UWEZO WA KIONGOZI MZURI KIROHO HUONEKANAJE?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU
 
Bwana YESU atukuzwe ndugu  yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.

Uongozi ni nini?

Uongozi ni uwezo wa  kushawishi watu au kundi ili kutimiza lengo lililokusudiwa.

Kanisa linahitaji viongozi wazuri na wanaomcha MUNGU.

Kanisani viongozi  wote wanatakiwa kuwa vielelezo katika mambo mema.

Katika  kikundi chochote Kanisani mfano kwaya, uinjilisti,  idara ya vijana  au wamama au watoto n.k kunahitajika viongozi wazuri wa kiroho.

Jambo lingine la kujua ni kwamba sio kila mtumishi mzuri Kanisani ni kiongozi mzuri. Sio watumishi wote wameitwa kuongoza mambo ya kiofisi Kanisani.

Unaweza kuwa mhubiri mzuri sana lakini ukikabidhiwa idara ya wamama au vijana itakushinda kwa sababu kuhubiri na uongozi ni vitu viwili tofauti.
Katika kuchagua viongozi tunahitaji MUNGU atusaidie na sio kwenda kwa akili zetu.

1 Samweli 16:7'' Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali BWANA huutazama moyo. ''
 

Watu wengi pia hawakai katika nafasi zao zinazoambatana na wito wao ndio maana wanapowekwa katika nafasi zingine hawafanyi vizuri kwa sababu haziambatani na wito wao.

Leo viongozi wengi makanisani wanaweza kuwa ni wale walioonekana kwa viongozi wa juu ya sio wale waliochaguliwa na MUNGU kukaa katika nafasi husika.

Mchungaji akimkubali mtu fulani kanisani basi anampa uongozi, hiyo ni sawa lakini kama hamna kusudi la MUNGU ujue kiongozi huyo anaweza kuharibu badala ya kujenga.

Ngoja nikupe mfano mimi kama Peter natambua kabisa kuna nafasi za kiuongozi kanisani siziwezi kwa sababu nikipewa zitanizuilia kuandaa masomo na kufanya huduma yangu kwa ufanisi. Mimi kama mimi, ROHO wa MUNGU alishaniambia kwamba ameniita kufundisha Neno la MUNGU, sijawahi kusikia sauti nyingine nje na hiyo ya kiutumishi, sasa inawezekana kabisa kwa viongozi wangu wa Kanisa naweza kuonekana kama mtumishi ambaye nitafaa sana hivyo unaweza ukapewa hata nafasi mbili au tatu za kiuongozi kanisani lakini kwa sababu wewe una wito wako basi uongozi unaweza kuvuruga wito wako.

Sasa katika Kanisa la MUNGU ni muhimu sana kutafuta mtu ambaye ni kusudi la MUNGU na sio kutafuta tu mtumishi mzuri, anaweza akawa mtumishi mzuri lakini asiwe kiongozi mzuri Kanisani.

Inawezekana pia kanisani ni pahali ambapo hakuna kuwajibishana ndio maana kiongozi anaweza kuchaguliwa na Mchungaji au Balaza la wazee na akajifanyia vile ambayo yeye anataka, kuwajibishana kunahitajika sana katika Kanisa la MUNGU.

Wakati mwingine kama kikundi ndani ya Kanisa mnaweza mkajikuta mnazidiwa ujanja na shetani wakati wa utekelezaji hivyo aina ya viongozi wazuri hujua nini cha kufanya ili kuwa washindi siku zote.

Wakati mwingine kama huna mzigo rohoni na kazi yako utakuwa mtu wa mazoelea tu kwa sababu umewekwa katika nafasi ambayo huna mzigo nayo. Hivyo kunahitajika viongozi wenye mzigo na kazi ya MUNGU husika waliyopewa.

Baada ya hayo sana tuangalie uwezo wa kiongozi mzuri jinsi unavyoonekana.

    1. Huonekana katika maono yake.

Kama ni kiongozi hakikisha una maono mazuri na maono hayo hakikisha yako sawa na Neno la MUNGU.
Hakikisha una macho ya kuona maono mazuri ambayo utayafanyia kazi.
 Yeremia 1:11-12 '' Tena neno la BWANA likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa mlozi. Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.''

Lazima uwe na maono na utembee katika maono hayo ili kuikuza kazi ya MUNGU.



     2. Kujidhibiti yeye binafsi na kudhibiti tabia binafsi. 

1 Petro 4:2'' Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya MUNGU, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani. ''.
 Inawezekana wewe una tabia ya ukali sana, kwenye uongozi wako jidhibiti tabia hiyo maana inaweza kukuondoa katika kundi la viongozi wazuri kiroho katika Kanisa la MUNGU.

Ziko tabia binafsi nyingi, wako viongozi wa tabia za kususa kila akikosewa na wenzake tu kidogo, wako viongozi ambao hawatoi nafasi ya wengine katika kundi kuchangia maono, wako viongozi wapenda sifa n.k. Ndugu kama umepewa kuwa kiongozi wa kiroho basi dhibiti tabia zako binafsi maana zinaweza kulivuruga kundi na wewe usiwe kiongozi mzuri. Tito 1:8



   3. Uwezo mzuri huonekana katika maamuzi yake mazuri.

  Warumi 14:13'' Basi tusizidi kuhukumiana, bali afadhali toeni hukumu hii, mtu asitie kitu cha kumkwaza ndugu au cha kumwangusha. ''

Kama kiongozi ni lazima kuna mahali atatakiwa kutoa maamuzi, sasa  maamuzi sahihi yanaweza kumfanya kiongozi awe mzuri au sio kiongozi mzuri. Maamuzi ya kuwaogopa wanadamu, yanamfanya kiongozi  asiwe mzuri.

Maamuzi ya kupendelea baadhi ya watu au marafiki zake, yanamfanya kiongozi asiwe kiongozi mzuri

Bwana YESU alisema ndio yetu na iwe ndio maana yake tusiwe watu wasioeleweka, wasio na msimamo, wanaosema mambo ambayo hawatendi. Kiongozi Kanisani lazima awe anaongozwa na ROHO MTAKATIFU ili kutoa maamuzi sahihi hata kama maamuzi hayo yatawakwaza marafiki zake, lakini kama ni maamuzi sahihi basi  basi ni heri kuyafanya. Isiwe kiongozi aamue mfano kwamba ‘’Siku ya jumamosi tutakutana hapa Kanisani kwenda kushuhudia’’ Kisha baadae rafiki yake mmoja au mke wake au mume wake amwambie kwamba ‘’Wiki hii tusishuhudie bali tukamtembelee Mchungaji’’ Sasa kama kiongozi umeshawaambia watu kuhusu kushuhudia na wote wakaenda wakijua kuna ushuhudiaji na wengine hata wakombea jambo hilo kisha inafika ijumaa unatangaza tena kwamba ushuhudiaji haupo jumamosi bila sababu ya msingi, unakuwa huna maamuzi sahihi. Hata kama umeshauriwa jambo jema basi hakikisha unafuata ratiba njema ya kwanza mliyokubaliana. Angalizo ni hili, Kwa sababu kila Mchungaji kanisani ndio msimamizi wa idara zote basi mipango yote kabla hujaipeleka kwa kikundi chako au idara yako hakikisha unamshirikisha Mchungaji ili akibariki Mchungaji basi asiwepo wa kuzuia maamuzi hayo mema ya kumtumikia MUNGU na kumpa utukufu.

Kama kiongozi wa aina yeyote Kanisani inakupasa kuwa makini sana katika maamuzi. unaweza ukawafanya unaowaongoza wakakujua kwamba huna maamuzi sahihi, hivyo hata ukiwaambia jambo hawatazingatia maana wanajua utabadilika tu.

Usiseme kitu kama huna uhakika nacho ili maamuzi yako yawe sahihi siku zote yasiyomuonea mtu  wala kumpendelea mtu yeyote.

  4. Kiongozi mzuri ni yule anayeweza kuwasikiliza wengine na kuwaona wa thamani. 

Wafilipi 2:3-4 ''Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.''

Hii ni changamoto kwa baadhi ya viongozi Makanisani. Kuna viongozi neno lao ndio la mwisho kwenye kikao. Askofu au Mchungaji au kiongozi wa idara yeyote akisema jambo ni muhimu sana kusikiliza mawazo ya watu wengine. Kama ni kwenye kikao hakikisha unasikiliza maoni ya watu wote na sio wewe kuamua mwanzo tu wa kikao, hivyo hata kama kuna maoni mazuri kuliko yako na yanayoweza kulisaidia kundi basi  hutatoa nafasi ya watu wengine kukupinga.  Mtu akikuita pembeni baada ya ibada mfano akikushauri jambo ili kuboresha usimpinge. Kuna viongozi wengine akipingwa kidogo ananuna, hiyo sio sifa nzuri ya  kiongozi.

Ni muhimu kutambua kwamba ukiwa kiongozi kanisani au kwenye kikundi chako au idara yako haina maana ya kwamba wewe ndio una akili kuliko wote unaowaongoza, ndugu inawezekana nusu nzima ya unaowaongoza wana akili kuliko wewe, wana maono na mipango mizuri kuliko wewe hivyo wasikilize ushauri wao na ushauri mzuri fanyia kazi kwa faida ya  kanisa la MUNGU.

Usiwe kiongozi ambaye huwapi nafasi watu kuwasikiliza, kumbuka basi kwamba tu viungo katika mwili mmoja wa KRISTO.

  5. Kiongozi mzuri ana juhudi kwa MUNGU na katika kazi yake aliyopewa kuongoza. 

1 Petro 3:13 ''Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?''

Wapo viongozi wao  huonekana tu katika vikao vya kiuongozi lakini katika kazi nyingine na utumishi mwingine kanisani huwezi kuwaona.

Kiongozi mzuri lazima ahusike na ibada siku zote, ahusike na maombi na mikesha ya maombi.

Usiwe kiongozi ambaye huna juhudi kwa MUNGU. Kumbuka umepewa uongozi ni katika kazi ya MUNGU, katika Kanisa la KRISTO hivyo maisha yako  ni kumwabudu MUNGU Baba katika Roho na kweli na kumtumikia Bwana YESU.

Kiongozi  lazima uwe na juhudi kubwa katika kazi ya MUNGU hata ambayo haikuhusu.

Usiwe kiongozi wa wamama au vijana au shemasi au mzee wa kanisa na huwa unatoa michango yako katika idara yako tu lakini kwenye Kanisa hutoi hata mia maana hutaki Kanisa lifanikiwe ila wewe idara yako tu ndio ifanikiwe.

Usiwe kiongozi mwenye wivu wala husuda. Niliwahi kushuhudia Kanisa fulani vijana wakifanya sherehe na katika sherehe hiyo walimtegemeza vizuri Mchungaji wao na kufanya mambo mengi sana mazuri, lakini katika ibada hiyo na matukio hayo waliokuwa na furaha ni vijana tu lakini wamama na wababa hawakuwa na furaha kabisa, baadae baada ya ibada mama mmoja nikamsikia akisema ‘’Vijana wamefanya vizuri katika sherehe yao kuliko sisi’’ Niliwaza sana na kujua kwamba hapo kuna tatizo.

Mko Kanisa moja lakini imefika wakati hamtaki kikundi kingine kifanikiwe kuwazidi, YESU hakumuita mtu yeyote katika hayo.

Kwanza Kanisani hatushindani. Ukiwa kiongozi wa namna hiyo utashangaa  kundi lako halifanikiwi kamwe kwa sababu malengo yako ni kushindana na idara zingine ili muwazidi na kupata heshima.

Ndugu, fanya kwa sehemu yako na fanya kazi ya MUNGU kwa juhudi lakini epuka mashindano.



  6. Kiongozi mzuri hafanyii kazi jambo bila kulipima kwanza

Mithali 18:17  '' Ajiteteaye kwanza huonekana kuwa ana haki; Lakini jirani yake huja na kumchunguza.''

Tuko katika nyakati ambazo watu hugeukageuka hivyo ukiwa kiongozi unayetaka kumpendeza MUNGU basi usiwe wa kufanyia kazi kila unachoambiwa, hata kama hakistahili.

Ni kweli kabisa unatakiwa kila mara utoe nafasi ya kuwasikiliza wengine lakini  hakikisha unachuja pumba na mchele safi.

Sio watu wamekosana na kisha mmoja anakuja kwako mzee wa Kanisa na kukuambia kwa uongo na hila kwamba  ‘’Mpendwa  fulani jana alikuwa disko’’ Wewe mzee wa Kanisa au Mchungaji kesho unasimama madhabahuni na kutangaza mtu huyo kwamba jana yake alionekana disko hivyo aache mara moja tabia hiyo, Jambo hilo kama ni la uongo basi hakika utakuwa umebomoa sana na sio kujenga.

Kiongozi mzuri lazima asikilize watu lakini pale wanapomshawishi anaowasikiliza ili aamue maamuzi fulani basi awe makini maana kuna ushawishi mwingine ni tamaa za watu au ushawishi wa kipepo kabisa ili kuvuruga kundi.

Wako watu hadi wamehama makanisani kwa kusingiziwa na kunenewa uongo. Hata ndoto na maono wanayokuambia watu kuhusu watu wengine usiamue tu dakika hiyo hiyo hata kama hujui kama ni kweli au uongo.

Kiongozi lazima uwe kama kiongozi sahihi kwa kusikiliza watu na kisha fanyia kazi hata ujilidhishe kwanza na toa maamuzi kulingana na Biblia na sio mtazamo wako. Ndugu mmoja alikwenda kwenye mkutano wa injili wa mtumishi fulani, kwa sababu madhehebu yale hawaelewani basi aliporudi kanisani kwake Mchungaji alitangaza akisema ‘’Huyu kuanzia sasa muoneni kama mtu wa mataifa maana amemwasi MUNGU na Kanisa’’

Kuna Madhehebu mengine muumini akihama dhehebu tu wanaanza kumwita mtu wa mataifa, muasi na ameasi imani.

Ndugu zangu, kumwasi MUNGU  ni kuacha Wokovu wa YESU KRISTO  ulio wa thamani sana na sio kuhama dhehebu. Kama mtu atahamia dhehebu ambalo YESU  KRISTO sio Mwokozi basi huyo amejipoteza mwenyewe, lakini kama mtu husika ameokoka na amehama dhehebu kwa sababu zake  za msingi  na kuhamia dhehebu lingine la Wokovu wa KRISTO  vilevile wanaoihubiri kweli ya MUNGU huyo hajaasi. Sasa viongozi wengi hufanyia kazi mambo yasiyo sahihi na hayo kuwakosesha wengine.



  7. Kiongozi mzuri wa kiroho hausiki na dhambi na anakemea dhambi.

Kitu cha kwanza kabisa ambacho MUNGU anahitaji kwa Kanisa lake yaani kwa waliompokea YESU kama Mwokozi wao ni utakatifu.

1 Petro 1:15-16 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.''

Utakatifu ndio jambo la muhimu zaidi baada ya kuokoka.

Kwa kiongozi ni lazima uwe kielelezo katika mema.

Uongozi wako  unaweza kuuharibu kama unafanya dhambi za siri.

Kuna hadi viongozi wa kiroho wana watoto nje ya ndoa, kiongozi kama huyo anaweza akafika wakati akasema ‘’Msifuate matendo yangu bali fuateni maneno yangu’’ Huyo hajitambui kwa sababu ya dhambi, kiongozi kama huyo hafai kuongoza kundi la MUNGU. Ni heri sana mkachagua kiongozi asiyejua kusoma wala kuandika lakini ni Mcha MUNGU kuliko kuchagua kiongozi msomi lakini mdhambi.

Kanisa linaweza likatukanwa na watu wa nje kwa sababu yako kiongozi mtenda dhambi.

Kufanya dhambi kwako kunaweza kuwazuiliwa watu hata kuokoka.

Ukitaka uwe kiongozi mzuri kiroho hakikisha sana unaishi maisha matakatifu ya Wokovu.

Nyongeza  ni hizi;

Ø Huwezi kuwa kiongozi mzuri kama huna maono mazuri.

Ø Huwezi kufanikiwa kiuongozi kama hakuna ushirikiano  baina yako na unaowaongoza.

Ø Kiongozi bila ROHO MTAKATIFU na Bila YESU KRISTO hawezi kuwa kiongozi anayempendeza MUNGU.

Ø Kiongozi anayefanya dhambi hawezi kuwa kiongozi mzuri wa kiroho.

Ø Kiongozi mwenye tamaa na vitisho hawezi kuwa kiongozi mzuri wa kiroho.

Ø Kiongozi ambaye Neno la MUNGU sio kiongozi wake, huyo hawezi kamwe kuiwa kiongozi mzuri



Kwanini uongozi wa kiroho katika baadhi ya maeneo  Makanisani haufanikiwi?

1.  Hofu ya MUNGU inapoondoka kwa kiongozi husika na kwa anaowaongoza.

Hofu  ya MUNGU ni nyezo kuu ya kufanikiwa kwa Kanisa, idara au kundi katika kazzi ya MUNGU.

2. Kufanyia kazi jambo jipya , kabla yya jambo la kwanza kumalizika.

Mnaweza mkapanga kujenga Kanisa kwa mwaka huu, kabla ya mwezi wa 4 mnapanga tena mwaka huu mtamnunulia Mchungaji Gari, kabla ya mwezi wa 8 mnapanga tena kwamba mwaka huu mtasafiri kihuduma n.k kwa jinsi hiyo mnaweza mkajikuta mwaka mzima umeisha na hamjafanya hata moja katika mipango yenu kwa sababu ya kupandikiza mambo.

1 Kor 15:58 ''Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya BWANA sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika BWANA. ''
  Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
0786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments