TU WANA WA MUNGU KWA JINSI GANI?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe mteule wa MUNGU popote ulipo.
Karibu tujifunze Neno la uzima.
Kuna watu wengi sana hujiuliza kwanini unapookoka unafanyika mtoto wa MUNGU yaani unatoka kutoka kundi la watu tu wa MUNGU unaenda kundi la watoto wa MUNGU.
Kuna watu pia wanajiuliza kwanini MUNGU tunamwita BABA?
Je ni kweli kila aliye kanisani ni mtoto wa MUNGU?
Naomba niseme yafuatayo.
Bwana YESU alitupa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU sisi tuliookoka.
Yohana 1:12-13 " Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."

Chanzo cha mtu kuwa mtoto wa MUNGU ni Kumwamini YESU KRISTO Mwokozi, kisha kumpokea kama Bwana na Mwokozi, hapo unakuwa umefanyika mtoto wa MUNGU. 
Bila YESU hakuna anayeweza kufanyika mtoto wa MUNGU, Kumbuka YESU KRISTO ndiye mtoto wa Pekee wa MUNGU ambapo kupitia Huyo na sisi anatupa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU.
MUNGU alimleta YESU ili sisi tufanyike watoto wa MUNGU.
Yohana 3:16-18 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.''

Ni kwa jinsi gani YESU alitupa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU?

Mambo matano(5) yanayomthibitisha  mtu kwamba sasa ni Mtoto wa MUNGU ni haya.

1. Tumezaliwa kwa Neno la MUNGU.

1 Petro 1:23 '' Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la MUNGU lenye uzima, lidumulo hata milele.''
Ulilisikia Neno la MUNGU la injili ya KRISTO, Ukalikubali na kumpokea YESU kama Mwokozi wako, hapo umezaliwa kwa Neno la MUNGU.
Ulikubali Neno la KRISTO likubadilishe kutoka kuishi nje na kusudi la MUNGU na sasa unaishi katika kusudi la MUNGU la Wokovu, hapo hakika umezaliwa kwa Neno la MUNGU.
Kuzaliwa kwa Neno kunakufanya uwe na nguvu za MUNGU.
 Tumezaliwa Mara ya pili ili tuwe watu wa MUNGU walio tayari kwa uzima wa milele.
Neno kuzaliwa mara ya pili lina maana ya kuzaliwa kutoka juu mbinguni baada ya SISI kuanza kuufuata utaratibu wa mbinguni ambao ni Wokovu wa YESU KRISTO.
Wewe uliyemwamini YESU KRISTO, ukampokea kama Mwokozi na kutubu, kisha ukampokea ROHO MTAKATIFU kwa imani hakika wewe umezaliwa Mara ya pili. Umezaliwa Mara ya pili kwa maji na kwa ROHO, kumbuka maji huwakilisha toba.
Kuzaliwa Mara ya pili ni kupokea utakatifu ambao Adamu na Eva waliupoteza pale Edeni.

Ni lazima sasa tuiishi asili yetu ya kwanza ambayo ni utakatifu katika MUNGU aliye hai.

1 Petro 2:2-3 '' Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;  ikiwa mmeonja ya kwamba BWANA ni mwenye fadhili. ''


2. Tumemwamini YESU KRISTO kama Bwana na Mwokozi wetu.

 1 Yohana 5:1 ''Kila mtu aaminiye kwamba YESU ni KRISTO amezaliwa na MUNGU. Na kila mtu ampendaye mwenye kuzaa, ampenda hata yeye aliyezaliwa na yeye.''
Kitu kimoja ambacho watu wengi hawajui ni kwamba kipimo namba moja cha kumpenda MUNGU ni kumpenda YESU KRISTO, ndivyo Biblia inasema hapo juu.
Na anayempenda YESU ni mtu yule anayemwamini kama Mwokozi kisha kumpokea kama Mkombozi na kisha kuanza kuliishi Neno lake.
Wanaosema wanamwamini MUNGU huku huku wanakataa kuokolewa na YESU KRISTO hao hakika hawampendi MUNGU.
Wanasema wanamwamini YESU KRISTO lakini wasimpokee kama Mwokozi wao, hao hakika hawamwamini YESU.
Kumwamini YESU ni jambo la muhimu sana kwa kila mtu, kumwamini YESU kunatoa nafasi namba moja ya mtu kufanyika mtoto wa MUNGU.
Kumwamini YESU kunaunganisha mambo mawili.
A. Kumkubali kama Mwokozi wako Binafsi.
B. Kumpokea kama Mwokozi wako milele.
Ukiona mtu hahusiki na hayo huyo hata kama kwa kinywa anasema anamwamini YESU lakini ukweli ni kwamba hamwamini YESU huyo.
Ndugu utafanyika mtoto wa MUNGU kama tub utamwamini YESU KRISTO na kumpokea kama Mwokozi wako.

3.Tumezaliwa kwa ROHO MTAKATIFU.

Kuzaliwa Mara ya pili ni mtu kupokea upya utakatifu kutoka kwa MUNGU, aliye mtakatifu.
Kuzaliwa katika ROHO MTAKATIFU ina maana ya ROHO MTAKATIFU na nguvu zake kuingia ndani yako, ni tukio la muhimu sana na la thamani sana.
Yohana 3:3,5 "YESU akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa MUNGU. YESU akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa ROHO, hawezi kuuingia ufalme wa MUNGU. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa ROHO ni roho. "
Ulizaliwa Mara ya kwanza na wazazi wako, MUNGU akaona kuzaliwa Mara ya kwanza tu haitoshi hivyo akaleta Wokovu ili wewe uzaliwe Mara ya pili.
Kupitia kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako unazaliwa Mara ya pili.
Unazaliwa Mara ya pili kwa toba na kwa ROHO MTAKATIFU ili uwe wa MUNGU.

Kuzaliwa kwa ROHO MTAKATIFU kunakufanya uwe huru.
ROHO MTAKATIFU ndiye anayetakiwa kuwaongoza waenda mbinguni wote.
Ukimuona mtu anamkataa ROHO MTAKATIFU ujue huyo anakataa kuwa mtoto wa MUNGU.
Kumbuka MUNGU Baba aliuleta Wokovu, YESU KRISTO akaukamilisha Wokovu na kazi ya ROHO MTAKATIFU ni kuwaongoza walio katika Wokovu ili wampendeze MUNGU na baada ya kuondoka duniani iwe ni uzima wa milele.

4. Tumeyaacha ya kale ambayo ni dhambi na sasa tunayaishi mapya yaitwayo maisha matakatifu.

 2 Kor 5:17 '' Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.''
Ni jambo la ajabu sana lililofanya na Neno la MUNGU kwetu.
Tulikuwa wazinzi zamani, tulikuwa wezi, tulikuwa makahaba, tulikuwa wachawi, tulikuwa waongo n.k Lakini kwa Neema ya ajabu sana(Amazing grace) kupitia maisha ya Wokovu katika KRISTO tumefanyika watoto wa MUNGU. 
Ya kale yote yamepita na sasa tunayaishi mapya. 
Tumesamehewa dhambi na sasa tunaishi maisha matakatifu katika YESU KRISTO Mwokozi wetu.
Tumefanyika kuwa wana wa MUNGU na tumehesabiwa haki baada ya kumpokea YESU na kutubu. 
Tulikuwa waenda  jehanamu kwa sababu ya dhambi zetu na kukosa msamaha wa MUNGU lakini sasa ni waenda mbinguni kwa sababu YESU KRISTO ndio Mwokozi wetu, tumeokolewa kwa Neema na sasa tu wana wa MUNGU kwa sababu tunaishi maisha matakatifu katika YESU KRISTO shujaa wa msalaba ambaye ndiye Mwokozi wetu.

5. Tumeumbwa katika KRISTO YESU ili tutende mema ambayo tangu Mwanzo wa uumbaji MUNGU aliyatengeneza mema hayo.

 Waefeso 2:8-10 '' Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika KRISTO YESU, tutende matendo mema, ambayo tokea awali MUNGU aliyatengeneza ili tuenende nayo.   ''
Tumefanyika watoto wa MUNGU kwa sababu tumeumbwa upya ili tuiishi asili ya uumbaji ya MUNGU.
Neno la MUNGU ndilo hutuumba na kuturudisha katika asili yetu ya uumbaji wa MUNGU ambayo Adamu na Eva waliipoteza.
Damu ya YESU umetutakasa na sasa hakuna hati ya mashtaka kutuhusu.
Tumefanyika watakatifu, wakamilifu na waaminifu.
1 Petro 1:15-16 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''
Mimi Mabula ninaandika somo hili nikiwa na furaha na kicheko katika ROHO MTAKATIFU labda kuna watu leo wanaenda kuongezeka katika kundi la watoto wa MUNGU waliosafishwa kwa damu ya YESU. Nina furaha sana hakika na naamini ndugu unayesoma ujumbe huu utaenda kumpokea YESU KRISTO, Kujazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU na sasa utaanza kuishi maisha matakatifu ambayo MUNGU aliyaumba tangu tangu sikun ile anamuumba mwanadamu wa kwanza.
Adamu alipoteza utakatifu lakini YESU akaja kuturudishia utakatifu ambao kwa huo tunafanyika wana wa MUNGU.
Haijalishi wewe ni mwanaume au wewe ni mwanamke, ukimpokea YESU kama Mwokozi, ukatubu na kuanza kuishi maisha matakatifu ya Wokovu hakika wewe utakuwa mtoto wa MUNGU mwenye haki zote kwa BABA yako wa mbinguni.
2 Kor 6:17-18 '' Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,''

6. Tunao uzima wa milele.

1 Yohana 2:24-25 '' Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana(YESU KRISTO), na ndani ya Baba(MUNGU). Na hii ndiyo ahadi aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele.''
Tunafanyika watoto wa MUNGU ambayo sasa tunao uzima wa milele.
Tuko ndani ya MUNGU na ndani ya YESU KRISTO, tu wa MUNGU na ahadi ya MUNGU kwetu  tulio katika Wokovu wake ni uzima wa milele.
 Warumi 6:23 '' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA wetu.''
Watoto wa MUNGU halisi tunangoja uzima wa milele. 
Tumeokoka na tunaishi maisha matakatifu katika Mwokozi wetu YESU KRISTO.
YESU alipokuja kutupa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU aliondoka na kwenda kutuandalia makao ya uzima wa milele, ni shangwe kwa wateule wa MUNGU wanaoishi maisha matakatifu katika KRISTO.
YESU alituweka wazi sana juu ya hilo katika maandiko haya.
Yohana 14:1-3 ''Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi. Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali.  Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo.'
 

7. Tunamsikiliza ROHO MTAKATIFU na kumtii.

Warumi 8;14  '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.'' 
Sifa kuu sana ya watoto wa MUNGU ni kumsikiliza ROHO MTAKATIFU na kumtii.
Wanaoongozwa na ROHO MTAKATIFU hao ndio wana wa MUNGU, kumbe kuongozwa na ROHO MTAKATIFU kunakuthibitisha kwamba wewe u mtoto wab  MUNGU.
Tu wana wa MUNGU kwa sababu tunaongozwa na ROHO MTAKATIFU.
Kumbuka pia kwamba ROHO MTAKATIFU hapatikani nje na KRISTO YESU, Hivyo kumpokea YESU kama Mwokozi hutoa nafasi ya ROHO wa MUNGU kuingia kwetu na kuanza kutusaidia katika kila jambo ili tumpendeze MUNGU na ili tupate uzima wa milele.
Katika Yohana 14: 16-17 Bwana YESU anasema '' Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.'' Na YESU alipoondoka tu basi ROHO MTAKATIFU alikuja na huyo atakuwa na sisi milele kama ahadi ya Bwana YESU inavyosema katika andiko hapo juu.
Hivyo watoto wa MUNGU ni lazima waenenda katika ROHO MTAKATIFU.
Wagalatia 5:25 '' Tukiishi kwa ROHO, na tuenende kwa ROHO.''
Tu wana wa MUNGU kwa sababu ROHO MTAKATIFU Ndiye kiongozi wetu.

Naamini umeelewa ndugu maana ya sisib kuwa watoto wa MUNGU, Ngoja niseme yafuatayo pia.
Tunamhitaji YESU katika maisha yetu ya kila siku.
  =Tunamhitaji YESU KRISTO kwa ajili ya uzima wa milele.
  =Tunamhitaji YESU KRISTO kwa ajili ya ukombozi wetu wa mwili, nafsi na roho.
  =Tunamhitaji YESU KRISTO ili kutoa nafasi kwa ROHO MTAKATIFU kutuhudumia, kutusaidia na kutuongoza.
  =Tunamhitaji YESU KRISTO ili tupate kumshinda shetani na mawakala zake na ili shetani na mawakala zake watuogope.
  =Tunamhitaji YESU KRISTO ili kurudisha uhusiano wetu na MUNGU Muumbaji wetu, na sasa tunakuwa watoto wa MUNGU kupitia yeye YESU KRISTO Mwokozi.
  =Tunamhitaji YESU KRISTO kwa faida yetu ya sasa hadi milele.
Ndugu mhitaji sana YESU KRISTO Mwokozi kwenye maisha yako.
Amua kumpokea kama Mwokozi kama hujampokea.
Ongeza juhudi katika yeye wewe uliyeokolewa na yeye.


Kumbuka pia jambo hili kwamba sheria wala haiwahusu wenye haki yaani waliompokea YESU kama Mwokozi wao na wanaishi maisha matakatifu
1 Timotheo 1:9-10 " akilifahamu neno hili, ya kuwa sheria haimhusu mtu wa haki, bali waasi, na wasio wataratibu, na makafiri, na wenye dhambi, na wanajisi, na wasiomcha MUNGU, na wapigao baba zao, na wapigao mama zao, na wauaji, na wazinifu, na wafiraji, na waibao watu, na waongo, nao waapao kwa uongo; na likiwapo neno lo lote linginelo lisilopatana na mafundisho yenye uzima;"
Ukitaka uwe mwenye haki hata sheria isikuhusu mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako, tubu na anza kuliishi Neno la MUNGU, huku ukienenda katika ROHO MTAKATIFU na iishi haki ya MUNGU ambayo injili ya KRISTO.



Unataka Bwana YESU akufungulie mlango wa ushindi katika maisha yako?
YESU atakufungulia mlango wa ushindi kama tu unahusika na haya.
Ufunuo 3:8 " Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu, wala hukulikana jina langu."

  =YESU atakufungulia mlango wa ushindi kama unamwamini.
 =Zingatia mambo ya MUNGU ili uwe na nguvu za kiroho.
Kwa maombi na utakatifu.


 =YESU atakufungulia mlango wa ushindi Kama unalitunza jina lake.
Jinsi ya kulitunza jina la YESU KRISTO ni wewe kuokoka na kisha kuishi maisha matakatifu katika yeye.


  =YESU atakufungulia mlango wa ushindi kama humkani.
Hivyo hakikisha katika maisha yako yote humkani YESU Mwokozi wako.

  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments