisema ‘’Eee roho ya mauti mwachie binti huyu na usimfuate tena’’ Hapo hapo Binti yule aliinuka na kupona, nilijifunza kitu muhimu sana kwamba Kumsikiliza ROHO MTAKATIFU  ni faida kuu kwa Mtumishi wa MUNGU. Huo ni ufunuo aliopewa Mchungaji hivyo wengine tulikuwa  tunapiga risasi kwa adui lakini tulikuwa tunapiga pembeni.
Sasa nimesema hapo ili aliye Mtumishi ahakikishe anatimiza wajibu wake vyema.
Leo agizo la MUNGU la wahubiri kupata riziki katika hiyo kazi yao wengi wanaitumia vibaya sana baadhi ya watumishi.
Leo ni rahisi kuona Kanisa linamchangia pesa kwa nguvu sana Mchungaji wao za kumnunulia gari la nne(4), yaani ana magari matatu na sasa kanisa liko kwenye changizo ya lazima ili kumnunulia  Mtumishi wao gari ya 4. Inawezekana sio kosa la moja kwa moja lakini ni heri sana tuhusike zaidi kuchangia upelekaji wa injili na sio mambo ya anasa, ni heri kuhusike zaidi kujenga Kanisa na sio anasa. Mchungaji mmoja alikataa Kanisa kumjengea nyumba ya kawaida, akidai anataka Kanisa limjengee ghorofa, kama kanisa hawataki waache maana kama ni nyumba za kawaida anazo 3. Ndugu zangu, riziki wanazopewa watumishi hazitakiwi kugeuka anasa.
Lakini pia kuna maeneo watu wamewaacha wachungaji wao kabisa kiasi kwamba hata utumishi umekuwa mgumu sana.
Nilienda mkoa fulani  na Mchungaji alikuwa anahubiri vizuri sana lakini koti la suti limechanika na kila wiki anavaa hilo hilo.  Kanisani kuna waumini zaidi ya 60, hiyo binafsi naiona sio sawa.
Ni vyema sana kanisa kujitambua ili kuwasaidia wachungaji wao.
Hata kama  riziki ni jambo stahiki lakini basi riziki imuhudumia mchungaji na mkewe na sio Kanisa hadi linakuwa na michango ya kuchangia karo za watoto watatu wa Mchungaji wanaosoma shule za gharama kubwa.
Biblia inasema ni heri watu watoe zaka na sadaka ili kiwepo chakula nyumbani mwa MUNGU na sio chakula hicho kwenda kinyume na kusudi la MUNGU
Malaki 3:10 ''Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la.''
Ni vyema sana kanisa kuwapatia riziki wachungaji wao lakini iwe kwa upendo na sio amri wala kulazimishana.
Mimi ninachojua Neno sahihi la MUNGU hata kama halihusu utoaji ndilo linaloweza kumpa mtu mzigo wa kutoa riziki kwa mtumishi.
Kuna watumishi wengine ni watumishi majina tu. Ndugu kazi ndizo zinatakiwa zikuonyeshe kwamba wewe ni Mtumishi  wa MUNGU, sio maneno tu.
Leo kuna manabii  na mitume ambao baadhi kazi yao ni kutapeli tu watu, hiyo ni hatari sana.
Ndugu, kama Bwana YESU amekuita hakikisha unamtumikia yeye na sio kutumikia tumbo lako, na sio kutafuta sifa zako na heshima yako na ufahari wako.
Hubiri wokovu na sio mafanikio tu ambayo hata wewe hujawahi kuyapata, hivyo wewe wala sio mfano bora.
Watu wa Kanisa timizeni wajibu wenu kwa Kanisa  na kwa watumishi wa MUNGU.
Kule unakolishwa Neno la MUNGU na kuombewa kila mara pakumbuke, watumishi wanaokesha kwa ajili yako ili ufanikiwe, uwe mzima na ushinde vita wakumbuke sana.
Wako watumishi hujitoa sana katika kazi ya MUNGU na wanaifanya kwa uaminifu sana lakini Kanisa wala halina habari na kuwapatia riziki zao, watumishi wamejaa madeni hadi wanajificha. Ndugu nakuomba husika sana na Mtumishi wa MUNGU anayekusaidia kiroho kila leo.
Kuna watumishi wengine wanatamani kuacha kukuhudumia kwa sababu ya maisha yao kuwa magumu sana lakini hawana jinsi kwa sababu agizo la MUNGU kwao ni kwamba wakuhudumie ili usiende jehanamu.
Nilisoma kitabu cha Moses Kulola ambaye  mimi Peter nilifunuliwa kwa ndoto kuwa  ndiye mmoja wa  wahubiri aliyefanya kazi kubwa zaidi Tanzania, ni Baba wa kiroho wa maelfu ya wachungaji wakubwa wanaofanya kazi ya MUNGU vizuri sana leo, Mwalimu wa Mwakasege siku moja nilimsikia akisema kwamba ni mara kwa mara alikuwa anamtembelea Moses Kulola ili kushauriana, alikuwa hazina njema sana kwa Tanzania. Lakini katika mambo wa huduma yake kuna kipindi alijiombea afe maana hakukuwa na chakula na familia yake wanamlilia wakitaka hata uji, ndipo mtu mmoja asiyejulikana kutoka Kwimba alipomtumia kwa njia ya posta pesa kidogo na akawa anamtumia kila mwezi, mtu yule aliwahi kumfanyia huduma na MUNGU akamfungua.
Hivyo kuna watumishi wa MUNGU wanafanya kazi ya MUNGU katika mazingira magumu sana, sio kwamba MUNGU hajali bali MUNGU amewakabidhi  waumini kuwategemeza wachungaji wao na ili MUNGU awabariki waumini hao, Katika Kanisa wengi hawajui. Nigeria kuna mhubiri alitoka Marekani, watu wakajaa uwanja mzima na Kabla ya matoleo akapata ufunuo kwamba awaambie baadhi ya watu kwamba sadaka hiyo hiyo waliyopanga kutoa basi wakatoe kwa wachungaji wao Makanisani kwao, sasa hapo baadhi ya watu walianza kuiona pesa hiyo ni kubwa sana kuwapa wachungaji wao, lakini kwa mhubiri wa kutoka mbali waliona ni jambo la kawaida sana. Kanisa kama hilo linahitaji sana kusaidiwa kiroho.
Mchungaji mmoja ambaye ni rafiki yangu sana alipoona  anakoswa hata chakula na wakati mwingine wanalala njaa familia yake aliamua kuacha utumishi na kwenda kuomba kazi serikalini na kupata. Akapata kazi lakini MUNGUB akampiga mapigo akamwambia arudi katika utumishi, alirudi kwenye uchungaji akilia.
Sasa jiulize, MUNGU alitaka Kanisa kumlisha Mchungaji wao na kumhudumia lakini kanisa lilikuwa halijitambui japokuwa walikuwa zaidi ya 70.
Ndugu yangu unayesoma ujumbe huu nakuomba tambua hili ya kwamba una wajibu sana wa  kumhudumia Mchungaji wako kwa pesa yako.
Una wajibu wana wa kumsaidia mtumishi wa MUNGU anayekesha kwa ajili yako ili ufanikiwe.
Wakati mwingine ukimuona Mtumishi anafundisha soma usidhani somo hilo alilipata tu kienyeji. Kuna masomo Mengine ili usemeshwe na ROHO MTAKATIFU unahitaji kuwa na muda mwingi wa kuomba, kuna masomo uandaaji wake tu unaweza kufika masaa manane, kuna watumishi kila siku wanalala nje ya nyumba zao wakiombea Kanisa la MUNGU, Ni vyema sana kundi la MUNGU kuwategemeza watumishi hawa ambao wamepewa jukumu na MUNGU na kuwa waangalizi wa kundi la MUNGU.
Luka 10:7-9 '' Basi, kaeni katika nyumba iyo hiyo, mkila na kunywa vya kwao; maana, mtenda kazi amestahili kupewa ujira wake. Msihame-hame kutoka nyumba hii kwenda nyumba hii.  Na mji wo wote mtakaouingia, wakiwakaribisha, vileni vyakula viwekwavyo mbele yenu;
 waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa MUNGU umewakaribia. ''
Biblia  pia  inasema kwamba Mwanafunzi amshirikishe Mwalimu wake katika mema yote wagalatia 6:6 ''Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote. ''
 Mema yote ni pamoja na kumtegemeza.
Hata Mtumishi akikuombea sana na MUNGU akakubariki kwa maombi yake basi mshirikishe kwa mema hayo.
Kuna watumishi hata nguo tu hawana lakini wameombea watu wengi kupata kazi nzuri na hakika walipata.
Ndugu nakuomba uwe mtu wa kumshirikisha mema yote unayoyapata huyo Mtumishi wa KRISTO anayekuombea kila leo.
Inawezekana wewe kila wiki unaombewa, kila jumapili unaombewa au kila mara unamfuata Mtumishi akuombee na unafanikiwa sana, basi mshirikishe katika hayo mema yote uliyobarikiwa.
Mtumishi hana mamlaka ya kulazimisha kupewa kitu chochote lakini kwa wateule wanaojitambua basi kuwashirikisha baraka watumishi ni jambo jema sana.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

 

Comments