MUNGU WA REHEMA ANAREHEMU SASA NA SI BAADA YA KUFA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU

Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kitu kibaya zaidi katika maisha yako sio kifo, kitu kibaya zaidi katika maisha yako ni kukosekana kwa jina lako katika kitabu cha uzima ambacho anacho tu Bwana YESU.
Kufa  kifo cha dhambi kinachofuata ni  jehanamu kwa mhusika lakini kufa ukiwa mteule wa KRISTO unayeishi maisha matakatifu kinachofuata ni uzima wa milele.
Ufunuo 14:13 "Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana(YESU) tangu sasa. Naam, asema ROHO, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao."

Lijue hilo na fanyia kazi ili jina lako liwe kwenye kitabu cha uzima.
Kumbuka kama jina lako litakosekana katika kitabu cha uzima cha Bwana YESU ni hatari ya milele kwako.
Ndugu, mpokee YESU KRISTO Leo, tubu na kuacha dhambi zako zote, okoka na acha mazoelea. Liishi Neno la MUNGU la injili ya KRISTO.
Ni muhimu sana ujumbe huu.

Kumbuka
Ufunuo 20:12 Biblia takatifu inasema " Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao."


Kuna watu wana njia nzuri za kuishi na kuna watu wana njia mbaya za kuishi.
Njia ni sehemu mtu anapita.
Maisha matakatifu ya wokovu ni njia ya kwenda uzima wa milele.
Maisha ya dhambi ni njia ya kwenda jehanamu.

Je wewe ndugu unaenda katika njia gani?
  Njia ya uzima wa milele ina faida kuu sana.

Njia ya jehanamu ina hasara ya milele.
Kuna faida iitwayo uzima wa milele na KRISTO YESU na kwa waovu na waliomkataa YESU kama Mwokozi kwao kuna  ziwa la moto linawasubiri.

Ndugu zangu hatuna cha kupoteza katika ulimwengu huu, Bali tunapaswa sana kuishi maisha matakatifu katika Wokovu wa KRISTO YESU Mfalme wa uzima wa milele.
Ng'ang'ania kwa YESU ili hukumu ya watenda dhambi isikuhusu.

Mhubiri 12:14 ''Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya. ''
Ndugu hakikisha Unataa dhambi, ikimbie dhambi, jitenge na dhambi na usitende dhambi tena.


Nimesema kwamba MUNGU ni wa rehema kwa sasa, labda ngoja tuangalie hilo sasa.
Rehema ni nini?
Rehema ni kuachilia, Ukitubu sana katika Bwana YESU hakika MUNGU anakusamehe na unaachiliwa kabisa wala hukumu isikuhusu tena.
Rehema ni msamaha, ukimpokea YESU sasa bna kutubu hakika unasamehewa dhambi zote, hata kama unaziona dhambi zako kuwab ni nyingi sana au kubwa sana hakika unasamehewa.
Rehema ni kuhurumia.
Matokeo ya Rehema ni kuachilia yote.
MUNGU ni mwenye Rehema na anasema ;
"Heri wenye rehema ; Maana hao watapata rehema -Mathayo 5:7"

Ndugu omba Rehema kwa MUNGU huku na wewe ukiwaachilia wote waliokukosea maana usipowasamehe na wewe hautasamehewa na MUNGU.
Kumbuka uhai wa mwili u katika damu, bila damu uhai haupo.
Na uhai(Uzima) wa mteule wa MUNGU u katika damu ya YESU KRISTO. Pasipo damu ya YESU hakuna uhai(Uzima wa milele)
Walawi 17:11 "Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi."
Uhai wa kanisa la MUNGU u katika damu ya YESU KRISTO, Pasipo damu ya YESU hakuna uzima wa milele.
Jinsi ya kutaka damu ya YESU ikupe uhai(Uzima wa milele) ni wewe kuokoka kwa kumpokea Bwana YESU kama Mwokozi wako, kutubu na kuanza kuliishi Neno la MUNGU.
Damu ya YESU ndio hututakasa hata tukawa na uhai(Uzima).
Damu ya YESU ndio inayotusafisha na kutufutia dhambi zote.
1 Yohana 1:9" Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote."


Ndugu yangu, Toba ni muhimu sana kwako, Toba ni tendo la kiimani la
kuungama dhambi na maovu yote
yaliyokwisha kufanyika kwa nia ya
kujenga upya mahusiano na MUNGU aliye
hai sawasawa na Neno lake.

Kutubu ndio  kugeuka kutoka dhambini na sasa unakuwa nuruni.

Ndugu unahitaji kutubu na unahitaji kuongozwa  sala ya toba na watumishi wa MUNGU, ili sasa jina lako liandikwe katika kitabu cha uzima, na ili jina lako liendelee kudumu katika kitabu cha  uzima inakupasa baada ya kumpokea YESU kama Mwokozi wako uanze kuishi kama Neno la MUNGU linavyokuagiza, kutubu ni muhimu sana kwako kama huna YESU KRISTO moyoni mwako.
Sala ya toba ni maombi maalumu ya kutubu kwa MUNGU kisha kuahidi kuanza kuishi kwa kumpendeza MUNGU.
Kwa kila anayempokea YESU ni lazima ajue kwamba sala ya toba ya kinywa ni lazima ihamie katika matendo, Hilo ndilo kusudi la MUNGU.
1 Timotheo 6:11-12 ''Bali wewe, mtu wa MUNGU, uyakimbie mambo hayo(Maovu); ukafuate haki, utauwa(Ucha MUNGU), imani, upendo, saburi, upole. Piga vita vile vizuri vya imani; SHIKA UZIMA ULE WA MILELE ULIOITIWA, UKAUNGAMA MAUNGAMO MAZURI MBELE YA MASHAHIDI WENGI.''
 
Neema ya MUNGU bado ipo  kwa ajili yako ili uokoke  na ili uwe huru mbali na uonevu wa shetani na mawakala zake.
Usiwe tena kama wale ambao hutekwa na shetani na usiwe  kama wale ambao humsingia hadi shetani wakati ni wao waliompigia magoti na kumkaribisha maishani mwao.
Kuna watu hujaribu kumsingizia shetani wakati ni wao ndio walimkaribisha huyo shetani maishani mwao ili awatumie atakavyo.
Umeenda kwa mganga na umeambulia majini, sasa vifungo vya kipepo vinakutesa.
Umeingia mikataba ya shetani, sasa unateseka.
Umeruhusu uasherati na uzinzi na sasa unateseka na vifungo.
Ndugu hakikisha unatubu kwa MUNGU aliye hai.
Omba damu ya YESU ikukomboe kutoka mikononi mwa maagano ya Giza.
Ishi sasa maisha matakatifu ya wokovu ili shetani asihusike tena na wewe.

Yakobo 4:7-10 ''Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza.   ''


Kwanini unatakiwa kutubu kwa YESU KRISTO mbele za MUNGU?

1. Tubu ili nyakati za burudishwa zije maishani mwako.

Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''
 Ulikuwa unateswa na majini au nguvu za giza zingine, ukitubu kwa usahihi na kuacha dhambi zako hakika milango waliokuwa wanaitumia  majini kukuonea itakuwa imefungwa hivyo hawatapata nafasi ya kukuonea tena.

2. Tubu maana ufalme wa MUNGU umekaribia.

Mathayo 3:2 ''Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. ''
Bwana YESU atakuja na kuchukua watakatifu hivyo ni muhimu sana kama unaitaka mbingu basi ishi maisha ya toba na hakikisha uko safi mbele za MUNGU.

3. Tubu ili damu ya YESU KRISTO ikusafishe.

1 Yohana 1:7 '' bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote. ''
Unatubu ili uwe safi, hivyo hakuna haja ya kuendelea kuwa mchafu bali hakikisha unakuwa safi mbeleb za MUNGU kwa toba yako ya kweli.

4. Tubu ili kuuruhusu ufalme wa MUNGU kufanya kazi kwenye maisha yako.

Marko 1:15 '' akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili. ''
Ufalme wa MUNGU ni mfumo wab  utendaji kazi wa MUNGU kwako.
Ukimpokea YESU na kutubu unakuwa umeuruhusu ufalme wa MUNGU kuhusika na wewe.
Ukiwa katika ufalme wa MUNGU dunianib utamruhusu ROHO MTAKATIFU kukuongoza na kukusaidia.
Neno la MUNGU litafanya kazi kwako, macho yako ya rohoni yatatiwa nuru na mambo mengi sana utapata ambayo yanahusiana na ufalme wa MUNGU.

5. Tubu ili MUNGU akurehemu.

Isaya  55:6-7 '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.''
Kurehemiwa maana yake kusamehewa jumlisha kuachiliwa.
Hivyo ukitubu unasamehewa dhambi kabisa na adhabu zilizokuwa zikufuate zinafutika.
 

6. Tubu ili uovu wako uvutwe kwa damu ya YESU .

1 Yohana 1:9 '' Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. ''
Tubu ili uovu wako uvutwe, damu ya YESU inaweza hata kuingia kwenye nafsi yako na kwenye jina lako na kukusafisha.
Damu ya YESU inaweza kufuta hadi maagano ya kishetani uliyoingia zamani, ndugu kutubu katika KRISTO YESU ni muhimu sana kwako.

7. Tubu ili uwe safi, mteule wa MUNGU unayesafiri kwenda uzima wa milele.
Isaya 35:8 '' Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo. ''
Tubu ili uwe safi, tubu ili mashtaka yote kukuhusu yafutike.

Fanyia kazi ujumbe huu kwa Mwokozi YESU KRISTO utaitwa heri, na hudhuria ibada kanisa la kiroho katika eneo lako, utapata fundisho la kukuimalisha ili usiingie upotevuni tena.

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments