HUKUJA NA KITU DUNIANI NA HUTAONDOKA NA KITU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

 Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Nakuomba usome somo hili hadi mwisho.
Namshukuru MUNGU Baba maana imempendeza ili kwa majira haya nikuletee ujumbe huu alionipa kupitia ROHO MTAKATIFU.
Biblia inasema ''Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; .......... -Mhubiri 3:1-2''

 Tena Biblia takatifu inasema '' kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa.  Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua.-Mhubiri 9:5-6 ''

Kumbe kuna kuzaliwa na  kuna kufa. 
Kama ambavyo kila mmoja duniani alizaliwa na hakika ni kwamba siku moja atakufa.
 1 Timotheo 6:7  '' Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ''
Wanadamu wengi wanaishi kama kwamba wataishi duniani milele. Wanadamu wengi hata wakiambiwa kutubu na kuokoka wanachukia, wao hujifanya kwamba hawajui kama kuna jehanamu kwa waovu.
Ni watu wachache sana ambao hufanya juhudi katika MUNGU ili watengeneze njia zao na kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO.
 Ndugu zangu wote mnaojifunza somo hili, ingekuwa heri sana kila mwanadamu wakati wa uhai wake akampokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake na kuanza kuishi maisha matakatifu ya wokovu, ili tu kuitengeneza kesho yake, ili iwe faida kwake hata kipindi atakuwa hayupo duniani.
Watu wengi sana katika kuishi kwao wanamsahau MUNGU Muumbaji wao na wanaiona injili ya KRISTO kuwa ni kero tu kwao.
Mtu yuko tayari siku zote awe busy tu kutafuta pesa, hana muda na ibada kanisani, hana muda na kuhudhuria mikesha ya maombi, hana muda na kuhudhuria mikutano ya injili, hana muda na kuishi maisha matakatifu.
Kuna watu wako makini sana kuitengeneza leo yao kwa makini sana, huku hawana nafasi ya kuitengeneza kesho yao kwa YESU KRISTO ili hata wakifa wasiende jehanamu.
Kwa watumishi wa KRISTO kama mimi wakati mwingine tumekutana na matusi makubwa sana ya watu ambao hawamtaki huyu YESU tunayemhubiri, wako watu hata wanatiishia kuwaua watumishi waaminifu wa MUNGU ili tu watumishi hao wa MUNGU wasiwahubirie kuhusu kumpokea YESU na kuokoka.
Mtu mmoja ambaye anajiita mtumishi wa MUNGU siku moja alinishangaza sana, mtu huyo aliniambia kwamba niache kuwa naanza somo langu kwa kusema ''Bwana YESU atukuzwe'' maana  hilo ni jambo baya na halipendezi na amenivumilia muda mrefu lakini hakuona nikiacha tabia hiyo ambayo kwake haifai, nilibaki kucheka tu maana watu katika kizazi cha leo hatawaki hata useme Bwana YESU asifiwe.
Ndugu, inawezekana na wewe ni mmoja wao ambao huwa unakwepa mafundisho sahihi ya Neno la MUNGU katika KRISTO YESU.
Inawezekana wewe ni mmoja wa watu ambao huwa unawaona wanaohubiri injili wanapoteza muda tu, wala huna muda wa kuwasikiliza.
Inawezekana wewe unafanya kila juhudi utajirike, ni sawa lakini hata kama utakuwa tajiri kiasi gani lakini kama hutaishi maisha matakatifu katika KRISTO hakika jehanamu itakuhusu.
Ndugu yangu ni heri ukautafuta kwanza ufalme wa MUNGU.
Mathayo 6:33 '' Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.''
Unaweza ukafanya juhudi zote kuburudisha moyo, kuipendeza duniani au kuwa maarufu sana au mtu anayeheshimiwa sana, ni sawa lakini kama YESU KRISTO sio Bwana na Mwokozi wako na hauishi maisha matakatifu hakika ni hasara kuu kwako.
Hakuna atakayeondoka na pesa zake, hakuna atayeondoka na umaarufu wake, hakuna atayeondoka na cheo chake au heshima yake, wote wanaoondoka huwa wana jina moja tu yaani marehemu, na baada ya kuondoka duniani ni mbinguni kama uliishi maisha matakatifu ya haki katika KRISTO au ni jehanamu kama ulimkataa YESU na kuishi maisha ya dhambi.
Kumbuka jambo hili muhimu sana sana kwamba '' Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu;-1 Timotheo 6:7 ''
 Hata kama baada ya kifo chako watu watakusifia sana na kukusema vizuri sana lakini hiyo haitakusaidia lolote kama hutakuwa kule aliko YESU KRISTO Mwokozi.
Hata kama watu duniani wataomboleza siku nyingi kwa sababu yako, bado hiyo haikusaidii lolote kama hutakuwa Mbinguni kwa MUNGU Baba.
Hata kama watu wa kila taifa na kila kabila, wa kila rangi na kila umri watasema ''Ulazwe mahali pema peponi'' bado kabla hata hawajasema maneno hayo wewe utakuwa kwenu tayari, utakuwa mbunguni au kuzimu.
Hata kama kila mmoja atasema ''BWANA alitoa na BWANA ametwaa'' bado hiyo haitakubadilishia makazi yako baada ya kuondoka duniani.
Biblia inasema matendo  yako yatakuwa juu ya kichwa chako(Obadia 1:15)
Wanaoombea wafu hao wanajifariji uongo maana mwanadamu aliyekufa hana sehemu katika walio hai, hata ukimwombea utakuwa unajifurahisha tu maana kabla hujaanza kuomba yeye alishafika kwao tayari kulingana na matendo yake na mlango wa kutoka huko ulishafungwa kama ambvyo MUNGU aliufunga mlango wa Safina ya Nuhu kiasi kwamba hakuna mabye angeweza kuingia katika safina.
Biblia inasema kwamba wafu hawana sehemu katika jambo lolote duniani, hivyo hata maombi yako kwao hayana sehemu yeyote ya kuwasaidia kwa lolote, sasa wewe tenda dhambi ukidhani kanisa watakuombea siku ukifa, ndugu kabla Kanisa hawajakuombea utakuwa kwenu tayari.
Mhubiri 9:5-6 ''kwa sababu walio hai wanajua ya kwamba watakufa; lakini wafu hawajui neno lo lote, wala hawana ijara tena; maana kumbukumbu lao limesahauliwa.  Mapenzi yao na machukio yao, na husuda yao, imepotea yote pamoja; wala hawana sehemu tena katika jambo lo lote lililofanyika chini ya jua. ''

Tena Biblia inakutaka sasa kuchagua hatima yako.
Bwana YESU KRISTO aliyee pekee Mwokozi aliyeletwa na MUNGU Baba anasema '' Mwenye kudhulumu na azidi kudhulumu; na mwenye uchafu na azidi kuwa mchafu; na mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa. Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.-Ufunuo 22:11-13''

 Ndugu, hukuja na kitu duniani na hautaondoka na kitu duniani.
Pesa zako ulizotunza benki hutaondoka nazo, majumba yako mazuri na mali zako hutaondoka navyo. Ulikuja duniani wewe tu na utaondoka duniani wewe tu.
Hata waliokudanganya na kukufanya utende dhambi hutaondoka nao, waliokuingiza kwenye dhambi hutaondoka nao, waliokuwa wanakushawishi umwache YESU hutaondoka nao, waliokuwa wanakutumia kama chombo chao cha starehe hutaondoka nao.
Waliokuwa wanakukataza kuokoka hutawaona wakati huo.
Ulikuja wewe tu na utaondoka wewe tu.
Ayubu 1:221 '' ......... Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, nami nitarudi tena huko uchi vilevile;........ ''
 Hata mumeo au mkeo uliyempenda sana wakati huo utatengana naye tena kama mmoja ataenda mbunguni na mwingine jehanamu basi mtatengana milele hata kama mliitana wa kufa na kuzikana.
Upendo wote wa wanadamu utaishia kaburini, tena hata mke wako au mume wako baada ya siku kadhaa atakusahau na kuoa mwingine au kuolewa na mwingine na maisha yataendelea. Ndugu kama umelijua hili leo nakuomba sana sana mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako na anza kuanzia leo kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU.
 Ingia katika safina leo maana mlango ukifungwa hutaweza kuingia ndani ya safina hiyo, safina yetu ni Bwana YESU hivyo hakikisha unaingia katika safina.
Usikubali mtu yeyote akutoe kwa YESU Mwokozi.
Kama hujawahi kwenda Kanisani kumwabudu MUNGU Baba katika Roho na kweli basi kuanzia leo lifanye kanisa kuwa rafiki yako na litii Neno la KRISTO unalofundishwa Kanisani.
 Ulikuja duniani wewe tu na utaondoka wewe tu, ukilijua hilo ndugu nakuomba sasa anza kuishi maisha matakatifu ya wokovu wa KRISTO YESU, Hakikisha wewe ni mtakatifu kila siku.
Siku moja niliumia sana rohoni mwangu, nilitoka Kanisani kwenye maombi  nikapitia kwenye duka fulani kutoa pesa kwa tigopesa, nilipokuwa natoa pesa nikaona flash nzuri ila sikuwa na pesa siku hiyo ya kutoshkuinunua flash ile, nikamwambia muuzaji kwamba kesho yake asubuhi nitaenda pale kuinunua ile flash. Nikaondoka kwenda nyumbani. Kesho yake nikaenda pale dukani asubuhi kwa ajili ya kununua ile flash lakini nikakuta duka limefungwa. Watu wakasema kwamba ndugu yule amekufa jana yake  usiku. Yaani baada ya mimi kuondoka pale dukani ulipita muda mfupi ndugu yule akafunga duka na kuchukua bodaboda ili impeleke nyumbani kwake, akiwa njiani  kuna gari ikawagonga kwa nyuma na ndugu yule akafa pale pale, nilumia sana baada ya kusikia hivyo.
Ayubu 14:1-2 ''Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe. ''
Ndugu zangu ni heri sana kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU.
Ndugu huyu alikuwa na mipango mingi sana na rafiki zake walisema kwamba alikuwa na mpango wa kununua gari nzuri mwaka huo huo.
Ndugu yangu unayejifunza somo hili nakuomba sana tambua kwamba hakuja na kitu duniani na hutaondoka na kitu vilevile, ni heri uokoke sasa na kuishi maisha matakatifu ya Wokovu kwa muda wao uliobaki wa kuishi duniani.
Huko huko uliko tafuta Kanisa linalofundisha Wokovu wa KRISTO kwa usahihi, okoka na anza kumtumikia KRISTO  huko.
Inawezekana mali zako ulizozitafuta kwa miaka mingi hata ukasahau kuokoka, utakaowaachia watazitumia kwa  muda mchache sana.
Ndugu sikukatazi kufanya kazi au kutafuta pesa lakini hakikisha unaokoka na ishi maisha matakatifu.
Usikubali kuwa mtu wa kwenda kanisani Christmas tu au pasaka tu, bali hakikisha unakuwa mtu wa ibada siku zote.
Hakikisha unaokoka na kuishi maisha matakatifu, Mche MUNGU na kataa dhambi zote na ziache kuanzia leo.
Kumbuka baada ya kifo inayofuata ni hukumu tu hivyo watenda dhambi sehemu yao ni ziwa la moto.
Ukimbie moto wa jehamau leo kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako.
Waebrania 9:27 '' Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;''
Ni heri uokoke maana hukumu ya adhabu kwa wateule wa KRISTO.
Warumi 8:1 ''Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika KRISTO YESU.''

'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22   ''
 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments