MAOMBI YA KUIFUTA HUKUMU YA KIPEPO KUKUHUSU.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
Bwana YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU na tuombe maombi ya ushindi.
ujumbe wa leo ni maombi ya kufuta hukumu ya kipepo iliyopitishwa kukuhusu wewe.
Hukumu ni nini?
Hukumu ni kutoa uamuzi fulani kwa kutumia mamlaka aliyonayo mtoaji wa uamuzi huo.
Hukumu ni kuamua jambo fulani liwe kama atakavyo aliyeliamua jambo hilo.
Hukumu ya kipepo ni nini?
Hukumu ya kipepo ni kutoa uamuzi mbaya ili jambo baya lililokusudiwa litokee.
Hukumu ya kipepo ni maamuzi yanayofanyika kwenye kikao cha giza ili yampate mtu.
Kumbuka jambo hili ya kwamba ulimwengu wa roho unaenda kwa matamshi hivyo matamshi yaliyonenwa kinyume chako hutengeneza hukumu , leo futa hukumu za kipepo zote kwa damu ya YESU KRISTO ya agano.
Zaburi 31:13-15 ''Maana nimesikia masingizio ya wengi; Hofu ziko pande zote. Waliposhauriana juu yangu, Walifanya hila wauondoe uhai wangu. Lakini mimi nakutumaini Wewe, BWANA, Nimesema, Wewe ndiwe MUNGU wangu. Nyakati zangu zimo mikononi mwako; Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia.''
 Watu wengi sana wanatumia vinywa vyao vibaya na watu wengine ni mawakala wa shetani kabisa kwa ajili ya kutoa hukumu za kipepo kwa baadhi ya watu.
Mama mmoja alitamkiwa na mtu zamani kipindi yuko binti maneno haya '' Hutaolewa  hadi labda mimi nife''
Wakati wa kuolewa ulipofika kwa huyo dada hakika ilishindikana kwa miaka 12 hadi alipokufa kweli yule aliyemtakimkia kwamba hataolewa hadi yeye mtamkaji afe.
Yaani ilichukua miaka kumi na mbili mtamkaji ndipo akafa na mwaka huo wa kumi na mbili ndipo yule aliyetamkiwa akaolewa.
Ndugu hukumu za kipepo zipo nyingi sana na leo hakikisha kila hukumu ya kipepo iliyopitishwa katika ulimwengu wa roho wa hiza kukuhusu wewe inafutika kwa damu ya YESU KRISTO.
Kuna watu wameshikiliwa na maneno mabaya waliyotamkiwa zamani sana au muda uliopita.
Maneno yanaumba na maneno ya kipepo yanayotamkwa kwenye madhabahu za giza Yakiambatanishwa na kafara yanaweza kumshikilia mtu hata miaka makumi kadhaa au mamia kadhaa, ni hatari sana hivyo leo futa hukumu za kipepo zote.
Kumbuka maneno yanaumba.
Mithali 18:8 '' Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo.''

Siku moja usiku mimi P Mabula nilikuwa natembea kwenda nyumbani nikitokea Kanisani, nilipofika njiani nilikutana na binti mdogo wa miaka kama 14 akiwa kabeba mtoto mdogo kama wa miaka miwili, yule mtoto alikuwa analia kidogo huku ukiomba kitu fulani alichokiona njiani, yule binti kwa kama dakika moja alimtamkia yule mtoto maneno mabaya sana hadi nikashtuka huku watu waliokuwa pembeni wakicheka, baada ya kwenda mbele kama hatua kumi na tano nilijikuta  naanza  kumuombea yule mtoto mdogo nikifuta maneno mabaya aliyotamkiwa. Nilijikuta nawaza sana maana hata msichana wa kazi anaweza kumtamkia mtoto wako maneno mabaya ambayo yatakuwa kifungo kibaya ambacho kitamtesa baadae hata hajui chanzo chake, hata ndugu zako unaoishi nao wanaweza kumtamkia maneno mtoto wako mabaya ambayo ulimwengu wa roho wa giza watafanyia kazi na kuwa kifungo kibaya sana kwake baadae. Binti yule alimtamkia maneno mengi mtoto yule na baadhi ya maneno hayo ni haya ''Katoto haka kamelaaniwa, kamejaa laana, kamelaaniwa hata kabla hakajazaliwa na katakaa na laana milele''
Nilishangaa sana na nikawaza sana, inawezekana ndugu hata wewe unashikiliwa na maneno mabaya ambayo ulitamkiwa tangu hata hujitambui.
Biblia inakataza kumhukumu mtu mwingine '' Mtoa sheria na mwenye kuhukumu ni mmoja tu, ndiye awezaye kuokoa na kuangamiza. U nani wewe umhukumuye mtu mwingine?   -Yakobo 4:12''
 Lakini leo kuna watu hutoa hukumu za kipepo kwa watu wengine.
Siku moja nilikuwa namuombea mtu mmoja na wakati nikiomba nikasikia sauti ikisema futa maneno yote mabaya aliyotamkiwa tangu utotoni mwake kutoka kwa ndugu zake, majirani, marafiki na watu aliowahi kuishi nao.
Hata hapo nikajifunza kitu kwamba wapo maelfu ya watu wameshahukumiwa hukumu za kipepo ambazo ndizo wanang'ang'ana nazo sasa kuzifuta kimaombi.
Siku moja pia nilikuwa namuombea mtu na nguvu za giza zikaongea ndani yake kwamba ''Wewe ni nani unataka kututoa humu ndani wakati tuna uhalali wa kukaa humu?''  Kisha yale mapepo yakasema kwamba ''Ni  bibi yake huyu ndio alitupa uhalali kukaa humu kupitia maneno yake kwa huyu''
niliomba na mtu yule akafunguliwa lakini nikagundua kwamba wapo watu yalishatolewa maamuzi zamani katika ulimwengu wa roho wa giza kuwahusu, ndio maana kwa sasa kuna vitu vinagoma kwa sababu hiyo. Ndugu leo omba ukifuta hukumu zote za kipepo kukuhusu wewe. Kumbuka nguvu za giza huwa hazibembelezwi kutoka bali tunatumia mamlaka ya jina la YESU KRISTO kuzilazimisha kutoka na hakika zinatoka. 
Biblia inaathibitisha ya kwamba hata vikao vya kipepo kukuhusu wewe vinaweza kuwepo, ila kama una YESU sasa na unajua kuomba hakika MUNGU anaweza kukushindi sasa hata katika hilo.
Isya 54:15 ''Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako.''

 HUKUMU YA KIPEPO NI IPI?

1. Mipango mibaya yote kukuhusu wewe inayotoka ulimwengu wa roho wa giza.
Waefeso 6:12 '' Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.''
Kwenye ulimwengu wa roho wa giza kuna wakuu wa giza, madhabahu za kishetani, waganga wa kienyeji, wachawi, majini na kila anayetumika kishetani, kutoka kwa hao kunaweza kutoka hukumu za kipepo kukuhusu wewe.

2. Maneno mabaya ya wanadamu wasiokutakia mema yanayoumba.
Mitahli 26:20 '' Moto hufa kwa kukosa kuni; Na bila mchongezi fitina hukoma. ''

3. Agano la kipepo lililoambatanishwa na hukumu ya kipepo kukuhusu wewe.
Waamuzi 2:2-3 '' nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani? Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu.''

 4. Mikataba ya kipepo ya urithi iliyo na hukumu ndani yake.
Maombolezo 5:7-8 '' Baba zetu walitenda dhambi hata hawako; Na sisi tumeyachukua maovu yao. Watumwa wanatutawala; Hakuna mtu wa kutuokoa na mikono yao.   ''

 Kuna mambo mengine huwa hata unayaona kwa ndoto yakijulisha kinachoendelea katika ulimwengu wa roho wa giza, ndugu usidharau kila ndoto.
Unaweza ukaota kabisa umekufa kumbe ni taarifa kwako kwamba wachawi wameshapitisha mamuzi(hukumu) kwamba ufe siku chache zijazo, ndugu futa hukumu zote za kichawi na haribu roho ya mauti iliyotumwa kwako.
Unaweza ukaota unafilisika, kumbe maamuzi mabaya yameshapitishwa katika madhabahu za kichawi kwamba ufilisike, ndugu katika jina la YESU KRISTO leo futa hukumu za kipepo zote kukuhusu wewe.
Unaweza ukaota ndoto una pesa na hizo pesa ghafla mtu anakuibia au zinabeberuka zote, kumbe ni taarifa kwako kwamba katika ulimwengu wa roho wa giza wameshatoa maamuzi tayari kwamba uchumi wako upeperuke wote, ukizubaa utashangaa unafukuzwa kazi au matatizo yanakukumbuka yanayoenda kuufuta uchumi wako.
Ndugu leo hakikisha hukumu za kipepo zote kukuhusu wewe zinafutika.
Unapofuta hukumu za kipepo kumbuka pia na kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU hapo ndipo wakuu wa giza hawatapata nafasi ya kuvamia maisha yako tena maana utaendelea na maombi na ulinzi wa MUNGU utakuwa juu yako.

Lakini pia ROHO MTAKATIFU alinifunulia jambo la ajabu sana.
Kwamba kuna watu wanateseka sasa kwa sababu ya hukumu za kipepo walizojitamkia wenyewe binafsi.
Inawezekana kuna watu walisema ''Hatutapata  mkuu wa kazi kama huyu'' Ndugu futa hiyo hukumu ya kipepo  uliyoipitisha  maana mkuu wako wa kazi wa sasa anaweza akahamisha na akaja mwingine na huyo akaja kutimiza kusudi la kishetani mlilojiwekea kwamba hatakiwi kuwa na kiwango kama yule aliyepita maana mmeshaweka mipaka kabisa katika ulimwengu wa roho kwamba hatakiwi kuja mkuu wa kazi kupita yule mliyempenda.
Inawezekana mnateseka sasa katika familia yenu kwa sababu kuna siku mlisema ''Hakutakuja kutokea mtu mzuri na wa kutujali kama alivyokuwa Baba mkubwa aliyefariki karibuni''
Sasa mnaweza kutamka hayo na kwenye wanaofuata watawatesa maana mlishawawekea mipaka kwa maneno yenu kwamba hawatakiwi kuwa wazuri kumfikia Baba mkubwa, hivyo wakiharibu au kuwatesa ni halali kabisa maana ni ninyi mlitaka hivyo.
Inawezekana unateseka katika ndoa yako kwa sababu uliwahi kusema zamani kwamba ''Sitapata mchumba safi anayenijali kama fulani'' sasa wakati huu uko katika ndoa na huyo mkeo/mumeo hakujali maana ulishaweka mipaka mwenyewe kwa maneno yako kwamba huyo hatakiwi kumfikia fulani wa zamani, ni hatari sana.
Kumbuka hii '' Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,   -Mitahli 6:2''

 Mama mmoja baada ya kuumizwa katika mahusiano alisema kwamba hawataki wanaume  maana wote ni wabaya na mama yao ni mmoja. Baadae alinishirikisha nimuombee ili aolewe, lakini kwa ufunuo nikaambiwa nimwambie atubu kwa maneno ya kinywa chake aliyojifunga nayo.
Kitu kimoja nimejifunza ni kwamba shetani anaweza kumfanya mtu achukie  na katika hasira hizo ajinenee maneno mabaya ya kumfunga kipepo baadae, hiyo ni hukumu ya kipepo inayomfunga mtu mwenyewe.
Leo kwa maombi katika jina la YESU KRISTO futa hukumu za kipepo zote ulizojitamkia mwenyewe na ulizotamkiwa na mawakala wa shetani wote.
Mithali 26:28 '' Ulimi unenao uongo huwachukia wale uliowajeruhi; Na kinywa cha kujipendekeza hutenda uharibifu.''

Maombi ya leo.

1.  Tubu kwa ajili ya hukumu ya kipepo uliyojitamkia mwenyewe na uliyotamkiwa na watu wengine kwa sababu ya kosa lako.
Zaburi 103:3-4 '' Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,''

2. Futa hukumu za kipepo ulizojitamkia mwenyewe.
Mitahli 18:21 '' Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.''

3. Futa hukumu za kipepo ulizotakiwa na wanadamu.
Yeremia 18:18b ''Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote.''

4. Futa hukumu za kipepo ulizotamkiwa na mawakala wa shetani.
Isaya 54:15 '' Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako. ''
Hi
5. Amuru mapigo ya MUNGU yawapate mawakala wa shetani waliofanya hukumu ya kipepo kuhusu wewe.
Zaburi 71:13 ''Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya.'' 

 Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane na nitakujulisha jinsi ya kukipata na  Naamini kitakusaidia sana.
Hapa chini ni MAOMBI YA KUIFUTA HUKUMU YA KIPEPO KUKUHUSU.   Maombi haya naomba yamsaidie mtu yule ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea. Kumbuka pia fundisho ni muhimu kuliko maombi hivyo wewe ambaye huwa unahusika na maombi tu hakikisha unajifunza kwanza somo lote ndipo utapata nguvu za kuomba na kushinda. 

 
MAOMBI YA KUIFUTA HUKUMU YA KIPEPO KUKUHUSU.


 Baba katika jina la YESU KRISTO ninakushukuru Eee MUNGU wangu na nasema mbele zako kwamba asante kwa uzima ulionipa na asante maana ninaishi leo kwa sababu ni wewe tu YAHWEH MUNGU  pekee umetaka niishi.
Eee MUNGU wangu na BABA yangu wa  mbinguni nakuomba BWANA nyoosha mkono wako ili watu wauone na walitukuze jina lako  wewe MUNGU muumbaji.
Nisamehe MUNGU BABA kwa makosa yangu kwa sababu ya kujihukumu hukumu za kipepo. Ninatubu leo juu ya kila Neno au tendo la kihukumu ambalo ni mimi mwenyewe nilijitamkia na kujihukumu na neno hilo likaishi katika maisha yangu, leo ninatubu naomba MUNGU wangu unisamehe. Bwana YESU wewe ndiye kielelezo changu na ulisema '' Jitieni nira yangu, MJIFUNZE KWANGU; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;-Mathayo 11:29 '' hakika Bwana YESU najifunza kwako katika Neno lako Biblia na hakuna popote ulipojitamkia mabaya wala kujilaani, ndio maana leo nakiri kwamba sikujifunza kwako vyema hivyo ninatubu mbele zako MUNGU wa uzima naomba unisamehe kwa maneno mabaya ya kinywa changu ambayo kwa hayo nilijihukumu hukumu za kipepo.
Ninatubu pia kwa ajili ya kila maneno mabaya ya hukumu waliyonitamkia wanadamu wote, naomba unisamehe MUNGU wangu, natubu kwa ajili ya kila neno baya la mchawi, mkuu wa giza au jini yeyote, natubu kwa ajili ya neno la mizimu au mababu wa zamani, natubu kwa ajili ya hukumu za kipepo za vizazi au za famili au za ukoo, hivyo kama kuna Neno la kuhumu walitamkiwa babu zangu zamani na mimi leo nafuatiliwa na hukumu hiyo, leo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO ninatubu mbele zako MUNGU BABA na naomba sasa mlango huo wa kipepo ujifunge kwangu ili mabaya yaliyokusudiwa yasinipate.
 Niko mbele zako sasa ninafuta kila hukumu ya kipepo niliyojitamkia mwenyewe. Neno la MUNGU linasema
'' Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,   -Mitahli 6:2'' nafuta hukumu za kipepo zote nilizojinenea mimi mwenyewe, inawezekana nilikuwa na hasira, inawezekana nilitendwa, inawezekana sikujua kama maneno yanaumba hivyo nikajitamkia, leo kwa mamlaka ya jina la YESU ninaomba sasa nikifuta kila hukumu niliyojihukumu mimi mwenyewe, Damu ya YESU KRISTO ya agano nainyunyuzia katika kila neno la Hukumu na damu ya YESU KRISTO inafuta sasa kila neno la hukumu nililojitamkia mimi mwenyewe, ninaamini imekuwa sasa kwa jina la YESU KRISTO.
Katika jina la YESU KRISTO ninafuta kila neno la hukumu nililotamkiwa na wanadamu wasionitakia mema.
Ninafuta kila Neno la hukumu nililotamkiwa na watu ambao niliwaudhi na nafuta kila Neno la hukumu walilonitamkia watu wanaonichukia na nafuta kila Neno la hukumu lililonenwa na watu niliowachukiza, kwa damu ya YESU KRISTO nafuta maneno hayo ya hukumu.
Kila neno la hukumu nililotamkiwa na wazazi wangu, ndugu zangu, majirani, wafanyakazi wenzangu na watu wote popote walipo, nalifuta neno hilo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Neno la MUNGU katika Isaya 54:15  linasema '' Tazama, yamkini watakusanyana; lakini si kwa shauri langu. Watu wo wote watakaokusanyana juu yako wataanguka kwa ajili yako. ''
 Hivyo wachawi wote walioamua chochote kunihusu mimi, leo hukumu zao nazifuta kwa damu ya YESU KRISTO.
Wakuu wa giza wote na majini wote kila hukumu waliyoipitisha kunihusu mimi, leo kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO nafuta hukumu zao zote.
Waliopanga nipate ajali au balaa, naifuta hukumu hiyo ya kipepo, naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Waliopanga nisiingie kwenye ndoa au nisipate mchumba,  naifuta hukumu hiyo ya kipepo, naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Waliopanga nisifaulu masomo au nisiwe na biashara nzuri, naifuta hukumu hiyo ya kipepo, naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Waliopanga niwe kichaa au nisipendwe na watu, naifuta hukumu hiyo ya kipepo, naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Walitamka kwamba sitazaa au sitaishi miaka mingi, naifuta hukumu hiyo ya kipepo, naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Waliotamka sitapata kazi au sitaishi maisha ya furaha, naifuta hukumu hiyo ya kipepo, naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Kila walionitamkia maneno mabaya ya namna yeyote mabaya na ya kunizuia, naifuta hukumu yao hiyo ya kipepo, naifuta kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
 Sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninaamuru mapigo yawapate wakuu wa giza wote, wachawi wote, washirikina wote, majini wote, mizimu yote na kila ajenti wa kuzimu. Ni kweli walinitamkia hukumu na ikanitesa, leo kwa damu ya YESU KRISTO nimefuta hukumu zao zote na sasa '' ''Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya.-Zaburi 71:13'' 
na sasa katika jina la YESU KRISTO '' Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!-Zaburi 40:14-15 ''
 na sasa katika jina la YESU KRISTO '' Waaibishwe, wafedheheshwe, Wanaoitafuta nafsi yangu. Warudishwe nyuma, wafadhaishwe, Wanaonizulia mabaya. Wawe kama makapi mbele ya upepo, Malaika wa BWANA akiwaangusha chini.  Njia yao na iwe giza na utelezi, Malaika wa BWANA akiwafuatia.  Maana bila sababu wamenifichia wavu, Bila sababu wameichimbia shimo nafsi yangu. Uharibifu na umpate kwa ghafula, Na wavu aliouficha umnase yeye mwenyewe; Kwa uharibifu aanguke ndani yake.-Zaburi 35:4-8 ''
 Mimi nimeshinda katika jina la YESU KRISTO. Eee Bwana YESU KRISTO  naomba unipe neema niishi maisha ya wokovu wako siku zote ili mawakala wa shetani wasinishinde kamwe.
Nakushukuru MUNGU BABA maana katika jina la YESU KRISTO nimeshinda.
Nakushukuru ROHO MTAKATIFU maana umenifunulia ushindi wangu, nakuomba BWANA nipe neema nitembee kwenye kusudi lako.
Katika jina la YESU KRISTO Mwokozi wangu nimeomba na ninashukuru sasa maana nimeshinda.
 Amen Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
Hakika umeshinda. Ukiweza kufunga unaweza kufunga hata siku 1 au 3 au 4 au hata 5 au zile ambazo wewe utaona unaweza ukihusika kila siku na kipengele kimoja kuombea na kumbuka baada ya maombi ya kufunga au hata maombi ya bila kufunga fanya tendo la imani kwa MUNGU kwa kutoa sadaka nzuri itakayoambatana na maombi  juu ya ukomo wa kuteswa na maadui zako katika ulimwengu wa roho
Nawaonya pia wanaotumia masomo yangu vibaya na kwa manufaa yao waache tabia hiyo.
 Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? 

Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292.
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments