EE MWANADAMU, MUNGU ANATAKA NINI KWAKO?

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

  Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Siku moja jumapili nilipewa ujumbe huu kwa ufunuo.
ROHO MTAKATIFU alisisitiza sana niwaeleze watu wote. Niliuandika ujumbe huu kwenye daftari yangu ya masomo na kumwomba MUNGU ili nitimize kusudi lake.
Najua kabisa wewe unayesoma somo hili sasa na yule ambaye  atasoma baadae au siku nyingine somo hili ndio hao waliokusudiwa. Najua kabisa yule ambaye wewe utamshirikisha ujumbe huu na yeye amekusudiwa, haijalishi ni miaka mingapi ijayo lakini kama kuna mtu atapata nafasi ya kujifunza somo hili hakika na huyo alikusudiwa.
Ujumbe ulisema hivi ''Ee Mwanadamu, MUNGU anataka nini kwako?''
Mika  6:8-14 '' Ee mwanadamu, yeye amekuonyesha yaliyo mema; na BWANA anataka nini kwako, ila kutenda haki, na kupenda rehema, na kwenda kwa unyenyekevu na MUNGU wako! Sauti ya BWANA inaulilia mji, na mtu mwenye akili ataliona jina lako; isikieni hiyo fimbo na yeye aliyeiagiza.
 Je! Hata sasa hazina za uovu zingalimo nyumbani mwa wabaya, na kipimo kilichopunguka, ambacho ni chukizo? Je! Naweza kuwa safi nami nina mizani ya udhalimu, na mfuko wa mawe ya kupimia ya udanganyifu? Kwa maana matajiri wake wamejaa jeuri, na wenyeji wake wamesema uongo, na ulimi wao una udanganyifu kichwani mwao. Basi, kwa ajili ya hayo, mimi nami nimekupiga kwa pigo liumizalo sana; nimekufanya kuwa ukiwa, kwa sababu ya dhambi zako. Utakula, lakini hutashiba; na fedheha yako itakuwa kati yako; nawe utahama, lakini hutachukua kitu salama; na hicho utakachochukua nitakitoa kwa upanga.'
'

 ''Ee Mwanadamu, MUNGU anataka nini kwako?''
 Ee Mwanadamu, MUNGU anataka haya kwako.

1. MUNGU anataka uishi maisha matakatifu ya haki.

Maisha matakatifu ya haki ni maisha wanayoishi tu waliompokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao na wanaliishi Neno la MUNGU.
 Warumi 6:23 '' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU Bwana wetu.''
Maisha ya haki ni maisha matakatifu ya Wokovu wa YESU KRISTO.
Maisha matakatifu ni kuliishi Neno la MUNGU linavyotaka.
Maisha ya haki ni maisha ya kumsikiliza na kumtii ROHO MTAKATIFU.
 Warumi 8: 8-9 ''Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza MUNGU. Lakini ikiwa ROHO  wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO wa KRISTO, huyo si wake. ''

 2. MUNGU anataka upende rehema.

Rehema ni maisha ya toba.
"Heri wenye rehema ; Maana hao watapata rehema -Mathayo 5:7"
Maisha ya toba ni maisha ya kutubu na kuacha dhambi zote ili toba yako iwe toba sahihi.
 Mathayo 3:2 ''Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia. ''
Rehema imebeba pia mambo mawili muhimu sana yaani kusamehe na kuachilia. 

''Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa.-Luka 6:37
 Kwahiyo Neno Rehema maana yake ni kusamehe na kuachilia.
Hivyo wewe Mwanadamu unatakiwa pia kuwa mtu wa kuwasamehe waliokukosea na kuwachilia makosa yao.
Tena inakupasa sana uwe mtu wa kutafuta msamaha kwa MUNGU na kwa watu uliowakosea.
 ''Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata kibali na akili nzuri, Mbele za MUNGU na mbele ya mwanadamu.-Mithali 3:3-4 ''

 Kuutafuta msamaha ni kutubu, kuomba msamaha kisha unaacha dhambi au makosa yaliyopelekea kukosea mwanzo.
Tafuta kuachiliwa, omba MUNGU uachiliwe kwenye makosa yako na usikubali kuyarudia tena.
Kumbuka   ''Kwa maana MUNGU ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.-Mhubiri 12:14 ''
Kumbuka usipotubu kwa MUNGU hata kama unamtumikia lakini
''Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.-Luka 13:3''

 3. MUNGU anataka uende kwa unyenyekevu katika yeye.

Watu wengi sana sio wanyenyekevu kwa MUNGU.
 Kuonyesha kwamba watu hawa sio wanyenyekevu kwa MUNGU unaweza kuwajua katika mambo haya.
a. Kuacha kumtolea MUNGU fungu la kumi.
b. Kuacha ibada.
c. Kuacha kujifunza Neno la MUNGU.
d. Kuacha maombi
e. Kuacha kumtegemea MUNGU n.k
Biblia inasema '' Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza.-Yakobo 4:8-10  ''
Kinyume cha unyenyekevu ni kujikuta na kiburi.
Hivyo watu wengi wamejaa kujikuza na kiburu na sio unyenyekevu.
Hivyo unaweza ukakosa neema ya MUNGU kwa sababu tu ya kukosa unyenyekevu kwa MUNGU.
1 Petro 5:5-7 ''Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu MUNGU huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.  Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa MUNGU ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.  ''
Neema ya MUNGU ni jambo la muhimu sana.
Neema ni kustahilishwa pasipo kustahili.
Ndugu yangu, Bwana YESU anataka mambo hayo matatu uyazingatie sana.
ROHO MTAKATIFU anataka sana uzingatie.
MUNGU Baba anataka sana uzingatie na kufanyia kazi.
Sio kwamba MUNGU anataka hayo matatu tu bali yako mengi sana na hayo nakuomba jifunze Biblia utayajua, ila leo amenipa hayo matatu kwa msisitizo mkubwa sana kwamba uyashike sana.\
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments