SHUHUDA ZA KUJENGA KUTOKA KWA MTUMISHI PETER MABULA.

 Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la BWANA YESU.
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Karibu ujifunze kitu muhimu.
Kazi za ushuhuda aliokutendea MUNGU.
1. Ushuhuda hujulisha matendo ya MUNGU, hivyo tunamtukuza.

2. Ushuhuda huongeza imani ya kumwamini MUNGU kwa wanaosikia ushuhuda huo.
3. Ushuhuda huifunua kweli ya MUNGU ambayo ipo na haijawahi kupungua.
4. Ushuhuda humwaibisha shetani na mawakala zale waliokuwa wamemfunga mtu, lakini Bwana YESU anamfungua na kumtendea muujiza.
5. Ushuhuda ujenga imani ndani ya watu wa MUNGU.
6. Ushuhuda hupelekea ulinzi zaidi wa MUNGU kwa aliyeshuhudia, ili shetani azidi kuabika.
7. Ushuhuda humwinua MUNGU na kumshudha chini shetani.
Baada ya hayo ngoja nikupe ushuhuda wa Dada mmoja ambaye kwa muda mrefu katika ndoa yake hakupata mtoto, na Dada huyu alikuwa anasumbuliwa na Majini mahaba sana.
Akajifunza masomo Yangu mtandaoni kisha akanipigia Simu tukaomba kwa siku kazaa na MUNGU wa Neema akamhurumia, akawafukuza majini mahaba na wachawi na sasa MUNGU amembariki kupata mimba.
Alichokisema ni hiki hapa.


USHUHUDA  WA KWANZA

"shalom,mtumishi Peter, ahsante kwa maombi yako kwa sasa ni mjamzito mi ni yule dada nilikwambia ninahitaji Mungu anisaidie nipate mtoto na aniondolee jini maimuna ahsante kwa maombi yako hatimaye Mungu amenijibu ubarikiwe sana.

Kwani uko wapi mtumishi, ningekuja kushuhudia.
basi nitakutafuta ili nije nimshukuru Mungu mi nipo kibaha ,ahsante sana Mungu wa mbinguni akubariki na kukutumia zaidi na wengine wapone kupitia wewe ubarikiwe sana Mtumishi wa Mungu maana nilihangaika sana lakini toka nilipo pata mawasiliano yako nikapata nguvu mpya Mungu azidi kukuinua usiache kuniombea."


Baada ya kufundisha somo la MAOMBI YA KUHARIBU NA KUBOMO MADHABAHU ZA UHARIBIFU kuna rafiki yangu ambaye ni Mtumishi wa MUNGU kaniandikia ujumbe huu juu ya jinsi yeye alivyomsaidia dada mmoja kuhusu kuharibu madhabahu za giza.
Mtumishi huyo wa MUNGU aliniandikia hivi:
Asante kwa somo Mtumishi nitalipitia lote, hiki usemacho ni kweli. Kuna dada moja alikuwa ananishirikisha mambo Ya kazini kwake. Alipata kazi kwenye ofisi moja na mshahara mzuri kweli kweli. Boss wake ni mwanamke na alimpenda sana yule dada Sababu ya utulivu wake na uchapakazi wake. Yule dada hakujua kama yule bosi wake anatumia nguvu za giza ikiwemo kafara na kuna muda bosi anamwambia "uje ulale kwangu" maana anakaa mwenyewe kwenye jumba Lake. Ananishirikisha nikamwambia usihamie kwake kaa kwenu huyo bosi wake anatumia nguvu nyingine. Kwa kufupisha, huyu dada nilimpa mbinu za kuombea eneo Lake la kazi pamoja na bosi wake Sababu alikuwa anamwota amemfunga na wafanyakazi wenzake anawaambia wamchape. Akapiga ile madhabahu haswaa baada ya siku mbili bosi kamwita Kumpata mshahara wake wote aondoke akamwambia tangu uje hapa ofisini mambo yangu hayaendi. Kumbe usiku kwenye ile ofisini kuna wafanyakazi wachache huwa wanarudi ofisini kuja kufanya ibada za kichawi na kwenye kila kiti cha mfanyakazi. Yule bosi mwisho akamwambia huyu Dada aliyeokoka kwamba MUNGU unayemwabudu endelea kumshika usimwache."

Mwisho.

Ndugu umejifunza nini?
Usipokuwa muombaji wanaotumika kipepo wanaweza hata kutaka kukutoa kafara wewe kwenye madhabahu zao za Giza.
Hakikisha unaomba ukiharibu madhabahu za uharibifu zinazofuatilia maisha yako.
Unaweza kujikuta unakalia kiti chako ofisini kwako kumbe wamekiwekea maagano ya kipepo ili mshahara wako hata kama ni mkubwa sana lakini usione mafanikio maana madhabahu ya Giza inakufilisi.
Ndugu unahitaji kuwa muombaji na fuata kanuni za ki MUNGU hasa urakatifu na utoaji ili madhara ya madhabahu za Giza yasikupate.




USHUHUDA WA PILI.
Mama mmoja wa dini tofauti na Ukristo alikuwa mimba na mimba ile ilimletea matatizo, pia ndoa yake ilikuwa katika mgogoro na tatizo kubwa. Alikuwa hana msaada na alijua anakufa kutokana na Bali iliyokuwepo huku aliyempa mimba amemkimbia. Mama Yule alikuwa ni mtu wa kujifungia chumbani kwake na kulia tu. Miezi michache kabla ya kujifungua alikata tamaa kabisa ya kujifungua salama na ya kuishi maana alikuwa anaumwa sana. Usiku mmoja akiwa chumbani peke yake wazo lilimjia kichwani kwamba a-search Google labda atapata kitu cha kumsaidia alijikuta katika hali asiyoitarajia akaandika MAOMBI YA KUHARIBU NGUVU ZA GIZA. Akakutana na masomo mengi ya watu tofauti tofauti lakini akajikuta anafungua link yenye somo langu na kuanza kusoma, alivutiwa na akatamani anitafute Facebook. Alipofungua Facebook alikutana na somo lingine ambalo linagusia hasa hitaji la moyo wake, somo hilo liliitwa MAOMBI YA KUMWAMBIA MUNGU AKUTANGULIE. Alisoma somo lile kisha akaomba maombi ya somo lile na kuona nafuu kubwa sana. Kesho yake tena akaomba maombi Yale na siku hiyo hiyo akaamua kuprint maombi Yale na akaweka ratiba kila siku saa sita usiku anaamka na kuanza kuyaomba katika jina la YESU KRISTO maombi yale. Alifanya hivyo kwa muda mrefu, kila siku na kisha akawa anaota ndoto YESU akimfungua vifungo vya Giza vingi alivyokuwa navyo. Baada ya hapo akaenda hospital na madaktari wakamwambia atajifungua salama maana amepona magonjwa ghafla, kweli siku ya kujifungua ilipofika akajifungua salama. Baada ya pale akawa anafanyia kazi masomo yangu na siku moja akaamua kuja kuniona na kunisimulia yote, kisha akataka nimuwekee mikono kichwani na kumuombea, nikafanya hivyo. Baadae nikamwambia habari za kuokoka akakataa akidai hawezi kuiacha dini ya wazazi wake maana yeye anatokea mikoa ya pwani ya Habari ya Hindi ila akanunua kitabu changu cha maombi. Baada ya hapo amekuwa muombaji sana kila siku usiku anaamka na kuomba katika jina la YESU. Mimi naamini ipo siku atapata neema ya wokovu wa Bwana YESU KRISTO.
Nilimuuliza kwamba je anamwamini YESU akasema anamwamini na tena YESU ndiye amemponya na kumsaidia katika mambo mengi.
Akasema bila YESU yeye angeshakufa, ila kumpokea YESU kama Mwokozi ndio imekuta mtihani kwake.
Mimi naamini ipo siku atapata neema.

Ndugu zangu nilichotaka kusema ni hiki YESU KRISTO ni kwa ajili ya watu wote.
Ukitaka akusaidie kwenye mahitaji yako anaweza akakusaidia hata kama hutaki kuokoka kwa kuingia uzima wa milele, kwa sababu unakataa kumpokea YESU kama Mwokozi wako.
Kumbuka tu kwamba YESU anaweza kumsaidia yeyote atakayehitaji msaada wake
Maana yeye YESU alikuja Kwa ajili ya watu wote.
Matendo 4:12 ''Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.''

Jambo muhimu kwa kila mwanadamu ni kwamba usimhitaji YESU akuponye tu au kukuondolea vifungo vya Giza Bali mhitaji pia YESU awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako, mtii na anza kukiishi Neno lake.
Ukitaka YESU akuponye tu basi hakika anaweza kukuponya lakini usihusike na uzima wake wa milele maana humhitaji kwa ajili ya uzima wa milele.
Mimi nakushauri mhitaji YESU kwa yote yaani mhitaji kwa ajili ya uzima wa milele na akufungue.
Wengi sana wamewahi kwenda makanisani ili YESU awaponye tu kisha warudi kwenye uovu wao na dini zao, ni sawa YESU anaweza kuwaponya lakini wasihusike na uzima wa milele.
Ndugu mhitaji YESU kwanza kama Mwokozi wako ndipo utake akuponye na kukushindia dhidi ya nguvu za Giza.
Kumbuka ni YESU huyo huyo siku moja atakuja kuwahukumu wanadamu wote unaowaona na wa dini zote.
Ufunuo 1:7-8 '' Tazama, yuaja na mawingu; na kila jicho litamwona, na hao waliomchoma; na kabila zote za dunia wataomboleza kwa ajili yake. Naam. Amina. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana MUNGU, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi.''

Unataka kujua zaidi juu ya siku ya YESU kurudi?
Biblia inakujibu vyema kabisa ikisema
''Tazama, siku ya BWANA inakuja, siku kali, ya hasira na ghadhabu kuu, ili iifanye nchi kuwa ukiwa, na kuwaharibu watu wake, wenye dhambi, wasikae ndani yake.-Isaya 13:9''

MUNGU akubariki
By Mwinjilisti Peter Mabula

Comments