USHUHUDA KAMILI WA ASKOFU EMMANUEL LAZARO

Askofu Emmanuel Lzaro, Askofu mkuu wa kwanza wa Kanisa la T A  G
BWANA YESU ALINITOKEA

Nilizaliwa katika kijiji cha Modio, wilaya ya Hai mkoa wa Kilimanjaro Tanzania. Nilisoma elimu ya msingi katika shule ya msama, na baadaye nilienda Mombasa kwa mafunzo ya miaka miwili. Baba yangu anaitwa kunandumi na mama yangu anaitwa Firayandiani . Wazazi wangu walipenda sana mambo ya dini inagawaje wakati huo neno la wokovu lilikuwa halijahubiriwa kwa hiyo hawakujua wokovu.
Katika siku za utoto wangu, neno la uponyaji kwa jina la Yesu halikuhubiriwa kabisa, wala hatukusikia kuwa Yesu anaweza kumponya mtu mgonjwa kwa jina lake. Nilipokuwa na umri kama wa miaka saba niliugua, hali yangu ilizidi kuwa mbaya ikabidi nilazwe kwenye zahanati ya kanisa la Kilutheri Masama. Hata hivyo hali yangu iliendelea kuwa mbaya na Daktari akataka nirudishwe nyumbani. Mwili wangu ulidhoofika sana, na kutoa harufu mbaya. Chumba nilimokuwa nikilala kilinuka harufu hiyo, na kwa ajili ya udhaifu pia sikuweza kula kabisa.
Nilipokuwa nikiongea , niliisikia sauti yangu nyuma ya kichwa changu. Siku moja asubui, kama saa nne niliskia baridi sana mwilini mwangu: nikamwomba mama anitoe nje ili nipate joto la jua. nikiwa nje mama aliniangalia kaanza kulia nilipomwona mama analia nilimuuliza "Unalia nini?" Akaniambia "Nalia kwa sababu nimefanya kila niwezalo ili upone lakini huponi" kwa ghafla nikatokewa na maneno haya yafuatayo "SITAKUFA YESU NI UWEZA" nikamwambia mama.
Wakati maneno hayo yalipokuwa yakinitoka, yalibadilika kuwa moyo ndani ya kinywa changu, ikawa kama kunga donge la moto kinywani. Nikiwa nashangaa yanayonitokea ule moto ulishuka tumboni nikaanza kusikia joto kali katika mwili wote. Nilitokwa na jasho mwili wote na hapo hapo nikajikuta mimi ni mzima kabisa. Nikiwa sielewi ni nini kimetokea nilijiskia hamu ya kula, nikamwomba mama anipe chakula. mama hakuamini kuwa naweza kula, akaniuliza , "wewe waweza kula?" Nikamjibu "ndiyo". Akanitengenezea chakula nikala na tangu wakati ule sikuwa mgonjwa tena "JINA LA BWANA LITUKUZWE"
Ingawa jambo hilo lilitokea mbele ya mama yangu sikuweza kumweleza ile hali iliyonitokea , bali ilinikaa moyoni mwangu bila kumweleza ile hali iliyonitokea , bali ilinikaa moyoni mwangu bila kumweleza mtu , Tangu zamani Mungu amekuwa akidhihirisha mambo yake yajayo na ndiyo awafunguaye vinywa wanadamu kwa wakati ulioamriwa ili wayanene. wakati nilipokuwa kwenye masomo yangu huko Mombasa niliugua tena. Hali yangu ikawa mbaya sana hata nikashindwa kula , Nilibebwa nikapelekwa katika hospitali ya madaraka Mombasa, na mjomba wagu Wilson Kimaro.
Nilipofika hospitalini nilikaa nikimngojea Daktari aje, Wakati nipo nje ya hospitali Mwili wangu ulionyesha hali ambayo nilihisi kama ninakufa. Mawazo yangu yakafikwa na hali ya kumwomba Mungu ingawaje sikuwa mtu mwenye hali ya kuomba wala sikuwamtu wa kutaka mambo ya Mungu kwa wakati huo. Ninakumbuka wakati huo, hofu ya kifo ilinitisha ndipo nilimwambia Mungu maneno haya "KAMA UKINIPONYA NITAKUTUMIKIA" sielewi nilipata wapi fikra hizo. Mara baada ya kusema hivyo , nilizimia nilipochukuliwa kupelewa ndani ya hospitali kulazwa sikuwa na fahamu kabisa. Kufuatana na taarifa nilizozipata baada ya fahamu zangu kunirudia daktari alisema hakuna uwezekano wa matibabu, kwa kuwa nisingeweza kupona.
Nilizimia tena kwa siku tatu na daktari alikuwa anaangalia mapigo ya moyo tu. Hii ikiwa na maana alikuwa akipima kuona kama nipo hai au nimekwisha kufa. Wakati wote nilipikuwa nimezimia, niliona malaika wa Bwana akija na kunipakata , akinionyesha maua mazuri ya ajabu. Malaika huyo alikuwa akinitokea hasa wakati ambao natokewa na hali ya kutoweka kabisa (Yaani kufa). Aliendelea kunitokea hivyo mpaka niporudiwa na fahamu zangu nikajikuta nimepona.
Niliwauliza wale wangonjwa waliolazwa chumba kile pamoja nami "Yuko wapi yule mtu anayeniletea maua?" wote walishangaa kuskia nimerudiwa na fahamu zangu, wakanieleza kuwa daktari alikuwa anaongea saa yangu ya kukata roho, na kwamba sikupewa dawa yoyote wala sindano tangu nilipolazwa hapo. Wala hakuna mtu yeyote aliyekuja kuniletea maua. "MUNGU NA ATUKUZWE KWA REHEMA ZAKE KWA WANADAMU"
Hata hivyo baada ya kupona sikuwa na mawazo tena kwamba nilimwahidi Mungu kuwa kama angeniponya ningemtumikia . Niliendelea kuwa mwovu kama kawaida.

NATOKEWA NA SHETANI NA KUOKOLEWA NA YESU
 
Katika siku za ujana wangu, mimi sikuamini shetani ni kitu cha kweli, wala katika kanisa langu hakukuwepo na fundisho lolote kuhusu shetani , na pia, tulipokuwa shuleni hatukupata elimu yoyote au tamko lolote lisemalo kuwa shetani yupo. Katika kijiji nilichozaliwa kulikuwa na dini mbili tu, Dini ya kiislamu na dini ya Kikristo (Dhehebu la Kilutheri). Mimi nilikuwa mkristo ingawa sikupenda mambo ya dini sana kama wazazi wangu walivyopenda. Tena nilipuuzia sana elimu juu ya mashetani. Waislamu katika Kijiji chetu waliamini sana nguvu za mashetani na uchawi lakini mimi sikuyasadiki hayo kabisa wala sikuyaogopa.
Ilikuwa siku moja saa nne usiku, nikiwa kitandani nikivuta sigara, kwa ghafla alitokea mtu mfano wa mwarabu, akiwa na taa kubwa iliyowaka chumbani kote. Macho yake yalikuwa kama nyoka, aliponiangalia niliona hali ya uadui machoni pake. Hungehitaji kufahamu kama ni mtu mbaya au mwema, kwani macho yake yalidhihirisha wazi kuwa ni adui, tena muuaji. Alisimama na taa yake kunikabili. Nilianza kujiokoa naye kwa kutupa mikono na miguu ili asinisogelee. Mara baada ya jitihada zote hizo ambazo hazikumuogopesha, niliona ametokea mtu mwingine upande wangu, na yule mtu aliyeshika taa alipomwona yule mtu aliyekuwa nami aliogopa kama vile mbwa aliyekemewa na bwana wake, Aligeuka akakimbia na kutoweka kabisa. Yule mtu alikuwa upande wangu alipoona yule adui amekimbia, naye aliondoka na kutoweka. Mambo hayo sikuyaona kwenye ndoto bali niliyaona kwa macho yangu kwani sikuwa nimelala. Pamoja na mambo hayo yote mimi sikumfahamu Kristo kama Bwana na mwokozi wangu na sikuwahi kusikia mtu akihubiri neno la Wokovu.
 
NAUGUA TENA.
 
Wakati niliokuwa na umri wa miaka ishirini na mbili, nilishikwa na hali ya mfadhaiko wa kufa, Niliwaona madaktari lakini hawakuona kama kuna ugonjwa wowote ndani yangu , ila walinambia niache mawazo. Hali ile ilizidi ndani yangu ikanifanya niwe mlevi sana, Niliamua kulewa ili kujisahaulisha hali iliyokuwa ndani yangu, lakini hata hivyo hali hiyo haikunitoka.
Baada ya kuona sipati msaada kwa hayo yote, ndipo nilimwomba baba yangu aniazime Biblia. Nilijaribu kusoma Biblia lakini sikupata msaada wowote, mwisho nilisema kama Mungu yupo basi nitaweka kichwa changu juu ya Biblia kila nilalapo na kama Biblia ni neno lake basi atanisaidia. Nililalia biblia kwa muda wa miezi mitatu. Kila siku jioni, kabla sijapanda kitandani nilale nilimwomba Mungu aniruhusu niweke kichwa changu juu ya Biblia nikasema "Ee Mungu nisamehe kama kuna kitu nimekosea au kama nimenunua pombe au sikumlipa muuzaji pesa zake naahidi nitamrudishia kesho, lakini niruhusu tu niweke kichwa changu juu ya Biblia."
Siku moja nilipokuwa kitandani ili nilale kama kawaida nikaweka kichwa changu juu ya Biblia mara chumba changu kikatokewa na nuru kali sana iliyong'aa kuliko uwezo wa jua, ndani ya nuru ile akatokea mtu akasema nami na kuniambia amekuja kunijulisha kuwa nitakufa!. Nikamwuliza, "Kwa nini nife?" Akaniambia ni kwa sababu mimi ni mwenye dhambi. Nikamwambia mimi si mwenye dhambi kwa sababu nilibatizwa tangu nikiwa mtoto mdogo. Akanijibu kwamba ningelikuwa nimebatizwa nisingelikuwa natenda mambo mabaya. Nikamwuliza "mambo gani?" Ndipo aliponyoosha mikono yake akanionyesha matendo yangu yote mabaya niliyokuwa nimeyatenda tangu utoto wangu.
Akanambia "Je , Matendo haya ni yako?" Nikamwambia "Ndiyo" Kila tendo alilonionyesha lilikuwa kweli na nililikumbuka nilivyotenda. Nikamwambia, "Ninakubali mimi ni mwenye dhambi." kwa ajili ya matendo hayo utakufa, lakini nimetumwa nikujulishe kuwa kama utampokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wako utaokoka nawe hutakufa" Ndipo nikamwambia ninakubali kumpokea Yesu, naye akanimbia nipige magoti ili aniongoze sala ya toba. Nikapiga magoti akaniongoza salam ya toba, na ya kumkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yangu. Pale pale litatokea ziwa la maji na akaniambia njoo nikubatize, akanichukua na kunizamisha ndany ya maji, Akanibatiza kwa jina la baba na la mwana na la Roho Mtakatifu. Mimi kabla ya hapo sikuwa nimeona au kusikia kuwa kuna ubatizo wa kuzamishwa ndan ya maji mengi.
Asubuhi baba yangu aliniuliza "Ulikuwa unaongea nini usiku mwenyewe?" Ndipo nilipomweleza yote yalionitokea na jinsi nilivyobatizwa ndani ya ziwa la maji. Kumbe nilipokuwa nasema na yule mtu nilikuwa nikisikika hata kwenye chumba ndani ya ziwa la maji alinionya na kuniambia nipunguze ulevi. Hata baada ya kutubu kwenye yale maono sikupona ule ugonjwa nilokuwa nao mara baada ya yale maono niliondoka kwenda mjini arusha. Wakati nikiwa Arusha nilielezwa juu ya kikundi kidogo kilichouwa kinaimba na kuhubiri Injili . Mimi na wenzangu tuliamua kwenda hapo ili tukaangalie. Jambo lililotufanya twende ni kule kusikia kuwa kuna mama wa Kizungu ambaye alikuwa akiimba nyimbo za Mungu kwa kutumia gitaa . Siku zile gitaa ilitambulikana kama chombo cha shetani kabisa. kwa hiyo tulienda ili kuona dini ya kishetani inavyoimba. Tukaingia ndani mara yule mama akaanza kuimba na wimbo aliouimba maneno yake ni kama ifuatavyo. "Usisumbuke kwa safari, Mungu akulinda utegemee pendo lake , Mungu akulinda..."
Kabla mama yule hajamaliza kuimba, Nilishukiwa na nguvu zilizoingia moyoni na kuondoa ile hali ya siku zote ya kufa nikawa mzima kabisa. Kwa sababu zile nguvu zilisisimua mwili wangu wote, nilijikuta natokwa jasho jingi sana. Wenzangu niliofuatana nao walipigwa na mshangao wakajaribu kunituliza lakini sikuweza kusema nao , baada ya zile nguvu kutulia nikaamua kumwona huyo Mmisionari na mke wake ili niwaulize ni kitu gani kilichonitokea na imekuwaje mtu aimbe kisha nipone. Ndipo waliponihubiria habari za Yesu na uweza wake wa kuokoka na kuponya , Na kwa kuwa alikuwa akinisomea Biblia nikadhani Biblia ile siyo kama ya kanisa letu huenda ni nyingine .
Ndipo nilipoamua kurudi nyumbani nikachukua biblia ya baba yangu kwa kuwa mimi sikuwa na biblia yangu. Nilipoona Biblia ya yule mmisionari na ileile ya baba yangu ni sawa neno kwa neno, na mstari kwa mstari nilishangaa na kujiuliza, "Mbona maneno ya wokovu na uponyaji hayahubiriwi kanisani kwetu?" Nilirudi tena Arusha kukutana na Yule Mmishionary, Ndipo nilipokubali kumpokea Yesu. Naye akaniongoza sala ya kumpokea Yesu kuwa Bwana na mwokozi wangu. Nilibatizwa ndani ya ziwa la aina ile ile niliyoona kwenye yale maono. Niliamua kufata kila neno la Biblia lilivyokuwa linaeleza kuhusu wokovu. Kisha wakanifundisha juu ya ubatizo wa Roho Mtakaifu : Nikawa na hamu kubwa ya kupokea Roho Mtakatifu . Nilikesha kwa muda mrefu nikimsihi Mungu anibatize kwa Roho Mtakatifu. 
 
SHETANI ATAFUTA KUNIANGAMIZA TENA
 
Nikiwa natafuta ubatizo wa Roho Mtakatifu alinitokea mwanamke ambaye alikuwa amepanga chumba kilichokuwa karibu na chumba changu. Alinipenda sana akataka nizini naye, lakini upendo wa Kristo ulikuwa mkuu ndani yangu kiasi ambacho kishawishi chake hakikunitia shida yeyote bali niliendelea kumshuhudia neno la Mungu. Bila mimi kujua makusudi yake, alinitengenezea dawa, akaweka kwenye kahawa akanipa . Nilikunywa ile kahawa na baada ya kunywa nilianza kusikia kifua changu kikiwa kizito.
Baadaye kikatokea kitu kifuani kama ndege na mtu akitoa sauti mbele yangu au akinisalimu kile kitu kilizunguka kifuani na kutoa miiba ambayo iliniumiza kwa maumivu makali sana. Wakati huo nilikuwa sijajazwa Roho Mtakatifu. Nilienda hosipitalini na daktari aliponipima alinambia kuwa sina ugonjwa kifuani bali ni mawazo tu. Niliendelea kuumwa na nikazidiwa sana. Yule mwanamke alipoona nakaribia kufa alinijia akiwa amejaa chuki na akaniambia kuwa haya yote yamenipata kwa sababu nilikataa kuzini naye. Wale wenzangu waliokuwa wameokoka walinieleza juu ya uponyaji wa Yesu na kunisomea maandiko ya
"Marko 16:17-18 ''Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya;" 
 
Wakaniuliza "je unaamini jina la Yesu?" nikawaambia ndio. Ndipo walipoweka mikoni juu yangu na kwa jina la Yesu wakamwamuru pepo ndani yangu anitoke, saa hiyo hiyo , kile kitu kikapiga kelele ndani yangu kikatoka nikawa mzima pale pale. Nikapigwa na mshangao mkubwa nikabakia nikiangalia kulikuwa na nini kwenye mikono yao na nilipoona hakukuwa na kitu chochote isipokuwa jina la YESU tu ndipo nilipoamua mimi na maisha yangu yote nitamtumikia Bwana Yesu. Yule mwanamke alipoona nimepona alikasirika sana na kuniambia ni lazima ataniua . Nilikuwa tayar nina ujasiri mkubwa wa jina la Yesu hivyo nikampuuzia na kumwambia "Hutaniweza kwani mimi nina jina la Yesu" kuanzia wakati ule yule mama aliogopa sana, mwishowe alihama Arusha na hatimaye aliugua ugonjwa wa kuvimba mwili na akafa
Shetani aliazimia kuniua tena wakati huu waziwazi, lakini Mungu aliniandaa kwa wakati wangu ili adhihirishe Uweza wake kwa watu wa kizazi chetu, naye shetani hali akijua hayo alijitahidi kutaka kuniangamiza mara nyingi ili kusudi la Mungu lisitimie lakini kama vile Neno lake lisemavyo katika Isaya 55:11 "Ndivyo litakavyokuwa neno langu litokalo katika kinywa changu halitanirudia bure bali litatimiza mapenzi yangu nalo litafaikiwa katika mambo yale niliyolituma" katika Yeremia 1:12 amesema "Ninaliangalia neno langu ili nilitimize" kwa maana halisi ni kwamba Mungu hulilinda Neno lake, na kuhakikisha kuwa limefanikiwa na kutekeleza yale aliyolituma. Mimi nilishangazwa sana na matokeo ya mambo ambayo yalikuwa yakinipata kwani nilipokuwa nikiangalia wenzangu hawakuwa wakipatwa na jambo lolote mfano wa hayo.
 

 NAJAZWA NGUVU ZA ROHO MTAKATIFU.

Nilianza kuutafuta uso wa Bwana, ili nipate ahadi ya Roho wake; nakumbuka nilikesha mbele zake kwa maombi kwa muda kama wa miezi mitatu. Siku moja tulikuwa kwenye Conference huko puge Tabora, na nguvu za Mungu zilikuwepo kwa wingi sana. Yule mtu aliyekuwa akihubiri alipomaliza alisema "wote tuseme moto" na watu wote tukasema moto. Mara zikanishukia nguvu nyingi nikajikuta nanena maneno nisiyoyafahamu. Niliendelea kunena kwa lugha kwa masaa mengi , moyo wangu ulifurika nguvu za Mungu na hapo hapo nikaanza kupokea moyo wa kwenda nyumbani kwetu Moshi nikawaeleze mambo ambayo Mungu amenitendea.
 
Tuliporudi Arusha kutoka Puge Tabora niliendelea kukesha na kuomba. Siku moja Mmisionari  tuliyekuwa naye ambaye aliitwa Claeson aliniita akaniambia "Mungu amesema nenda nyumbani kwenu" Mimi sikujua maana yake ni nini ila moyoni  mwangu nilishataka sana kwenda nyumbani niwaeleze yale yaliyonitokea. Mara nilipofika, nilienda kanisani kwetu nikamwomba Mchungaji aniruhusu niwaambie mambo ambayo Mungu amenitendea . Akaniuliza ni mambo gani nikamweleza jinsi nilivyookoka na jinsi Mungu alivyoniponya kwa jina la Yesu na jinsi nilivyojazwa Roho Mtakatifu kama mitume.
 
Mchungaji akaniambia "Siwezi kukuruhusu kwa kuwa wewe unataka kuleta dini mpya hapa" Nikamwambia sio kweli ila tu nataka kushuhudia Bwana alivyonitendea . Kwakwel mimi sikuwa na haja ya kuhubiri ila tu  hamu yangu kuwaeleza yale Bwana aliyonitendea. Nilipoona Mchungaji amekataa niliwafuata vijana nikawaeleza jinsi nilivyookoka, nilivyoponywa na kujazwa Roho. 
 
Vijana wakashangaa sana wakaniuliza "je hata sisi tunaweza kujazwa Roho vile vile kama wewe? " Nikawaambia "ndio" wakaniuliza "tufanyeje ili tupate huo ujazo?" Nikawaambia ni kwa njia ya kuomba tu. Wakaniambia "Tuko tayari tuongoze jinsi ya kuomba" Mimi nikaanza kuogopa nikifikiri kama tukiombea kanisani na Roho Mtakatifu akashuka itatokea hali ambayo viongozi wa kanisa hawataipenda, na mimi nitasumbuliwa na sikutaka niwakosee viongozi wa kanisa langu.
 
Kwa hiyo nikawaambia kama mnataka kujazwa Roho, twendeni porini tukaombee huko. Huku nikijua kama Roho akishuka huko hakuna mtu atakayetusikia. Vijana kwa kuwa walitamani sana kujazwa Roho walikubali kwenda porini bila kujali, kwa kuwa hamu yao ilikuwa ni kujazwa Roho tu
 
ITAENDELEA HAPA HAPA KWENYE POST HII.

Comments