MAOMBI YA KUFUNGA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Leo kwa sehemu kidogo tunaangalia maombi ya kufunga na umuhimu wake.
Kwa wateule wa KRISTO ukiulizwa ''Maombi ya kufunga nini nini?'' Jibu rahisi kabisa unaweza kusema hivi ''Maombi ya kufunga ni maombi ya kumuomba MUNGU Baba ili atende kitu ambacho asingetenda kama usingefunga''
Yanapoitwa maombi ya kufunga ni muhimu sana kujua kwamba maombi haya yanahitaji kuomba sana na sio kufunga tu.
Kuna watu kufunga wala haiwasumbui kabisa lakini katika funga yao maombi hawaombi, hiyo haileti maana sahihi ya maombi ya kufunga.
Maombi ya kufunga ni ya muhimu sana.
Maombi ya kufunga sio sheria wala sio lazima lakini ni ya muhimu sana kwa kila Mteule wa KRISTO, ni agizo bora lenye msaada mkubwa sana kwako mtu wa MUNGU.
Kuna mambo mengine ili ufanikiwe vyema unahitaji kuwa na maombi ya kufunga.
Najua kuna mambo huwa unaomba na yanafanikiwa, ni sawa kabisa lakini kuna mambo pia yanahitaji maombi ya kufunga.
Mathayo 17:21 [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]

Biblia inajulisha kwamba mengine yanahitaji maombi ya kufunga.
Inawezekana kuna mambo umeyahitaji sana , umeomba sana na umefunga Mara kadhaa lakini hukufanikiwa. Ndugu usihesabu gharama Bali tambua kwamba unahitaji kuwa nI maombi ya kufunga tena.
Inawezekana maombi yako uliyoomba yalitengeneza point A ya mafanikio yako katika ulimwengu wa roho. Inawezekana kuombewa kwako na watumishi kulitengeneza Point B na Point C ya ushindi wako lakini kufunga kwako wakati huu kutatengeneza point D yenye ushindi mkubwa na ambao utauona live kwenye maisha yako.
Ndugu, kuwa na maombi ya kufunga ni muhimu sana.
Esta na Waisraeli walifunga siku tatu kavu ili MUNGU atende  muujiza wa kuzuia kifo kwao

Esta 4:16 ''Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.''
 Na kweli MUNGU akafanya muujiza huo na sasa kifo kilichopangwa kiwapate watu wa MUNGU kikampata aliyekipanga kifo hicho.
Esta 7:10 ''Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari Mordekai. Ghadhabu ya mfalme ikatulia. ''

Faida ya maombi yale ya kufunga haikuishia tu kwa adui kufa bali  watu wa MUNGU walipanda viwango na kuchukua madaraka makubwa katika taifa la ugenini, mfano hai  ni Mordekai alipandishwa maradaka baada baada ya aliyetaka kuwaua watu wa MUNGU kufa. Hata wenyeji wa nchi waliamua hata kujifanya waisraeli kwa sababu MUNGU alifanya muujiza mkuu kupitia maombi  ya kufunga ya siku tatu ya Waisraeli.
Esta 8:15-17 '' Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawi na nyeupe, mwenye taji kubwa ya dhahabu, na joho ya kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Shushani wakapaza sauti, wakashangilia. Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi. Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, kwa kuwa hofu ya Wayahudi imewaangukia. ''

 Maombi yao yakatengeneza kitu kikubwa sana katika ulimwengu wa roho, maana maombi Yale yalipelekea adui yao kufa na adui alipokufa wao walipandishwa kiwango.
Ndugu unahitaji wakati mwingine kuwa na maombi ya kufunga.
Huamuriwi muda wa kufunga Bali ni hiari ya moyo wako kwa faida yako kiroho.

Inawezekana wewe unawindwa na wachawi ili wakuue, ndugu unaweza ukafunga na kuomba katika uwepo wa MUNGU na wachawi wale wakafa wao na sio wewe.
Anaweza akakuendea kwa waganga mtu ili akumalize lakini maombi yako ya kufunga na kuomba katika ROHO MTAKATIFU hakika yanaweza kumfanya anayetaka kukumaliza ajimalize mwenyewe, anayetaka kukulaani laana impate yeye, anayetaka kukuua afe mwenyewe, anayetaka ubaki na cheo hcho  hicho usipande  hakika atashuka cheo yeye na wewe kupandishwa cheo.
MUNGU anaweza kukuinua hata maadui zako wanaanza kujitangaza kwamba ni ndugu zako.
Maombi ya kufunga yana maana kubwa sana kwako kama katika funga yako unaomba katika ROHO MTAKATIFU.
Mimi Mabula nakujulisha tena ndugu kwamba bMaombi ya kufunga ni ya muhimu sana.

Kuna faida nyingi sana za maombi ya kufunga, baadhi tu ni hizi;


1. Ukifunga unainoa imani yako.

2. Ukifunga unaongeza ujasiri wako kiroho.

3. Kufunga huleta unyenyekevu mbele za MUNGU.

Tangu zamani watumishi wa MUNGU kuna wakati walikuwa na maombi ya kufunga maana walijua kuna siri kubwa ya ushindi katika maombi ya kufunga.
Ona mfano huu.
Ezra 8:21 " Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za MUNGU, na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote."


Hata wewe unaweza kufunga kwa maombi wikihii au  ijayo au kwa muda wako mwenyewe, ili kama maajenti wa kuzimu hawajawahi kukuona ukiwa unang'aa kama jua basi wakuone hivyo na wakimbie, ili kama kama wakuu wa Giza hawajawahi kukuona ukiwaumbia uharibu kwa jina la YESU basi watashangaa uharibifu unawapata ghafla
Zaburi 40:14-15 '' Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe! ''
 
Ziko faida nyingi mno katika maombi.

Itese nafsi yako kwa ajili ya ufalme wa MUNGU.
Kuna watu pia nimekutana nao ambao binafsi sikuielewa vyema funga yao.
Mtu  anakuambia amefunga masaa 6 au 4 au 7 n.k
Yaani mtu anakuambia kwamba Mtumishi nimefunga masaa 6 hivyo sitakunywa chai ila nitakula chakula cha mchana, kufunga kwa namna hii naona kuwa ni mzaha wa maombi ya kufunga.
Inawezekana hakuna kosa hata moja katika mtu anayefunga kwa  namna hiyo ila ushauri wangu ni vyema kufunga kuanzia asubuhi hadi jioni au kufunga bila kula kwa siku nzima ya masaa 24 au siku 2 au 3 au 4 au 5 au kama unaweza kuvuka basi unaweza.
Au kufunga siku nyingi hata 10, au 21, au 40 au 70 au hata 100 ukifunga asubuhi na jioni unakula katika hizo siku zote.
Lakini habari za kufunga masaa matano yaani unaacha chai unakula mchana kisha unasema umefunga, hiyo sikushauri.
Habari za kunywa chai nyingi kisha mchana usile ila unakuja kula usiku hapo mimi naona kama hujafunga. Habari za kula kila  siku mchana na usiku kwa siku kadhaa na wewe unasema umefunga kwa sababu hukunywa chai, hiyo haiko sawa.
Kuna wengine akikosa pesa ya kula mchana anasema amefunga ili akiipata jioni anakula, hiyo haiko sawa.
Hatutakiwi kufunga kwa staili hiyo bali tunatakiwa kufunga Kibiblia, mfano unaweza kuangalia katika Biblia maombi ya Danieli ya siku 21, Maombi ya Waisraeli n.k
Nyenyekea kwa MUNGU, Mtumikie KRISTO na natembea katika kusudi la MUNGU.
1 Wakorintho 15:58 " Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA."

Ishi maisha matakatifu na hakikisha YESU KRISTO ni Mwokozi wako.
Ikatae dhambi, simama imara katika hali zote.
Kataa kiburi na majivuno, kataa kila mipango ya kipepo.
Hakikisha unawashinda mawakala wa shetani Mara zote.
Enenda kwa ujasiri.
Kataa dhambi na jitenge mbali na dhambi ili isikuondolee ujasiri wa kiroho.
Enenda kwa ROHO MTAKATIFU.


Maombi ya leo.

Leo omba kuiombea NAFSI yako katika mambo yafuatayo.
Kumbuka nafsi yako ndio ina akili yako, maamuzi yako na kila nia yako.
Kumbuka pia mtazamo wako wa nafsini mwako ndio hukuonyesha jinsi ulivyo(Mithali 23:7)


1. Mfukuze kwa maombi kila aliyeishikilia nafsi yako kipepo.
Awe ni jini , mwanadamu au dhambi hakikisha unafukuza kwa damu ya YESU KRISTO.
Mithali 6:26


2. Mfukuze kila wakala wa shetani aliyewashikilia nafsi kipepo wanaokuhusu
Mithali 6:32-33


3. Ikomboe nafsi yako na kila mashambulizi ya kipepo.
Zaburi 124:7


4. Itiishe nafsi yako ili ikubaliane na KRISTO YESU Mwokozi.
2 Kor 10:3-5


5. Itakase nafsi yako na iambie imuhimidi MUNGU.
Zaburi 103:2


6. Ikomboe nafsi yako ili ipitishe mafanikio yako.
3 Yohana 1:2


7. Omba maombi ya kuishibisha nafsi yako mambo ya MUNGU, ili mabaya yasipate nafasi nafsini mwako.
Zaburi 107:9


8. Iombee nafsi yako ili isikate tamaa kusubiri baraka za MUNGU.
Zaburi 35:13


  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments