MAOMBI YA TOBA.

Na Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.

Bwana YESU atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Leo kwa sehemu kidogo sana nazungumzia umuhimu wa maombi ya toba.
Kuna aina moja tu ya maombi ya mtu mwenye dhambi ambayo MUNGU anaweza kuyasikia na kujibu, Ni maombi ya toba na kuhitaji kuokolewa.
Ukisoma Biblia utagundua aina hiyo moja tu ya maombi ya watenda dhambi ambayo maombi hayo yanaweza kupata kibali kwa MUNGU.
Mfano hai ni huu.
Waamuzi 3:15 ''Lakini wana wa Israeli walipomlilia BWANA, BWANA akawainulia mwokozi, Ehudi, mwana wa Gera, Mbenyamini, mtu aliyekuwa mwenye shoto; ..........  ''

MUNGU anakutazama wewe kama mtu wa thamani sana mbele zake.
Je wewe ndugu unatunza thamani yako uliyopewa na MUNGU?

Kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO ndio kuitunza thamani yako.
Kama uhusiano wako na MUNGU Muumbaji wako ulivunjika, basi ni toba tu katika KRISTO ndio inayoweza kuurudisha uhusiano huo.
Wako watu wanaishi maisha ya dhambi, ndugu nakuomba sana okoka na acha dhambi hizo.
 Mtu mmoja ambaye na kanisa huenda lakini aliniambia siku moja jambo la ajabu sana. Mtu huyo alisema kwamba yeye ni kahaba wa hatari sana, nilishangaa kwamba anajiita Kahaba wa hatari, anajielewa kwamba yeye ni kahaba wa hatari na anajua kabisa kwamba akifa katika dhambi hiyo hawezi kuingia uzima wa milele. Nilimwambia kwamba ampokee YESU KRISTO kisha atubu na kuacha dhambi hiyo, kisha atumie muda wake kumtumikia Bwana YESU. Ndugu inawezekana na wewe ni mtenda dhambi mkubwa sana, nakuomba ndugu acha dhambi hizo.
Inawezekana wewe huwa unahukumu wengine lakini hata na wewe unatakiwa kutubu maana unafanya dhambi za siri.
Ndugu achana na uzinzi na uasherati, tubu na anza kuishi maisha matakatifu.
Kijana mmoja ambaye hakuwa ametulia lakini alikuwa anahitaji mke mwema, Wakati mmoja  alimpenda binti mmoja na kutaka kumchumbia lakini ghafla akaacha na kuanza kumsema vibaya yule binti baada ya kugundua kwamba yule binti ana mtoto. Yule ndugu alimuona yule binti kama malaya tu hivyo hakutaka tena kumuoa. Baadae alipokuwa anaomba ushauri alikutana na majibu yaliyomvunjavunja na ndipo akaona hata umuhimu wa kumuoa binti yule yule ambye kwa sasa ameokoka na anaishi maisha matakatifu. Kijana yule aliambiwa kwamba anaweza akamkataa mwanamke ambaye alishazaa, ila kwa sasa anaishi maisha matakatifu na yeye huyo huyo akampata binti ambaye hajazaa ila ameshatoa mimba zaidi ya tano. Maana yake anataka kumkimbia mwamake wa mtoto mmoja ili apate mwanamke wa watoto saba aliowaua mwenyewe wakipokuwa ndani ya tumbo lake. 
Ndugu yule baada ya kuambiwa hivyo aliona heri kuoa mwanamke ambaye alishazaa ila sasa anaishi maisha matakatifu, kuliko kuoa mwanamke ambaye hajazaa ila aliua watoto wake tumboni.
Ndugu zangu, kama mtu ameokoka sasa na anaishi maisha matakatifu ya wokovu ya haki katika KRISTO YESU hakika mtu huyo alishasamehewa na uovu wake wa zamani haumhusu tena kwa sasa. Ndugu hata wewe kwa maombi yako ya toba kwa YESU KRISTO kisha unaacha dhambi zako na sasa unaanza kuishi maisha matakatifu ya wokovu hakika historoa ya maisha yako inaweza kubadilika na wewe sasa kuitwa mtakatifu wa MUNGU.
Ni nafasi yako leo ya kutubu na kuacha dhambi zako zote.
Hata kwa watu ambao wameokoka ni muhimu sana kuomba maombi ya toba kwa ajili ya ndugu, taifa, jamii au watu wa karibu yako maana maombi ya toba ni ya muhimu sana.
Kwanini utubu kwa ajili ya wengine?
Unapotubu kwa ajili ya wengine unamshawishi MUNGU kwa ajili ya hao wengine.
Unaposimama kutubu kwa ajili ya nchi tambua kwamba wewe ndio hiyo nchi na uko kuiwakikisha nchi yote. Kuna mataifa au miji au maeneo wewe wala hujazaliwa huko lakini MUNGU amekuweka ili uwe nabii kwa mataifa na maombi yako ya toba kwa ajili ya taifa lako yataiponya nchi yako.
MUNGU anaheshimu Neno la mtumishi wake.

Yeremia 1:5 "Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni nalikutakasa; ninekuweka kuwa nabii kwa mataifa.''
Kama ulianguka dhambini inakupasa sana kutubu na kuacha dhambi zako zote.
Nakuomba ndugu usiishie kutubu tu bali hakikisha unatubu na kuacha dhambi zako.
Kumbuka ni wapi ulianguka ili ukatubu.
Ufunuo 2:5 "Basi, kumbuka ni wapi ulikoanguka; ukatubu, ukayafanye matendo ya kwanza. Lakini, usipofanya hivyo, naja kwako, nami nitakiondoa kinara chako katika mahali pake, usipotubu."

Je uasherati na uzinzi ndio mwanzo wa vifungo kwako?
Kumbuka ni wapi ulianguka ili sasa ukatubu na kuacha dhambi hizo.
Je kwenda kwa mganga ndio mwanzo wa wewe kuteswa na mapepo na kila aina ya uonevu?
Kumbuka ni wapi ulianguka ili ukatubu.
Je kiburi chako ndio anguko lako?
Je anasa za dunia ndio zimekuwa chanzo cha anguko lako hata shetani sasa anakutesa?
Ndugu kumbuka ni wapi ulianguka ili utubu.
Wengi walimwacha YESU kwa sababu za mambo ya kidunia, ndugu kumbuka ni wapi ulianguka ili ukatubu.
Kuna watu waliacha ibada ndio maana sana wanateswa na vifungo vya Giza, kuna watu waliacha huduma walizopewa na MUNGU ndio maana kwa sasa shetani anawapepeta vile atakavyo, ndugu kumbuka ni wapi ulianguka ili utubu na kurejea katika Bwana YESU Mwokozi.
Je, wizi wako ndio imekuwa mlango wa shetani kukutesa? Je mikataba ya ki shetani ulioingia ndio imekuwa chanzo cha laana kwako? Ndugu, kumbuka tena kumbuka sana ni wapi ulianguka ili sasa ukatubu.

Kuna watu kutoa mimba kwao ndio umekuwa mlango wa shetani kuwaonea.
Kuna watu uongo na dhambi za siri ndio vimekuwa chanzo cha maroho ya kuzimu kuwatesa.
Ndugu, Biblia iko wazi mno kwamba kumbuka ni wapi ulianguka ili ukatubu.
Je ukahaba wako ndio imekuwa chanzo cha kufungwa vifungo vingi vya Giza?
Ndugu ni saa ya kutubu na kurejea kwa Bwana YESU Mwokozi.

Je ni wapi ulianguka ili sasa utubu kwa Bwana YESU na vifungo vikuachie?
Je uliua hata damu ya uliyemuua inakulilia na shetani sana amekukalia kichwani?
Ndugu kumbuka ni wapi ulianguka ili ukatubu.
Je uliacha ibada?
Je uliwasema vibaya watumishi wa kweli ya Bwana YESU? Je uliwatukana watumishi wa MUNGU waliokuambia ukweli.
Ndugu kumbuka ni wapi ulianguka ili Leo utubu.
Najua unajua kabisa ni wapi ulianguka hivyo nakuomba utubu.
Ndugu Yangu, ni muhimu sana kutubu kutengeneza kwa Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
Matendo  3:19 " Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"


 Kuna mahali katika makanisa ukifundisha utakatifu watasema unawahukumu.
Kuna watu ukifundisha waache dhambi watakuona unawahukumu, kumbe unawasaidia.
Maombi ya toba ni muhimu sana sana.
Hata kutubu kwa ajili ya uzao wa mama yako ni muhimu, tubu kwa ajili ya ndugu zako na juu ya ukoo wako maana kuna milango mingi ya giza inaweza kuendelea kuwatesa katika familia au ukoo, lakini kutubu kunapelekea hati za mashtaka zote kufutika na milango walioitumia mawakala wa shetani inafungwa, maombi ya toba ni muhimu sana.
Hebu ngoja nikupe mfano mmoja hai ambao ni huu; Ulipozaa mtoto kitovu chake ulikipeleka wapi?
Ulipozaliwa je kitovu chako alipewa nani?
Ezekieli 16:4 ''Na katika habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuoshwa kwa maji usafishwe; hukutiwa chumvi hata kidogo, wala hukutiwa katika nguo kabisa. ''
Jamii nyingi sana shetani amewadanganya wazazi mapema kabisa ili tu ahakikike watoto wanapandikiziwa maroho ya kishetani wakiwa wachanga kabisa.
Nimewahi kukutana na kesi hizi nyingi sana maana uongo umetawala sana kiasi kwamba kuna wamama wana miaka zaidi ya 5 wameficha nywele za kwanza za watoto wao, kucha za kwanza za watoto wao na kitovu kilichokatwa.
Wengine vitu hivyo wamewapa akina bibi na wengine wamewapa waganga. Ndugu zangu, shetani akitaka akupate kwamba anakutengenezea vitisho ili ujipeleke kwake mwenyewe wakati anakudanganya tu.
Mama mmoja aliniambia kwamba ilifika kipindia akaona neno la MUNGU nimeandika kama miaka 2 iliyopita la kumtaka kama ana vitu hivyo avitupe tu wala mtoto hatadhurika, tena neno lile lilisema kwamba hata avichome moto na sio kumpa mganga. Yule mama baada ya kulielewa Neno la MUNGU alichukua na kwenda chooni lakini akitaka tu kutupa anaghairi maana alikwishaambiwa zamani kwamba akivitupa mtoto atakufa hivyo ampe mganga ili kutengeneza ulinzi kwa mtoto, kumbe mganga anataka kumwekea mtoto roho ya shetani. Baadae yule mama alinitafuta na kuniomba ushauri, nikamwambia avitupe tu na wala mtoto wake hatadhurika kwa lolote, nikamuombea na nikamuombea mtoto na akavitupa, maana Bwana YESU ana ulinzi wa milele. Baada ya hapo hata magonjwa yaliyokuwa yanamtesa mtoto mara kwa mara yakaondoka na mpaka leo wanaendelea vizuri sana.
Ndugu zangu waganga wamedanganya wengi sana.
Ninaomba kuanzia leo wewe mzazi ambaye unaogopa kuhusu kitovu basi mweleze mchungaji wako akusaidie. Usikubali kumpa bibi wala babu wala shangazi wala mganga bali tupa au mwite mchungaji wako akusaidie kuvitupa au kuvichoma moto kisha atakuombea wewe na mtoto wako.
Ukimtegemea Bwana YESU hakika atakuokoa wewe na mtoto wako.
Unaweza kuwa wewe ni mtu wa kanisa lakini huwa unafanya mambo hayo, ndugu unahitaji kutubu na kuacha uovu huo.
Siku moja nitakuja na somo la maombi ya kuombea vitovu na kufuta maagano yote ya kishetani yaliyofanyika kupitia vitovu vyetu siku tunazaliwa, kama yalifanyika.
Unaweza kuwa unakatatiliwa Leo kwa sababu ulitengenezewa kukataliwa tangu ukiwa mchanga.
Unaweza kuwa mtu wa balaa na mikosi kumbe hayo yalitengenezwa wakati ukiwa mchanga.

Maombi ya toba ni ya muhimu sana.
Yoeli 2:12-14 ''akini hata sasa, asema BWANA, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea; rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie BWANA, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya. N'nani ajuaye kwamba hatarudi na kugeuka, na kutuachia baraka nyuma yake, naam, sadaka ya unga, na sadaka ya kinywaji, kwa BWANA, Mungu wenu?''
 
 Moja ya silaha kubwa sana ya mteule kuikwepa dhambi kirahisi ni wewe mteule kukiri mbele ya watu kwamba umeokoka.
Sema kwa ujasiri mbele za watu kwamba Bwana YESU KRISTO amekuokoa hivyo huna haja na mambo ya dunia.
Hata marafiki zako wanaotaka kukuingiza dhambini wataogopa maana watauona msimamo wako kwa YESU Mwokozi.
Lakini pia ndugu zingatia haya kwamba ukiwa umeokoka kweli hakikisha unabadilika usemi, nikiwa na maana ya kuacha matusi na kuongea maneno yasiyofaa yote.
Usivae mavazi mabaya yanayoweza kukutambulisha kama mtu asiyemcha MUNGU.

Kama kuna uovu kwako hakikisha unatubu leo na kuacha uovu huo, waone wachungaji katika maeneo yako wakusaidie.
Acha matendo mabaya na thibitisha Wokovu wako asubuhi, mchana, jioni na usiku wote, yaani kila muda thibitisha Wokovu wako.

Waefeso 2:8-10 ''Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha MUNGU; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika KRISTO, tutende matendo mema, ambayo tokea awali MUNGU aliyatengeneza ili tuenende nayo.'


'' Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa.-Ufunuo 3:22   ''
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu pia kitabu changu cha MAOMBI YA KINA kinapatikana, tuwasiliane nitakujulisha jinsi ya kukipata.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
BWANA YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na BWANA YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee BWANA YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0714252292(Hadi whatsapp).
mabula1986@gmail.com
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu.

Comments