HUSIKA NA UPENDO WA MUNGU KWAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Hata upendo una kiwango chake na kipimo chake.
Kuna upendo wa mama kwa mtoto.
Kuna upendo wa Mke kwa Mume wake au Mume kwa mke wake.
Kuna upendo wa Mtoto kwa wazazi wake.
Upendo wote ni mzuri na husika na kila upendo ambao hauna dhambi ndani yake, maana kuna upendo mwingine unaweza Kukufanya utende dhambi jambo ambalo ni baya sana.
Katika jamii ya Leo tunasikia kwa upendo watu wakisema hakuna kama Mama au hakuna kama Baba, ni sawa kwa muono wao.
Kuna wengine husema hakuna kama mke/Mume ni sawa kwa muono wao
Lakini kwa sababu upendo una kipimo na kiwango naomba kukujulisha kwamba kuna upendo upendo ulio na kipimo kikubwa kuliko upendo wa aina yeyote.
Upendo huo ambao Biblia inauita upendo wa Agape ni Upendo wa MUNGU kwa wanadamu watakatifu wake na upendo mwingine ni upendo wa KRISTO kufa msalabani ili kuwaokoa wanadamu watii.
Ndugu, hata kama unahusika na upendo mwingine wote, uko sahihi kabisa lakini usiache kuhusika na upendo wa MUNGU kwako tena usikubali upendo wa KRISTO usihusike na maisha yako.
Kwa upendo wa ajabu kwako, MUNGU aliamua kumleta Mwanaye wa pekee ili wewe ukimwamini huyo upate uzima wa milele.

Upendo wa MUNGU unaanzia hapa '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.-Yohana 3:16-18''
Ndugu, husika na upendo huo itakusaidia maisha yako yote.
Upendo wa mama kwako unaweza ukakoma, mfano akifariki.
Upendo wa mke/mume unaweza ukakoma, mfano akifariki.
Lakini upendo wa MUNGU ni wa milele kama ukihusika na upendo huo.
Mama anaweza kumwacha mtoto wake lakini ukiokoka na kuishi maisha matakatifu hakika MUNGU hatakuacha.

Isaya 49:15-16 " Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake anyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.
Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima."


Ndugu husika na upendo wa MUNGU kwako.
Kuhusika na upendo wa MUNGU kwako ni wewe kumpokea YESU kama Mwokozi wako kisha kuanza kuishi maisha matakatifu katika yeye.
Inawezekana wewe unajua kwamba upendo wa rafiki yako kwako ndio upendo zaidi ya upendo wote.
Inawezekana wewe unadhani upendo wa wazazi ndio upendo namba moja, inawezekana wewe unadhani upendo wa mke/mume ndio upendo namba moja.
Ndugu Biblia imeshaweka mpaka siku nyingi sana kwamba kwa vipimo vya upendo hakuna upendo kama upendo wa YESU KRISTO kwako mwanadamu, YESU aliacha ukuu sana mbinguni ili aje akuokoe wewe, sio tu kukuokoa kirahisi Bali alilipa gharama kuu kuliko zote, gharama hiyo ni kufa msalabani kwa aibu.
Yohana 15:13-14 " Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo."


Ndugu Yangu, hakikisha unahusika na upendo huu wa YESU KRISTO kwako.
YESU alilipa gharama na sasa kazi yako ndugu ni nyepesi sana, kazi yako ni kumpokea YESU kama Mwokozi wako binafsi kisha kuyashika akuamuruyo,
Injili yake ina yote akuamuruyo na muhimu ni haya,
1 Petro 1:15 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; ''
Ukilijua hilo inakupasa sasa kuliishi kusudi la MUNGU la kuokolewa kwako.
MUNGU hataki uendelee na mambo ya kwanza yaani matendo mabaya  uliyoyafanya kabla hujaokoka.
Biblia inakushauri ikisema '' Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;-1 Petro 1:14'' 
Kumbuka umenunuliwa kwa damu ya thamani sana ya YESU KRISTO hivyo ishi katika utahamni mpya uliopewa na MUNGU Baba.
1 Kor 6:20 ''maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.'' 

Damu ya YESU ni thamani sana kwako na imekupa thamani.
Jina lako baada ya kumpokea YESU na ktubu limeandikwa katika kitabu cha uzima mbinguni. Kwa sababu gani?
Ni kwa sababu Damu ya YESU KRISTO ya agano imekutakasa na kukuondolea dhambi zote na kuzifuta hivyo wewe kuanzia dakika hiyo kutambuliwa mbinguni kama mtakatifu kwa MUNGU, baada ya kukubali una dhambi na kuhitaji msaada pekee wa kuzifuta dhambi hizo ambao ni YESU KRISTO.
1 Yohana 7-10 ''bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote.  Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu. Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.'' 
Damu ya YESU haishiii kukutakasa tu na kukufanya kuwa safi mbele za MUNGU bali hata leo damu ya YESU ukiitumia katika maombi yako inaweza kukufungua vifungo vyote, laana zote, balaa zote na kuharibu kila mipango yote ya shetani.
Damu ya YESU ni kila kitu katika maisha ya Mteule wa MUNGU anayeliishi Neno la MUNGU.
Ndugu hakikisha damu ya Thamani ya YESU KRISTO inakukomboa, inakomboa afya yako, uchumba wako, ndoa yako, biashara yako, kazi yako uchumi wako, uzao wako na kila kitu chako, ita damu ya YESU kwenye maombi yako ili ikuweke huru mbali na uonevu wa shetani.
Hayo yote mema ya MUNGU yatakupata kwa sababu umehusika na upendo wa MUNGU kwako kwamba uokkoke na uishi maisha matakatifu. 
Kuokoka ndilo jambo la kwanza ambalo MUNGU analokuamuru.

Maana YESU alikuja kuwaokoa wanadamu.
Luka 19:10 '' Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.''
Ndugu ulikwa umepotea sana kwa sababu ya dhambi, ulikuwa umepotea sana kwa sababu ya kuabudu shetani, sanamu au mizimu. Ulikuwa umepotea sana kwa sababu hukuwa unamwabudu MUNGU Baba katika Roho na kweli. Lakini kwa sababu ya upendo wa ajabu sana wa YESU KRISTO yeye amekuja kukuokoa. Haijalishi ulifanya dhambi mbaya kiasi gani au ulikosea makosa mengi kiasi gani, ndugu kwa dakika moja tu ukimpokea YESU kisha ukatubu na kuacha dhambi hizo na kuanza sasa kuishi maisha matakatifu ya kulitii Neno la MUNGU ambalo ni Biblia takatifu hakika utakuwa umeokoka na damu ya YESU KRISTO ya agano itakuwa imekuweka huru kabisa na dhambi zako wala hazitakumbukwa mbinguni.
Nimewahi kuongea na watu kadhaa wakisema kwamba wamefanya dhambi nyingi kiasi kwamba wanaamini hawawezi kusamehewa. Ndugu yangu unayewaza hivyo nakuomba umkumbuke Mtume Paulo ambaye kabla hajaitwa Paulo alikuwa anaitwa Sauli Muuaji. Alikuwa muuaji na alikuwa kwa vyovyote amehusika kuua watu, Lakini YESU wala hakujali hivyo Bali aalipomwita na akaitika na kukubali kumpokea YESU kama Mwokozi wake, akabatizwa na kuanza kujifunza Neno la MUNGU hakika YESU aliitwa Mtume Paulo na Mtume kwa mataifa yote hata ambayo wewe unayafahamu leo yote.
Hata wewe hakika YESU anaweza kukubadilishia historia yako mbaya na kuwa mtu mzuri, husika tu na upendo wa MUNGU katika maisha yako.
MUNGU hakika ni mwema mno kwako ndugu, hivyo husika tu na upendo wake kwako ndugu.
Isaya 55:6-9 ''Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa. Maana mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu; asema BWANA. Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.''
Huo ni upendo wa MUNGU wa ajabu sana hivyo hakikisha unahusika na upendo wa MUNGU kwako.
Kuishi maisha matakatifu ndio jambo la pili analokuamuru MUNGU baada ya wewe kumpokea YESU.
Ndugu husika na upendo wa KRISTO kwako.
Kumbuka upendo wa mwanadamu kwako huishia kaburini.


Labda pia ngoja nikuambie jambo hili ya kwamba hatuendi mbinguni kwa sababu tuna dini.
Tunaenda mbinguni kwa sababu tuna YESU KRISTO kila siku, kila saa, kila wakati.
Maana unaweza kujua hata Biblia yote na mbinguni usiende kwa sababu unaweza kujaza maandiko moyoni kichwani lakini usiwe na YESU kama Mwokozi wako.
Jambo muhimu sana ni kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi kisha uaanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu katika yeye.

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments