MAMBO MATATU(3) MUHIMU YANAYOWEZA KUZUIA MAOMBI YAKO.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.


Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Najua wewe ni muombaji mzuri, ubarikiwe sana kwa kufanya hivyo.
Viko vizuizi vingi vinavyoweza kuzuia maombi yako, Nakumbuka nilishawahi kukuletea somo hapa linalosema mambo 10 yanayoweza kuzuia maombi yako, Lakini ROHO wa MUNGU amenipa tena mambo haya matatu akisema kwamba wengi sana pia wanashindwa kupokea ushindi wao kutokana na haya.
Ndugu Nakuomba fanyia kazi itakusaidia.
Hakikisha unakuwa mwombaji lakini fanyia kazi mambo haya 3 ili maombi yako yawe ni maombi yenye kibali, inawezekana maombi yako yanazuiliwa tu na mambo haya 3 nje na yale 10 niliyowahi kukufundisha.

Mambo matatu yanayoweza kukuzuia maombi yako.
 
1. Kuwaza mabaya kwako kunaweza kuzuia maombi yako.
 
Zaburi 66:18 "Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, BWANA asingesikia."


Kuwaza mabaya ni kizuizi kimojawapo cha maombi yako.
Ndugu mmoja ni muombaji mzuri lakini wakati mwingine huwaza kwenda kwa mganga wa kienyeji.
Ndugu, kuwaza mabaya tu kunaweza kuzuia maombi yako usipokee kwa MUNGU ulichoomba.
Baadhi ya waombaji wana roho mbaya na huwaza mabaya juu ya baadhi ya watu ndio maana hawapokei mahitaji yao, maana mawazo mabaya huzuia maombi.
Mfano unaomba upate Mume au Mke ili marafiki au majirani uwakomoe, huko ni kuwaza mabaya.
Mko katika kwaya na akiimbisha mtu ambaye humpendi unawaza kwamba heri hata mic izime asisikike, huko ni kuwaza mabaya.
Binti mmoja akasema siku moja kanisani kwao kwamba yeye ndio wa kwanza kuolewa kati ya mabinti wote na hivyo wengine watasubiri sana. MUNGU wala hayuko hivyo. Unaweza ukawaza hivyo na wewe ndio pekee ambaye utachelewa kuolewa katika hilo kundi hata kama unaomba sana.
Ndugu kataa kuwaza mabaya maana mabaya hayo yanaweza kuzuia maombi yako.

Kwenye nafsi yako kuna dhamiri hivyo hata dhamiri yako ni ya kuiangalia sana.
 Hata kama ni dhambi ndogo tu inakusumbua wewe, inakupasa uishughulikie dhambi hiyo kama ambavyo huwa unashughulikia dhambi kubwa.
Kibiblia hakuna dhambi kubwa wala ndogo ila kuna baadhi ya watu huzidharau baadhi ya dhambi wakiziona ni dhambi ndogo kumbe hizo hizo ndogo zinaweza kumfanya mtu asifike uzima wa milele.
Ndugu usidharau baadhi dhambi ukiziona ni ndogo Bali zishughulikie hizo dhambi kama unavyoshughulikia dhambi unazoziona ni kubwa. Kuwaza mabaya ni moja ya dhambi hivyo usiwe mtu wa kuwaza mabaya.

Inawezekana wewe unaomba sana lakini ili tu ukifanikiwa uwakomoe wengine, ndugu ukiomba huku unawaza mabaya unaweza usipokee kwa MUNGU yale uliyohitaji.


2. Dhambi isiyotubiwa inaweza kuwa kikwazo kikubwa cha mtu kujibiwa maombi yake.

Isaya 59:1-13 ''
Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia. Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong'ona ubaya.  Hapana adaiye kwa haki, wala hapana atetaye kwa kweli; hutumainia ubatili, hunena uongo; hupata mimba ya madhara, na kuzaa uovu.  Huangua mayai ya fira, na kusuka wavu wa buibui; yeye alaye mayai yao hufa, na hilo livunjwalo hutoka nyoka.  Nyavu zao hazitakuwa mavazi, wala hawatajifunika kwa kazi zao; kazi zao ni kazi za uovu, na vitendo vya udhalimu vimo mikononi mwao. Miguu yao hukimbilia mabaya, nao hufanya haraka kumwaga damu isiyo na hatia; mawazo yao ni mawazo ya uovu; ukiwa na uharibifu zaonekana katika njia kuu zao.  Njia ya amani hawaijui; wala hapana hukumu ya haki katika miendo yao; wamejifanyizia njia zilizopotoka; kila apitaye katika njia hizo hajui amani.
  Kwa sababu hiyo hukumu ya haki i mbali nasi, wala haki haitufikilii; twatazamia nuru, na kumbe! Latokea giza; twatazamia mwanga, lakini twaenda katika giza kuu. Twapapasa-papasa kutafuta ukuta kama kipofu, naam, twapapasa kama watu wasio na macho; twajikwaa wakati wa adhuhuri, kana kwamba ni wakati wa ukungu wa alfajiri; kati yao waliowanda tumekuwa kama wafu. Sisi sote twanguruma kama dubu; twaomboleza kama hua; twatazamia hukumu ya haki, lakini hapana; na wokovu, lakini u mbali nasi. Maana makosa yetu yamezidi kuwa mengi mbele zako, na dhambi zetu zashuhudia juu yetu; maana makosa yetu tunayo pamoja nasi, na maovu yetu tumeyajua; katika kukosa na kumkana BWANA, na katika kugeuka tusimfuate MUNGU wetu, tukinena jeuri na uasi, na kukusudia maneno ya uongo na kuyatoa moyoni. ''
 

Dhambi ni uasi kwa MUNGU, ndivyo maandiko yasemavyo, na uasi huo inaweza kumfanya mtu asijibiwe maombi yake hata kama ni muombaji sana.
Dhambi zinauficha uso wa MUNGU usiuone kamwe.
Maovu yako yanamfanya MUNGU asikusikie na kukutendea mema kama ulivyoomba.
Toba ya kweli ni jambo la muhimu sana ili mahitaji yako yajibiwe na MUNGU.
1 Yohana 1:8-10 " Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu."


Kutubu ndiko kumruhusu MUNGU akuangalie hata kukutendea mema.
Ndugu, dhambi isiyotubiwa inaweza kuzuia maombi yako hata kama unaomba sana sana.
Inahitajika sana toba kwa mtu wa namna hiyo ili ndipo mema aliyoyahitaji kwa MUNGU yaje.
Matendo 3:19 " Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"

Huwezi kuwa mwasherati  huku kila siku unaomba MUNGU akupe mke/mume mwema na huku kila siku pia unafanya uzinzi na uasherati, hiyo dhambi inaweza kukuzuilia maombi yako.
Huwezi kuwa mwizi, muongo, tabeli na bado kila siku unalia kwenye maombi kwamba MUNGU akubariki uchumi wako, dhambi zako zinaweza kukuzuilia maombi.
Kuna aina moja tu ya maombi  ya mtenda dhambi ambayo MUNGU huisikia na kuijibu, ni maombi ya toba tu.
Ukitaka kujua hilo soma Biblia yako vizuri, kagua wana wa Israeli walipokuwa wanamwasi MUNGU ilikuwaje, walikuwa wanaonewa na maadui zao lakini walipotubu kwa MUNGU ndipo MUNGU aliwainulia msaada. Sasa wewe unatenda dhambi na bado unaomba kwamba MUNGU akubariki, ndugu dhambi yako ya siri inaweza kukuzuilia maombi.
Unatoka na mume/mke wa mtu  harafu unaomba MUNGU akukumbuke, ndugu dhambi ya siri ni mbaya sana na inaweza kukuzulia maombi yako.


3. Unafiki unaweza kuzuia maombi ya mtu.
 

Maana halisi ya neno mnafiki ni kama kama ifuatavyo;
=Mnafiki ni mtu anayesema kinyume na anavyotenda.
=Mnafiki ni mtu anayetoa ahadi kisha asitimize.
=Mnafiki ni mtu mwenye tabia ya kutokusema ukweli.
=Mnafiki ni yule mtu anayefanya jambo ambalo anajua kabisa kwamba sio la kweli.
=Mnafiki ni mtu yule anayetumia hila kwa lengo la kujinufaisha yeye.
Sasa unafiki unaweza kukuzuilia maombi yako kujibiwa.
Mathayo 6:5 "Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao."

Unafiki ni hali ya mtu kujifanya anakubalika kuliko wengine.
Kama kwenye maombi unajaribu kujionyesha kwamba wewe ni bora kuliko wengine au unajiona unastahili kuliko wengine, huo ni unafiki.
Unafiki kama huo unaweza hata ukazuilia maombi yako.
Ndio maana Biblia inasema msiwe kama wanafiki.
Luka 18:9-14 "Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee MUNGU, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee MUNGU, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa."

Kwenye maombi usiombe ili kutazamwa na watu.
Kwenye maombi usiombe ili usifiwe na watu.
Kwenye maombi usiombe ili watu wakusikie na kukukubali.
Kama ni kuomba kwa sauti omba ila usiwe na nia nyingine ndani yako.
Hata Mimi Peter Mabula huomba kwa sauti lakini sio kwa kutafuta heshima au sifa za wanadamu.
MUNGU akiiona nia nyingine katika maombi yako, unaweza ukakwama hata kama umeomba kwa kulia sana na kuruka ruka.
Ndugu mmoja alimpenda binti Fulani, sasa wakiwa kanisani alikuwa anamsogelea binti huku akiomba kwa sauti kwamba akubaliwe, huo ni unafiki na ni kutafuta thawabu za wanadamu.

Epukab maombi ya kulipiza kisasi kwa wanadamu waliokukwaza au kukuudhi. Warumi 12:19 "Wapenzi, msijilipizie kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, kisasi ni juu yangu Mimi, Mimi nitalipa, anena BWANA"

Ni heri kuomba MUNGU akulipizie kisasi juu ya mawakala wa shetani wanaoshindana na wewe kwenye ulimwengu wa roho.
Ni heri kuomba MUNGU awaadhibu wakuu wa giza wote wanaokupangia na kukuwazia mabaya.
Ni heri kuomba MUNGU akupe moyo wa msamaha ili uruhusu kisasi cha MUNGU kupita juu ya adui zako.


                          Maombi ya Leo.

1. Kila jambo linahitaji hatua, kila baraka inahitaji hatua.
Mfano ukitaka kufunga ndoa unahitaji hatua hizi, kupata mchumba, posa, mahari, kibali cha wazazi na Kanisa na kisha ndoa. Hivyo unahitaji kuombea hatua zako.
Mfano unahitaji kufungua biashara, hatua zake ni kupata mtaji, kupata eneo la kufanyia Biashara, kupata kibali cha biashara na kibali kwa watu n.k. Hizo zote ni hatua ndio maana maombi ya Leo ni kuombea hatua zako za Kukufanya upate baraka timilifu uitakayo.
Inawezekana wewe umewahi kabisa kuona ukiwa unafanya kazi ofisi Fulani, kumbuka jambo hilo linaweza kuwa ni kweli kabisa lakini halitakuja ghafla Bali kuna hatua za kupitia hadi kufikia hatua uliyoiona kwa ndoto.
Inawezekana wewe uliona kwenye ulimwengu wa roho umevaa shela kanisani na watu wakishangilia, kama ni ndoto ya kweli basi tambua kwamba utatakiwa kupitia hatua zote ndipo uifikie siku hiyo, hata kununua shela tu au kukodi ni hatua hivyo kwa sababu zipo hatua nyingi basi ombea hatua zako zote, maana ikipindishwa kipepo hatua moja unaweza usiipate baraka yako.
Leo ombea hatua zako katika kila hitaji lako unalohitaji MUNGU akubariki.
Zijue hatua za hitaji lako zote na uziombee ukiharibu kila hila ya Giza inayoweza kupindisha hatua zako.
Ombea hatua zako za kupata mahitaji yako au baraka zako unazohitaji kuzipata.


2. Omba ROHO MTAKATIFU akuongoze siku zote za maisha yako. Zaburi 32:8
Kumbuka kwamba wanaoongozwa na ROHO MTAKATIFU tu ndio watoto wa MUNGU, Warumi 8:14
Biblia inakushauri kwamba kama umeamua kuishi katika ROHO MTAKATIFU basi enenda katika ROHO MTAKATIFU siku zote, Wagalatia 5:25.
Hivyo Leo muombe ROHO MTAKATIFU kwamba akuongoze siku zote za maisha yako.


3. Kila jambo katika maisha yako linahitaji kibali ili kufanikiwa.
Baraka yako inahitaji kibali cha MUNGU ili uipate.
Ombea kibali cha MUNGU kwako katika 

kufanikiwa kwako, omba pia MUNGU akupe kibali mbele za wote watakaohusika kukufanikisha katika mahitaji yako.
Kila jambo linahitaji kibali hivyo Leo ombea kibali katika kila hatua zako na mahitaji yako. Zaburi 19:14.

Mwisho kumbuka kwamba MUNGU hakupi tu kila unachoomba Bali hukupa unachostahili hivyo zingatia sana suala la kuongozwa na ROHO MTAKATIFU katika maisha yako maana yeye ndiye anajua kila kitu stahiki kwako na sahihi kwako, ROHO MTAKATIFU anaweza kukujulisha jambo la kuombea na ukapata mambo makubwa zaidi kuliko hata uliyohitaji wewe kwa MUNGU.

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments