TAFUTA KUSUDI LA MUNGU KATIKA MWAKA MPYA AMBAO MUNGU AMEKUPA ILI UISHI.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu.
Wiki ya mwisho ya mwaka uliopita nilimuomba MUNGU anipe ujumbe wa kuwaeleza watu wake wote kokote waliko kabla mwaka mpya haujaanza, ili wajue nini cha kufanya katika mwaka mpya, ROHO MTAKATIFU ni mwaminifu sana na akanipa somo hili.
Somo hili ni ufunuo unaotakiwa kuufanyia kazi wewe ndugu unayesoma somo hili.
Unapopata neema ya kuingia katika mwaka mwingine ni jambo jema sana lakini unahitaji kujua kusudi la MUNGU katika mwaka huo mpya ambao MUNGU amekupa kuishi, sio wote wamefika mwaka huu, wengine wamefariki dakika chache kufika mwaka huu, wewe umefika kwa sababu MUNGU anataka ulitafute kusudi lake katika mwaka huu mpya ambao MUNGU amekupa.
Kwanini Kusudi la MUNGU? Hebu ngoja nianzie hapo.

Neno ''Kusudi'' limebeba mambo mawili.
1. Neno kusudi limebeba ''Nia''
Nia ni dhamira ya kutaka kukamilisha jambo.

2. Neno kusudi limebeba ''Azimio''
Azimio ni mpango wa kufanya kitu fulani.

Kwahiyo tunaposema ''Kusudi la MUNGU'' maana yake ni dhamira ya MUNGU ya kukamilisha mpango ambao yeye mwenyewe MUNGU ameshaupanga kwa ajili ya mwanadamu fulani  katika majira fulani.
Mwaka unaweza kuwa ndani ya majira husika.
Ujumbe wangu leo unasema tafuta kusudi la MUNGU katika mwaka mpya ambao MUNGU amekupa kuishi..
Watu wengi sana katika mkesha wa mwaka mpya hushangilia na kufurahi sana, ni jambo jema lakini unapofurahi kupokea mwaka tafuta pia kusudi la MUNGU la mwaka husika.
Mwaka unaweza kuwa ndani ya majira ambayo MUNGU amekusudia jambo fulani kwa ajili yako.
Kwa sababu ya kutokujua wengi sana hupishana na kusudi la MUNGU katika mwaka mpya ambao wanauingia.
 Kumbuka '' Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung'oa yaliyopandwa;-Mhubiri 3:1-2''
 Kumbe kila jambo lina majira yake.
Je mwaka huu mpya uliopewa na MUNGU ili uishi umebeba kusudi gani kwako kiroho na kimwili?
Kuna wengine huu mwaka mpya ambao wameuingia kuishi ndio mwaka wao wa mwisho kuishi duniani, ndugu usiogope maneno haya lakini ukweli ni kwamba kila mara tunasikia misiba, na kifo kipo tu, na kila mtu kwa majira yake na mwaka wake ataondoka.
Sizungumzii vifo ambavyo ni kazi ya shetani na mawakala zake, vifo hivyo tunaweza kuvifuta na kuvikataa kwa maombi na havitatokea, ila sasa mimi nazungumzia kifo kilicho mpango wa MUNGU kabisa kwamba kwa mujibu wa mbingu ratiba ya mtu fulani kuishi imefika mwisho, hapo lazima aondoke, maombi na kufunga havitafanya kazi maana ratiba ya MUNGU ya kumchukua mtu huyo inakuwa imefika.
Ndugu, jambo muhimu sio kufa bali muhimu uelekee uzima wa milele baada ya kufa, hilo tu ndio muhimu sana.
Muhimu sasa ni kulitafuta kusudi la uzima wa milele la MUNGU. Kusudi la MUNGU la uzima wa milele linaanza na mtu husika kuokoka.
Yohana 3:16-18  '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana(YESU KRISTO) ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye(YESU KRISTO) hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.'' 
Kisha baada ya kuokoka ni kuishi maisha matakatifu katika KRISTO Mwokozi.
1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''
 Ndugu, nisikilize kwa makini sana hadi mwisho itakusaidia.
Kulingana na Mhubiri 3:1-8 unaweza ukapata mambo mengi sana lakini baadhi ni haya.
Kuwa watu mwaka huu wala sio mwaka wao wa kufa, ila ni mwaka wao wa kupanda katika ufalme wa MUNGU, ili baadae waje wavune.
Kuna watu mwaka huu mpya waliouingia ni mwaka kwao wa kubomoa madhabahu za giza , ili baadae waje wafanikiwe.
Kuna watu inawezekana mwaka uliopita ulikuwa mwaka wa kulia na kuonewa, lakini mwaka huu utakuwa mwaka wa kucheka, kama ni wewe ndugu basi tafuta kusudi la MUNGU linalotengeneza kicheko  chako.
Inawezekana miaka mitatu mfululizo kwako ilikuwa miaka ya furaha na amani lakini kwako mwaka huu ukawa mwaka wa vita kubwa ya kiroho.
Ndugu nakuomba tafuta kusudi la MUNGU katika mwaka mpya uliopewa na MUNGU ili uuishi.
Miaka minne(4) Mfululizo ROHO MTAKATIFU alinifunulia mambo ya kufanya katika mwaka husika ambao nilikuwa nauingia, hata mwaka huu kwa Neema ROHO MTAKATIFU alinijulisha juu ya mwaka huu kwamba utakuwa wa nini.
ROHO MTAKATIFU anaweza kukujulisha juu ya yajayo, ndio kazi yake hiyo.
1 Kor 2:10 '' Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU.''

KWANINI UTAFUTE KUSUDI LA MUNGU KATIKA MWAKA MPYA AMBAO MUNGU AMEKUPA KUISHI?
Hapa sasa nisikilize kwa makini zaidi sana katika points hizi saba(7) muhimu

1. Kuna miaka mingine ni utimilifu wa wakati ili jambo fulani lililokusudiwa na MUNGU lifanyike.
 Mfano hai ni Wagalatia 4:4 '' Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, MUNGU alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,''
 Utimilifu wa wakati ulipotimia YESU alikuja.
Inawezekana na wewe katika maisha yako kuna mambo yalisubiri tu utimilifu wa wakati ili yaje kwako.
 Inawezekana ulijaribu sana kupata mchumba ili mfunge ndoa lakini ikashindikana, ulifanya hivyo kwa kusudi la kibinadamu na sio la MUNGU, Kama sasa ni majira ya MUNGU ya kukubariki ndoa hakika hakuna atakayekuzuia wakati huu maana ni utimilifu wa wakati kwako ili upate.
Inawezekana kuna mambo mengi sana umewahi kuyaombea na mengine uliyaona kabisa katika ulimwengu wa roho, ndugu, kuna mengine yalikuwa yanasubiri utimilifu wa wakati, kama utimilifu huo umefika hakika baraka yako itakuja kwako.
Muhimu tu litafute kusudi la MUNGU katika mwaka huu mpya ambao MUNGU amekupa kuishi.
Wengine pia hupishana na majira yao. Mfano binti anaona kusubiri kuolewa imeshindikana sasa anaamua kukubali kutoroshwa na anaacha kanisa, kumbe majira yake kwa mujibu wa mbingu ilikuwa mwakani ndipo angefunga ndoa takatifu kanisani na kwa ushindi tena ikiwa kusudi la MUNGU kabisa.
Ndugu litafute kusudi la MUNGU katika majira haya ya mwaka huu mpya ulipewa. Iko mifano mingi sana ila nimesema kwa uchache ili utafakari ni katika mambo gani kwako utimilifu wa wakati umetimia hivyo ukikaa vizuri kwa YESU hakika utapokea.

2.Kuna miaka kwako inaweza kuvikwa taji ya wema.
Zaburi 65:11 '' Umeuvika mwaka taji ya wema wako; Mapito yako yadondoza unono. ''
 Hili ndilo andiko la mwaka ambalo mimi nimepewa kwa ajili ya mwaka huu. Najua ufunuo huo nimepewa sio tu kwa ajili yangu bali ni kwa ajili ya wote ambao nitawaombea, watajifunza masomo yangu, nitakaoshirikiana nao katika kazi ya MUNGU na wale ambao MUNGU amewakusudia.
Najua kabisa sio kila mtu huu  kwake utakuwa umevikwa jati ya wema na MUNGU, Mimi nakuombea wewe unayejifunza somo hili huku ukiishi maisha matakatifu katika KRISTO huu uwe mwaka wako uliovikwa taji ya wema.
Mwaka wako ukivikwa taji ya wema magonjwa utakuwa unayasikia tu kwa watu, wachawi hawatakuweza, utapata baraka nyingi na milango mingi ya mafanikio itafunguka kwako, kuna fursa na huduma yako inaweza kufanikiwa.
Muhimu tu tafuta kusudi la MUNGU katika mwaka huu ili ushirikiane na majira yako ya MUNGU kwa mwaka huu kwako.

3. Inawezekana huu ni mwaka wa nyongeza kwako ili tu uifanye kazi ya MUNGUau utengeneze njia zako.
Mfano hai ni huu, Isaya 38:5 '' Enenda ukamwambie Hezekia, BWANA, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano.''
 Unapoona umeongezewa miaka maana yake miaka yako ilikoma kabisa ila kwa neema umeongezewa miaka ili uifanye kazi ya MUNGU au utengeneze njia zako.
 Unaweza kuwa wewe ni mdhambi na MUNGU amekupa neema ya kukuongezea mwaka ili utubu, uokoke na uishi maisha matakatifu, ndugu tafuta kusudi  la MUNGU.
Inawezekana ungekuwa umeshakufa, ila kwa neema umeongozewa mwaka huu ili umtumikie Bwana YESU, Ndugu litafute kusudi la MUNGU katika mwaka huu.
 Ukisikia nyongeza maana yake ungeshakufa ila MUNGU amekuongezea tu, sasa je kama umeongezewa mwaka ili utimize kusudi la MUNGU lakini wewe umelikimbia hilo kusudi la MUNGU itakuwaje?

 4. Inawezekana kumcha MUNGU kwako ndiko kumeleta mwaka wa uzima na amani kwako.
Mithali 3:1-4 '' Mwanangu, usiisahau sheria yangu, Bali moyo wako uzishike amri zangu.  Maana zitakuongezea wingi wa siku. Na miaka ya uzima, na amani.  Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za Mungu na mbele ya mwanadamu.''
 Ndugu, kusudi la MUNGU ni wewe uendelee kuishi maisha matakatifu ili uendelee kupewa miaka ya kuishi na ili miaka yako ijaye uzima na amani.
Endelea kulitafuta kusudi la MUNGU na endelea kuliishi Neno la MUNGU lenye kusudi la MUNGU kwako.
Sheria ya MUNGU ni Neno la MUNGU na amri za MUNGU ni maagaizo ya MUNGU yote juu ya maisha yako. Uko katika wakati wa injili ya KRISTO hivyo hakikisha Neno la KRISTO linakuwa sheria yako na maagizo ya KRISTO yanakuwa amri yako ya kuiishi.

 5. Kuna miaka ni ya kusudi la MUNGU mtu aondoke duniani.
Zaburi 90:10 ''Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara.''
Biblia inaposema Neno hilo inakuwa inakujulisha kwamba miaka ya mwanadamu ya kuishi duniani ina ukomo.
Biblia imesema miaka 70 maana yake mwisho wa kusudi kwa mtu husika kuwapo duniani, na miaka 80 maana yake ni miaka ya nyongeza ambayo mtu anaongezewa na MUNGU kwa sababu maalumu.
Sio lazima mtu afe akiwa na miaka 70 au 80 bali kila mtu ana 70 yake na kuna baadhi wana 80 zao.
Ndio maana kila leo tunasikia watu wanakufa katika miaka tofauti tofauti.
Mfano unaweza kuona kwamba Yohana Mbatizaji alikufa akiwa na miaka chini ya 34 lakini Mtume Yohana alikufa akiwa na miaka zaidi ya 80. Hawa wote waliondoka duniani kipindi ambacho Neno la MUNGU la Zaburi 90:10 limeshajulisha.
Ninachotaka ujue ni nini?
Mtu akifariki na miaka 20, hiyo ndio sabini yake.
Mtu akifariki na miaka 50 hiyo ndio sabini yake. Ndio maana sio kwamba kila mtu akifikisha miaka 70 ndipo anakufa.
Ndugu, muhimu sana litafute kusudi la MUNGU katika mwaka huu. Kama kwa neema au kwa njia yeyote ukadhani kabisa kuna uwezekano wa kuondoka hata mwaka huu basi okoka na ishi maisha matakatifu siku zote.
Inawezekana uko katika sabini yako,  na inawezekana wewe uko katika themanini yako, ni heri kutengeneza kwa Bwana YESU KRISTO Mwokozi.

 6. Kuna miaka ndio majira yako ya kutokea ili ufanye kazi ya MUNGU au ufanye jambo fulani jema katika maisha yako.
Luka 3:1-8 utasoma yote ila   kwa mistari 3 ya kwanza  Biblia inasema hivi ''Mwaka wa kumi na tano wa kutawala kwake Kaisari Tiberio, Pontio Pilato alipokuwa liwali wa Uyahudi, na Herode mfalme wa Galilaya, na Filipo, ndugu yake, mfalme wa Iturea na nchi ya Trakoniti, na Lisania mfalme wa Abilene,  wakati wa ukuhani mkuu wa Anasi na Kayafa, neno la MUNGU lilimfikia Yohana, mwana wa Zakaria, jangwani.  Akafika nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi,''
 Huu ni mfano hai kabisa. Yohana mbatizaji habari zake tunazisoma tu kuhusu kuzaliwa kwake na baada ya hapo miaka zaidi ya 28 za umri wake hazisemwi katika Biblia, Lakini wakati wa kutokea kwake ili afanye kazi ya MUNGU ulipofika ndipo tunamuona Mtumishi wa MUNGU Yohana Mbatizaji akitokea na kuhubiri toba na kubatiza.
Hata kwako inawezekana kabisa mwaka huu mpya ambao MUNGU amekupa kuishi ndio mwaka wako wa kutokea kuanza kazi ya MUNGU Binafsi aliyokuitia ROHO MTAKATIFU.
Inawezekana ndio mwaka wako wa kurekodi nyimbo za injili, inawezekana ndio mwaka wako wa kuanza kutembea Tanzania nzima kuhubiri injili ya KRISTO.
Hata mimi Peter Mabula kuna Miaka ilikuwa imebeba kusudi la MUNGU la kufanya kazi fulani ya MUNGU.
Ndugu, lijue kusudi la MUNGU la mwaka huu ili ilifanye hilo.
Inawezekana ndio mwaka wa wewe kufungua huduma, inawezekana ndio mwaka wako wa kuanza kuhubiri redioni au kwenye TV. Kuna makusudi ya MUNGU mengi kwa kila Mtumishi kulingana na wito, mazingira na kazi aliyoitiwa.
Muhimu litafute kusudi la MUNGU na majira haya, ila ufanye tu kile ambacho ni ROHO MTAKATIFU anakuelekeza katika kusudi la MUNGU la majira haya, usiruke hatua kwa matamanio yako au mtazamo wako.
Inawezekana huu ndio mwaka wako wa kufunga ndoa, kufungua Biashara kubwa n.k
Litafute kusudi la MUNGU ndugu.

7. Kuna miaka ni miaka ya kutokea yale ambayo uliyaona zamani kwenye ndoto au maono.
Habakuki 2:2-3 ''BWANA akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.  Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.''
 Mstari wa 2 wa Habakuki 2 unasema kwamba njozi(ndoto) uiandike maana sio ya kutimia wakati huu. Lakini Mstari wa 3 unaonyesha kuna wakati ndoto hiyo itatimia.
Inawzekana sasa kuna mambo uliyaona zamani ndotoni au kwenye maono, mambo hayo hayakutimia wakati huo kwa sababu majira yake yalikuwa bado hayajafika.
Ndugu litafute kusudi la MUNGU maana kuna ahadi ambazo uliahidiwa zamani na MUNGU na ukathibitisha kabisa kwamba MUNGU amekujulisha, lakini haikutokea wakati huo kwa sababu hayakuwa majira yake, ndugu inawezekana kabisa huu mwaka mpya ndio mwaka wa hayo kutimia.
Muhimu litafute kusudi la MUNGU la wakati huu.

Katika maombi yako leo omba MUNGU akupe kulijua kusudi la MUNGU.
Hakikisha kuanzia leo unaishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU Mwokozi.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments