WEKEZA KWENYE UFALME WA MUNGU.


Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Je umewekeza kwenye ufalme wa MUNGU?
Je unaendelea kuwekeza kwenye ufalme wa MUNGU?
Labda ngoja nianze na maana ya Neno ''kuwekeza''
Maana ya ''Kuwekeza'' ni kutumia fedha yako au Mali yako kwa lengo la kuzalisha zaidi.
Inawezekana mambo ya uwekezaji yamefahamika zaidi katika mambo ya kimwili na sio mambo ya kiroho.
Hata kiroho uwekezaji kwenye ufalme wa MUNGU ni jambo la muhimu sana kwa kila mteule wa KRISTO.
Mathayo 6:19-21 " Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako."
Ufafanuzi wa Mathayo 6:21 kwenye BHN inasema "Maana pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako."


Kumbe hazina yako ndipo pia moyo wako utakuwa.
Hazina ni nini?
Hazina ni mahali pazuri kulikohifadhiwa vitu vya thamani.
Vitu vyako vya thamani unahifadhi wapi?
Ndugu, kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwekeza kwenye ufalme wa MUNGU. Furaha ya wateule wa MUNGU ni kwamba uwekezaji wao ni mbinguni na sio duniani tu.
Je hazina yako umekeza wapi?
Mtu aliyefanikiwa sana kiroho ni yule aliyewekeza mbinguni.
Kumbuka kama umeokoka hakika utaishi pahali ambapo hazina yako ilipo.
Kama humtaki tena YESU ujue hazina yako haitakuhusu maana hutaenda huko.
Je hazina yako kiroho umewekeza wapi?
Je umewekeza duniani hata moyo wako uwe kwenye hazina yako.
Je umewekeza wapi?
Najua unakijua kisa cha Lazaro na tajiri.
Lazaro aliwekeza mbinguni ndio maana alipokufa alienda mbinguni.
Na tajiri aliwekeza duniani na kwenye dhambi ndio maana alipokufa alienda kuzimu kuteseka. Alipokuwa anahitaji tone la maji alikuwa anajuta sana kwanini maisha yake hakuwekeza kwenye ufalme wa MUNGU. Alitamani hata ndugu zake waambiwe kwamba wawekeze mbinguni lakini jibu la Biblia ni kwamba hapa duniani kuna watumishi wa MUNGU wa kweli, hivyo kama mtu hatawasikiliza hakika hata angekuja Malaika wasingemsikiliza.

Luka 16:19-31 " Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia, akasema, Ee baba Ibrahimu, nihurumie, umtume Lazaro achovye ncha ya kidole chake majini, auburudishe ulimi wangu; kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahimu akasema, Mwanangu, kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya; na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo, kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze; wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu. Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu, kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao. Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu. Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu."
Kuwekeza kwenye ufalme wa MUNGU ni muhimu sana.

Uwekezaji mbinguni hauhitaji pesa nyingi Bali unahitaji moyo uliopondeka wa kumcha MUNGU.

Uwekezaji kwenye ufalme wa MUNGU unahusika mambo matatu kwa pamoja ya lazima na muhimu sana.


1. Kuishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU.
 
1 Petro 1:15-16 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu."

 Kuishi maisha matakatifu katika YESU KRISTO ni kufanya uwekezaji muhimu sana katika ufalme wa MUNGU.
Ni maisha matakatifu tu ndiyo yanakayokufanya ukauone vyema uwekezaji wako mbinguni kwa MUNGU.
Mathayo 5:8 ''Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona MUNGU.''
Bila utakatifu hutamuona MUNGU hivyo inakupasa sana kuishi maisha matakatifu katika RISTO YESU.

2. Utoaji matoleo kwa upendo.
 
Luka 12:33-34 " Viuzeni mlivyo navyo, mtoe sadaka. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, akiba isiyopungua katika mbingu, mahali pasipokaribia mwivi, wala nondo haharibu. Kwa kuwa hazina yenu ilipo, ndipo itakapokuwapo na mioyo yenu."

 
Angalizo; Biblia haisemi uuze kila ulichonacho Bali katika Mali yako au biashara yako au kazi yako unatakiwa katika hicho chanzo chako cha pesa kumtolea MUNGU vizuri sana. ROHO wa MUNGU akikupa msisitizo hata wa kitu cha thamani sana na ukipendacho sana usiache kutoa.

Sadaka ni muhimu sana sana kwa ajili ya kustawi kwako kiroho na kimwili.
Sizungumzii mtumishi wa MUNGU akushawishi kutoa bali wewe mwenyewe binafsi rohoni mwako upate msukumo wa kumtolea MUNGU.
Kumbuka kufanikiwa kiroho kunahitaji madhabahu sahihi na sadaka sahihi. Inawezekana wewe hutoa sadaka hekaluni lakini ni katika hekalu ambalo madhabahu ya MUNGU aliye hai haimo. Hakikisha unatoa sadaka katika madhabahu ambayo YESU KRISTO ndiye Mwokozi. Usitoe tu hekaluni bali hakikisha ni hekalu ambalo lina madhabahu ya JEHOVAH MUNGU wa pekee.
Kuna watumishi sio watumishi wa Bwana YESU, kwa hao usitoe  sadaka yako hata kama watumishi hao wana mahekalu makubwa ya kuabudia, husika zaidi na madhabahu sahihi ndipo utoaji wako utakuwa na maana mbele za MUNGU aliye hai.

3. Kumtumikia KRISTO kwa usahihi.
 
1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."

 Kumtumikia KRISTO ni uwekezaji muhimu sana katika ufalme wa MUNGU.
Kwanza Biblia inasema kwamba Ikimtumikia KRISTO  hakika MUNGU atakuheshimu.
Yohana 12:26 ''Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba(MUNGU) atamheshimu.''
Pia katika ufalme wa MUNGU utang'aa kama jua kama ulikuwa unamtumikia YESU KRISTO kwa usahihi.
 Danieli 12:3 '' Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.''

Ndugu hakikisha unawekeza kwenye ufalme wa MUNGU kama una mpango wa kwenda huko.

Ni muhimu sana kutengeneza hazina yako mbinguni.
Utajiri wa dunia utakoma na kuisha ndugu, weka hazina mbinguni.

Mathayo 19:21 "YESU akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate."

Sadaka yako ya hiari ni uwekezaji katika ufalme wa MUNGU, na sadaka hiyo itakusaidia baadae.
Maombi yako ni sadaka njema itakayokusaidia baadae.
Utajiri wa kidunia hauna maana kama huishi maisha matakatifu, ni dhambi na ni hasara.
Yakobo 5:1-6 "Haya basi, enyi matajiri! Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza, na mavazi yenu yameliwa na nondo.
Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba katika siku za mwisho.
Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu, ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia masikioni mwa BWANA wa majeshi.
Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki mkamwua; wala hashindani nanyi."


Ndugu, hakikisha unaishi maisha matakatifu huku ukiweka hazina mbinguni.
Ndugu, mche MUNGU hata wakati umebarikiwa sana.
Mche MUNGU hata kama utakuwa tajiri.
Kumbuka uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu alivyonavyo.
Uchoyo wako kwa MUNGU ni hasara yako binafsi.
Kuna watu wakihubiriwa utoaji wananuna, wanachukia na wakati mwingine wanaanza kuzusha uongo juu ya wachungaji wao wanaowahubiria.


Ndugu, zingatia maandiko haya itakusaidia.
Luka 12:15-21 " Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini MUNGU akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?
Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa MUNGU."

Ndugu hakikisha unajitajirisha kwa MUNGU.
Ni neno muhimu sana hilo.
Hakikisha unajitajirisha kwa MUNGU na sio kwa shetani. Shika hilo katika maisha yako yote na katika baraka zako zote.
Wengi hujitajirisha kwa shetani tena kwa kufanya matendo ya kishetani kabisa.
Ndugu jitajirishe kwa MUNGU.
Nasema tena jitajirishe kwa MUNGU, weka hazina mbinguni.
Kumbuka dunia ya vyote vilivyomo, ikiwemo Mali yako vyote vitapita, lakini anayemcha MUNGU huyo atadumu milele.
1 Yohana 2:17 "Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele."


Una heri wewe unayejifunza Neno hili Leo.
Ndugu, Mtumikie MUNGU hata kwa Mali zako, kwa pesa zako, kwa kazi yako na kwa mshahara wako.
Kumbuka unaweza ukaondoka duniani kabla hujaweka hazina yako mbinguni.


 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments