JINSI YA KUPONA JERAHA LA MOYO ULIROJERUHIWA

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU la ushindi.

Katika maisha wakati mwingine kuna kupitia majeraha makubwa sana ya moyo.

Majeraha ya moyoni ni majeraha mabaya sana kuliko hata majeraha ya mwili.

Nimewahi kuongea na watu kwa simu na kujikuta nina maswali mengi sana juu ya maumivu yao.

Mtu mmoja alinipigia simu huku analia sana akisema kwamba yeye ni mke wa mtu na ndoa yao ilikuwa ya amani na furaha sana lakini baadae alikuja kupata maumivu ambayo hayabebeki ndio maana amekuwa ni mtu wa kulia tu na wakati huo roho ya mauti inamfuatilia kutokana na majeraha hayo ya moyoni aliyotendewa na msichana wake wa kazi. Akasema kwamba wakati akiwa mjamzito aliamua kwenda kijijini kwao kutafuta msichana wa kazi maana mimba ilikuwa imeanza kuwa kubwa hivyo alihitaji mtu wa kumsaidia, alimpata binti mmoja na kuja naye mjini na kumwajiri kama msichana wa kazi, baada ya miezi mitatu yaani bado kama mwezi mmoja ajifungue alishangaa kuona mume wake amebadilika ghafla na kuanza mipango ya kuvunja ndoa, alipochunguza aligundua mume wake yuko katika mahusiano ya kimapenzi na yule Msichana wa kazi na hakika siku chache sana baadae  yule mama akafukuzwa na mume wake. Alipomwambia yule Msichana wa kazi alikutana na matusi makali sana na yule binti akasema kwamba kwa sasa yeye ndiye mama wa familia hivyo yeye aondoke haraka. Mama yule alidhani ni kama ndoto lakini ndio hivyo ndoa yake ilikufa  kwa sababu ya msichana wa kazi, maumivu moyoni mwake yalikuwa makubwa sana na majeraha yalikuwa makubwa sana.

Ndugu yangu unayeteswa na majeraha moyoni mwako kutokana na mambo mabaya uliyofanyiwa au matukio yaliyokupata nakuomba  nisikilize kwa makini sana katika somo hili maana utapona.

Wakati mwingine inaumiza sana kama ni mtu wako wa karibu na uliyemwamini na kumpa siri zako zote ndiye anakuumiza moyoni kwa uzushi wake kuhusu wewe.

Zaburi 55:12-14 '' Kwa maana aliyetukana si adui; Kama ndivyo, ningevumilia. Aliyejitukuza juu yangu siye anichukiaye; Kama ndivyo, ningejificha asinione. Bali ni wewe, mtu mwenzangu, Rafiki yangu, niliyejuana nawe sana. Tulipeana shauri tamu; na kutembea Nyumbani mwa MUNGU pamoja na mkutano.''
 

Utajisikiaje ukisikia mtu wako wa karibu ndiye aliyekuwekea sumu au ndiye  aliyesababisha ufukuzwe kazi?

Utajisikiaje mtu wako wa karibu ndiye aliyevunja ndoa yako na sasa unatanga tanga?

Utajisikiaje mtu wa karibu katika ukoo wako au mnayefanya kazi pamoja ndiye anataka kukuua?

Hakika ni maumivu makubwa moyoni.

Unajisikiaje mtumishi mwenzako wa MUNGU ndiye anafanya kampeni za siri ili huduma yako ife?
Ona mfano huu hai ambapo watu aliowasaidia Nabii Yeremia walimgeuka na kuanza kufanya mipango mibaya ya siri dhidi yake.

Yeremia 18:18-20 '' Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote. Niangalie, Ee BWANA, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.''
Unaweza ukawafanyia watu mema mengi sana lakini ni hao hao wanakuja kukugeuka na kutaka kukuangamiza, inauma sana hakika.

Watu wengi kazi yao ni kuwakosesha wengine.

Mama mmoja aliiishi na mume wake katika ndoa kwa amani na furaha sana kwa zaidi ya miaka 20 kwenye ndoa. Walipata mali nyingi, nyumba na magari  na maisha yao  yalikuwa ya furaha sana, lakini baadae mume wake akaumwa na kufariki. Ndugu wa mume wake baada ya msiba wakakaa kikao cha ukoo kulingana na kabila lao na kuamuru kwamba yule mama arudi kwa wazazi wake, wadogo wa marehemu ndio watachukua watoto  na kuwasomesha, mali zote ndugu wakagawana  na yule mama akafukuzwa katika nyumba yake mwenyewe waliyojenga na mume wake, maumivu ya mama huyo ya rohoni yalikuwa magumu sana, moyo wake ulikuwa na majeraha mengi sana. Inawezekanaje una miaka zaidi ya 45 uambiwe kwamba urudi kwa wazazi wako baada ya mume wako kufariki?
Mali ulizoshiriki wewe mwenyewe kuzitafuta kwa miaka mingi wenzako wanazitumia ndani ya muda mfupi tu huku ukiangalia?
Ni maumivu makali hakika.

Ndio maana Bwana YESU anasema ole wake anayeleta mambo ya kuwakosesha wengine

Mathayo 18:6-7 '' bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari.  Ole ni wa ulimwengu kwa sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha! ''

Ziko familia wanaishi kama watumwa kwa sababu tu ya kushindana na matajiri.

Wako watu wana maumivu kupita kawaida kwa sababu tu ya chuki zisizo na maana.

Mtu mmoja aliniambia ya kwamba alishamfumania  live mke wake kwa nyakati tofauti  akifanya mapenzi na watu zaidi ya 4.

Mama mmoja aliniambia kwamba mume wake ameshamgeuza ngoma kwa kumpiga kila siku bila kosa lolote.
Kuna watu walibakwa na kuachiwa majeraha ya moyo mionyoni mwako yasiyopona kirahisi.

Wako watu wanatembea na majeraha mabaya mioyoni mwao.

Utajisikiaje ukisikia kwamba mmekuwa na matatizo sana katika familia yenu tangu Baba yenu afariki na aliyemuua Baba yenu  yupo na anawatambia kabisa.

Wako watu wamedhulumiwa na kujikuta wana maumivu mabaya moyoni mwao yaliyotengeneza vidonda vya moyo vibaya sana.

Wako watu walisalitiwa na kujikuta wana majeraha mabaya moyoni.

Wako watu hata wako jela kwa kusingiziwa, hayo ni majeraha mabaya ya moyo.

Wako watu waliwekewa sumu na watu wao wa karibu ili wafe lakini neema ya MUNGU ikawapata hawakufa lakini wamebaki vilema au wagonjwa wa kudumu, majeraha yao ni makubwa sana.

Majeraha ya moyo wakati mwingine hayaji tu kwa sababu umefanyiwa mabaya bali wakati mwingine kuna watu wana majeraha mazito rohoni mwao kwa sababu ya kufiwa ghafla na wapendwa wao waliowategemea sana.

Ndugu mmoja wazazi wake wote pamoja na wadogo zake walifariki siku moja kwa ajali yeye akiwa shuleni na hakuwa na ndugu wa kumlea, maumivu yake ni makubwa sana.

Ndugu somo hili ni ufunuo ili kukusaidia.

Hata wakati napewa ufunuo huu nilimuona katika ulimwengu wa roho mama mmoja ambaye moyo wake umetobokatoboka yaani moyo wake kwa jinsi ya kiroho una mashimo na unavuja damu, ana majeraha ya moyo yaliyo mabaya sana.

Baadae nikaona tena kwenye ulimwengu wa roho Mwanamke mmoja moyo wake umevuja damu na damu ile ikaganda na kuwa na rangi nyeusi nyeusi, nikaambia kwamba yule ana majeraha mabaya ya moyoni.

Ndugu, kuna kupona hakika katika jina la YESU KRISTO.

Inawezekana umejaribu hata kuwasamehe waliokukosea lakini umeshindwa kabisa.

Mama mmoja alinipigia simu akisema ‘’Mtumishi peter Mabula naomba nikutafute unifanyie darasa la ushauri na nitakulipa maana nina maumivu makubwa rohoni niliyotendewa katika maisha yangu kiasi kwamba nikikumbuka naumwa na kichwa kinaumwa hadi nahisi kufa’’ Nilichofanya kwa mama yule nilimwambia kwamba mimi nitamuombea kwa MUNGU na ahakikishe anawasamehe waliomkosea ila kuhusu ushauri wa kisaiklojia nilimwelekeza kwa watumishi wa MUNGU walio wataalamu wa kushauri watu kama alivyohitaji.

Kuna watu wanapitia magumu sana ambayo kibinadamu hayabebeki kwa sababu ya majeraha ya moyo, majeraha yale yanawafanya kutenda dhambi kila leo na majeraha hayo wengine yanawakosesha uzima wa milele.

Ndugu nisikilize itakusaidia.

Mimi Peter namshukuru MUNGU sana maana ni mmoja wa ambao waliwahi kupata majeraha mabaya sana ya moyo lakini MUNGU alikuja kunipa neema na kuniponya majeraha yale mabaya.

Kuna ushuhuda mmoja niliutoa kama somo ukisema kwamba ‘’JINSI NILIVYOSAMEHE MTU AMBAYE NILIAPA SITAMSAMEHE’’ unaweza ukasearch ukiandika somo na jina langu kisha utasoma kwa kirefu maana nilipitia mambo mengi hadi kupona rohoni kuhusu hicho ambacho nilitendwa.

Namshukuru ROHO MTAKATIFU maana aliponipa ujumbe huu alinipa mambo matano ya kufanya ili  uweze kupona majeraha ya moyo uliyonayo.

Jinsi ya kupona majeraha ya moyo.

    1. Omba toba kwa MUNGU kwa ajili ya yaliyotokea. 

Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; ''

Inawezekana kabisa ni wewe ndio ulisababisha hata ukaingia kwenye tatizo baya lililojeruhi moyo wako, inakupasa kutubu kwanza kwa yaliyotokea.

Inawezekana ulikuwa unasikia msukumo wa kuomba au kufunga lakini wewe ulidharau ndio maana mabaya yakaja na kukuachia maumivu mengi rohoni, tubu ndugu.

Inawezekana familia yenu au ukoo ulitumainia madhabahu ya  kishetani ndio maana mabaya hayo yanawafuata, tubu ndugu kwa MUNGU kwa kilichosababisha hata wewe uteseke na kupata majeraha ya moyo.

Inawezekana uliona katika ulimwengu wa roho ukiambiwa nini cha kufanya ili usiingie katika mambo yaliyokuja kukusababishia majeraha ya moyoni mwako, ndugu tubu kwanza.

Kutubu ndio kumruhusu MUNGU akusaidie, kutubu ndio kufungua neema ya MUNGU ya msaada kwako.

Tanguliza toba, tubu kwa ajili ya yaliyotokea, tubu kwa ajili ya waliokukosea, tubu kwa ajili ya familia au ukoo.

Andiko hapo juu linaonyesha kwamba wakati mwingine ili mema yaje kwako unatakiwa kutubu kwanza na kuwa safi mbele za MUNGU.

     2. Muombe MUNGU ili akuponye jeraha hilo la moyo.

Yeremia 30:17 '' Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema BWANA, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, ............... ''

Mwambie MUNGU akuponye jeraha hilo la moyo.

Kumbuka majeraha ya moyo yanaweza yakaambatana na roho ya mauti hivyo unaweza ukajikuta unakufa siku ambazo wala sio zako, hivyo mwambie Bwana YESU akuponye jeraha hizo za moyo wako.

Kumbuka jeraha za moyo zinaweza kukufanya hata usifanikiwe popote, uwe mtumwa wa shetani na uwe mtu asiye sahihi rohoni, ndugu unahitaji  kwenda kwenye maombezi na ukasema bila woga mbele ya watumishi wa KRISTO juu ya majeraha yako ya moyo, utaombewa na Bwana YESU ataponya jeraha zako zote za rohoni kama ilivyo ahadi katika Neno lake.

Usifanye moyo mgumu na kufanya siri wakati unaendelea kuteketea kupitia maumivu moyoni yasiyoisha.

Jambo lingine muhimu sana kukumbuka na kuzingatia ni kwamba usilipe kisasi kwa aliyekukosea na kukusababishia majeraha ya moyo.

Ukilipa  kisasi MUNGU hawezi kuwa upande wako kamwe.

Ukimkabidhi MUNGU jambo hilo  hakika yeye atakulipizia kisasi kama jambo husika litahitaji kisasi.

Warumi 12:19 '' Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya MUNGU; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena BWANA.''

Usilipe kisasi ndugu katika jambo lolote  lililoleta majeraha moyoni mwako.

    3. Samehe na kuachilia.

Luka 6:37 ''Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.''

Kumbuka jambo hili kwamba usiposamehe umefungulia mlango wa shetani kukutesa katika maisha yako.

Usiposamehe na wewe hauwezi kusamehewa na MUNGU dhambi zako hivyo huwezi kuupata uzima wa milele kama hujasamehe. Mathayo 6:14 '' Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.''

Najua wakati mwingine  ni ngumu sana kusamehe lakini kama kweli unataka uzima wa milele inakupasa tu kusamehe ndugu.

Najua wakati mwingine ni ngumu sana lakini ndugu haina jinsi inakupasa uwasamehe hao waliokukosea.

Siku moja mimi Mabula niliandaa somo la jinsi ya kuponya ndoa, Mwanaume mmoja kwa hasira baada ya  kujifunza somo hilo aliamua kunitukana sana akisema kwamba ‘’wewe ni kijana mdogo tu na hujui kuhusu matatizo ya ndoa maana ndoa yako haina hata miaka mitano’’ Baada ya kutukana na kusema maneno hayo niligundua yule ndugu yuko katika maumivu makubwa sana yaliyosababishwa na mwenzi wake. Ndugu usiufanye moyo wako kuwa mgumu bali samehe na kuachilia.

Kuna madhara mengi sana usiposamehe.

Inawezekana hujibiwi maombi yako kwa sababu ya kutokusamehe kwako.

Inawezekana unateswa na magonjwa kwa sababu ya kutokusamehe.

Inawezekana roho ya mauti inakufuatilia kwa sababu umeshindwa tu kusamehe.

Inawezekana shetani anaipiga kazi yako, biashara yako na kila chanzo chako cha uchumi kwa sababu wewe umemfungulia mlango kwako, kwa wewe kushindwa tu kusamehe na kuwaachilia waliokukosea wote.

Ndugu ukitaka ufanikiwe katika maisha yako jifunze kusamehe na kusahau.

Ukitaka uwe mkristo anayeenda mbinguni basi ishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU huku ukisamehe na kuachilia watu waliokukosea.



    4. Kubaliana na yaliyotokea.

Ayubu 2:10 '' Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa MUNGU, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake. ''

Ayubu ni mfano hai kwetu kwamba alipitia magumu sana sana na alikuwa na maumivu mengi sana sana mwilini na rohoni.

Ilifika kipindi hata mke wake akamwambia ni heri amkufuru MUNGU na kufa, Ayubu yeye aliikubali hali iliyomtokea ndio maana alimkemea mke wake juu ya ushauri mbaya.

Wako watu leo wakipata mabaya tu basi watu wao wa karibu wanawashauri kwenda kwa waganga wa kienyeji na kwa njia hiyo wanakuwa wamemkataa YESU Mwokozi.

Ndugu yangu kama kuna mambo yametokea ghafla na yameumiza moyo wako na kukuachia  vidonda vikubwa sana inakupasa kukubali yaliyotokea kama njia ya kupona kutoka kwenye tatizo.

Mfano wewe maumivu yako ni kwa sababu Baba yako alifariki ghafla na hivyo kujikita unateseka sana maana Baba ndio alikuwa msaada wako mkubwa, inawezekana huwa hata unaongea kwa uchungu sana huku unalia kwamba ‘’Angekuwepo Baba yangu au mama yangu nisingekuwa hivi’’

Ndugu kubaliana na hali halisi kwamba kwa sasa Baba yako au mama yako au mtu wako wa karibu aliyekuwa anakusaidia sasa kwamba kwa sasa hayupo, hata ukilia huwezi kumrudisha, hata ukifanya jambo lolote huwezi kumfanya awe hai na akusaidie kama zamani. Wengi sana wanateseka na majeraha ya moyo kwa sababu hawataki kukubaliana na hali halisi iliyotokea.

Inawezekana wewe ulisalitiwa na mwenzi wako wa ndoa ambaye ulimfanyia kila kitu chema lakini akaiishia kukusaliti, ukikumbuka jinsi ulivyomuona live kifuani mwa mtu mwingine wakifanya dhambi ya uzinzi huwa unalia sana, huamini na tukio hilo likijirudia moyoni mwako unakosa raha kabisa na unaojiona huna thamani hata moja.

Ndugu hata ukilia sana au hata ukifanya kitu chochote hauwezi kufuta kwamba ulisalitiwa.

Huo muda na hiyo dakika hauwezi kufuta kwamba ndio dakika ulisalitiwa, kubaliana na yaliyotokea na songa mbele ukiganga yajayo na sio yaliyopita.

Unaweza ukakonda na kuwa mtu wa kuumwa na kuteseka huku waliokukosea wananenepa na wanaendelea na maisha kama kawaida, ndugu kubaliana na yaliyotokea maana hiyo ni njia ya kupona jeraha la moyo.

Kama walimuua mzazi wao au mtu umpendaye kubaliana na yaliyotokea na sio kubaki nayo moyoni yakiendelea kukujeruhi tu moyo wako.

Muige Ayubu ambaye kwa siku moja watoto wake saba wote walikufa, wewe wala hujapata tatizo kubwa kama la Ayubu.

Ayubu kwa siku moja tu mali zake zote zilitekete, Ayubu akakumbuka  ghafla kwamba hakuja na mali duniani na wala hakuja na mtu duniani hivyo ni heri amuishie MUNGU aliyemleta duniani.

Ayubu 1:21-22 ''  akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile; BWANA alitoa, na BWANA ametwaa; jina la BWANA na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala hakumwazia MUNGU kwa upumbavu.''
 

Inawezekana hata unataka kulipiza kisasi kwa sababu umeshindwa kukubaliana na ukweli uliotokea. Ndugu kubaliana na yaliyotokea kisha samehe na kusahau, usikubali mabaya hayo yakautafuna moyo wako.

 5.  Waombee waliosababisha majeraha kwako.

Mathayo 5:43-45 ''Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. ''

Njia mojawapo kubwa sana ya kupona majeraha ya moyo ni wewe kuwaombea waliokuudhi.

Hiyo ni kwa faida yako mwenyewe.

Bwana YESU kama kielelezo alisema Neno hili mbele ya wanaotaka kumuua kipindi ambacho alikuwa anatukamilishia wokovu wetu.
 Luka 23:34 ''Yesu akasema, Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo. Wakagawa mavazi yake, wakipiga kura.''
 Kumbuka Neno la Bwana YESU kwamba ''Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo.'' Hata wewe inakupasa kuwasamehe na kuwaombea hata msamaha kwa MUNGU.

Stefano kama mfano hai aliwaombea msamaha kwa MUNGU watu waliokuwa wamempiga sana, na wakati huo anawaombea msamaha walikuwa wanashindana kwa kumpiga na mawe mazito kila sehemu ya mwili wake, Yeye aliwaombea msamaha hata katika hilo, yeye aliwaombea watu wale waliomuudhi. 
Matendo 7:60 '' Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, BWANA, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.''
Neno gumu sana kwamba ''BWANA, usiwahesabie dhambi hii.''
Aliwaombea msamaha kwa MUNGU.

Ndugu waombee tu  na kimaombi pambana na madhabahu za giza zinazowatumia ili kufanya mabaya.

Naamimi umepona, fanyia kazi points hizo ambazo ROHO wa MUNGU amenipa nikujulishe na hakika itakuwa heri kwako.

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments