KAZI ZA MWALIMU WA NENO LA MUNGU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.



Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu, karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Ualimu wa Neno la MUNGU ni moja ya huduma tano ambazo MUNGU amezitoa katika Kanisa lake.

Ili kuukamilisha Mwili  wa KRISTO ambao ni Kanisa kunahitaji Mitume, Manabii, Wainjilisti, Wachungaji na Walimu.

Waefeso 4:11-12 ‘’ Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;
12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; ‘’

Kila mwenye wito wa huduma anatakiwa kutimiza majukumu yake.

Mimi binafsi kama Peter Sitasahau mwaka mmoja  Tarehe 2 Mwezi wa Nne   ambapo ROHO MTAKATIFU alisema na mimi kwamba ameniita katika Kazi ya ualimu wa Neno la MUNGU. Tangu siku hiyo nilijitambua na kujielewa.

Kibinadamu  kama ningeambiwa kuchagua huduma ya kumtumikia Bwana YESU basi hakika ingekuwa vigumu kwangu kuchagua huduma ya ualimu. Lakini hakuna Mkristo hata mmoja ambaye anaweza kujichagulia huduma ya kumtumikia Bwana YESU.

ROHO MTAKATIFU ndiye anayechagua watu kwa upendo wake mwenyewe.

Zamani nilikuwa naomba juu ya karama ambazo nilitaka nimtumikie MUNGU kwa hizo lakini nikakatazwa maana huwezi wewe mwanadamu kujichagulia huduma au karama utakayo bali ROHO MTAKATIFU ndiye hugawa  kama vile apendavyo yeye.

Katika Kanisa la leo huduma zimekuwa kama vyeo, Hayo ni makosa makubwa.

Kuna watu leo ingawa  wamepewa kuwa Walimu au wainjilisti, wao wameamua kujiita Mitume au Manabii wakidhani kuwa Mtume au Nabii ni kupata heshima kubwa, wengine wamejiita Mitume au Manabii ili kujitafutia mali ndio maana Katika Kanisa leo Walimu ni Wachache sana.

Jambo muhimu sana  kwa kila mtu aliyeitwa katika huduma fulani katika Mwili wa KRISTO anatakiwa abaki katika huduma yake.

Katika Kanisa majina  ya huduma hayana maana sana kama mhusika haifanyi kazi yake aliyoitiwa.

Kama utajiita Mchungaji harafu huna kondoo hata mmoja uliyemshuhudia basi wewe sio Mchungaji.

Kama utajiita Nabii wakati hufanyi kazi za Nabii hakika wewe sio Nabii.

Kama utajiita Mtume na hujawahi kufungua hata makanisa 50 basi wewe sio Mtume.

Kama utajiita Mwinjilisti na hujawahi kuwaleta kwa YESU hata watu 20 basi wewe sio Mwinjilisti.

Kumbuka MUNGU alituita kwa kusudi na yeye ndiye hufanya kazi zake kupitia sisi, hivyo ukikataa wito au kujichagulia wito utajikuta unafanya kazi  peke yako maana umelikataa shauri la MUNGU.

Wafilipi 2:13 ‘’Kwa maana ndiye MUNGU atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema. ‘’



Leo nazungumzia kazi za Mwalimu wa Neno la MUNGU.

Kazi za Mwalimu wa Neno la MUNGU.

    1. Kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa YESU.
 Mathayo 28:19 ‘’ Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;‘’

Kazi ya kwanza kabisa ya kila mwalimu wa Neno la MUNGU ni kuwafanya watu wote anaowafundisha kuwa wanafunzi wa YESU.

Mwalimu wa Neno la MUNGU anatakiwa kuzingatia hilo siku zote za utumishi wake katika kazi ya MUNGU.

Ni YESU KRISTO Mwenyewe alisema kwamba tuende Duniani kote ili tu tukawafanye watu wote kuwa wanafunzi wake.

Wanafunzi wa YESU ni wale ambao wako tayari kujifunza kwa YESU huku wakiwa wamempokea  yeye kama Mwokozi wao.

Usikubali kuwa Mwalimu wa Neno la MUNGU wa kuwafundisha watu kuwa wanafunzi wako, bali wafanye wawe wanafunzi wa YESU.

Usikubali kuwa Mwalimu wa Neno la MUNGU wa kuwafanya watu wawe wanafunzi wa dhehebu lako, bali wafanye kuwa wanafunzi wa YESU wanaomtii MUNGU katika YESU KRISTO.

Usikubali kuwa mwalimu wa Neno la MUNGU wa kuwafanya watu kuwa wanafunzi wa mwanzilishi wa dhehebu lako aliye mwanadamu, bali wafanye watu wote kuwa wanafunzi wa YESU KRISTO.

Kumbuka hakuna Mwokozi nje na YESU KRISTO Yohana 14:6 na kumbuka pia Bwana YESU alikuwa kuwatafuta watu  wote ili wawe wanafunzi wake

Hivyo epuka sana kuwafanya watu kuwa wanafunzi wako bali wafundishe jinsi ya kuwa wanafunzi wa YESU KRISTO.

Ukizingatia hayo huku ukifanya huduma yako kwa bidii hakika utakuwa Mwalimu mzuri wa Neno la MUNGU.

    2. Kuwafundisha watu kuyashika yote aliyofundisha Bwana YESU.
 Mathayo 28:20 ‘’ na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.‘’

Hii ni kazi muhimu sana kuizingatia kila mwalimu wa Neno la MUNGU.

Hakikisha unawafundisha watu kuyashika yote aliyofundisha Bwana YESU.

 Bwana YESU alifundisha kwa miaka 3 mambo mengi sana na hayo kama msingi yako katika injili zake nne.

Ukisoma agano jipya lote linarudia tu kile alichofundisha Bwana YESU.

Agano la kale pia lina ufunuo mkubwa mno kuhusu YESU KRISTO na mafundisho yake.

Mafundisho makuu ya YESU ni injili yake ya wokovu wa milele.

Kwa hiyo hata unapolisoma agano la kale lisome na kwa jinsi ya KRISTO na fundisha watu kwa jinsi ya KRISTO maana huu ndio wakati wa injili iokoayo na wakati huu utaenda hadi kurudi kwa YESU.

Hakuna kitu ambacho YESU alibakiza katika mafundisho yake hivyo alipokamilisha kazi aliagiza wafundishaji wote wa Neno la MUNGU kufundisha watu wote kuyashika aliyofundisha.

Tunapofundisha  kuyashika aliyoyafundisha Bwana YESU hatuna maana ya kwamba tufundishe watu kusoma Vitabu  vinne tu vya Mwanzo vya agano jipya ambavyo ndivyo vinafunua injili yake, bali tusome  Biblia nzima huku tukijua kwamba huu ni wakati wa injili ya KRISTO, Ukijua hivyo utakuwa mwalimu mzuri wa Neno la MUNGU usiyewachanganya watu.

Tunajua kabisa kulikuwa na wakati wa Watu kuongozwa Dhamiri zao wenyewe, leo hatuwezi  kuwafundisha watu kuongozwa na dhamiri zao wenyewe, bali leo tunawafundisha watu kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.

Tunajaua kuna wakati ulikuwa wakati wa torati, leo hatuwezi kuwafundisha watu kushika torati wakati tuko na KRISTO na  sio torati.

Wakati huu ni wa injili hivyo ni lazima tuhubiri injili ili watu waokolewe na KRISTO na ili watu wafunguliwe  na KRISTO.

Ukiniuliza kazi mbili zilizomfanya YESU kuja duniani nitajikujibu hivi.

a.  YESU alikuja kutafuta na kuokoa watu wote maana wote tulikuwa tumepotea.

Luka 19:10 '' Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.''

b.  YESU alikuja kuziharibu kazi zote za shetani.

1 Yohana 3:8 ‘’ Kwa kusudi hili Mwana wa MUNGU alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. ‘’

Hivyo ni lazima tuwafundishe watu kuyashika yote  aliyofundisha YESU huku tukiwaombea ili YESU awafungue vifungo.

YESU anataka kumweka huru kila mtu

Yohana 8:36 ''Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. ''

Hivyo ni lazima sana tuwafundishe watu kuyashika yote aliyofundisha YESU. YESU alifundisha watu wote kumpokea kama Mwokozi, usipompokea YESU kama Mwokozi umepotea.

YESU alifundisha kumwabudu MUNGU katika roho na kweli.

YESU alifundisha utakatifu n.k

Hayo ndiyo ambayo YESU anatuagiza walimu wote wa Neno la MUNGU kuwafundisha watu wote kuyashika.


3.  Kujibu kibiblia maswali yote yanayowatatiza watu kuhusu Wokovu wengine . 
1 Petro 3:15 ''Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. ''

Hii ni kazi muhimu sana ya mwalimu wa Neno la MUNGU yaani kujibu maswali kuhusu tumaini lako la wokovu.

Katika Elimu ya Kidunia Mwalimu hujibu maswali ya wanafunzi wake ili wanafunzi waelewe kwa usahihi, hata wewe mwalimu wa Neno la MUNGU inakupasa kuwa mtu wa kujibu maswali ya wanafunzi wako maana umeitwa katika ualimu basi ulijue na hilo.

Ili uweze kujibu vyema maswali ya wanafunzi wako ni lazima sana wewe mwenyewe uwe mtu wa kujifunza sana sana.

Haiwezekana Mwalimu unafundisha kila siku watu kuokoka kisha mwanafunzi akuuulize kwamba kuokoka ni nini kisha wewe useme sijui, hakika wewe utakuwa sio Mwalimu sahihi wa Neno la MUNGU. Mtu akuulize Wokovu ni nini, wewe useme hujui wakati umefundisha kwa msisitizo mkubwa kuhusu wokovu, ndugu ukijijua wewe ni mwalimu wa Neno la MUNGU hakikisha unajifunza sana Neno la MUNGU na hata kujifunza kwa watumishi wa KRISTO wengine ili uelewe kwa upana zaidi.

Hakikisha unajua kabisa kwamba kujibu Maswali kuhusu MUNGU, kuhusu YESU, kuhusu ROHO MTAKATIFU, kuhusu Kanisa, Kuhusu Injili na kuhusu Biblia nzima hakikisha unajua ili upate kuwasaidia watu wengi.

Pia katika kila somo unalofundisha hakikisha ukiulizwa swali kutokea katika somo hilo hakikisha unajibu, maana huwezi kufundisha kitu usichokijua.

Najua kabisa kuna  wakati ukifundisha mfano ibada kuu Kanisani hakuna maswali kuulizwa lakini katika madarasa huru mfano Sunday School ukiulizwa swali lijibu na hata kama umefundisha mfano kwenye mkutano wa injili  au ibada kuu na hakukuwa na nafasi ya kuulizwa maswali basi ikitokea mtu baada ya ibada akataka umweleweshe kulingana na somo lako basi mjibu vyema maana ni moja ya kazi zako kujibu maswali ya watu wa MUNGU kuhusu MUNGU wao na mpango wake kwao.

Kuna watumishi akiulizwa swali tu basi anachukia na  anawaona waulizaji kuwa ni watu wakorofi tu, kumbe kuna wengine kabisa wanataka tu kuelewe ili wafanyie kazi kwa usahihi.

(unaweza ku-search pia Somo langu linalotiwa  aina za maswali na utajifunza aina mbalimbali za maswali na jinsi ya kujibu)



4.  Kuwafundisha watu kutafakari Neno la MUNGU.
 Zaburi 27:4 ‘’ Neno Moja nimelitaka kwa BWANA, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa BWANA Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa BWANA, Na kutafakari hekaluni mwake. ‘’

5.  Kuwafanya watu wa MUNGU wasikate tamaa katika maisha ya safari ya wokovu. 
Luka 18:1 ‘’ Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba MUNGU sikuzote, wala wasikate tamaa.‘’

6.  Kuisikiliza sana sauti ya ROHO MTAKATIFU na kuifanyia kazi katika mwili wa KRISTO. 
Kumbu 28:1 ‘’ Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani; ‘’

7.  Kujifunza sana kwa KRISTO ili upate kitu cha kuwafundisha watu. 
Mathayo 11:29a ''Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; ''
 

8.   Kuweka Misingi mizuri ya Kiroho kwa unaowafundisha.

Misingi ya kiroho ipo mingi sana baadhi ya misingi muhimu ambayo unatakiwa wewe mwalimu wa Neno la MUNGU kuiweka katika Kanisa ni hii.

Misingi muhimu zaidi ni pamoja na hii.

1.  Utakatifu. 
1 Petro 1:15 ''bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;''
 
2.  Wokovu wa KRISTO . 
Yohana  14:6 '' YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba(MUNGU), ila kwa njia ya mimi. '' Pia soma Matendo 4:12 na Luka 19:10

3.  Imani .
 Warumi 10:17 ''Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO. ''
Pia soma Waebrania 11:6
 

4.  Utoaji. 
2 Kor 9:6-7 '' Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. ''

5.  Kumtegemea MUNGU. 
Yeremia 17:7 ''Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea BWANA, Ambaye BWANA ni tumaini lake.''
 

6.  Maombi.
 1 Thesalonike 5:17 '' ombeni bila kukoma; ''
 

7.  ROHO MTAKATIFU na nguvu zake .
Yohana 14:16-17 ''Nami nitamwomba Baba(MUNGU), naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye ROHO wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. '',
 Pia soma Matendo 1:8, Wagalatia 5:25, Warumi 8:14

8.  Kukataa dhambi zote na kujitenga mbali nazo. 
Zaburi 34:14 '' Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie. ''
 

9.  Toba.
Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; '' 
Mathayo 3:2, Isaya 55:6-7 

10.       Kushuhudia injili na kuikiri hadharani.
 Marko 16:15-16 ''Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. ''

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).
+255786719090
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments